read

Mkutano Wa Kwanza

(Usiku wa Alhamisi, 23 Rajab, 1345 A.H.)

Hafidh Muhammad Rashid, Sheikh Abdu’s-Salam, Sayyid Abdu’l-Hayy, na wanachuoni wengine wa eneo hilo walihudhuria. Mjadala ulianza mbele ya mkusanyiko mkubwa. Katika majarida na magazeti, walimuita mwandishi kama “Qibla-o-Ka’ba,” lakini katika kurasa hizi nimejiita mwenyewe kama “Muombezi” na Hafidh Muhammad Rashid kama “Hafidh.”

Hafidh: Tumefurahishwa sana kupata fursa hii ili kujadili nukta za msingi ambazo kwazo tunahitilafiana. Kwanza lazima tuamue jinsi tutakavyo endesha mjadala huu.

Muombezi: Niko tayari kushiriki katika mjadala huu kwa masharti kwamba tunaweka kando mawazo yote tuliyokuwa nayo kabla (juu ya imani zetu), na kujadili masuala kwa mantiki, kama ndugu.

Hafidh: Mimi pia niruhusiwe kutoa sharti moja: kwamba mjadala wetu uwe chini ya msingi wa maamrisho ya Qur’ani Tukufu.

Muombezi: Sharti hili halikubaliki kwa vile Qur’ani Tukufu ni yenye habari nyingi katika maelezo machache ambayo maana zake za ndani lazima zitafsiriwe kwa kurejea kwenye matukio mengine na hadithi.

Hafidh: Sawa, hili ni wazo la maana, lakini vile vile ni muhimu kwamba rejea zote zifanywe kwenye hadithi na matukio ambayo chimbuko lake ni juu ya ushahidi usiopingika. Lazima tujizuie kutokana na kurejea kwenye vyanzo vyenye mashaka.

Muomezi: Imekubalika. Kwa mtu kama mimi, ambaye ana fahari ya kutosha kudai uhu- siano na Mtume, sio haki kwenda kinyume na mifano iliyowekwa na jadi wangu, Mtume wa Uislamu. Ametambulishwa katika Qur’ani kama ifuatavyo:

وَإِنَّكَ لَعَلَىٰ خُلُقٍ عَظِيمٍ {4}

“Na hakika una tabia njema kabisa.” (68:4)

Vile vile sio vizuri kutenda dhidi ya maamrisho ya Qur’ani Tukufu ambayo inasema:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُمْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ{125}

Waite watu katika njia ya Mola wako kwa hikima na mauidha mema, na ujadiliane nao kwa nama iliyo bora…” (16:125)

Uhusiano Na Mtukufu Mtume

Hafidh: Samahani, unatoa rejea kwenye uhusiano wako na Mtukufu Mtume. Hiyo inajulikana sana, lakini naomba kwamba unifahamishe nasaba yako ili nipate kujua vipi jadi yako kinasaba imefikia kwa Mtume.

Muombezi: Nasaba ya jadi yangu humfikia Mtume kupitia kwa Imamu Musa Kadhim kama ifuatavyo: Muhammad, mtoto wa Ali Akbar (Ashrafu’l-Waidhin), mtoto wa Mujahid al-Waidhin, mtoto wa Ibrahim, mtoto wa Salih, mtoto wa Abi Ali Muhammad, mtoto wa Ali (ajulikanye kama Mardan), mtoto wa Abi’l-Qasim Muhammad Taqi, mtoto wa (Maqbulu’d-Din) Husein, mtoto wa Abi Ali Hasan, mtoto wa Muhammad bin Fadhullah, mtoto wa Is’haq, mtoto wa Hashim, mtoto wa Abi Muhammad, mtoto wa Ibrahim, mtoto wa Abi’l-Fiyan, mtoto wa Abdallah, mtoto wa Hasan, watoto wa Ahmad (Abu Tayyib), mtoto wa Abi Ali Hasan, mtoto wa Abu Ja’far Muhammad al-Hari (Nazil-e-Kirman), mtoto wa Ibrahim Az-Zarir (ajulikanaye kama Mujab), mtoto wa Amir Muhammad al-Abid, mtoto wa Imamu Musa Kadhim, mtoto wa Imamu Muhammad Baqir, mtoto wa Imamu Ali Zainu’l-Abidin, mtoto wa Imamu Husein, mtoto wa Amir’l-Muminin, Ali bin Abi Talib.

Hafidh: Safu hii ya nasaba hufikia kwa Amir’l-Muminin, Ali bin Abi Talib (Mungu ambariki) ingawa umesema kwamba huishia kwa Mtukufu Mtume. Kwa kweli, pamoja na nasaba hii unapaswa kujiita miongoni mwa jamaa za Mtukufu Mtume na sio miongoni mwa kizazi chake cha moja kwa moja. Dhuria ni yule ambaye moja kwa moja anaungana na Mtume.

Muombezi: Safu ya jadi wetu hufikia kwa Mtume kupitia kwa Bibi Fatima Zahra, mama wa Imamu Husein. Sielewi ni kwa nini unasisitiza mno juu ya nukta hii.

Hafidh: Nafikiri nimeeleweka vibaya. Ni mtazamo wangu kwamba dhuria hutambuliwa kutoka upande wa kiume tu. Nanukuu ubeti wa Kiarabu: “Watoto wangu, wajukuu, na mabinti wanatokana na mimi, lakini watoto wa binti wangu hawatokani na mimi.” Kama unaweza kuthibitisha vinginevyo, tafadhali fanya hivyo.

Muombezi: Kuna ushahidi imara, kutoka katika Qur’ani na kutoka katika hadithi, kuthibitisha nukta yangu.

