read

Jumapili, Sha’ban 4, 1345 A.H Wilada Ya Imam Husein.

Tafrija kubwa kabisa ilifanyika kuadhimisha wilada ya Imam Husain. Mwandishi huyu, Seyyed Muhammad Sultanu’l-Wa’idhin Shirazi, aliihutubia hadhara hiyo. Ilikuwa ndio khotuba yake ya mwisho, na kama alivyoahidi usiku uliopita, alijibu lile swali kuhusu Uimam, idadi na majina ya Maimam katika Qur’ran tukufu na hadithi. Aliianza hotuba yake kwa aya ifuatayo:

“Enyi mliamini! Mtiini Allah, na mtiini Mtume na wale wenye mamlaka miongoni mwenu. Kisha mtakapohitilafiana katika jambo lolote, lirud- isheni kwa Allah na Mtume, kama mnamuamini Allah na Siku ya Mwisho. Hii ni bora sana na ni kheri nzuri mwishoni. (4:59)

Uhuru Halisi

Fikra ya uhuru, kwamba watu wawe huru, limekuwa kwa muda mrefu ni wazo la kawaida. Fikra ya juu juu kuhusu uhuru ni kwamba ina maana ya mtu kufanya kama anavyotaka, fikra ambayo imeishia kwenye kupuuza sheira tukufu. Lakini kwa kweli uhuru halisi ni unyenyekevu, utii kwa Allah, Muumba wa vitu vyote.

Qur’ani Tukufu mara nyingi inawamrisha waumini kumtii Allah na wale wanaofaa kufuatwa kutoka miongoni mwetu wenyewe. Ile aya tukufu ambayo nimeisoma kama dhamira ya mazungumzo yangu ni moja ya aya kama hizo ambayo inaashiria ni nani tunapaswa kumtii.

Inatuamrisha kumtii Allah, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na wale waliopewa mamla- ka. Hakuna tofauti ya maoni miongini mwa Waislam kuhusu utii unaomstahili Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Hata hivyo kuna tofauti ya maoni juu ya maana ya maneno. “Wale waliopewa Mamlaka miongoni mwenu.”

Imani Ya Sunni Kuhusu Maana Ya “Wale Waliopewa Mamlaka”

Ndugu zetu Sunni, wanaamini kwamba katika aya hiyo hapo juu, yale maneno “wale waliopewa mamlaka (ulu’l-amr) yanawahusu viongozi wa nchi. Kwa hiyo, wao wanachukulia utii kwa wafalme na magavana ni wajibu hata kama viongizi hawa wangekuwa waovu.

Kwa hakika imani hii ni ya makosa. Uhaba wa muda hauniruhusu kutoa mazungumzo marefu kuunga mkono maoni yangu, hivyo nitawasumbueni tu na maelezo mafupi.

Njia Tatu Za Uteuzi Wa ‘Ul’l-Amr’ (Wale Waliopewa Mamlaka)

Kwa hakika watawala wanapata mamlaka yao katika mojawapo ya njia hizi:

1. Wanachaguliwa kwa Ijma (makubaliano ya wengi)
2. Wanapata Mamlaka kwa nguvu.
3. Wanawekwa ki-Mungu - (kuteuliwa na Allah)

Ikiwa kiongozi anapata mamlaka kwa makubaliano ya Umma, sio wajibu kumtii yeye kama mtu anavyomtii Allah au Mtume. Haiwezekani kwa Waislam wote kumteua kiongozi mwadilifu kwa sababu hata wawe waerevu kiasi gani au waangalifu kiasi watakavyokuwa, wataweza tu kumuamulia mtu kutokana na muonekana wake wa nje. Hawawezi kuusoma moyo wake au kujua kiwango cha imani yake.

Viongozi Wa Bani-Israel Walioteuliwa Na Musa Walionekana Hawafai

Ni dhahiri kwamba Waislam hawawezi kudai kuwa na uelewa bora zaidi ya Nabii Musa. Yeye alichagua watu sabini kutoka kwenye maelfu kadha kwa uaminifu wao wakuonekana dhahiri na akawachukua kwenda pamoja naye mpaka mlima Sinai. Lakini wote katika kuchunguzwa, wakathibitika kwamba ni bure tu kwa sababu imani zao hazikuwa thabiti.

Ukweli huu umetajwa katika Qur’ani Tukufu, aya 154 ya sura ya 7. Ikiwa wale walioch- aguliwa na Musa walithibitika kuwa sio waumini mioyoni, ni dhahiri kwamba mtu wa kawaida atakuwa na uwezo wa chini zaidi wa kuchagua watawala wao wenye uwezo. Inawezekana kabisa kwamba wale waliochaguliwa kwa ucha-mungu wao wa dhahiri, haltimaye wanaweza kutokea kuwa sio waumini. Hakika utii kwa watawala kama hao utad- hoofisha dini.

Maneno ‘Uli’l-Amr’ Hayaashirii Kwa Watawala

Kwa hakika Allah asingewataka waja wake kumtii mtenda dhambi kama ambavyo wangemtii Yeye au Mtume Wake. Zaidi ya hayo, kama uteuzi wa ‘Ul’l-Amr’ ungefanywa kupitia makubaliano ya kweli, upiga kura ungebidi ufanyike kwa kila uteuzi mpya.

