read

Sehemu ya Pili Pamoja na Shi'atul-Imamiya

Je, kuna dalili?

Swali hili hili ambalo tulilielekeza katika kundi la Sunni tunalielekeza katika kundi la wafuasi wa Ahlul-Bait (a.s); Je, kuna dalili juu ya kufuata Ahlul-Bait (a.s); Je, kuna aya? Kuna dalili nyingi katika vitabu vya Sunni na zote zinatilia mkazo juu ya wajibu wa kuwafuata Ahlul-Bait (a.s) na katika kurasa zifuatazo tutataja zilizo muhimu zaidi.

Dalili Kutoka Katika Sunna Hadith ya Thaqalayn

Kutoka kwa Zaid bin Thabit amesema: "Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu: "Hakika mimi nimekuachieni makhalifa wawili baada yangu, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu, watu wa nyumba yangu na hakika havitatengana hadi vitakaponijia katika birika."1

Na katika Sahihi Tirmidhi na Mustadrak-as-Sahihain amesema ni sahihi: "Hakika mimi nimewaachieni ambayo kama mtashikamana nayo hamtapotea baada yangu kimojawapo ni kitukufu kuliko kingine; Kitabu cha Mwenyezi Mungu kamba yenye silsila kutoka mbinguni hadi ardhini na kizazi changu, watu wa nyumba yangu, na wala havitatengana hadi vitakaponijia kwenye birika, angalieni mtanifuatiaje kwavyo?"2
Na imepokewa kutoka Sahihi Muslimu kutoka kwa Zaid bin Arqam amesema : "Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu siku moja alipotuhutubia katika dimbwi la maji linaloitwa Khum baina ya Makkah na Madina, alimshukuru Mwenyezi Mungu, akamtukuza, akatoa waadhi, na akakumbusha kisha akasema:
"Amma baada: Enyi watu hakika mimi ni binadamu nahofia anaweza kunijia mjumbe wa Mwenyezi Mungu na nikamwitikia na mimi nimewaachieni vizito viwili, cha kwanza ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu, humo kuna uongofu na nuru basi chukueni, katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na shikamaneni nacho;" akahimiza juu ya Kitabu na akasistiza humo kisha akasema: "Na watu wa nyumba yangu nakukumbusheni Mwenyezi Mungu katika watu wa nyumba yangu."3

Usahihi wa Hadith ya Thaqalayn

Hadith hii ni mutawatiri katika vitabu vya Sunni kabla ya vitabu vya Shi’a na wameipokea Hadith hii masahaba 35 na Tabiina19,4 na maulamaa wengi wamesema kuwa ni sahihi. Kati ya hao ni:
At-Tabari
Al-Hakim katika Mustadrak

Al-Haithami katika majmau zawaid, Adhahabi katika Talkhisul-Mustadrak, Ibn Kathri katika tafsiri yake; As-Suyutwi katika Al-Jaamius-Swaghiry Al-Munawiy Muhammad Is'haq.5

Na Ibn Hajar ameshasema: "Kisha jua kwamba Hadith ya kushikamana na hayo imepokewa katika njia nyingi na imepokewa na maswahaba zaidi ya ishirini;" na akaitoa katika njia kumi na moja zinazofanana, na katika baadhi ya njia hizo amesema: "Hiyo ilikuwa katika Hijjatul-Wida'a huko Arafa; na katika njia nyingine ni kwamba ameisema Madina wakati wa maradhi yake hali chumba chake kimejaa maswahaba wake, katika njia nyingine ni kwamba alisema hayo katika bonde la Khum, na katika njia nyingine alisema alipotoka Twaifu kama ilivyotangulia na hakuna mgongano ambapo hakuna kizuizi pamoja na kuwa alikariri hayo kwao katika sehemu hizo na nyinginezo kwa umuhimu wa kushikamana na Kitabu Kitukufu na Ahlul-Bait wake watukufu.6

Na katika Muhadithyna wa wakati huu Sheikh Al-Albany amesema kuwa ni sahihi.7

Na muhadith wa Kishafii, Hasan bin Ali Assaqaf amethibitisha usahihi wa Hadith Athaqalayn na akasema: "Hadith ya Kitabu llahi wasunnatiy, ni ya uongo na haya ni maneno yake: Niliulizwa juu ya Hadith nimewaachieni vitu viwili hamtapotea baada yake; Kitabu cha Mwenyezi Mungu na …Je, Hadith sahihi ni kwa tamko la kizazi changu na watu wa nyumba yangu?

