read

Neno la Mchapishaji

Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza, kwa jina la "Ikramataniy Al-Samai" kilichoandikwa na Mwanachuoni mkubwa, mwanahistoria na mtafiti Mar'wan Khaliyfat.

Kitabu hiki kama kile cha "Ukweli wa Ushi'a" ni utafiti na mjadala juu ya hitilafu baina ya Shi'a na Sunni. Mwandishi ametumia njia nyepesi sana ya kumuwezesha kila msomaji wa kiwango chochote kuweza kuelewa mada zote alizozijadili katika kitabu hiki.

Katika kufanya hivyo ametumia vyanzo sahihi na vinavyokubaliwa na Madhehebu zote, ambapo rejea nyingi amezinukuu kutoka vitabu sahihi vya Kisunni.

Nia na madhumuni ya mwandshi sio kuleta malumbano, bali kufahamiana na kuleta mkuruba baina ya madhehebu hizi. Ni ukweli ulio wazi kwamba maadui wa Uislamu huzitumia sana hitilafu zetu hizo ili kutugombanisha wenyewe kwa wenyewe. Ukweli ni kwamba hitilafu hizi sio za msingi za kuweza kutugombanisha, wala haziwezi kumtoa mtu katika Uislamu. Kinachoweza kumtoa mtu katika Uislamu ni kuacha moja ya Misingi mikuu ya Uislamu, nayo ni mitatu:

• Tawhid (Upweke wa Allah)

• Nubuwwat (Utume-Adam (a.s) akiwa wa mwanzo na Muhammad (s.a.w.w) akiwa wa mwisho).

• Qiyamah (Siku ya Hukumu)

Shi'a wanamkubali Mwislamu yeyote mwenye kuikubali misingi hii kama ndugu yao katika imani. Ama Adil na Imamat, hii ni misingi ya imani ambayo hukubaliwa na shi'a tu. Lakini kama mtu haikubali misingi hii miwili ya imani, haambiwi kwamba yeye sio Mwislamu. Misingi yote hii mwandishi ameijadili katika kitabu hiki.

Taasisi yetu ya Al-Itrah Foundation imekiona kitabu hiki ni chenye manufaa kwa Waislamu hususan wa zama hii tuliyonayo, hivyo kama ilivyo ada yetu tumeamua tukitoe kwa lugha ya Kiswahili, kwa lengo letu lile la kuwahudumia Waislamu wazungumzaji wa Kiswahili.

Tunamshukuru Ndugu yetu Abdul-Karim J. Nkusui kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vile vile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.

Ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitakuwa ni mwanga kwa wasomaji wetu na kuzidisha upeo wao wa elimu katika dini.