Raia wote wa mataifa yote ya Kiislam wangepaswa kukubaliana juu ya mteuliwa katika kila uchaguzi. Katika miaka 1300 ya Uislam tunaona kwamba, baada ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), hakuna makubaliano kama hayo yaliyowahi kutokea, sasa hivi ni vigumu kupata makubaliano kama hayo kwa sababu ulimwengu wa kiislam umegawanyika katika idadi ya nchi, kila nchi ikiwa na mtawala wake.

Zaidi ya hayo, kama kila nchi itachagua ‘Uli’l- Amri wake, pangekuwa na idadi kubwa ya ‘Uli’-l- amr’ wake, pangekuwa na idadi kubwa ya ‘Ul-l amr’ kila mmoja akitiiwa ndani ya nchi yake, na watu wa nchi moja wasingeweza kumtii ‘Uli’l-amr’ wa nchi nyingine.

Bila shaka basi kuna suala la kiapo cha utii wakati kunapotokea tofauti - kama zilivyotokea mara kwa mara katika miaka 1300 iliyopita - baina ya ‘Mamlaka’ mbili. Halafu tunao Waislam wanaowaua Waislam wengine kwa jina la Uislam.

Lakini Uislam wa kweli hauhitaji tabia ya kichekesho kama hiyo ambayo itapelekea kwenye ugomvi wa wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa Waislam. Kwa hiyo, ina maana kwamba huyo ‘Uli’l-amr’ ambaye tunayomriwa kumtii amepata mamlaka yake kwa makubaliano( Ijma). Mjadala huu uliotokea kwenye magezeti.

Mtawala Anayetwaa Madaraka Kwa Nguvu Hawezi Kuitwa ‘Uli’l-Amr.’

Ni sawa na kichekesho kushauri kwamba utii kwa dhalimu ni wajibu. Kama ingekuwa hivyo, kwa nini wanazuoni wa Sunni wanawashutumu watawala waonevu na makhalifa, kama Mu’awiya, Yazid, muovu Ziyad Ibn Abib, Ubaidullah, Hajjaj, Abu Salma na Muslim.
Ikiwa yeyote atadai kwamba utii kwa watawala wakarofi ni wajib (na baadhi ya Ulamaa kwa kweli wamesema hivyo) itakuwa ni kinyume kabisa na amri za Qur’ani. Allah mara kwa mara amewalaani watenda madhambi katika Qur’ani Tukufu na amewakataza Waislam kuwatii.

Hivyo inawezekanaje katika aya hii Yeye atuamuru kuwatii madhalim? Ni dhahiri kabisa, sisi hatuwezi kuhusisha amri mbili zinazopingana kwa Allah Muweza. Hivyo, Imam Fakhru’d-din Razi kwa uwazi, anasema kuhusu aya hii tukufu kwamba hawa ‘Uli’l-amr’ lazima wawe na uadilifu kamili. Vinginevyo Allah asingeweza kuunganisha wajibu wetu wa kuwatii wao pamoja na wajibu wa kumtii Allah Mwenyewe na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

‘Uli’l-Amr’ Lazima Aagizwe Na Kuteuliwa Na Allah

Kwa mujibu wa Shi’ah, hawa ‘Uli’l-amr’ lazima wawe huru kutokana na dhambi na wasiokosea. Na kwa vile hakuna yeyote isipokuwa Allah, anayeweza kujua ukweli wa kina wa moyo, hawa ‘Uli’l-amr’ lazima wateuliwe na Allah. Hivyo Allah ambaye anawaagiza Mitume pia ndie anawaagiza ‘Uli’l-amr’ aliye ‘Uli’l-amr’ ni dhahiri kwamba lazima awe na sifa zile zile alizokuwa nazo Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Katika aya hii tukufu, neno atwi’u (Mtii) limetumika mara mbili.

Anasema “Mtii Allah na mtii Mtume.” Anapozungumzia juu ya ‘Uli’l-amr’ Yeye hatumii hili neno atiw’u tena lakini anatumia kiunganisha ‘na’ yaani, pamoja na ‘Uli’l-amr.’ Kuunganisha haya maneno katika njia hii ina maana kwamba ‘Uli’l-amr’ wana sifa sawa na alizonazo Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) isipokuwa zile ambazo ni Makhsusi, za kipekee tu kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), kwa mfano ‘Wahyi’ (ufunuo), Utume, na kadhalika. Kwa ufupi sifa za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ni budi awe nazo ‘Uli’l-amr’ isipokuwa bila shaka, kwa kile cheo cha Utume.

Kwa hali hiyo Shi’ah wanaamini kwamba haya maneno ‘Uli’l-amr’ yanawalenga hawa Maimam kumi na mbili, yaani Amirul-Mu’munin na wengine kumi na mmoja wa kizazi chake, Ahlul-Bayt wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Aya hii ni moja uthibitisho wa Uimam wa Maimam hawa kumi na mbili. Mbali na hii, kuna aya nyingine nyingi zenye kuunga mkono maoni yetu juu ya nukta hii.

