read

Mwanzo wa Safari

Mbingu inaiangazia ardhi, na kuangaza njia zake zinazopitika, mwanadamu hajui lugha yake, na wakati mwingine hufanya njama bila ya kuelewa ili kuzuia mionzi yake pamoja na yote hayo halichoki, mikono yake inabaki imekunjuka ili huenda ataongoka yule atakayeikamata na kupata uongofu.

Jua linaelea angani na udanganyifu umemeza sehemu kubwa miongoni mwa nuru yake katika wakati huu, na katika moja ya njia za kijiji changu kilichojawa na ugeni, ilinijia taufiq iliyokuwa imejificha katika maneno ya rafiki yangu ambaye amekuwa rafiki yangu tangu utotoni.

Nilijadiliana naye mara nyingi ili avue itikadi yake ambayo aliichukua kutoka kwa Ahlul-Bait (a.s) na avae Usunni, ulikuwa ni wakati wa mjadala mkali kati yangu na yeye, nilitamani aingie katika madhehebu yangu. Siku zikapita nikasajiliwa katika kitivo cha Sheria na masomo ya Kiislam, ambapo waalimu wangu walikuwa hawawataji Ahlul-Bait (a.s) kwa kheri.

Pamoja na kwamba mimi nilikuwa katika madhehebu ya Shafi, isipokuwa nilianza kuathirika kwa yale waliyofundisha waalimu wangu wa kisalafia katika yanayohusu itikadi, basi nikaanza kukariri mafunzo ya itikadi ya salafia. Kadhalika yale yanayosemwa juu ya Shi’a darasani ili nianze kumuongoa rafiki yangu lakini alikuwa ananijibu kwa hoja zenye nguvu.

Na katika matembezi yetu wakati nilipokuwa namsimulia juu ya fadhila za Abubakari na Omar akanikata kauli kwa kusema - kama vile mwenye kunusurika - "huzuni ya siku ya Alhamisi!" Nikasema: "Kheri, unakusudia nini?" Akasema: "Hakika hilo ni tukio lililotokea kwa siku chache kabla ya kifo cha Mtume (s.a.w.w) ambapo Mtume (s.a.w.w) aliwaambia masahaba wake: "Njooni niwaandikie maandiko hamtapotea kamwe baada yake," Omar akasema: "Hakika Mtume amezidiwa na maumivu, au anaweweseka, kinatutosha kitabu cha Mwenyezi Mungu."

Nikamwambia: "Nyinyi mmefikia kunasibisha maneno haya kwa Al- Faruuq, ambaye hakumuasi Mtume katu?" Akasema: "Tukio hili utalikuta katika Sahihi Bukhariy na Muslim"1

Hapo nikakata tamaa kutokana na jibu lake, nikahisi kushindwa na nikasema haraka: "Hata kama amesema hayo bado anabaki kuwa sahaba." Namuomba Mwenyezi Mungu msamaha. Sentensi hii haikuja bure tu, bali ni ishara juu ya itikadi iliyokita mizizi katika akili zetu. Nikamuuliza: "katika kitabu gani umesoma tukio hili?" Kwa sababu mimi hata kama nitasimama msimamo wa mpingaji aliyeshindwa na kukiri, lakini nilikuwa nateketea kwa uchungu.

Akasema: "katika kitabu cha mmoja wa maulamaa wa Sunni ambaye ameingia katika madhehebu ya Ahlul-Bait (a.s)." Nikaomba kitabu kutoka kwake nikaanza kukisoma upesi, baada ya kukipokea, na huzuni ya Alhamisi inazunguka katika akili yangu na nilikuwa naogopa kulikuta tukio hilo. Kikanivutia kisa cha mwandishi, nikasoma hoja za uimamu wa Ahlul-Bait (a.s) na baadhi ya masahaba mashuhuri kumhalifu Mtume (s.a.w.w) na huzuni ya Alhamisi na mwandishi anathibitisha kila tukio katika vitabu vyetu sahihi vinavyozingatiwa, nilishangaa niliposoma na nikahisi mategemeo yangu yote yameporomoka, nikajaribu kuikinaisha nafsi yangu kwamba haya matukio hayapo katika vitabu vyetu.

Na katika siku ya pili niliazimia kuhakikisha hoja hizo katika maktaba ya chuo na nikaanza na huzuni ya Alhamisi nikaikuta imethibitishwa katika Sahihi Bukhariy na Muslim kwa njia mbalimbali.

Mbele yangu kulikuwa na hiyari mbili. Ama nimuafiki Omar juu ya kauli yake kwamba Mtume anaweweseka - Mwenyezi Mungu- apishe mbali na kwa hiyo nitaondoa tuhuma kwa Omar na ama nimtetee Mtume (s.a.w.w) na nikiri kwamba masahaba chini ya uongozi wa Omar walifanya kosa kubwa katika haki ya Mtume (s.a.w.w) hadi akawafukuza, na hapa nitaivua mbele ya rafiki yangu itikadi ambayo mara nyingi nimeikariri na kujifaharisha nayo mbele yake.

Katika siku hiyo rafiki yangu aliniuliza juu ya usahihi wa yaliyomo ndani ya kitabu, nikasema na moyo wangu unateketea kwa uchungu, "ndio ni sahihi."

Nikabaki muda mrefu nikiwa na bumbuwazi rafiki yangu akanionyesha kitabu "Liakunu ma'as-swadiqiyna" mtunzi wake ni Tijaani na kitabu chake kingine Fas'al ahla dhikri" na vinginevyo, vitabu hivyo vikafungua mbele yangu uhakika mwingi, bumbuwazi na shaka yangu ikazidi.

Nilijaribu kuzuia pumzi za bumbuwazi langu kwa kusoma majibu ya maulamaa wetu juu ya ukweli uliotajwa lakini havikunifaa bali vilinizidishi’a mwanga juu ya ukweli wa madhehebu ya Ahlul-Bait (a.s) hadi ilipokamilika picha ya ukweli katika akili yangu na nikaingia katika madhehebu ya Ahlul-Bait (a.s) kwa kukinaika na kwa utulivu wa moyo.

Na ndio hivi sasa na baada ya kuhitimu katika kituo cha sheria, nina yakini tosha juu ya usahihi wa ninayofuata, na nasema maneno haya na huku inanijia katika akili yangu, namna gani niliazimia juu ya kumuongoa rafiki yangu Mshi’a na watu wake, mambo yakawa kinyume - yeye ndiye akawa, kwa taufiq ya Mwenyezi Mungu, ni sababu ya kuongoka kwangu. Sisahau neema hiyo - rehema ya Mwenyezi Mungu ambayo ilikuwa inanifuata daima, shukrani ni zako ewe Mola wangu shukrani nyingi zinazolingana na utukufu Wako mkubwa na neema Yako kubwa.

  • 1. Rejea tukio hilo katika Sahihi Bukhary kitabu Al-maradhu watwib babu Qaulul- maridh Qumuu aniy, Sahihi Muslim kitabu ul-waswiyat babu tarkul-waasiyatu, Twabaqaatu Ibnu Saad Juz. 2. uk. 37