read

Sehemu ya Kwanza Pamoja na Ash’ariah

Kwa nini niwe Asha'riah?

Kwa nini ni wajibu nimfuate Ash'ariy na moja ya madhehebu manne? Je, kuna dalili? Je, kuna Aya? Kuna Hadith?

Tukirejea kwenye Qur'an na Sunna hatupati hata ishara ndogo juu ya jambo hili, anasema Jaadul -haqi Ali Jaadul-haqi- Sheikh wa Azhari: "Hailazimu kauli ya mwenye kusema kuwa kuna ulazima wa kumfuata mmoja wa maimamu, Abu Hanifa, Maaliki, Shaafiy na Ahmad bin Hanbali wakati hakuna dalili juu ya hilo."1

Maimamu Kukataza Kufuatwa Kwao

Kati ya matatizo yanayotupata hapa ni kukataza kwa maimamu wanne wao wenyewe kufuatwa na katazo hili limepokelewa kwa ishara na kwa wazi na hizi ni baadhi ya kauli zao:-

Kauli za Abu Hanifa

Si halali kwa yeyote kufuata kauli yetu maadamu hajui tumeichukua wapi.2

Shaukani amesema katika kueleza kauli hii "Na huku ni kukataa wazi kufuatwa, kwa sababu anayejua dalili basi ni mujitahidi anayetakiwa kutoa hoja, si mwenye kufuata, kwani yeye ni mwenye kufuatwa, ambaye anafuata na anakubali kauli hatakiwi kutoa hoja."3

Kauli yetu ni maoni nayo ni maoni bora tuliyoyafikia na atakaye kuja na maoni bora kuliko kauli yetu basi yatakuwa ni bora zaidi kuliko kauli hii yetu"4 na amepokea Ibnu Hazim kauli miongoni mwa kauli za Abu Hanifa juu ya kukataza kufuatwa.

3. Ilisemwa kwa Abu Hanifa, "Ewe Abu Hanifa haya unayotolea fatwa kwayo; ni ukweli ambao hauna shaka? Akasema: "Sijui, huenda ni batili ambayo hakuna shaka humo."

Zafar anasema: "Tulikuwa tunaenda kwa Abu Hanifa na yuko pamoja nasi Abu Yusuf na Muhammad bin Al-Hasan, tulikuwa tunaandika kutoka kwake, siku moja akamwambia Abu Yusufu ole wako! Usiandike kila kitu unachokisikia kutoka kwangu, kwani mimi naweza kuona rai leo, kisha nikaiacha kesho na naona rai kesho na naiacha keshokutwa. "5

Kauli za Malik Bin Anasi

"Hakika mimi ni binadamu nakosea na kupatia angalieni katika rai yangu, kila itakapoafikiana na kitabu (Qur'an) na Sunna basi ichukueni na yoyote isiyoafikiana na kitabu na sunna iacheni."6

Ibnu Hazim akielezea maneno ya Malik anasema: "Huyu ni Malik anakataza kufuatwa, vile vile Abu Hanifa na Shafiy".7

Na Shaukani amesema: "Haifichikani kwako kuwa hii ni kauli kutoka kwake yaani Maliki kwa kukataza kufuatwa kwake."8

Malik amesema: "Sisi tunadhani dhana tu na wala hatuna yakini."9

Al-Qaa'naby amesema: "niliingia kwa Malik katika maradhi yake aliyofia na kumsalimia, nikamuona analia, nikasema: "Ewe Abu Abdillah kitu gani kinakuliza?"

Akaniambia: "Ewe mtoto wa Qaa'nab, kwa nini nisilie! Na nani anahaki ya kulia zaidi kuliko mimi? Natamani nipigwe mijeledi, nilikuwa na nafasi katika niliyoyatanguliza, laiti nisingetoa fatwa kwa rai yangu."10

Imepokewa kuwa Malik alitoa fatwa katika talaka ya Al-battah (talaka ambayo haina kurejea) kuwa ni talaka tatu, akaangalia kwa Ashihabu naye ameshaiandika akasema: "Ifute, mimi kila ninaposema kauli mnaifanya (kama) Qur'an, unajuaje huenda mimi nitaiacha kesho na nitasema kuwa ni moja."11

Kauli za Shafi

1- "Ambayo nimeyasema Mtume alikwishasema kinyume na kauli yangu, basi ambayo yamesihi kutoka Hadith ya Mtume ni bora zaidi na wala msinifuate mimi."12

As-Sakabiy ametoa dalili kwa kauli hii ya Sharifiy juu ya kukataza kwake kufuatwa.