(1) Kwa mfano, Qur’ani Tukufu inasema:

وَإِذِ ابْتَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ رَبُّهُ بِكَلِمَاتٍ فَأَتَمَّهُنَّ ۖ قَالَ إِنِّي جَاعِلُكَ لِلنَّاسِ إِمَامًا ۖ قَالَ وَمِنْ ذُرِّيَّتِي ۖ قَالَ لَا يَنَالُ عَهْدِي الظَّالِمِينَ {124}

“Akasema: Hakika nitakufanya wewe kuwa Imam wa watu.” (Ibrahim) akasema: Na katika kizazi changu?” Akasema (ndiyo, lakini) Ahadi yangu haiwafikii madhalim.” (2:124)

النَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنْفُسِهِمْ ۖ وَأَزْوَاجُهُ أُمَّهَاتُهُمْ ۗ وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّهِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ{6}

“Nabii anayo haki zaidi juu ya waumini kuliko nafsi zao, na wake zake ni mama zao; na wenye nasaba wana haki zaidi wao kwa wao katika Kitabu cha Allah kuliko wengine wauminio au Muhajirina (33:6)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَكُونُوا مَعَ الصَّادِقِينَ {119}

“Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na kuweni pamoja na wakweli.” (9:119)

ۗ إِنَّمَا أَنْتَ مُنْذِرٌ ۖ وَلِكُلِّ قَوْمٍ هَادٍ {7}

“.....Hakika wewe ni muonyaji tu, na kila Umma una Kiongozi wake.”(13:7)

وَأَنَّ هَٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَنْ سَبِيلِهِ ۚ{153}

“Na kwa hakika hii ndio njia yangu iliyonyooka, basi ifuateni, wala msifuate njia mbali mbali zikakutengeni mbali na njia yake.” (6:153)

وَمِمَّنْ خَلَقْنَا أُمَّةٌ يَهْدُونَ بِالْحَقِّ وَبِهِ يَعْدِلُونَ {181}

“Na katika wale tuliowaumba, kuna watu wanaongoza kwa haki na wanafanya uadilifu kwa haki hiyo.” (7:181)

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا ۚ{103}

“Na shikamaneni katika kamba ya Mwenyezi Mungu wote kwa pamoja na wala msifarikiane” (3:103)

فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِنْ كُنْتُمْ لَا تَعْلَمُونَ {43}

“Hivyo basi waulizeni wenye kujua (Ahlu’l-Dhikr) ikiwa ninyi hamjui .” (16:43)

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنْكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا {33}

“Hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwaondoleeni uchafu, enyi watu wa nyumba (ya mtume) na kukutakaseni kwa utakaso ulio kamili.” (33:33)

إِنَّ اللَّهَ اصْطَفَىٰ آدَمَ وَنُوحًا وَآلَ إِبْرَاهِيمَ وَآلَ عِمْرَانَ عَلَى الْعَالَمِينَ {33}

ذُرِّيَّةً بَعْضُهَا مِنْ بَعْضٍ ۗ وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ {34}

“Hakika Mwenyezi Mungu amemchagua Adam na Nuh na kizazi cha Ibrahim na kizazi cha Imran juu ya walimwengu. Kizazi cha wao kwa wao, mmoja kutokana na mwingine.(3:33-34)

ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ{32}

“Kisha tukawapa Kitabu (kama urithi) wale ambao tumewachagua kutoka miongo- ni mwa waja wetu.....” (35:32)

“Mwenyezi Mungu ndie nuru ya mbingu na aridhi, mfano wa nuru yake ni kama shubaka (tundu) ndani yake mna taa, taa hiyo imo ndani ya tungi, na tungi hiyo ni kama nyota inayong’ara sana, inayowashwa katika mti uliobarikiwa wa mzaituni usio na mashariki wale magharibi, mafuta yake yanakaribia kung’aa, ingawa moto hauyagusa.....” (24:35)

Kuna aya nyingine nyingi ambazo zingeweza kunukuliwa. Wengi wa ulamaa wenu mashuhuri wamesimulia kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Moja ya nne ya Qur’ani Tukufu ni yenye kuitukuza Ahlul-Bayt.”

Ibn Abbas anasemekana kwamba alisema. “Zaidi ya aya 300 zimeshushwa katika kumtukuza Ali.”

Sasa, ninakuja kwenye hoja yangu ya asili kwamba hawa ‘Uli’l-amr’ ni lazima wawe wenye wa kutotenda makosa kwa sababu utii kwao umeugnanishwa na utii kwa Allah na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Imam Fakhru’d-din Razi katika Tafsiir yake anakiri kwamba kama hatuwachukulii ‘Uli’l-amr kama wasiotenda makosa (ma’sum) itakuwa, katika utekelezaji, kusimamisha vitu viwili vinavyopingana kuwa ni vya kweli. Wanazuoni wenu wenyewe wamethibitisha kwamba sifa hizI walikuwa nazo Maimam hawa kumi na mbili pekee. Hii aya tukufu ya Utakaso (33:33) pia inathibisha ukweli huu.

Kutotenda Dhambi Na Makosa (Uma’sum) Kwa Maimam Watukufu Kumesimuliwa Kwa Jumla Sana.

Sheikh Sulayman Balkhi Hanafi katika Yanabiu’l-Mawadda sura ya 77, uk. 445, na Hamwaini katika Fara’idus-Simtain wanasimulai kwamba Ibn Abbas amesema: “Nilimsikia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akisema: ‘Mimi na Ali, Hasan, Husain na watu tisa katika kizazi cha Husain tuko safi kabisa na tusiofanya makosa ( ma’sum).’”

Salman Farsi anasema kwama Mtukufu Mtume, akiweka mkono wake kwenye bega la Husein, alisema: “Huyu ni Imam na mtoto wa Imam, na katika kizazi chake watakuwapo Maimam tisa ambao watakuwa wote ni hujjat waadilifu wa Allah na wema sana.”

