read

Mkutano Wa Nne Jumapili Usiku 26 Rajab; 1345 A.H

Mjadala Kuhusu Uimamu:

Muombezi: Ninyi watu wema mnayo habari kwamba neno “Imam” lina maana nyingi. Kilugha lina maana ya “Kiongozi.” Imam al-Jama’at maana yake ni “yule mwenye kuongoza Sala za Jamaa.”

Anaweza pia kuwa kiongozi wa watu katika mambo ya siasa au ya kiroho. Imam al-Jum’a maana yake ni yule mtu mwenye kuongoza sala ya Ijumaa. Kwa hiyo, Sunni wafuasi wa madhehebu nne na sheria, wanawaita viongozi wao “Maimam” kama vile Imam Abu Harifa, Imam Maliki, Imam Shafi’i, na Imam Hanbal.

Wana-itiqadi na mafaqihi hawa ni viongozi wao katika mambo ya dini na wameweka Sheria za dini kwa mujibu wa utafiti wao au kwa mujibu wa kukisia kwao kuhusu uhalali wa matendo. Kwa hiyo wakati tunapovichunguza vitabu vya Fiqih vya Maimamu hawa wanne, tunakuta tofauti nyingi miongoni mwao zinazohusu misingi ya imani na Kanuni za utekelezaji wa imani.

Halikadhalika Madhehebu yote yana viongozi kama hao, na miongoni mwa Mashi’a, maulamaa na mafuqahaa wanashikilia nafasi kama hizo hizo.

Kwa kutoweka kwa Imam wetu wa zama aliye hai, wao wanatoa matamko ya kisheria kwa kutegemea elimu yao ya Qur’ani Tukufu, Hadithi sahihi za Mtume, na Maimamu wa kitume. Lakini hatuwaiti Maimamu kwa sababu Uimam ni wa washika makamu (wa Mtume) kumi na wawili peke yao - dhuria wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Kuna tofauti nyingine, Sunni baadae walifunga mlango wa ijtihad (juhudi ya kutafsiri sheria).

Kuanzia karne ya tano A.H wakati ambapo, kwa amri ya Mfalme, maoni yaliyoelezewa na Maulamaa na Mafuqhaa yalikusanywa, huu uitwao uimamu uliishilizwa kwa maimamu wanne. Na madhehebu manne (Hanafi, Maliki, Shafi’i, na Hanbali) yakaanzishwa. Watu walilazimishwa kufuata kati ya moja ya hiyo, kama ilivyo desturi kwa wakati huu wa sasa.

Haijulikani ni kwa misingi ipi kumfuata Imam mmoja kunapendekezwa. Sifa gani Imam wa Mahanafi alizonazo ambazo Imam wa Maliki hanazo? Ni sifa gani alizonazo Imam wa Shafi’i alizonazo ambazo Imam wa Hanbal hana.Na kama ulimwengu wa Kiislamu utalaz- imishwa wenyewe kufungwa kwenye kufuata moja ya Madhehebu manne, basi maendeleo ya Jumuiya ya Kiislamu yatakuwa yamefungwa kabisa, ingawaje kwamba Uislamu hutufundisha kwamba yatupasa kusonga mbele pamoja na nyakati.

Iufanya hivi, tunahitaji uongozi wa Maulamaa. Kuna mambo mengi ambayo haitupasi kufuata hukumu ya Mujtahidi aliyekufa. (Kuanzia Jihad, kujitahidi, humaanisha katika hali hii, mtu anayejitahidi kutafsiri na kuunda taratibu na Sheria, kwa vile Ijtihad inahusika kwenye njia ya kujitahidi), bali inapasa kumgeukia mujtahid aliye hai kwa ajili ya kupata mwongozo.
Mujitahidi wengi wamezaliwa baadae miongoni mwenu, ambao walikuwa na cheo cha juu katika elimu kuliko wale “Maimam wanne.” Sijui kwa nini upendeleo una- tolewa kwa wale waliopita ili kwamba si wengine ila wao tu waweze kufuatwa na haki za wengine kupuuzwa. Katika fiqih ya Shi’a, Mujtahid katika kila zama, mpaka wakati wa kujitokeza kwa Mtukufu Imam wa zama zetu, wao wanayo haki ya kufanya jitihada. Katika kuhusu matatizo mapya, hatuwezi kufuata hukumu ya Mujtahid aliyekufa.