Hafidh: Tafadhali usimulie ili tupata kuelewa.

Muombezi: Wakati ulipokuwa unaongea sasa hivi, nimekumbuka mazungumzo kati ya Harun ar-Rashid, Khalifa wa Kibani Abbas, na Imamu wetu Musa Kadhim juu ya suala hili. Imamu alitoa jibu la kuridhisha kiasi kwamba Khalifa mwenyewe alilikubali.

Hafidh: Ningependa kusikia kuhusu mazungumzo hayo.

Muombezi: Abu Ja’far Muhammad Bin Ali, mwenye lakabu ya Sheikh Saduq, katika karne ya nne A. H., katika kitabu chake Uyun-e-Akbar ar-Ridha (vyanzo vikubwa vya Ridha), na Abu Mansur Bin Ali Tabarsi, katika kitabu chake Ihtijajj, anatoa maelezo kinaganaga ya mazungumzo ambayo yalifanyika kati ya Harun ar-Rashid na Imamu Musa Ja’far katika baraza ya Khalifa. Khalifa alimuuliza Imamu: “Unawezaje kudai kwamba wewe ni dhuria wa Mtukufu Mtume? Mtume hana dhuria. Inakubaliwa kwamba dhuria ni kutoka upande wa kiume na sio upande wa kike. Wewe ni kizazi cha bint yake.” Imamu akasoma Aya ya 84-85 kutoka Sura ya 6 ya Qur’ani Tukufu:

وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ ۚ كُلًّا هَدَيْنَا ۚ وَنُوحًا هَدَيْنَا مِنْ قَبْلُ ۖ وَمِنْ ذُرِّيَّتِهِ دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ وَأَيُّوبَ وَيُوسُفَ وَمُوسَىٰ وَهَارُونَ ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ {84}

وَزَكَرِيَّا وَيَحْيَىٰ وَعِيسَىٰ وَإِلْيَاسَ ۖ كُلٌّ مِنَ الصَّالِحِينَ {85}

“Na tukampa (Ibrahim) Is’haqa na Yakuub, wote tukawaongoa. Na Nuh tulimuongoa zamani, na katika kizazi chake Daudi na Suleimani na Ayub na Yunus na Musa na Harun. Na hivi ndivyo tuwalipavyo wafanyao mema. Na Zakaria na Yahya na Isa na Ilyasa, wote walikuwa miongoni mwa watu wema.” (6:84-85)

Imamu akamuuliza Khalifa: “Ni nani aliyekuwa baba wa Isa?” Harun akajibu kwamba Isa alikuwa hana baba. Imamu akasema: “Kulikuwa hakuna yeyote aliyekuwa baba yake, na bado Allah alimjumuisha Isa katika dhuria wa mitume kupitia Mariamu. Hivyo hivyo ame- tujumuisha sisi katika dhuria wa Mtume kupitia kwa jadi wetu Bibi Fatima.” Aidha, Imamu Fakhur’d-Din Razi, katika kitabu chake Tafsir-e-Kabir, juzuu ya 4, uk. 124, anasema kuhusiana na aya hii kwamba, inathibitisha kwamba Hasan na Husein ni watoto wa Mtume wa Uislamu.

Kwa vile katika aya hii Mungu amemdhihirisha Isa kama kizazi cha Ibrahim, na Isa hana baba, uhusiano huu ni kutoka upande wa mama. Katika hali hiyo hiyo, Hasan na Husein ni dhuria wa kweli wa Mtume. Imamu Musa alimuuliza Harun kama anataka uthibitisho zaidi. Khalifa akamuambia Imamu aendelee. Imamu akasoma Aya ya 61 kuto- ka Sura ya 3 ya Qur’ani Tukufu: Watakao kuhoji katika haya baada ya kukufikia ilmu, waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu, na sisi na ninyi, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo,”

Aliendelea, akisema kwamba hakuna mtu hata mmoja ambaye amewahi kudai kwamba katika tukio hilo la maapizano (Mubahila) dhidi ya Wakiristo wa Najran kwamba Mtume alimchukuwa pamoja na yeye mtu yeyote isipokuwa Ali Bin Abi Talib, Fatima, Hasan na Husein.
Kwa hiyo hufuatia kwamba “sisi” (anfusana) maana yake ni Ali Bin Abi Talib. Wanawake” (nisa’ana) maana yake Fatima na Watoto” (abna’ana) maana yake Hasan na Husein, ambao Allah amewatambulisha kama watoto wa Mtume mwenyewe. Kwa kusikia hoja hii, Harun aliguta, “Hongera, Ewe Abu’l-Hasan.” Kwa uwazi mantiki hii huthibitisha kwamba Hasan na Husein (watoto wa Bibi Fatima) ni watoto wa Mtukufu Mtume.

Nyongeza Ya Ushahidi Kuthibitisha Kwamba Kizazi Cha Fatima Ni Dhuria

Wa Mtukufu Mtume.

Ibn Abi’l-Hadid Mu’tazali, mmoja wa wanachuoni wenu wakubwa, katika kitabu chake Sharh’l-Nahju’l-Balagha, na Abu Bakr Razi katika tafsir yake, wameionesha aya hiyo hiyo wakithibitisha kwamba Hasan na Husein wanatoka upande wa mama yao, ni watoto wa Mtukufu Mtume katika njia ile ile ambayo Allah katika Qur’ani Tukufu amemjumuisha Isa katika kizazi cha Ibrahim kutoka upande wa mama yake, Mariamu.