Zaidi Ibn Thabit anasimulia kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema; “Hakika kutokana na kizazi cha Husain watazaliwa Maimam watakaokuwa Hujjat wema sana, Mahakimu wasiokosea kabisa.”

Imran Ibn Hasin anasimulia kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimuambia Ali: “Wewe ni mrithi wa elimu yangu. Wewe ni Imam na khalifa baada yangu. Wewe utawaeleza watu kile wasichokijua. Wewe ni baba wa wajakuu zangu na mume wa binti yangu, katika kizazi chako watakuwepo Maimam wasiokosea (ma’sum).

Elimu Ya Ahlul-Bayt.

Abu Ishaq Hamwaini katika Fara’idus-Simtain, Hafidh Abu Nu’aim Ispahani katika Hiliyatu’l-Auliya, na Ibn Abi’l-Hadid katika Sharh-e-Nahjul-Balagha wanasimulia kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Kizazi changu kiliumbwa kutokana na mbegu ile ile ambyo kutokana nayo niliumbwa mimi. Allah Mwenye uwezo amejaalia juu yao elimu na hekima. Laana naiwe juu yake yule atakayewakataa.”

Ibn Abi’l-Hadid katika Sharh-e-Nahju’l-Balagha na mtunzi wa Siratus-Sahaba, wanasimulia kutoka kwa Hudhaifa Bin Asaid kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Ninawachieni nyuma yangu vizito viwili: Kitabu cha Allah na ‘Ahlul-Bait’ wangu. Kama mtashikamana navyo viwili hivi mtaongoka”

Tabrani anasimulia nyongeza. “Msikatae mamlaka yao, vinginevyo mtaangamia. Msionyesha utovu wa nidhamu mbele yao ama kuwapuuza, la sivyo mtaangamizwa. Msijaribu kuwafundisha wao kwa sababu hakika wanajua vizuri zaidi kuliko ninyi.”

Katika simulizi zingine Hudhaifa Bin Asaid anamukuu Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akisema: “Baada yangu kutakuwa na Maimam watokanao na kizazi changu. Idadi yao itakuwa sawa na idadi ya Wajumbe wa Bani Israil, yaani, kumi na mbili, ambao kati yao tisa watakuwa ni kizazi cha Husain.

Allah ameijaalia juu yao wote elimu yangu na hekima. Hivyo msiwafundishe kwa sababu kwa kweli wao wanajua vizuri zaidi kuliko ninyi. Wafuateni wao kwani kwa uhakika wako pamoja na haki, na haki iko pamoja nao.”

Kwa Nini Majina Ya Hawa Maimam Hayatokezi Ndani Ya Qur’ani Tukufu

Kwanza, Kitabu hiki kitukufu ni cha kifupi sana. Ndani yake kinazo kanuni nyingi za jumla lakini maelezo ni machache, ambayo yameachiwa mfasiri mkuu, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), kuyaelezea. Allah anasema: “Na chochote Mtume anachokupeni kipokeeni, na chochote anachokukatazeni, kiacheni. (59:7)

Kwa sababu haya majina na idadi ya Maimam hawa kumi na mbili hayakutajwa ndani ya Qur’ani Tukufu, baadhi ya watu hawayakubali. Lakini kwa msingi huohuo wangewakataa makhalifa wao wenyewe kwani hakuna aya ya Qur’ani Tukufu inayotoa utajo wowote wa makhalifa wao isipokuwa Ali Bin Abi Talib, wala Makhalifa wa Bani Umayya au wa Bani Abbas, au wa mamlaka waliyopewa umma kumchagua khalifa kwa makubaliano (ijma). Pili, ikiwa ni muhimu kukataa kitu chochote ambacho hakikuelezwa wazi ndani ya Qur’ani Tukufu, basi mngelikataa nyingi ya taratibu na namna za ibada zetu kwa vile hakuna utajo wa maelekezo yake ndani ya Qur’ani Tukufu.

Hakuna Utajo Wa Raka’a Za Swala Ndani Ya Qur’ani Tukufu.

Ibada ya sala pengine ndio tendo kuu la kiibada katika maisha ya Muislam. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisisitiza kuitenda kwake. Alisema; “Sala ndio nguzo na mlinzi wa Dini. Kama sala itakubaliwa, basi matendo mengine yote ya kidini yatakubaliwa. Kama itakataliwa, matendo mengine yote ya kidini pia yatakataliwa.”

Bila shaka, hakuna utajo ndani ya Qur’ani Tukufu wa idadi ya rak’aa za kutekelezwa kwa kila sala au maelezo maalum yoyote kuhusu namna gani sala zitakavyoendeshwa. Je, hii ina maana kwamba tuzitelekeze Sala? Qur’ani Tukufu inasema kifupi tu: “Simamisheni sala” Hakuna maelezo yoyote yanayotofautisha matendo ya wajib na ya sunna. Hayo yalielezwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Kwa njia hiyo hiyo amri zingine zimeandikwa katika Qur’ani Tukufu kwa kanuni tu. Maelezo yake, shuruti na maelekezo yanayostahili yalielezwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Vivyo hivyo, kuhusu Uimam na Ukhalifa, Qur’ani Tukufu inasema tu: “Mtiini Allah na mtiini Mtume na wale wenye Mamlaka miongoni mwenu.” Na tunalazimishwa kufuata amri ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuhusu hili kwa namna ileile tunavyofuata maelekezo yake kuhusu uchambuzi wa ibada ya sala.