Au ni kwa tamko la Muslim la Wasunnatiy? Tunataraji ufafanuzi wa hilo katika upande wa Hadith na sanadi yake.

Jawabu: Hadith iliyithibiti ni kwa tamko la Ahlu-Bait na Riwaya ambazo kuna tamko la Sunnatiy ni batili kwa upande wa Sanad na Matini. Saqaaf baada ya kuipokea Hadith ya Thaqalayn kutoka katika Sahihi Muslimu akasema: Hili ni tamko la Muslimu pia ameipokea kwa tamko hili Adarimiy katika Sunan yake J:2 uk 431-432 kwa sanad sahihi kama vile uwazi wa jua na wengineo…

Ama tamko la Wasunnatiy sina shaka kuwa ni la uongo kwa udhaifu wa sanad yake na uzushi wake, na kutokana na mazingira ya Bani Ummaya yakawa yameathiri katika hilo.

Na hii hapa ni Sanad na Matini yake:

Ameipokea Al-Haakim katika Mustadrak J: 1 uk 93 Hadith na Sanad yake kutoka katika njia ya Ibn Abiy Ausi kutoka kwa baba yake kutoka kwa Thaurit bin Zaid Adailiy kutoka kwa Ukrima kutoka kwa Ibn Abbas na humo kuna: "Enyi watu? Hakika mimi nimekwisha acha kwenu ambayo kama mtashikamana nayo hamtapotea kamwe, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake ….."

Nasema katika Sanad yake kwa Abiy Uweys na baba yake, Al- Haafidh Al-Maziniy katika Tahadhiybul-Kamaal J: 3 uk 127, katika kumueleza Ibnu Abiy Uweys na nanukuu kauli ya aliyemkosoa:-

"Amesema Muawiya bin Swalehe kutoka kwa Yahya bin Muiyin: Abu Ausi na mtoto wake ni madhaifu, na kutoka kwa Yahya Ibn Muuyn vile vile; Ibn Abi Uweys na babake wanaiba hadithi, na kutoka kwa Yahya amesema: "Amechanganya, anasema uongo si chochote."

Amesema Abu Hatimu: "Mahala pake ni kweli, alikuwa msahaulifu" na Anasaaiy amesema: "Ni dhaifu," na akasema katika sehemu nyingine: "Sio mkweli."

Amesena Abu Qasimul Laalkaaiy: "An-Nasaaiy amezungumzia sana juu yake hadi inapelekea kuachwa kwake."

Abu Ahmad bin Adiy amesema: "Na Ibni Abiy Uweys, huyu amepokea kutoka kwa mjomba wake, Malik, Hadith ngeni, hamfuati yeyote juu ya hilo."

Ninasema: "Amesema Al-Hafidh bin Hajary katika utangulizi wa Fatuhul-Barr, uk. 391 chapa ya Darul Maarifa, juu ya huyu Ibni Abi Uweys, kwa ajili hii haitolewi hoja yeyote katika Hadith zake, kwa yasiyokuwa katika sahihi kutokana na alivyomponda Annasaaiy na wengineo.

Amesema Al-Hafidh Ahmad bin Swadiq katika Fathul-Alaiy uk 15 na amesema Salmma bin Shabib: Nimemsikia Ismail bin Abiy Uweys amesema: "Huenda nilikuwa nazua kwa watu wa Madina wanapohitalifiana baina yao."

Mtu ametuhumiwa kwa uzushi, na Ibn Muiyn amemtuhumu kwa uongo, na Hadith yake ambamo humo kuna tamko la "wasunnatiy" siyo moja katika Hadith za Sahihi (Bukhari na Muslim).

Amesema baba yake Abu Hatimu Arraaziy kama ilivyo katika kitabu cha mtoto wake cha Jarhu wataadilyli J:5 uk: 12 "Hadith yake inaandikwa na wala haitolewi hoja kwayo na haina nguvu na amenukuu katika kitabu hicho hicho, Ibnu Habiy Hatim kutoka kwa Ibnu Muin kwamba amesema juu yake kwamba "sio mkweli" ninasema: "Katika sanadi kuna mfano wa hayo tuliyotangulia kuyazungumzia juu yao, haisihi hadi ngamia aingie kwenye tundu ya sindano na hasa ambapo aliyokuja nayo yanapinga yaliyothibiti katika sahihi, fikiria vizuri Mwenyezi Mungu akuongoze."