Muhammad Bin Yusuf Ganji Shafi’i, katika kitabu chake Kifayatut-Talib; Ibn Hajar Makki katika ukurasa wa 74 na 93 wa Sawa’iq Muhiriqa, kutoka kwa Tabrani na Jabir Bin Abdullah Ansari, na Khatib Khawarizmi katika Manaqib kutoka kwa Ibn Abbas - wote wanasimulia kwamba Mtume alisema: “Allah ameumba dhuria wa kila Mtume kutokana na kizazi chake mwenyewe, lakini dhuria wangu waliumbwa katika kizazi cha Ali.” Vile vile Khatib-e-Khawarizmi katika Manaqib; Mir Seyyid Ali Hamadani Shafi’i katika Mawaddatu’l-Qubra; Imamu Ahmad Bin Hanbal, katika Musnad, na Sulayman Hanafi Balkhi katika Yanabiu’l-Mawadda wanasimulia katika maneno hayohayo kwa zaidi au pungufu, kwamba Mtukufu Mtume amesema: “Watoto wangu hawa wawili, ni maua mawili ya ulimwengu huu, na wote wawili ni Maimamu, imma wawe ni Maimamu kwa wazi au kimya kimya wakiwa wamekaa nyumbani.”

Na Sheikh Sulayman Hanafi, katika Yanabiu’l-Mawadda, ameitoa sura ya 57 kwenye suala hili na akaonesha hadithi nyingi kutoka kwa wanachuoni wake mwenyewe, kama Tabrani, Hafidh Abdu’l-Aziz Ibn Abi Shaiba, Khatib-e-Baghdadi Hakim, Baihaqi, na Tabari - wote wanasimulia katika maneno yanayohitalifiana kidogo kwamba Hasan na Husein ni watoto wa Mtume.

Kuelekea mwisho wa sura hiyo hiyo, Abu Salih anaandika: Hafidh Abdu’l-Aziz Bin Al- Akhzar, Abu Nu’aim, Tabari Ibn Hajar Makki katika ukurasa wa 112 wa Sawa’iq Muhriqa, kutoka kwa Muhammad Bin Yusuf Ganji Shafi’i mwishoni mwa jalada la 1, baada ya sura

100 za Kifayatut-Talib, na Tabari katika simulizi ya Imamu Hasan anasimulia kwamba Khalifa wa pili, Umar Bin Khattab, alisema: “Nilimsikia Mtume akisema kwamba katika Siku ya Hukumu kila ukoo utatenganishwa isipokuwa kizazi changu. Kila kizazi cha binti ni kutoka upande wa baba isipokuwa kizazi cha Fatima, ambacho kimeunganishwa na mimi. Mimi ni baba yao na jadi wao.” Sheikh Abdullah Bin Muhammad Bin Amir Shabrawi Shafi’i, katika kitabu chake Kitabu’l-Ittihaf bi Hubbi’l-Ashraf, alinukuu hadithi hii kutoka kwa Baihaqi na Darqutni kutoka kwa Abdullah Bin Umar, na yeye kutoka kwa baba yake, kwenye harusi ya Ummu Kulthum. Na Jalalu’d-Din Suyuti akinukuu kutoka kwa Tabrani katika kitabu chake Ausat, amesimulia kutoka kwa Khalifa Umar na Sayyid Abu Bakr Bin Shahabu’d-Din Alawi katika ukurasa wa 39-40 wa sura ya 3 ya Rishfatus- Sadi min bahra Fadha’il Bani Nabiu’l-Hadi (iliyopigwa chapa katika Maktabi A’lamiyya, Misr 1303 A.H.) huthibitisha kwamba dhuria wa Fatima ni kizazi cha Mtume wa Uislamu.

Kwa hiyo, ubeti ambao umeunukuu hauna nguvu mbele ya ushahidi wote huu wa kinyume chake. Muhammad Bin Yusuf Ganji Shafi’i, katika kitabu chake Kifayatut-Talib, anathibitisha kwamba watoto wa binti wa Mtume ni watoto wa Mtukufu Mtume. Halikadhalika, kuna hadithi nyingine nyingi ambazo huthibitisha kwamba watoto wa Bibi Fatima ni watoto wa Mtume. Safu yetu ya jadi huenda mpaka kwa Imamu Husein; kwa hiyo, sisi ni dhuria wa Mtume.

Hafidh: Hoja yako ni ya mantiki na kuridhisha. Watu walitawanyika kwa ajili ya Swala ya Isha. Wakati wa mapumziko Nawab Abdu’l- Qayum Khan, ambaye anatokana na familia sharifu ya Kisunni, alitaka ruhusa kumuuliza Muombezi maswali fulani.

Kwanini Shia Wanachanganya Swala Zao

Nawab: Kwa nini Shia wanachangana Swala ya Dhuhr na Alasir na Maghari na Isha? Hii sio sawa kulingana na matendo ya ibada ya Mtukufu Mtume.

Muombezi: Kwanza kabisa, miongoni mwa wanachuoni wenu kuna tofauti nyingi za maoni kuhusu suala hili. Pili, unasema tunakwenda kinyume na mwenendo wa Mtume. Hapa umekosea kwani Mtukufu Mtume amezoea kuswali Swala zake katika njia zote, wakati mwingine kwa kuzitengenisha na wakati mwingine kwa kuzichanganya.

Hapo Nawab Swahib aliwageukia wanachuoni wake, aliwauliza kama ni kweli kwamba Mtume aliswali katika njia zote.

Hafidh: Ndio alifanya hivyo, lakini ni wakati tu alipokuwa safarini au wakati kama kuna vikwazo vingine fulani, kama mvua. Vinginevyo, wakati alipokuwa nyumbani siku zote alikuwa akiswali swala zake kwa kuzitenganisha.