Wafasiri wa Kiislam, imma Sunni au Shi’ah, hawawezi kutoa maelezo (sharh) yao wenyewe juu ya Qur’ani Tukufu. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Ikiwa mtu yoyote atatoa maelezo yake mwenyewe juu ya Qur’ani Tukufu, mahali pake ni Motoni.”

Kwa sababu hiyo, kila Muislam mwenye busara humgeukia mtafsiri halisi wa Qur’ani Tukufu, yaani, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Kwa miaka mingi nimezisoma tafsiri za Qur’ani za wote Sunni na Shi’ah na Hadithi lakini sijakuta hata hadithi moja ambayo ndani yake Mtukufu Mtume amesema kwamba ‘Ul’l-amr’ inawalenga viongozi wa kisiasa.

Kwa upande mwingine, vitabu vyao wote Sunni na Shi’ah vimejaa idadi kubwa ya simulizi kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliulizwa kuelekeza maana ya ‘ul’l’-amr’ na alijibu kwamba ‘ul’l-amr’ ilimhusu Ali na wengine kumi na mmoja wa kizazi chake. Nitatoa chache tu ya hizi hadithi nyingi ambazo zimesimuliwa kupitia vyanzo vinavyokubaliwa na Sunni.

‘Uli’l-Amr Inaashiria Kwa Ali Na Maimam Wa Ahlul- Bait.

1. Abu Ishaq, Sheikhu’l-Islam Hamwaini Ibrahim Bin Muhammad anaandika katika Fara’idus-Simtain yake: “Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ametuambia kwamba ‘Uli’l-amr’ inamhusu Ali Bin Abi Talib na Ahlul Bait wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

2. ‘Isa Bin Yusuf Hamadani anasimulia kutoka kwa Abu’l-Hasan na Salim Bin Qais, ambao wanasimulia kutoka kwa Amiru’l-Mu’minin Ali kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Wenza wangu ni wale ambao utii kwao umeunganishwa na Muweza Allah pamoja na utii Kwake Yeye mwenyewe. Ni wale ambao kwao anawaashiria wakati anaposema: ‘Wale wenye Mamlaka kutoka mingoni mwenu.’ Ni lazima kwamba hampingi wanachokisema. Muwatii na kufuata amri zao” Amirul-Mu’minin anaendela kusema kwamba: “Nilipoyasikia haya, nilisema: “Ewe Mtume, nifahamishe niwajue hao ‘Uli’l-amr’ ni akina nani.” Mtume akasema: “Oh, Ali! Wewe ndie wa kwanza wao.”

3. Muhammad Bin Mu’min Shirazi, mmoja wa wanachuoni wa kidini maarufu sana wa Sunni, anaandika katika Risala-e-ltiqadat yake kwamba wakati Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipomteua Amiru’l-Mu’minin kuwa mwakilishi wake hapo Madina aya ya “Uli’l-amr minkum” (Na wale wenye mamlaka kutoka miongoni mwenu) ilishushwa kumhusu Ali Bin Abi Talib.

4. Sheikh Sulayman Balkhi Hanafi katika Yanabiu’l-Mawadda, sura ya 38 anasimulia kutoka kwenye Manaqib kwamba imeandikwa katika Tafsir-e-Mujahid kwamba aya hii ilishushwa kumhusu Amiru-Mu’minin wakati Mtukufu Mtume alipomteua kama mwak- ilishi wake huko Madina. Imam Mtukufu alisema: “Oh! Mtukufu Mtume wa Allah (s.a.w.w.)! Umeniteua mimi kuwa Khalifa juu ya wanawake na watoto? Kisha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema “Wewe huridhiki kwamba una uhusiano nami sawa na Harun alivyokuwa kwa Musa?”

5. Sheikhu’l-Islam Hamwaini anamsimulia Salim Bin Qais Hilal kwamba amesema yafu- atayo: “Wakati wa Ukhalifa wa Uthman, niliona baadhi ya Muhajir na Ansar wamekaa pamoja wakijisifu wenyewe. Ali alikuwa kimya miongoni mwao. Wale watu wakamuomba Ali azungumze. Yeye akasema: “Hamjui kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema: ‘Mimi na Ahlul Bait wangu tulikuwa nuru moja. Iliyokuwepo kwenye umbaji wake miaka 14000 kabla ya kuumbwa Adam? Wakati alipomuumba Adam, Aliiweka nuru ile katika uti wa mgongo wakepale aliposhuka kuja dunaini.
Kisha akaiweka kwa Nuhu ndani ya safina yake, kisha katika mgongo wa Abraham alipokuwa kwenye moto, vivyo hivyo katika migongo safi ya mababa na katika matumbo safi ya akina mama, ambao hakuna mmoja wao aliyezaliwa kinyume cha sheria” Wale waliokuwemo kwenye lile kundi ambao walikuwa wa mbele katika vita vya Badr na Hunain wakasema: “Ndio, tumeyasikia maneno haya.” Kisha Ali akasema: “Niambieni kwa kiapo kama mnajua kwamba katika Qur’ani Tukufu Allah ametoa kipaumbele kwa wale wa mwanzo kabisa, na kwamba katika Uislam hakuna anaelingana na mimi kwa sifa.” Wao wakasema: “Ndio, tunalithibitisha hili.”

