Kitabu kilichoko mikononi mwako ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza kiitwacho, Peshawar Nights. Asili ya kitabu hiki ni cha lugha ya Kifarsi kwa jina la, Shab’ha-ye Peshawar. Sisi tumekiita, Mikesha ya Peshawar.

Mikesha ya Peshawar ni nakala ya mjadala kati ya wanavyuoni mbalimbali wa Kisunni na mwanachuoni mmoja wa Kishia mzaliwa wa Shiraz (Iran) aitwaye Sayyid Abdu ‘l-Fani Muhammad al-Musawi Sultanu ‘l-Wa’idhiin, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 31 tu. Mjadala huu ulifanyika katika mji wa Peshawar ambao wakati huo ilikuwa ni sehemu ya Bara Hindi na hivi sasa ni sehemu ya Pakistan. Ulifanyika kuanzia tarehe 27 Januari 1927 na kuundelea kwa mikesha kumi ndani ya msikiti ambako watu zaidi 200 walihudhuria kila usiku. Mjadala huu ulifanywa kwa muundo mzuri wa kuheshimiana pande zote bila ya kuvunjiana heshima. Mwandishi mwenyewe amejiita katika kitabu hiki kama “Da’i” yaani mtu anayewaombea mema watu wengine, sisi tumelitafsiri neno hilo kama “Muombezi”.