Muombezi: Imeandikwa katika vitabu vyenu wenyewe vya hadithi kwamba Mtume ali- zoea kusali Swala zake kwa kuzitenganisha na halikadhalika kwa kuzichanganya akiwa nyumbani na bila kikwazo chochote. Hadithi nyingi zinathibitisha ukweli huu. Muslim Bin Hajjaj katika Sahih yake, katika mlango wa “Jam’a Baina’s-Salatain fi’l-Hadhar,” anasema kwamba Ibn Abbas alisema: “Mtume alizoea kuswali Swala ya Dhuhr na Alasir kwa kuziunganisha na halikadhalika hivyo hivyo kwa Swala za Magharib na Isha bila ya kuwa na kikwazo cha kufanya hivyo, au wakati alipokuwa nyumbani.” Tena Ibn Abbas alisimulia:

“Tuliswali rakaa nane za Dhuhr na Alasir na baadae rakaa saba za Magharib na Isha kwa kuziunganisha tukiwa pamoja na Mtume.” Hadithi hiyo hiyo imesimuliwa na Imamu Ahmad Bin Hanbal katika Musnad yake jalada la kwanza, ukurasa wa 221. Halikadhalika, Imamu Muslim ananukuu idadi ya hadithi kuhusiana na suala hili.

Anamnukuu Abdullah Bin Shaqiq akiwa amesema kwamba siku moja Abdullah Ibn Abbas alikuwa anahutubia baada ya Swala ya Alasir mpaka jua likazama na nyota zikawa zinaonekana. Watu wakapiga makelele, “Swala, Swala,” lakini Ibn Abbas hakuwajali. kisha mtu mmoja wa Bani Tamimi alipiga kelele, “Swala, Swala.” Ibn Abbas akasema: “Unanikumbusha mimi kuhusu Sunna, lakini mimi mwenyewe nimemuona Mtume akikusanya Swala za Dhuhr na Alasir halikadhalika Magharib na Isha.” Abdullah Bin Shaqiq alisema alikuwa hana hakika kuhusu maneno haya na alikwenda kwa Abu Huraira kumuuliza kuhusu maneno hayo. Alithibitisha kile alichokisema Ibn Abbas.

Kupitia sanad nyingine ya wasimuliaji, Abdullah Bin Shaqiq alisimulia kutoka kwa Aqil kwamba siku moja Abdullah Ibn Abbas aliwahutubia watu juu ya mimbari. Alibaki pale kwa muda mrefu mpaka giza likaingia. Wakati mtu mmoja alipopiga kelele mara tatu, “Swala, Swala, Swala,” Abdullah Ibn Abbas alikasirika na akasema: “Ulaaniwe wewe. Unathubutu kunikumbusha mimi kuhusu Swala, ingawaje wakati wa Mtukufu Mtume tuli- zoea kukusanya Swala za Adhuhr na Alasir na halikadhalika Magharib pamja na Isha.” Zarqani katika Sharhe Mawatta cha Imamu Malik, jalada la 1, katika sura ya Jama’a Baina’s-Salatain, ukurasa wa 263, anaeleza, “Nisa’i alisimulia kutoka kwa Amru Bin Haram kutoka kwa Abi Sha’atha kwamba Ibn Abbas aliswali Dhuhr na Alasir na halikadhalika Magharib na Isha kwa pamoja mjini Basra bila kukawia au kitendo chochote kati yao. Alisema kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliswali katika njia hii hii.”

Vile vile Muslim katika Sahih yake na Malik katika Mawatta, sura ya Jam’a Baina’s- Salatain, na Imamu Hanbal katika Musnad wanamnukuu Ibn Abbas kutoka kwa Sa’id Bin Jabir kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliswali Swala zake za Dhuhr na Alasir pamoja mjini Madina bila kulazimishwa kufanya hivyo kwa hofu au hali mbaya ya hewa. Abu Zubair akasema alimuuliza Abu Sa’id kwa nini Mtume alikusanya Swala hizo mbili. Sa’id akasema yeye vile vile alimuuliza Ibn Abbas swali kama hilo hilo.

Ibn Abbas alijibu kwamba alikusanya Swala hizo mbili ili kwamba wafuasi wake wasije wakawekwa katika uzito na shida zisizo na sababu. Vile vile, katika hadithi nyingine nyingi, Ibn Abbas inasimuliwa kwamba alisema Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) wa Uislamu alikusanya Swala za Dhur na Alasir halikadhalika na Magharib na Isha bila kulazimishwa kufanya hivyo.
Hadith hizi katika Sahihi zenu na vitabu vyingine sahihi huthibitisha kuruhusiwa uku- sanyaji wa Swala mbili, nyumbani au safarini.

Hafidh: Hakuna nukuu kama hiyo ya hadithi katika Sahih Bukhari.

Muombezi: Kwa sababu waandishi wote wa Sahih, kama vile Muslim, na Nisa’i, Ahmad Bin Hanbal, na wafasir wa Sahih mbili, ya Muslim, Bukhari, na wanachuoni wengine wakubwa wa ki-Sunni wamenukuu mambo haya, hii inatosha kwetu kuishindisha nukta yetu. Lakini kwa kweli Bukhari vile vile ameziandika hadithi hizi katika Sahih yake, lakini kwa hila ameziweka mbali na sehemu zao husika, ile sehemu inayohusika na ukusanya- ji wa Salat mbili.