Al-Hakimu amekiri juu ya udhaifu wa Hadith, na hivyo hakuisahihisha katika "Mustadrak" isipokuwa kaitolea ushahidi kwamba ni ya uongo na sanadi yake ni yenye kuanguka, hivyo Hadith ikazidi udhaifu juu ya udhaifu wake. Na tunahakiki kwamba Ibnu Abiy Uweys au baba yake, ameiba mmoja wao Hadith hiyo ya uongo ambayo tutaitaja, na akaipokea mwenyewe, na Ibnu Muin amesema mtoto ametokana na baba na kwamba wao walikuwa wanaiba Hadith.

Amepokea Al-Hakim katika J:1 uk. 93 Hadith hiyo na "nimeshapata ushahidi wake toka katika Hadith ya Abu Huraira" kisha akapokea kwa Sanadi yake katika njia ya Adhabiy, ametusimulia Swaleh bin Mussa Al-Twalhi kutoka kwa Abdul-Aziz bin Rafiy kutoka kwa Abi Salih kutoka kwa Abu Huraira, imerufaishwa; "Hakika mimi nimeacha kwenu vitu viwili hamtapotea baada yake Kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna zangu na havitatengana hadi mtakaponifikia katika birika."

Nimesema huu ni uzushi vile vile, nafupisha maneno hapa kwa mtu mmoja katika sanadi; naye ni Swaleh bin Mussa Al-Twalahiy, na haya hapa ni maneno ya maimamu wa Hadith miongoni mwa wakubwa wa wanao hifadhi, ambao wamemtuhumu humo katika Tahadhiybul-Kamaal J:13 uk. 96; Yahya bin Muiyn amesema: sio chochote, amesema Abu Hatim Araaziy, Hadith zake ni dhaifu, amepingwa sana na wa kweli, Anasaaiy amesema; Hadith yake haiandikwi, na akasema katika sehemu nyingine; Hadith yake ni yenye kuachwa.

Na katika Tahadhiybul -Tahadhiyb J: 4 uk 355 cha Hafidh Ibnu Hajar amesema Ibnu Hiban, "alikuwa amepokea kutoka kwa wakweli ambayo hayafanani na Hadith iliyothibiti hadi anashuhudia msikilizaji kwayo kwamba imetungwa, haijuzu kutolea hoja kwayo, na amesema Abu Nuini, Hadith zake ni zenye kuachwa, anapokea Hadith zinazopingana.

Nimeshasema: “Ameshahukumu juu yake Al-Haafidh katika Taqiriyb" tarjama No. 2891 kwamba yeye ni mwenye kuachwa" na Dhahabiy katika Al-Kaashif (2412) kwamba "yeye ni mzushi, na amepokea Dhahabiy katika "Al-Mizan" J:2 ,uk. 302" Hadith yake hii katika tarjama yake kwamba ni miongoni mwa uongo wake.

Na Malik alishataja Hadith hii katika "Muwatwa "(899 no. 3) bila ya sanad wala hakuna thamani ya hilo baada ya kubainisha uongo wa sanadi yake.

Ametaja Al-Haafidh bin Abdul-Barri katika Atamhiyd J: 24 uk 331 sanadi ya tatu ya Hadith ya uongo yenye kuzuliwa akasema: Ametusimulia Abdulrahmani bin Yahya amesema ametusimulia Ahmad bin Saidi, amesema ametusimulia Muhammad bin Ibrahim Ad-Daibily amesema, ametusimulia Ali bin Zaidi Al-Faradhiy amesema ametusimulia Al-Hunaini kutoka kwa Kathiri bin Abdillah bin Amru bin Aufu kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake; nasema: "Tunafupisha kwa ubovu mmoja ulio humo nao ni Kathyri bin Abdilah, huyu ni ambaye katika Sanadi yake amesema Imamu Shaafiy: "Ni mmoja wa nguzo za uongo," na Abu Daudi amesema juu yake "Alikuwa ni mmoja wa waongo."8

Amesema Ibnu Hiban: Amepokea kutoka kwa baba yake nakala ya uzushi haifai kuitaja katika vitabu wala kupokea kwake isipokuwa katika upande wa mshangao."9

Amesema Annasaaiy na Daru Qutuniy: "Hadith zake ni zenye kuachwa: "Amesema Imam Ahmad Hadith zake zinakataliwa, sio chochote," na amesema Yahya bin Muiin: "Sio chochote."