"Asifuatwe yeyote isipokuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu."13

Shafi amemwambia Maziniy: "Ewe Ibrahim usinifuate katika kila ninayosema, tazama hili kwa ajili ya nafasi yako, hakika hii ni dini.”14

"Hakika nimetunga vitabu hivi bila ya jitihada, hivyo ni lazima kupatikana humo makosa! kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema: Kama (Qur'an) ingekuwa inatoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu basi wangekuta humo makosa mengi,"15 mtakapopata katika vitabu vyangu hivi yanayopingana na kitabu na Sunna basi nimeshayaacha hayo."16

Kauli za Ahmad Bin Hanbal

Msinifuate wala msimfuate Maliki, Shafi, Auzaaiy wala Thauriy bali chukueni walipochukulia."17

Abu Daudi anasema: Nilimwambia Ahmad: NimfuateAwzaiy au Malik? Akasema: Usimfuate yeyote katika dini yako miongoni mwa hawa, Chukua yaliyokuja kutoka kwa Mtume."18

"Katika uchache wa fahamu ya mtu ni kufuata watu katika dini yake."19

Ilitajwa kwa Ahmad bin Hanbali kauli ya Malik na ikaachwa isiyokuwa hiyo, akasema: "Haitazamwi isipokuwa Hadith, watu wanapata fitina (mtihani) hivi wanafuata kauli ya mtu na wala hawaijali Hadith."20

Kauli za Maulamaa

Amesema Sahanun - naye ni mashuhuri kati ya wanafunzi wa Malik "sijui ni rai gani hii ambayo kwayo imemwagwa damu na kwayo tupu zimehalalishwa, na kwayo zimestahiki haki."21

Amesema Ibnu Abdibarri Hafidhul-Magharib: "Hakika hakuna tofauti baina ya watu wa Miji katika uharibifu wa kufuata"22 na baada ya kunukuu aya za Qur'an katika kulaumu kufuata akasema: "Na hii yote ni katika kukataza kufuata na ni utanguzi kwa ambaye ameifahamu na akaongozwa kwa uongofu wake."23

Amesema kadhi Al-Baqalaaniy: "Atakayefuata basi asimfuate isipokuwa aliye hai na wala haijuzu kumfuata aliyekufa."24

Suyutwiy amesema: "Waliotangulia na waliokuja baadaye hawakuacha kuamrisha Ijitihadi na kusisitiza juu yake na wanakataza taqlidi (kufuata), wanailaumu na wanaichukia, na ameshatunga katika kushutumu taqlidi Al-Maziny, Ibnu Hazim, Ibnu Abdibarr, Abu Shaamah, Ibnu Qayyim Al-jauziy na mwenye Al-baharul-muhiytu.25

Ibnu Daqiyq Al-Iyd ambaye anahesabiwa kuwa ni mujadidu wa karne ya saba Hijiriya, anaona uharamu wa taqlidi na hakuweza kusema wazi isipokuwa wakati wa kufa kwake. Amepokea Al-Adufiy kutoka kwa Sheikh wake Imam Ibnu Daqiril-Iyd kwamba alimuomba karatasi na akaandika katika maradhi yake aliyokufa na akaiweka chini ya godoro lake alipokufa wakalitoa wakakuta kuna kuharamisha taqlidi kabisa.26

Amesema Sheikh-Akbar Ibnu Al-Arabiy: "Taqlidi katika dini ya Mwenyezi Mungu haijuzu kwetu, sio taqlidi ya aliye hai wala maiti."27

Shaukani anasema: Matamshi ya maimamu wanne katika kukataza taqlidi na kutangaza rai zao na rai za wengine juu ya Nassi (Qur'an na Sunnah) haifichikani kwa anayejua miongoni mwa wafuasi wao na wengineo, kadhalika maulamaa wanne wameongoa, wasiokuwa wao kuacha taqlidi yao na wakakataza juu ya hilo. "Hakika imesihi kutoka kwao yaani maimamu wanne - kukataza taqlidi."28

Al-Jauziy anasema: "Jua kwamba anayeqalidi hana uhakika katika aliyoyafanyia taqlidi na katika kuqalidi kunabatilisha manufaa ya akili kwa sababu imeumbwa ili itafiti na kufikiri."29