Kama utaipitia ile milango ya “Bab-e-Ta’akhiru’dh-Dhuhur li’l-Asr Min Kitabe Mawaqtu’s-Salat” na “Bab-e-Dhikru’l-Isha wa’l-Atma” na Bab-e-Waqitu’l- Maghrib,” utaziona hadithi zote hizi humo. Hadithi hizi kuandikwa chini ya kichwa cha habari: “Ruhusa na Mamlaka ya Kisheria ya kukusanya Salat mbili” huthibitisha kwamba ni imani ya kawaida ya wanachuoni wa madhehebu hizi mbili.

Usahihi wa hadithi hizi umekwisha kubaliwa katika vitabu vya Sahih. Kwa sababu hiyo, Allama Nuri katika Sharhe Sahih Muslim, Asqalani, Qastalani, Zakariyya-e-Razi katika sharhe ambayo imeandikwa juu ya Sahih Bukhari, Zarqani katika Sharhe yake juu ya Muwatta - kitabu cha Imamu Malik, na wengine wamesimulia hadithi hizi. Baada ya kunukuu hadithi ya Ibn Abbas, walikubali usahihi wake na wakakiri kwamba hadithi hizi ni uthibitisho wa kukubalika kwa kukusanya Salat mbili.

Nawab: Imewezekanaje kwamba hadithi hizi zimekuwa katika matumizi tangia wakati wa uhai wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), lakini wanachuoni wamechukuwa njia nyingine?

Muombezi: Hali hii haikomei kwenye nukta hii peke yake. Utaona mifano mingi kama hii baadae. Katika suala hili, Mafaqih wa ki-Sunni, kwa wazi bila ya kufikiria kwa makini, au kwa sababu nyingine ambazo mimi sizielewi, wametoa maelezo yasiyoleweka kukinzana na hadithi hizi. Kwa mfano, wanasema kwamba huenda hadithi hizi huzungumzia hali zinazohusiana na hofu, hatari, mvua, au upepo mkali.

Baadhi ya wanachuoni wenu wa zamani, kama Imamu Malik, Imamu Shafi’i, na baadhi ya wanachuo wa Madina wametoa maelezo kama hayo hayo. Namna hii, pamoja na ukweli kwamba hadithi ya Ibn Abbas kwa uwazi kabisa inasema kwamba ukusanyaji wa Swala mbili ulikuwa unafanywa bila kikwazo cha hofu au uwezekano wa kunyesha mvua.

Wengine wamesema kwamba huenda mawingu yalikuwa yametanda angani, na wale waliokuwa wakisali hawakujua ni saa ngapi. Pengine walipomaliza kusali Swala yao ya Adhuhur, mawingu yalitawanyika, na wakaona kwamba ilikuwa ni wakati wa Swala ya Alasir. Hivyo wakalazimika kusali Adhuhuri na Alasiri kwa pamoja. Sidhani maelezo zaidi yasiyo yamkinika yanaweza kupatikana.

Pengine wafasiri hawa hawakujali kufikiria kwamba mtu aliyekuwa akisali Swala hizo ni Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) wa Uislamu. Mawingu hayakumaanisha kwake kile ambacho kingemaanishwa kwa wengine. Anajua sababu zote na matokeo. Mbali na ukweli kwamba maelezo haya hayaridhishi, ukusanyaji wa Swala za Mahgarib na Isha unakataa maelezo yao. Katika wakati huo mawingu hayana uhusiano na suala hili. Kama tulivyosema, hadithi ya Ibn Abbas kwa uwazi inaeleza kwamba khutuba yake iliendelea kwa muda mrefu mpaka wasikilizaji wakapiga kelele, “Swala, Swala.”

Walimkumbusha kwamba nyota zimetokea na kwamba ilikuwa ni wakati wa Swala. Lakini aliichelewesha Swala ya Magharibi kwa makusudi ili aje kuswali zote, Magharib na Isha kwa pamoja. Abu Huraira vilevle alithibitisha kitendo hiki, akisema kwamba Mtume vile vile aliswali kwa nama hiyo hiyo. Maelezo ya uwongo kama hayo, katika mwanga wa mwongozo wa dhahiri, husikitisha.

Wanachouni wenu wenyewe wameyapuuza hayo. Sheikhu’l-Islam Ansari, katika kitabu chake, Tuhfatu’l-Bari fi Sharhe Sahihu’l-Bukhari katika sura ya Salatu’z-Dhuhr ma’l-Asr wa’l-Magharib ma’l- Isha ukurasa wa 292, jalada la 2, na halikadhalika Allama Qastalani, katika ukurasa wa 93 jalada la 2 la Irshadus-Sari fi Sharhe Sahihu’l-Bukhari, na hivyo hivyo na washereheshaji wengine wa Bukhari wanakiri kwamba aina hii ya maelezo ni kinyume na maana ya wazi ya hadithi na kwamba kusisitiza kwamba kila Swala iswaliwe peke yake ni mashrti yasiyo na msingi.
Nawab: Basi mgogoro huu umejitokeza vipi mpaka madhehebu mbili za Waislamu kila moja inataka kumwaga damu ya mwenzake, na kulaumu kitendo cha mwenzake?

Muombezi: Unasema kwamba madhehebu hizi mbili ni adui kwa kila mmoja, lakini sikubaliani na wewe. Sisi Mashi’a hatumdharau mwanachuoni yeyote au mtu wa kawaida katika ndugu zetu Masunni. Tunasikitika kwamba propoganda za Makhariji, Manasibi na Bani Umayyah zimeathiri nyoyo za baadhi ya watu. Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya Masunni wanawachukulia ndugu zao Mashi’a, ambao wako pamoja nao kwa kuhusiana na Qibla (Ka’aba), Kitabu Kitukufu (Qur’ani), Mtume, utekelezaji wa matendo ya dini, na kujiepusha kutokana na madhambi, kuwa kama Marafidhi (watofautishaji), waabudu masanamu, na makafiri.