Kuweka Mipaka Kwenye Madhehebu Manne Hakuna Msingi.

Ni ajabu kwamba mnawaita Mashi’a wazushi na waabudu wafu. Wao wanafuata amri za Maimamu kumi na wawili, dhuria wa Mtume (s.a.w.w.). Aidha haijulikani ni kwa misingi ipi mnajaribu kuwalazimisha Waislamu wawafuate Ashariyya au Mu’tazala kuhusiana na msingi (Usul) ya imani na mmoja kati ya Maimamu wanne katika sheria za matawi (Furu’) ya imani.

Wale ambao hawawafuati wanaitwa marafidhi. Kwa vile Abu’l-Hasan Ash’ari, Abu Hanifa, Malik bin Anas, Muhammad bin Idris Shafi’i, na Ahmad bin Hanbali walikuwa sawa na Maulamaa na mafaqihi wa Kiislamu wengine wengi, na kwa vile hakuna amri kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ya kuwafuata wao, mipaka ya kuwafuata wao tu yenyewe ni uzushi (bida’a). kama ningelileta madai haya, ungelisema nini katika kujibu?

Hafidh: Kwa vile Maimamu hawa walikuwa wana daraja ya juu ya utii kwa Allah, uchaji, ukweli, na uadilifu, pamoja na elimu kubwa mno ya Fiqih imekuwa lazima kwetu sisi kuwafuata.

Muombezi: Hatulazimiki na mantiki kujifunga sisi wenyewe kuwafuata wao peke yao. Wengi wa Maulamaa wenu wengine walikuwanazo sifa sawa kama hizi. Mpaka wa kuwafuata wao peke yao ni kebehi kwa Maulamaa wengine wenye sifa sawa na zao. Hatuwezi kulazimishwa kufuata mtu mmoja yeyote au watu wengine bila maelekezo ya kimamlaka kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Hakuna ruhusa kama hiyo kutoka kwa Mtume kuhusu Maimamu wenu wanne. Basi vipi muiwekee dini mpaka (kizuizi) kwenye madhe- hebu haya manne tu?

Ushi’a Kulinganishwa Na Madhehebu Manne.

Katika mikesha michache tu iliyopita uliyaita madhehebu ya Shi’a kuwa ni ya “kisiasa” na ukasema kwamba kwa vile hayakuwepo wakati wa Mtume - kwamba yalikujakuwepo wakati wa Ukhalifa wa Uthman - ilikuwa ni haramu kuyafuata. Usiku wa kabla ya jana tulithibitisha kwamba Ushi’a uliasisiwa wakati wa Mtume (s.a.w.w) kwa maelekezo yake mwenyewe.

Kiongozi wa Mashi’a, Amirul-Mu’minin Ali alilelewa na kufundishwa na Mtume tangu utotoni na kupata elimu yake ya dini kutoka kwake. Kwa mujibu wa riwaya zilizomo kwenye vitabu sahihi vyenu wenyewe, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amemwita yeye “Lango la Elimu.”

Kwa dhahiri kabisa alisema: “Utii kwa Ali ni utii kwangu, na kutomtii Ali ni kutomtii mimi.” Katika mkusanyiko wa watu 70,000 alimteua kuwa Amir na Khalifa, na akawaamrisha Waislamu wote, wakiwemo Umar na Abu Bakr, kula kiapo cha utii kwake.

Lakini haifahamiki ni vipi madhehebu yenu Manne yalivyokuja kuanzishwa, wala ni yupi kati ya Maimamu wanne aliyemuona Mtume au kama kuna ruhusa yoyote iliyosimuliwa kutoka kwa Mtume kuhusu wao ili angalau kuweza kueleza ni kwa nini Waislamu waweze kulazimika kuwafuata wao. Bila sababu za kukufungeni mnawafuata wakubwa zenu na hamusemi chochote cha kupasisha Uimamu wao isipokuwa tu kwamba walikuwa mujtahid wakubwa, watu wenye elimu na uchamungu.

