read

Utaratibu Wa Ahlul-Bait (a.s)

Utaratibu wa Ahlul-Bait (a.s) umesimama juu ya kushikamana na Kitabu na Sunna na kuepukana kutoka na kufuata qiyasi na rai ……. Imamu Ali (a.s) alishaandika Sunna Wakati wa Mtume (s.a.w.w) na kitabu chake kimejulikana kwa jina "Aswahifah" na Maimamu wa Ahlul-Bait wanaachiana kitabu hicho na wamekitegemea kwa mapokezi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w). Na hizi ni baadhi ya kauli za maimamu ili tujue mshikamano wa manhaji yao iliyo madhubuti.

Aliulizwa Imamu Swadiq (a.s) kwa kitu gani Imamu anatoa fatwa? Akasema; kwa kitabu, muulizaji akasema kama hakipo katika kitabu. Imamu akasema, kwa sunna. Muulizaji akasema kama halipo katika sunna? Imamu akasema: hakuna kitu isipokuwa kinapatikana ndani ya kitabu (Qur'an) na sunna. Amesema Imamu Ja'far As-swadiq (a.s), "Hadith yangu ni Hadith ya baba yangu, na Hadith ya baba yangu ni Hadith ya babu yangu na Hadith ya babu yangu ni Hadith ya baba yake, na Hadith ya Ali bin Abi Talib ni Hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na Hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.1

"Fuata watu ambao wanasema katika kauli yao na Hadith yao, amepokea babu yetu kutoka kwa Jibrili kutoka kwa Mwenyezi Mungu."

Amesema Imam Baqir (a.s): "kama tungewaeleza kwa maoni yetu na matamanio yetu basi tungekuwa ni katika wenye kuangamia, lakini tunawaeleza Hadith ambazo tumezihifadhi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kama wanavyohifadhi hawa dhahabu na fedha zao." Mtu mmoja alimlaumu Iban Taghlab juu ya mapenzi yake kwa Imamu Baqir, na kupokea kutoka kwake akasema, "vipi unanilaumu kwa kupokea kwangu kwa mtu ambaye sikumuuliza juu ya kitu isipokuwa husema: "Amesema, Mtume wa Mwenyezi Mungu..."

  • 1. Maalimu-shariati cha sub-hi Swalehe uk:52