read

Turbah ya Husein

Ma-Shi’a wanatumia turbah (kipande cha udongo) iliyotengenezwa kwa udongo kusujudia juu yake, na baadhi ya waandishi wamepata fursa ya kushambulia Shi’a, na katika kufafanua jambo hilo tunasema: "Hakika kanuni katika madhehebu ya Ahlul-Bait ni kwamba haijuzu kusujudu isipokuwa kwenye ardhi au kilicho ota ardhini ukiondoa vinavyoliwa na kuvaliwa.

Na baada ya kufa shahidi Imamu Husein imekuwa ni ada kwa Shi’a na kwa maelekezo kutoka kwa maimamu wao kusujudu juu ya Turbah ya Karbala, wao wanasujudu juu ya Turbah na sio kuisujudia, kama wanavyodai wapinzani, kama vile Sunni wanaposujudu juu ya Sujada, wanasujudu juu yake na wala hawaisujudii …

Na masahaba walikuwa wanasujudu juu ya changarawe na Mtume (s.a.w.w) hakuwakataza.

Anasaai amepokea kutoka kwa Jabiri bin Abdillah amesema "Tulikuwa tunasali pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu Adhuhuri basi nilikuwa nachukua changarawe kwa kiganja changu nazipooza kisha ninazihamishia kwenye kiganja kingine, ninaposujudu naziweka mahali ninapoweka paji la uso wangu."1

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alikuwa anasujudu juu ya mchanga, vile vile juu ya udongo kama ilivyo katika Sahihi Bukhariy."2

Na amesema Mtume (s.a.w.w): "Nimefanyiwa ardhi kuwa ni mahali pa kusujudia na ni tohara."3 Hivyo inajuzu kusujudu juu ya udongo kwa sababu ni sehemu ya ardhi na hakuna tofauti baina ya mtu kusujudu juu ya udongo au kutengeneza Turbah ya kusujudia juu yake kutoka kwayo, huu ni udongo na ule ni udongo na wala haizingatiwi tofauti ya umbo.

Mas'ala ya kusujudu juu ya udongo yanabaki kuwa ni mas'ala ya kifiqihi ambayo Shi’a wametofautiana na madhehebu mengine, kama ambavyo kila moja katika madhehebu manne lina mas'ala mahsusi linalofautiana na mengine, na Shi’a katika mas'ala haya na mengineyo wamefuata yaliyo sahihi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w).

  • 1. Sunanu nasaaiy J: 2 babu Tabriydil - haswaa
  • 2. Sahihi Bukhariy J: 2 kitabul itiqaaf katika kumi la mwisho
  • 3. Sahihil Bukhariy kitabu tayamam