Lakini, ikiwa sifa hizi zipo kwa kiwango cha juu sana katika kizazi cha Mtume, hivyo basi sio wajibu kwetu sisi kuwafuata wao? Hivi hizi madhehebu zisizo na kiungo na Mtume ndio za uzushi au Madhehebu iliyoasisiwa na Mtume na kuongozwa na dhuria wake ndiyo ya uzushi?

Katika njia hiyo hiyo, kuna Maimamu wengine kumi na mmoja, ambao kuhusu wao kuna Hadithi mbali mbali zinazoonyesha kwamba wao ndio wanaolingana na Qur’ani Tukufu. Katika Hadith al-Thaqalain imeelezwa wazi kwamba:
“Yeyote ambaye atashikamana na viwili hivi ataokolewa na yule ambaye atakaa mbali navyo amepotea. Katika “Hadithus- Safina.” Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Yule ambaye hukaa mbali navyo ataangamia na kupotea.” Ibn Hajar katika “Sawa’iq” (Bab-e-Wasiyyatu’n –Nabi, uk.135) ananukuu hadithi kutoka kwa Mtume isemayo kwamba: “Qur’ani na dhuria wangu ni dhamana zangu; kama mtashikamana wenyewe kwenye viwili hivi, kamwe hamtapotea.”

Kwa kuliunga mkono hili, Ibn Hajar ananukuu hadithi nyingine kutoka kwa Mtume kuhusu Qur’ani Tukufu na dhuria wake watoharifu: “Msivuke mipaka ya Qur’ani na dhuria wangu; wala msiwapuuze. Vinginevyo mtaangamizwa. Na msiwafundishe dhuria wangu kwa vile wao wanajua zaidi kuliko mlivyo ninyi.”

Baada ya hivi, Ibn Hajar akatoa maelezo kwamba, hadithi hizo hapa juu huthibitisha kwamba dhuria wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ni bora kuliko wengine wote katika elimu na katika kutekeleza wajibati za kidini.”

Maimamu Wanne Wa Kisunni Wametangazana Kuwa Makafiri.

Walakini hata hivyo, inashangaza kwamba, pamoja na kujua kwamba dhuria wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ni wabora kuliko wengine wote, Masunni wanamfuata Abu’l Hasan Ash’ari katika misingi ya dini na Maimamu wanne katika kanuni za utekelezaji wa Imani. Kufuata mwenendo huo ni kwa sababu ya ushabiki na kiburi. Na hata kama tukijaalia kuwa usemayo ni kweli, kwamba Maimamu wenu wanne wana haki ya ninyi kuwakubali kwa sababu walikuwa wanachuo na wachamungu, basi kwanini kila mmoja wao akamlaumu mwengine kwa ukafiri?

Hafidh: Wewe umkali sana. Unasema kila kinachokuja kwenye akili. Unawasingizia Maimamu wetu. Maelezo haya ni ya uwongo. Kama kuna kilichosemwa dhidi yao, ni kutoka kwa Maulamaa wa Kishi’a. Kutoka upande wetu hakuna chochote kilichosemwa dhidi yao. Tumeonyesha heshima kwao.

Muombezi: Ni dhahiri wewe hukusoma vitabu vya Maulamaa wako. Maulamaa wenu maarufu wenyewe wameandika vitabu vinavyohusu kukataa kwao. Hata hawa maimamu wanne wameshutumiana wenyewe kwa wenyewe kwa kukiuka sheria za dini.

Hafidh: Maulamaa hao ni akina nani? Nini maelezo yao?

Muombezi: Masahaba wa Abu Hanifa, Ibn Hajar (Ali bin Ahmad Andalusi aliyekufa 456 A.H.), na wengine wamekuwa kila mara wakiwasuta Imamu Maliki na Muhammad bin Idris Shafi’i. Kadhalika wafuasi wa Imam Shafi’i, kama Imamu’l-Haramain, Imam Ghazali na wengine wamemshutumu Abu Hanifa na Malik. Hebu ngoja nikuulize kitu: Hawa walikuwa watu aina gani – Imam Shafi’i, Abu Hamid bin Muhammad Ghazali, na Jarullah Zamakhshari?