Amma kwa swali lako kuhusu vipi tofauti hizi zilivyojitokeza, labda hili tunaweza kulijadili katika mikutano yetu ya baadae. Kuhusu kusali Swala kwa kutenganisha au kwa pamoja, wanachuoni wa sheria wa ki-Sunni wenye kutegemewa wamenukuu hadithi ambazo huruhusu kusali Adhuhuri na Alasiri na Magharibi na Isha kama jambo la wepesi, wasaa au usalama. Sijui kwa nini baadhi ya watu hawaoni kwamba inaruhusika kusali Swala mbili pamoja pasi na kuwa na udhuru wowote. Baadhi ya wanachuo, kama Abu Hanifa na wafuasi wake wameikataza katika hali yoyote, iwe kuna udhuru au la, au Swala iwe inasaliwa wakati mtu akiwa safarini au nyumbani.

Shafi’i, Maliki, na Hanbali, pamoja na hitilafu zao zote katika kanuni za msingi na zisizo za msingi, wameruhusu ukusanyaji wa Swala wakati wa safari ya halali. Lakini Maulamaa wa ki-Shi’a, wakiwa katika utii wa Imamu na kizazi cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) wameruhusu bila masharti yoyote ukusanyaji wa Swala mbili kwa pamoja.

Hakika kusali Swala katika wakati ulioanishwa kwa kila Swala ni bora kuliko kuzisali kwa wakati mmoja, kama ambavyo imeelezwa kwa uwazi katika vitabu vya tafsir vinavyoshughulika na matatizo ya utekelezaji wa masuala ya dini vilivyoandikwa na Maulamaa wa ki-Shi’ah. Kwa vile watu mara nyingi wanakuwa na shughuli nyingi katika mambo yao wenyewe na wasi wasi, wanaogopa huenda wakazikosa Swala zao. Kwa hiyo, kwa nafasi zao na kuepuka uzito na shida, Mashi’a wanasali Swala zao mbili katika wakati mmoja, mapema au kwa kuahirisha, katika wakati ule ule uliotengwa kwa ajili ya Swala. Sasa nafikiri kiasi hiki kinatosha kuwapa mwanga ndugu zetu Masunni ambao hutuangalia kwa hasira. Bila shaka tunaweza kurudi kwenye majadiliano yetu kuhusu misingi, ambapo baadae masuala yanayohusu ibada yatatatuliwa.

Jinsi Wazazi Wa Allama Walivyohama Kutoka Hijazi Kwenda Iran

Hafidh Sahib alimuomba Allama Sultanu’l-Wa’idhin amueleze ni vipi wazazi wake walivyohama kutoka Hijazi kwenda Iran. Alieleza historia ya wahenga wake ambao wali- uawa huko Shirazi kwa amri ya mfalme wa ki-Banu Abbas. Makaburi yao mpaka sasa bado yanawavutia mahujaji kutoka sehemu za mbali. Maarufu miongoni mwao ni Sayyid Amir Muhammad Abid, Sayyid Amir Ahmad (Shah Charagh), na Sayyid Alau’d-Din Husein, wote ni watoto wa Imamu Musa Kadhim. Maelezo kuhusu familia yake yanaondolewa hapa.

Jinsi Kaburi La Amiru’l-Mu’minin Ali (A.S.) Lilivyogunduliwa.

Vile vile ulitajwa ungunduzi wa kaburi la Amiru’l-Mu’minin ‘Ali (as).

Hafidh: Lakini kaburi la Amiru’l-Mu’minin liligunduliwa katika hali gani miaka 150 baada ya kifo chake?

Muombezi: Kwa sababu uonevu wa Banu Umayya ulikuwa mkali sana wakati wa mwisho wa uhai wa ‘Ali, hivyo aliagiza katika wosia wake kwamba azikwe kwa siri wakati wa usiku, na kwamba isiachwe alama yoyote ya kaburi hilo.

Ni jamaa zake wachache tu wa karibu na watoto wake ndio waliohudhuria mazishi yake. Asubuhi ya tarehe 21 Ramadhan siku ambayo ilikuwa ndio azikwe, misafara miwili ilitayarishwa. Mmoja ulielekezwa kwenda Makka, na mwingine kwenda Madina.
Hii ndio sababu iliyofanya kwa miaka mingi kaburi lake lisijulikane, isipokuwa kwa jamaa zake wachache na watoto wake tu.

Hafidh: Kwanini eneo la kaburi hilo likafanywa siri?

Muombezi: Huenda ni kwa sababu ya hofu ya tabia isiyo ya dini ya Banu Umayya. Walikuwa maadui makhususi wa jamaa ya kizazi cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w). Wangeweza kulivunjia heshima kaburi lake.

Hafidh: Lakini inawezekana kwamba Mwislamu, hata kama ni adui kiasi gani, anaweza kulifanyia vurugu kaburi la ndugu yake Mwislamu?

Muombezi: Umesoma historia ya Banu Umayya? Kuanzia siku ambayo utawala huu mbaya uliposhika madaraka, mlango wa maonevu ulifunguliwa miongoni mwa Waislamu. Subuhana-LLAH! Maovu yalioje waliyoyafanya! Damu iliyoje waliyoimwaga, na heshima zilizoje walizozivunja!