Kisha Ali akasoma kutoka kwenye Qur’ani Tukufu: “Na waliotangulia ni wa mbele kabisa, hawa ndio wale waliovutwa karibu na Allah.” (56:10-11)

Akasema: “Wakati aya hii iliposhushwa, watu walimuuliza Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ni nani walio wa mbele kabisa, na ni kuhusu nani aya hii imeshushwa. Sasa niambieni kwa kiapo kama mnajua kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliwaambia kwamba Allah Muweza Aliishusha aya hii kuhusu mitume na washika makamu (waandamizi) wao.

Mimi ni wa mbele kabisa miongoni mwa Mitume na Ali, wasii (mwandamizi) wangu ni wa mbele kabisa miongoni mwa washika makamu wote?”

Kisha Ali akasema: “Qur’ani Tukufu inatumbia, ‘Mtiini Allah na mtiini Mtume na wale waliopewa mamlaka kutoka miongoni mwenu’ (4:59) na hii aya: ‘Hakika, hakika kiongozi wenu (si mwingine) ila Allah na Mtume wake (Muhammad) na wale walioamini, wale wanaosimamisha swala na kutoa zaka, huku wakiwa wamerukuu (5:55) na hii aya: “Hawakuchukua yeyote kama mtegemewa mbali na Allah na Mtume wake na wale walioamini.” (9:16)

Allah baadaye alimuamuru Mtume wake Mtukufu kumtambulisha yule aliyodhamiriwa kwa haya maneno ‘Uli’l-amr’ wale waliopewa mamlaka kwa namna ile ile kama ibada ya Sala, Saumu na Hijja zilivyopambanuliwa. Kwa hiyo, pale Ghadir-e-Khum Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliniteua mimi kuwa juu ya watu na akatamka: “Enyi watu wakati Mwenyezi Mungu aliponipa utume nilihisi wasiwasi kwamba watu watanipinga mimi”

Kisha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akaendelea “Enyi watu mnajua kwamba Allah Mtukuka zaidi ndie Mola wangu? Ninayo mamlaka zaidi juu ya nafsi za waumini zaidi ya wao waliyonayo juu yao wenyewe? Wote walipothibitisha kwamba hivyo ndivyo ilivyokuwa, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akatangaza: ‘Ambaye yeyote mimi ni bwana kwake, Ali ni bwana wake; Ewe Allah kuwa rafiki wa yale ambae ni rafiki wa Ali na kuwa adui wa yeye ambaye ni adui wa Ali’

Kisha Salman akasimama na kuuliza: “Ewe Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ni upi mfano dhahiri wa ubwana wa Ali? Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akajibu: ‘Ubwana wa Ali ni kama ubwana wangu mimi mwenyewe. Ambaye yeyote mini ni bwana kwake Ali pia ni bwana wake.’”

Kisha aya hii ikashushwa: “Leo hii nimewakamilishia dini yenu na nimeitimiza neema Yangu kwenu na nimeweachangulia Uislam kama dini.” (5:3)

Hapo ndipo Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Allahu-Akbar, Mungu ni Mkubwa, aliyeikamilisha hii dini, akatimiza neema Yake juu yangu, na ameridhishwa na Utume wangu na ameridhika na Ali kuwa mshika makamu (mwandamizi) baada yangu.

Hadithi hii inathibitisha zile hadithi ambazo nimezisimulia katika mikesha iliyopita kuonyesha kwamba bwana (Maula) pia ina maana umiliki zaidi ya ule wa mtu mwenyewe.

“Kisha watu wakasema “Ewe Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) tuambie majina ya washika makamu (waandamizi) wako.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Wao ni Ali, ambaye ni ndugu yangu, mrithi wangu na wasii wangu na bwana wa kila muumini baada yangu, kisha mwanawe, Hasan, kisha Husein, kisha watoto tisa wa Husain wanaofuatana, mmoja baada ya mwingine. Qur’ani Tukufu iko pamoja nao na wao wako pamoja na Qur’ani Tukufu, Hawatatengana nayo, nayo haitatengana nao mpaka wanikute mimi kwenye Haudhi ya Kauthar.’”

Baada ya kuandika habari hii nzima amesimulia hadithi nyingine tatu kutoka kwenye Manaqib zilizosimuliwa na Salim Bin Qais, Isa Bin Sirri na Ibn Mu’awiya zinazoonyesha kwamba haya maneno ‘Uli’l-amr’ yanawahusu Maimam kumi na wawili wa ‘Ahle Bait.’ Ninaamini kwamba hadithi hizo hapo juu zinatosha kufafanua maana halisi ya ‘ul’l-amr.’

Na kuhusu idadi na majina ya Maimam watukufu, nitasimulia hadithi zilizosimuliwa na wanazuoni maarufu wa Sunni, bila kurejea, kama ilivyokuwa desturi yangu, kwenye hadithi nyingi za wanazuoni wa Shi’ah.

Majina Ya Maimam Na Idadi Yao - (Kumi Na Mbili).

(1) Sheikh Sulayman Balkh Hanafi katika Yanabiu’l-Mawadda yake, sura ya 76 anasimulia kutoka Fara’idus-Simtain cha Hamwaini, anayesimulia kutoka kwa Mujahid, anayesimulia toka kwa ibn Abbas, kwamba Myahudi anayeitwa Na’thal alikuja kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na akamuuliza maswali kuhusu Tawhid (Upweke wa Allah) Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akayajibu maswali yake na Myahudi yule akaingia Uislam. Kisha akasema: “Ewe Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), kila Mtume alikuwa na Wasii (mshika makamu) wake. Mtume wetu Musa Bin Imra, aliusia kwa Yusha Bin Nun. Tafadhal hebu niambie ni nani wasii wako?”