Hafidh: Walikuwa Mafuqaha wakubwa, wanachuo wasomi, watu wachamungu, na Maimamu wetu.

Shutuma Za Maulamaa Wa Kisunni Kwa Abu Hanifa:

Muombezi: Imam Shafi’i amesema: “Hajapata kuzaliwa mtu wa kuchukiza katika Uislamu kama Abu Hanifa.” Vilevile amesema: “Nimeangalia katika vitabu vya wafuasi wa Abu Hanifa, na nikaona mna kurasa 130 zenye mambo yenye kukinzana na Qur’ani Tukufu na Sunna.”

Abu Hamid Ghazali katika kitabu chake “Manqul-fi Ilmi’l-Usul” anasema: “Kwa hakika Abu Hanifa amepotoa kanuni ya dini, kaifanya njia yake kuwa ya mashaka, amebadilisha mpangilio wake, na amechanganya sheria katika hali ambayo kanuni iliyoelezwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) imeharibika kabisa. Mtu mwenye kufanya hivyo makusudi na kuiona hiyo kuwa ni halali; ni kafiri. Mtu mwenye kuifanya na hali akijua, ni fasiq.

Kwa mujibu wa Mwanachuo huyu mkubwa, Abu Hanifa alikuwa ama yeye ni kafir au fasiq. Vitabu vingi vingine vinamshutumu Abu Hanifa. Jarullah Zamakshari, mwandishi wa “Tafsirul’al-Kashshaf” na mmoja wa Maulamaa wenu wachamungu, anaandika katika “Rabiu’l-Abrar” kwamba Yusufu bin Asbat alisema:

“Abu Hanifa alizikataa karibu Hadith 400 za Mtume wa Uislamu.” Yusufu akaeleza kwamba: “Abu Hanifa alisema: Lau Mtume wa Uislamu angenifahamu, mengi ya maneno yangu angeyakubali.”

Maulamaa wenu wenyewe wametoa shutuma za namna hiyo kwa Abu Hanifa na kwa hao Maimamu wengine watatu. Zinaweza kupatikana katika “Mutahawwal” cha Ghazali,

Nuqtush-Sharifa” cha Shafi’i, “Rabiu’l-Abrar” cha Zamakhshari, na “Muntazim” cha Ibn Jauz. Imam Ghazil anasema katika “Mutahawwal” yake: “Kuna makosa mengi katika vitabu vya Abu Hanifa. Hakuwa na elimu ya balagha, nahau, au hadith.” Vilevile anaandika: “Kwa vile hakuwa na elimu ya hadith, alitegemea juu ya kukisia mwenyewe. Kiumbe wa kwanza aliyetenda kwa kukisia alikuwa ni Shetani.”

Ibn Jauzi anaandika katika “Muntazim” yake: “Ulamaa wote wameungana katika kumshutumu Abu Hanifa. Kuna Makundi matatu ya wakosoaji kama hao: kundi moja linashikilia kwamba imani yake katika misingi ya Uislamu ilikuwa haina uhakika; kundi lingine linasema kwamba, hakuwa na kumbukumbu imara na hakuweza kukumbuka hadith; kundi la tatu linaamini kwamba alitenda kwa kukisia na kwamba maoni yake yalikuwa siku zote tofauti na hadith za kweli.”

Maulamaa wenu wenyewe wemewalaumu Maimamu wenu. Maulamaa wa Kishi’a hawakuwahusisha na chochote, isipokuwa kile Maulamaa wenu wenyewe walichosema kuhusu wao.

Kwa upande mwingine, hakuna tofauti ya maoni miongoni mwa Ulamaa wa Kishi’a kuhusiana na nafasi za hao Maimamu kumi na mbili.