Amesema Asaydu Saabiq "maimamu wanne walikuwa wanakataza kufuatwa na wamesema: Haijuzu kwa yeyote kusema kauli yetu bila ya kujua dalili yetu, na wanasema wazi kuwa madhehebu yao ni Hadith sahihi …30

Saalim Al-Bahanasaawiy anasema: "Asili katika Uislamu ni Mwislam kuchukua hukumu ya kisheria katika kitabu na Sunna, kwa sababu hakuna uma’asum kwa yeyote hadi kauli zake na vitendo vyake viwe ni sheria kutoka kwa Mwenyezi Mungu, visivyo na makosa. Na kauli za Abu Hanifa, Malik, Shafi na wengineo, sio lazima kwa dhati yake bali ni kwa kuwa kauli za hao maimamu wanne zimetegemea kitabu na Sunna."31

 • 1. Durusul-husainiyah uk. 139
 • 2. "Al-intiqau" Ibnu Abdil barr uk. 145, Majumuatu rasailil- munirah Aswanaaniy J.1 uk 28, Hujatullahil -baaligha cha Shaha Dahalawiy J. uk 158
 • 3. Qaulul-mufiyd ya Shaukani uk. 49
 • 4. Tarekhu Baghidad "ya Al-baghidadiy J: 3 uk 42, Hujatullahi al-baligh J:1 uk:157. Mulakhis Abu
  Twalib-qiyaas wa raalji wal-Istihisan wataqilid “cha Ibnu Hazim uk: 66
 • 5. Tarekhu Baghidad "ya Al-baghidadiy J: 3 uk 42, Abu Hanifa cha Abu Zahra
 • 6. Jaamiu bayanil- ilmi wa fadhililhi "Ibnu Abdi Barr, kimehakikiwa na Abul- Ashibaal Azahiyr J: 2, uk 775 "Maana
  Qaulul-imam il-matwalabiy idha swahal- hadithu fahuwa madhihabiy "Cha Taqiyu Diyni As-sabakiy" mhakiki:
  Ali Nayf Buqai' uk. 125
 • 7. Al-ihkaam fiy usuulil Ah-kaam J: 6 uk 294
 • 8. Al-qaulul- mufiyd uk: 50
 • 9. Jamiu bayanil -ilimi wa fadhilihi J:2 uk: 33
 • 10. Amepokea Ibnu Abdibarr - rejea Qawlul- mufiyd uk: 79, Wafayatul- Aayan: cha Ibnu
  Khalkaan J. 3 uk. 246
 • 11. Al-ihkaam fiy usulil-akhaam J: 6 uk 314
 • 12. Adabu Shaafiy wamanaqibuhu Cha Ibnu Abiy Hatim Araaziy uk 93, Maana
  Qaulul-imamu - Matwalabiy cha Assabakiy uk 71
 • 13. Radu alaa man akhilada ilaal ardh waankara Al- ijitihadi fiy kuli asri faradhun cha Suyutwiy: 138
 • 14. Hujatullaahil balighah J :1 uk: 157
 • 15. Suratu Nisaa: 82
 • 16. Mukhutasarul-muamal cha Abu Shaamah Shafii uk: 60
 • 17. Rejea iliyopita uk: 61, Majumuatu rasailil-munira J: 1 uk: 27
 • 18. Majumuatu rasailil-munira, Juz. I''ilaamul-mauqi'iyn "cha Ibnu Qayim J: 2 uk 201
 • 19. Majumuatu rasail-munira Juz 1 uk 27 Ibnu Qayim J: 2 uk 201
 • 20. Radu alaa man akhilada ilal ardh uk: 134
 • 21. Alqawlul mufiyd uk. 79 lilamul mawqiin Juz. 1 uk 79
 • 22. Rejea iliyopita uk. 48
 • 23. Raddu alla man akhlada ilal ardhi, Alqawlul- mufiyd uk. 48
 • 24. Ibn Hazm ameinasibisha katika Al-hkami Juz. 6 uk. 97
 • 25. Raddun ala man akhlada uk. 42
 • 26. Al-qawlul mufid uk. 57
 • 27. Al-futuhaatul-makiyah, Al-babu thamin wathamanuna (mlango 88)
 • 28. Al-qawlul-mufiyd uk 42, 48 na 66
 • 29. Talbiysul-Ibliysi uk 124 - 125, Al - qawlul-mufiyd uk. 66
 • 30. Fiqihi Sunnah 1: uk. 13 - 14
 • 31. Assunnatul- mufutara alaiha uk. 194