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Mwandamizi (wasii) wangu ni Ali Bin Abi Talib, baada yake ni Hasan, na Husain na baada yao kuna Maimam tisa, ambao ni mfululizo wa kizazi cha Husain.”

Na’thal akamuuliza Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) majina ya Maimam hao. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Baada ya Hussein, mwanawe Ali atakuwa Imam, baada yake mwanawe Muhammad, baada yake mwanae Ja’far, baada yake mwanae Musa, baada yake mwanae Ali, baada yake mwanae Muhammad, baada yake mwane Ali, baada yake mwanae Hasan, baada yake mwanae, Muhammad Mahdi atakuwa ndio Imam wa mwisho. Watakuwepo Maimam kumi na mbili.

Zaidi ya majina haya ya Maimam tisa, hadithi hii inaeleza zaidi kwamba kila mmoja wao atafuata kama Imam baada ya baba yake. Na’thal aliulizia maswali zaidi na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akaelezea namna ya kifo cha kila Imam.

Kisha Na’thal akasema: “Nashuhudia kwamba hakuna mungu ila Allah na kwamba wewe ni Mtume wake Mtukufu. Nashuhudia kwamba Maimam, hawa kumi na mbili ndo washika makamu wako baada yako. Uliyoyasema ni sawa sawa hasa yale yaliyoandikwa kwenye vitabu vyetu na katika usia wa Musa.”

Kisha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Pepo ni yake yule anayewapenda na kuwatii hawa, na Moto wa Jahanamu ni kwa ajili yake yule atakayewachukia na kupinga hawa.”

Kisha Na’thal akasoma tenzi zenye maana kwamba ‘Allah aliyetukuka ashushe rehma juu yako, Mtume uliyechaguliwa na fahari ya Bani Hashim. Allah ametuongoza sisi kupitia kwako na watu watukufu kumi na mbili uliowataja. Hakika Allah amewatakasa na kuwahifadhi kutokana na uchafu.

Yule anayewapenda wao amefuzu. Yule anayewachukia hawa yu mwenye hasara. Wa mwisho wa Maimam hawa atakata kiu ya wenye kiu. Yeye ndiye yule watu watakayemngoja. Ewe Mtume wa Allah, kizazi chako ni rehma kwangu na waumini wote. Wale wanaogeuka na kuwapa kisogo punde watatupwa kwenye Moto wa Jahannam.

(2) Yule mwanazuoni mkuu, Sheikh Sulayman Balkhi katika Yanabiu’l-Mawadda yake, sura ya 76, anasimulia toka kwenye Manaqib ya Khawarizmi, ambaye anasimulia kutoka Wathila Bin Asqa’ Bin Qarkhab, ambaye anasimulia toka kwa Jabri Bin Abdullah Ansar, na pia Abu’l-Fazl Shaibani na yeye kutoka kwa Muhammad Bin Abdullah Bin Ibrahim Shafi’i, anayemnukuu Jabir Ansari (mmojawapo wa masahaba wakuu wa Mtume) kwam- ba amesema; “ Jundal Bin Junadab Bin Jubair, ambaye ni Myahudi, alikuja kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na kumuuliza kuhusu Tawhid.

Baada ya kusikia jibu lake, yule mtu akawa Muislam. Akasema kwamba katika usiku uliopita alimuona Musa katika ndoto akimuambia; ‘Ingia Uislam kwenye mikono ya wa mwisho katika Mitume, Muhammad, na ujiambatanishe wewe kwa washika makamu wake baada yake.’ Alimshukuru Allah kwa neema ya Uislam. Kisha ndipo akamuomba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amtajie majina ya Washika Makamu wake. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alianza kwa kusema: “Washika Makamu wangu ni kumi na mbili kwa idadi.”

Yule mtu akasema alikwishaliona jambo hili ndani ya Taurat. Alimuomba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amtajie majina yao, na Mtume akasema: “Wa kwanza wao ndiye mkuu wa washika makamu na baba wa Maimam hao, naye ni Ali. Kisha wanafuata wanawe wawili Hasan na Husain. utawaona hawa watatu.

Pale utakapofikia hatua ya mwisho ya uhai wako, Imam Zainu’l-Abidini atazaliwa, na kitu cha mwisho utakachokula cha dunia hii kitakuwa ni maziwa. Kwa hiyo sikamana nao hawa ili ujinga usije ukakupotosha.”

Kisha yale mtu akasema ameona katika Taurati na katika Maandiko mengineyo majina ya Ali, Hasan na Hussein kama Elias, Shabbar, na Shabbir. Akamuomba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amtajie majina ya hao Maimam wengine.

Kisha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akawataja wale Maimam tisa waliobakia pamoja na Lakab zao na akaongeza: “Wa mwisho wao, Muhammad Mahdi, ataishi, lakini atatowe- ka. Atatokeza baadae na ataujaza ulimwengu na haki na usawa, kwani utakuwa umekumbwa na dhulma na ukandamizaji.

Hakika pepo ni kwa wale watakaoonyesha uvumilivu wakati wa ghaib (kutoweka) kwake. Pepo ni kwa wale ambao ni imara katika mapenzi juu yake.