Kwa aibu kubwa, wanachuoni wenu wakubwa wameandika jinai zao nyingi. Allama Maqrizi Abu’l-Abbas Ahmad bin Ali Shafi’i ameandika maovu ya Banu Umayya yanayoumiza moyo kabisa katika kitabu chake Annaza’ Wat-takhasum fima baina Bani Hashim wa Bani Umayya.

Bani Umayya Na Utiaji Najisi Wa Makuburi

Kwa mfano wa yale waliyokuwa na uwezo nayo, nitaonesha matukio mawili: Kuuwawa shahidi kwa Zaid bin Ali bin Husein, ajulikanaye kama Zaid Shahid, na kuuwawa shahidi kwa mtoto wake, Yahya. Wanahistoria wote wa Shi’a na Sunni wameandika kwamba wakati Hisham bin Malik alipokuwa Khalifa, alitenda maovu mengi. Mwishowe, Zaid bin Ali, mtoto wa Imamu Zainu’l-Abidin na anayejulikana sana kama mwanachuo mkubwa na mwanatheolojia mchamungu, alikwenda kumuona Khalifa kutafuta haki kwa ajili ya manung’uniko ya Bani Hashim.

Lakini punde tu Zaid alipowasili, Khalifa badala ya kumsalimu kama mtoto wa moja kwa moja wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), alimtukana kwa lugha ya kuchukiza sana ambayo siwezi kuirudia hapa.

Kwa sababu ya kudhalilishwa huku alikofanyiwa, Zaid aliondoka Syria na kwenda Kufa, ambako aliunda jeshi dhidi ya Bani Umayya. Gavana wa Kufa, Yusuf bin Umar Thaqafi, alitoka na jeshi kubwa kumkabili. Zaid alisoma shairi lifuatalo: “Maisha ya udhalilifu na kifo cha heshima, vyote ni chembe zenye uchungu, lakini kama moja wapo lazima ichanguliwe, chaguo langu ni kifo cha heshima.”

Ingawa alipigana kishujaa, Zaid aliuwawa katika mapigano hayo. Mtoto wake, Yahya, alichukua mwili wake kutoka kwenye uwanja wa vita na akamzika mbali kutoka mjini karibu na ukingo wa mto, na kusabibisha maji kupita juu yake. Hata hivyo, kaburi hilo liligunduliwa, na chini ya amri ya Yusuf mwili huo ulifukuliwa, kichwa cha Zaid kilikatwa na kupelekwa Syria kwa Hisham.

Katika mwezi wa Safar, 121 A.H., Hisham aliamuru mwili mtakatifu wa mtoto huyu wa Mtume (s.a.w.w) uwekwe kwenye kiunzi cha kunyongea ukiwa uchi kabisa.

Kwa muda wa miaka minne ulikaa kwenye kiunzi cha kunyongea. Baadae, wakati Walid bin Yazid bin Abdu’l-Malik bin Marwan alipokuwa Khalifa katika mwaka wa 126 A.H., aliamrisha kwamba mifupa ile itolewe kutoka kwenye kiunzi cha kunyongea, ichomwe, na jivu lake lisambazwe juu lichukuliwe na upepo.

Mtu huyu aliyelaaniwa alitenda uovu kama huu huu kwenye mwili wa Yahya bin Zaid wa Gurgan. Mtu huyu mtukufu vile vile alipinga uonevu wa Bani Umayya. Yeye pia aliuwawa katika medani ya vita. Kichwa chake kilipelekwa Syria na kama alivyofanyiwa mtukufu baba yake, mwili wake ulitundikwa kwenye kiunzi cha kunyongea kwa muda wa miaka sita.

Marafiki na maadui wote kwa pamoja walilia walipouona mwili wake. Waliu’d-Din Abu Muslim Khorasani, ambaye alipigana dhidi ya Bani Umayya kwa niaba ya Bani Abbas, aliuchukuwa mwili wake na kuuzika huko Gurgan, ambako ni sehemu ya kuhiji (Ziyarat).

Matendo Maovu Ya Ufalme Huu

Kwa kuzingatia maovu ya ufalme huu uliolaaniwa, mwili wa Amiru’l-Muminin, ‘Ali (as) ulizikwa wakati wa usiku, na hakuna alama ya kaburi hilo iliyoachwa. Kaburi likabakia bila kuonekana mpaka wakati wa Khalifa Harun ar-Rashid. Siku moja Harun alikwenda kuwinda katika eneo la Najaf, ambako paa waliishi kwa wingi. Wakati mbwa walipofukuza paa, walichukua hifadhi juu ya kilima kidogo (kilichotutumka juu ya ardhi) cha Najaf, kilima ambacho mbwa hao hawakuweza kukipanda.

Mara nyingi wakati mbwa waliporudi nyuma, paa waliteremka chini, lakini wakati mbwa wanapowarukia tena, wale paa huchukua tena hifadhi juu ya kile kilima. Harun akatuma watu wake kwenda Najaf kuuliza. Walimleta mzee mmoja kwake na Khalifa akauliza kuhusu siri ya kwa nini mbwa hawakupanda juu kilima.

Kugunduliwa Kwa Kaburi Tukufu La Ali.

Yule Mzee akajibu kwamba anaielewa Siri yake, lakini alikuwa anaogopa kuitoa. Khalifa akamhakikishia usalama wake, na yule mzee akamwambia: Siku moja nilikuja hapa pamoja na baba yangu, ambaye alipanda juu ya kilima na akaswali pale. Nilipomwuuliza kuna nini pale, akasema kwamba waliwahi kuja pale na Imam Ja’far Sadiq kwa ajili ya Ziara. Imam alisema kwamba hili ni kaburi Tukufu la Mheshimiwa babu yake, Amur’l Mu’miniina Ali, na kwamba muda mfupi litakujajulikana.”