Tunawaona Maimamu watukufu kama wanafunzi wa fundisho moja. Maimamu hawa - wote walitenda kwa mujibu wa sheria za Ki-Mungu ambazo yule mwisho wa Mitume aliwapa. Kamwe hawakutenda kwa kukisia au kuafiki uzushi. Walichosema au kufanya kilikubaliana na maneno ya Mtume. Hivyo, hakukuwa na tofauti miongoni mwao.

Uimam Kwa Mujibu Wa Shi’a Una Maana Ya Uwakilishi Wa Allah.

Kwa mujibu wa ufafanuzi uliotolewa na Maulamaa, Uimamu au Uwakilishi wa Allah, ni moja ya misingi ya Uislamu. Tunaamini kwamba Uimamu ni uwakilishi wa Allah kwa viumbe wote na Khilafat-e-Rasul (Makamu/warithi wa Mtume) kwa ulimwengu huu na ujao.

Kwa hiyo, ni wajibu kwa wanadamu wote kufuata wapangaji wake katika mambo yote, ya kidunia na hali kadhalika ya kiroho.

Sheikh: Ingelikuwa vizuri kama usingelitamka kidhahiri kwamba Uimamu umeingizwa katika misingi ya imani, kwa vile Maulamaa wakubwa wa Uislamu wanakataa kuwekwa kwake humo. Umewekwa katika shuruti za matendo ya imani. Maulamaa wenu wameufanya sehemu ya misingi.

Muombezi: Maelezo yangu haya, hayakomei kwenye Imam wa Mashi’a tu. Hata Maulamaa wenu wakubwa wanayo imani kama hiyo. Mmoja wao ni mfasiri wenu mashuhuri Qadhi Baidhawi, ambaye anasema katika kitabu chake “Minhaju’l-Usul” kuhusiana na mjadala juu ya masimulizi ya Hadithi: “Uimamu ni moja ya kanuni za msingi za imani, ambazo kuzikataa na ukinzano juu yake hupelekea kwenye ukafir na uzushi.”

Mulla Ali Qushachi anasema katika kitabu chake “Sharh-e-Tajrid.” Uimamu kwa jumla ni Uwakala wa Allah kwa mambo yote ya ulimwengu huu na dini, kama Ukhalifa wa Mtume.” Na Qadhi Ruzbahan, mmoja wa washupavu mno (Shabiki) wa Maulamaa wenu anaashiria kwenye maana hiyohiyo.

Anasema: “Uimamu kwa mujibu wa wafuasi wa Abu’l-Hasan Ash’ari ni uwakilishi wa Mtume wa Uislamu kwa ajili ya kuimarisha imani na kulinda salama maslahi ya Jumuiya ya Kiislamu. Wafuasi wote wanafungwa katika wajibu wa kufuata maamrisho yake.”

Ungekuwa Uimamu sio sehemu ya shuruti za matendo ya imani, Mtume asingesema kwamba: “Yeyote yule anayekufa bila kujua Imamu wake wa zama, anakufa kifo cha kijahilia.”

Hii imenukuliwa na Maulamaa wenu maarufu, kama Hamidi katika “Jam’i-Bainus- Sahihain” na Mulla Sa’d Taftazani katika “Sharhe Aqa’id-e-Nasafi.” Kutoelewa sharti hata moja la utekelezaji wa imani hakuwezi kuwa sawa na ujinga ulioelezwa na Baidhawi kuhusu kutokujua misingi, yaani kwamba ujinga wake ni sababu ya ukafir.

Kwa hiyo Uimamu ni moja ya misingi ya imani na ni hatua ikamilishayo Utume. Kwa ajili ya hiyo, kuna tofauti kubwa kati ya dhana ya Uimamu wetu na ile inayotafsiriwa na ninyi.

Mnawaita Maulamaa wenu Maimamu, kama vile Imam Adhma, na Imam Maliki. Lakini hii ni maana ya mdomo. Sisi pia tunatumia neno Imam-e-Juma’a, Imam-e-Ja-ma’at.