Hawa ndio wale ambao Allah Muweza amewasifu ndani ya Qur’ani Tukufu na kwa ajili ya wale ambao Qur’ani Tukufu ni ‘muongozo kwa wale wanaojilinda ( kutokana na maovu). Wale ambao wanaamini katika yaliyo ghaib” Pia anasema “Hawa ni kundi la Allah: sasa hakika kundi la Allah ni la wenye kufuzu.”(58:22)

Idadi Ya Makhalifa Baada Ya Mtukufu Mtume Ni Kumi Na Mbili

Mir Seyyed Ali Shafi’i Hamadani katika Mawaddatu’l-Qurba yake, (Mawadda ya 13), anasimulia kwamba Umar Bin Qais alisema: “Tulikuwa tumekaa katika kundi ambamo Abdullah Bin Mas’ud pia alikuwemo. Mara akaja Mwarabu mmoja na kusema: “Yupi miongoni mwenu ndio Abdullah?” Abdullah akasema: “Ni mimi.” Akasema (yule Mwarabu): Abdullah! Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikueleza kuhusu Makhalifa baada yake.?”

Abdullah Bin Ma’sud akasema: “Ndio, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema: ‘Baada yangu watakuwepo Makhalifa kumi na mbili, wanalingana na idadi ya Maimam wa Bani Isra’ili.”

Hadithi hii pia imesimuliwa kutoka kwa Sha’bi ambaye ameisimulia kutoka kwa Masruq, aliyeisimulia kutoka kwa Abdullah Shiba.

Pia Jurair, Ash’ath, Abdullah Bin Mas’ud, Abdullah Bin Umar na Jubair Bin Samra wote wanamsimulia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwamba alisema: “Watakuwepo Makhalifa kumi na mbili baada yangu. Idadi yao italingana na Makhalifa wa Bani Isra’ili.” Kwa mujibu wa simulizi ya Abdul’l-Malik, Mtukufu Mtume aliongeza: “Na wote watakuwa kutoka Bani Hashim.”

Wanazoni wengi wa Sunni, akiwemo Tirmidhi, Abu Dawud, Muslim, Sha’bi wamesimulia vivyo hivyo. Yahya Bin Hasan, mwanazuoni mkubwa wa fiqh, amesimulia katika kitabu chake Kitab-e-Umda kutoka kwenye vyanzo kumi na mbili tofauti, kwamba “Hakika, kuna Makhalifa kumi na mbili baada ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), nao wote wanatokana na Maquraish.”

Bukhari amesimulia kutoka kwenye vyanzo vitatu, Muslim kutoka vyanzo tisa, Abu Dawud kutoka vyanzo vitatu, Tirmidhi toka chanzo kimoja, na Hamid toka kwenye vyanzo vitatu kwamba Mtukufu Mtume amesema: “Makhalifa na Maimam baada yangu ni kumi na mbili, na wote wanatokana na Maqurish.” Kwa mujibu wa baadhi ya simulizi zingine, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema. “Wote hao watatokana na Bani Hashim.”

Katika uk. 446 Yahya Bin Hasan anasema: “Baadhi ya wanazuoni wamesema kwamba hadithi zenye kuunga mkono hoja ya kwamba idadi ya Makhalifa na Maimam baada ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ni kumi na mbili ni zenye kujulikana sana.

Kila mmoja anafahamu kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipoainisha kwamba idadi ya Makhalifa wake itakuwa kumi na mbili, alimaanisha kuwa watatokana na ‘Ahlul-Bait’ wake.

Kusema kwamba alimaanisha Makhalifa waliokuwa sahaba zake itakuwa ni kinyume na ukweli (kwa vile wao walikuwa wanne tu).

Wala haiwezi kusemwa kwamba alimaanisha wale wafalme wa Bani Umayya, ambao wao walikuwepo kumi na watatu. Zaidi ya hayo, wao walikuwa wakandamizaji isipokuwa Umar Bain Abdu’l-Aziz (ingawa hata yeye aliupora ukhalifa na kumlazimisha Imam wa zama hizo kubalikia kizuizini ndani ya nyumba yake).

Kwa vile Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Wote wanatokana na Bani Hashim.” Bani Umayya sio wa kuhesabika.

Kwa hiyo ni dhahiri kwamba Makhalifa wa haki wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) walikuwa ni wale Maimam kumi na wawili waliokuwa ni kizazi cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ambao waliwazidi wengine wote katika elimu na ucha-Mungu. Ukweli huu unathibitishwa na hadithi hii ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) iliyosimuliwa sana (mutawatir). “Ninaacha nyuma yangu vizito viwili, Kitabu Kitukufu cha Allah (Qur’ani Tukufu) na ‘Ahlul-Bayt’ wangu. Kama mtashikamana na viwili hivi, kamwe, kamwe, hamtapotea baada yangu.

Hakika viwili hivi havitatengana mpaka vinikute mimi kwenye Haudhi ya Kauthar. Kama mtashikamana na viwili hivi, hamtapotoshwa kamwe.”

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Tafuteni elimu hata ikiwa china.” Tumetumia mikesha kumi mirefu kujadili mambo yahusuyo elimu adhimunjia ya Uislamu.

Tumeona tofauti nyingi baina ya madhehebu ya Sunni na ile ya Shi’ah, na tunatumaini kwamba ukweli wa kihistoria na hoja zenye mantiki vimefafanua asili ya tofauti hizo. Inshallah mijadala hii itawavuta watafutaji elimu wakweli kwamba: “Anaeongozwa na Mwenyezi Mungu hakuna yeyote wa kumpoteza.”