Na sema: "Alikosea Al-Hafidh bin Hajar (Mungu amrehemu) katika: Taqiriyb" alipofupisha kauli yake kwake; kwa kusema: "Ni dhaifu" kisha akasema "Amechupa mipaka aliyemtuhumu kwa uongo" Nasema: "Hapana hakuchupa mipaka bali hiyo ndio hali halisi kama unavyoona katika maneno ya maimamu juu yake.

Na hasa aliposema Adhahabi juu yake katika "Al-Kashif: "ni muongo," naye yuko hivyo na Hadith zake ni za uzushi haifai kuzifuata wala kuzitolea ushahidi bali zinatupwa, na taufiqi ni ya Mwenyezi Mungu.

Imebainika wazi kwamba Hadith (Kitabullahi wa Itratiy) Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu ndio sahihi, imethibiti katika Sahihi Muslim, na kwamba tamko la (kitabullah wassunnatiy) ni batili, sio sahihi kwa upande wa sanad. Hivyo ni juu ya makhatibu, watoa waadhi na maimamu wa misikiti kuacha tamko ambalo halikupokelewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na wawatajie watu tamko sahihi lililothibiti kutoka kwake (s.a.w.w) katika Sahihi Muslim (Kitabullah wa Ahlul-Bait) au (Itratiy)."10

Pamoja na hayo kama tutaijaalia kwa mfano - kusihi Hadith ya (kitabullah wassunnaty) basi hakuna mgongano baina yake na Hadith ya Thaqalayni, na inabaki kushikamana na Ahul-Baiti (a.s) ni sababu ya msingi ya kufaulu, na aliisha unganisha Ibnu Hajar baina ya Hadith mbili akasema; "na katika riwaya; Kitabullah wassunnaty; ndio makusudio ya Hadith zilizofupishwa kwa kutaja Kitabu.

Kwa sababu Sunna zimebainisha, ikawa kutaja kitabu imetosheleza kutaja Sunna na majina ni kwamba mkazo umekuja katika kushikamana na kitabu, Sunna na maulamaa miongoni mwa Ahlul-Bait (a.s) na tumepata faida kwa mkusanyiko huo kwa kubaki mambo matatu hadi siku ya Qiyama.11
Na kama itasihi Hadith "Wassunnatiy"basi itakuwa imehukumiwa kushikamana na Ahlul-Bait (a.s) kwa sababu Hadith ya thaqalayn ni katika Sunna za Mtume (s.a.w.w)."12

 • 1. Sunan Ibn Majah cha Abu Asim amekitoa Al-al-baniy na amesema ni sahihi uk:337 hadithi No: 754, musnad Ahmad J:5 uk:182
 • 2. Sahihi Tirmidhiy kitabu Manaqib J: 633, uk 3788, Mustadrak j:3 uk 148
 • 3. Kitabu Fadhailus-sahaba babu min fadhail Ali bin Abi Twalib
 • 4. Rejea upokezi wao katika Abaqatul-anuwar na J: 1 na J: 2
 • 5. Rejea Hadith Thalaqayn Tawaturuhu -fiqihihu cha Ali al-Hussainiy Al-Milaainiy
 • 6. As-Swawaiqul-Muhuriwah J: 2 uk 440
 • 7. Silsilatul-Ahaadithis - sahihi J: 2 uk 355 - 358
 • 8. Amenukuu Saqafu, kauli ya Imamu Shafi na Abu Daudi kutoka: Tahadhibul-tahadhiyb J:8 uk 377 chapa ya Darun-Fkri na Tahadhiybul- Kamaal J: 24 uk 138
 • 9. Tazama Al-Majruhiina J; 2 uk 221 cha Hafidh bin Hiban
 • 10. Swahihi swifatus-swalati Nabiyi uk 289 - 294 na toleo la Saqaf limejibu kila aliyejaribu kuisahihisha Hadith mfano: Dkt. Ali Saalusi na wengineo
 • 11. Asawaiqul-Muhuriqat J: 2 uk 439
 • 12. Hakika vitabu vya kisuni ambavyo vimetaja Hadith ya thaqalayn vinakaribia mia mbili kati ya hivyo ni:- Musnad bin Hanbali J: 5 uk 182. Twabaqaat Ibnu Saad J: 2 uk 192, Al- Muujamu swaaghiru cha Twabarany uk 73, Asunanul-Kubura ya Al-Baihaqiy J:10 uk :113 KanzulUmal J: 1uk:322 na ameisahihisha Al-Albaniy katika sehemu nyingi kati ya hizo ni Silsilat hadith Sahihi J:4 uk:355 Sunan Tirimidhiy na Jamius-Swaghir