Kwa amri ya Khalifa sehemu ile ilichimbuliwa, na alama za kaburi zikaonekana wazi pamoja na ubao wenye maandishi ya Ki-Syria yenye maana; “Kwa jina la Allah, Mwenye rehema, Mwenye kurehemu. Kaburi hili limetayarishwa na Mtume Nuh kwa ajili ya Ali, wasii wa Muhammad miaka 700 kabla ya gharika.”

Khalifa Harun alitoa heshima zake kwenye sehemu ile na akaamuru ule udongo urudish- we. Kisha akasali rakaa mbili. Alilia sana na akajilaza juu ya kaburi. Baadae, kwa amri yake, taarifa ya tukio lote ilitolewa kwa Imam Musa Kadhim huko Madina. Imam alithibitisha kwamba kaburi hilo ni la Mheshimiwa babu yake, Amiru’l-Mu’minin Ali, lipo mahala hapo. Kisha Harun akaamuru jengo la mawe lijengwe juu ya kaburi tukufu la Amiru’l-Mu’minin, ambalo lilikuja kujulikana kama “Hajar Harun.” Kwa wakati huo habari zilisambaa na Waislamu wakaizuru sehemu hiyo tukufu.

Ibrahim Mujab, babu yake mkubwa wa Sultani’l-Wa’idhin (Muombezi) pia alitoka Shiraz kwa ajili ya Ziara hii tukufu na baada ya kukamilisaha Ziara hii, yeye akafariki huko Karbala. Alizikwa karibu na kaburi tukufu la Babu yake Mkubwa, Imam Husein. Kaburi lake liko pembe ya Kaskazini Mashariki ya kuba lake tukufu na linazuriwa mara kwa mara na wapenzi wake.

Khitilafu Kuhusu Sehemu Aliyozikwa Amiru’l- Mu’minin.

Hafidh: Pamoja na maneno haya ya kuthibitisha na yenye nguvu, nafikiri kwamba kaburi la Ali (R.A) haliko Najaf. Wanachuoni wanatofautiana juu ya nukta hii. Baadhi wanasema liko kwenye Ikulu mjini Kufa; baadhi wanasema liko kwenye Kibla ndani ya Msikiti Mkuu wa Kufa; baadhi wanasema liko kwenye lango linalojulikana kama Ba-e-Kinda katika Msikiti wa Kufa; baadhi wanashikilia kwamba liko ndani ya Rahba huko Kufa; na bado wengine wanasema liko pembeni mwa kaburi la Fatima huko Baqi. Katika Afghanistan yetu, pia kuna sehemu karibu na Kabul inajulikana kama Kuba la Ali. Kutokana na maelezo fulani, mwili Mtukufu wa Ali uliwekwa kwenye Kasha na ukalazwa juu ya mgongo wa ngamia na ukapelekwa kuelekea Madina.

Kikundi cha watu kikanyakua lile kasha, wakidhania lina vitu vya thamani. Wakati wanalifungua, wakaona mwili ule Mtukufu, wakaule- ta Kabul, na ukazikwa katika sehemu hii. Ndio maana watu wanaitukuza sehemu hii.

Muombezi: Tofauti zilitokea kwa sababu ya maelezo ya wasia wake, ambao umeweka sharti kwamba matayarisho ya mazishi yake yatatize sehemu yake ya kuzikwa. Inasimuliwa na Imam Ja’far Sadiq kwamba katika wakati wake wa kufa, Amiru’l- Mu’minin alimwambia mtoto wake, Imam Hasan kwamba baada ya kumzika Najaf, ata- yarishe makaburi manne kwa ajili yake katika sehemu nne tofauti.
Katika Msikiti wa Kufa, katika Rahba, katika nyumba ya Ju’da Hira, na Ghira. Shia wanakubali kwamba kaburi lake tukufu liko Najaf. Chochote walichojifunza kutoka kwa Ahli Bait ni sahihi. Watu wa nyumba wanajua vizuri zaidi kuhusu kinachohusiana na nyumba yao.

Kwa hakika nawashangaa wanachuo wenu ambao wamezitelekeza simulizi za Kizazi cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika kila jambo. Hawakuuliza kuhusu mahala pa kaburi la baba kwa watoto wake wenyewe ili kuelewa ukweli. Ni hakika kabisa kwamba watoto wanajua zaidi kuhusu kaburi la baba yao kuliko wengine. Kama nadharia hizi za sasa zingekuwa sawsawa, Maimam Watukufu wangewajulisha wafuasi wao juu ya hilo.

Lakini wamelithibitisha mahala lilipo Najaf, wamezuru hiyo sehemu wao wenyewe, na wamewahimiza sana wafuasi wao kuizuru sehemu hiyo. Sibt Ibn Jauz katika kitabu chake “Tadhkira” amezitaja tofauti hizi. Anasema: Maoni ya sita ni kwamba liko Najaf katika ile sehemu inayojulikana sana, ambayo kwa kawaida hufanyiwa Ziara. Kwa yote yaliyojitokeza, haya ndio maoni ya sawasawa.”

Halikadhalika, wanachuo wenu wengine kama Khatibu-e-Khawarizmi katika “Munaqib,” Muhammad bin Shafi’i katika “Matalibus- Su’ul”, Ibn Abi’l-Hadid katika “Sharhe Nahaju’l-Balagha”, Firuzabadi katika “Qamus,” yake chini ya neno Najaf, na wengine, wameshikilia kwamba kaburi la Amirul’-Mu’minin liko Najaf.