Hivyo wanaweza wakawepo mamia ya Maimamu kwa wakati mmoja, lakini katika maana ya kitaalamu (kiistilahi) ambayo kwayo tunatumia neno “Imam,” ina maana muwakilishi wa Allah. Katika maana hii kuna Imam mmoja tu kwa wakati mmoja. Sifa bora za elimu, Maadili, ushujaa, upenzi kwa Allah, na uchamungu zimekamilishwa ndani yake.

Anawashinda binadamu wote katika tabia zote na hushikilia hali ya kutofanya makosa. Dunia haitakuwa bila Imam wa aina hiyo mpaka siku ya malipo. Imam wa ubora kama huo anakuwa katika kiwango cha juu kabisa cha mafanikio ya kiroho. Imam kama huyo anaidhinishwa na Allah na anateuliwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Hushinda viumbe wote pamoja na Mitume waliopita.

Hafidh: Kwa upande mmoja unawashutumu Maghulat, na kwa upande mwingine wewe mwenyewe kiububusa unawasifu Maimamu na kuiona nafasi yao ya juu zaidi kuliko ile ya Mitume. Akili ya kawaida inalikataa hili, na Qur’ani Tukufu vilevile imeeleza kwamba Mitume wamewekwa katika nafasi ya juu zaidi. Nafasi yao iko baina ya uhuru wa ki-ungu na lile lenye kuwezekana. Kwa vile maelezo yako hayaungwi mkono na akili, hayawezi kukubaliwa.

Cheo Cha Uimam Ni Juu Zaidi Kuliko Cha Utume Wa Kawaida.

Muombezi: Bado hujaniuliza ni kwa misingi ipi nimeyatoa maelezo haya, na kwa hiyo unasema ni ya bila hekima. Ushahidi mzuri kwa maelezo yangu ni Qur’ani Tukufu, ambayo ikizungumzia maisha ya Mtume Ibrahim, inasema kwamba, baada ya kumpa mitihani mitatu (ya maisha, mali, na watoto), Allah alikusudia kufanya cheo chake cha juu zaidi. Kwa vile Utume na Cheo cha Khalil (Rafiki) havikuruhusu dhahiri cheo cha juu, nafasi ya Uimamu ndiyo iliyokuwa nafasi pekee ya Cheo cha juu ambayo hata Mtume wa Allah anaweza kuaminishwa. Qur’ani Tukufu inasema: “Na wakati Mola Wake alipomjaribu Ibrahim na maneno fulani, aliyatekeleza.

Alisema:

قَالَ إِنِّي جَاعِلُكَ لِلنَّاسِ إِمَامًا ۖ قَالَ وَمِنْ ذُرِّيَّتِي ۖ قَالَ لَا يَنَالُ عَهْدِي الظَّالِمِينَ {124}

“Hakika nitakufanya Imam wa watu. Ibrahimu akasema: Na dhuria wangu? Akasema ahadi yangu haiwafikii madhalimu.” (2:124).

Aya hii ambayo inaonyesha nafasi ya Uimamu, pia inathibitisha kwamba cheo cha Uimamu ni cha juu kuliko cha Utume. Kwa vile nafasi ya Mtume Ibrahimu ilinyanyuliwa kutoka Utume kwenda Uimamu.

Hafidh: Hii ina maana, kwa mujibu wa maelezo yako, ni kwamba nafasi ya Ali ilikuwa ya juu kuliko ile ya Mtume wa Mwisho. Hivi ndivyo Maghulat walivyoamini, kama wewe mwenyewe ulivyokiri.

Mitume Wa Kawaida Na Wale Maalumu:

Muombezi: Sina maana ya hivyo ulivyohitimisha wewe. Kama ujuavyo kuna tofauti kubwa kati ya Utume wa kawaida na Utume maalumu. Cheo cha Uimamu ni cha juu zaidi kuliko cheo cha Utume wa kawaida, lakini kiko chini kuliko cha Utume Maalumu. Mtume wa mwisho ndiye kiwango cha hali ya juu cha utume maalum.

Nawab: Nisamehe kwa kuingilia kwangu. Je; Mitume wote hawakutumwa na Allah? Hapana shaka wote wana cheo kile kile. Qur’ani Tukufu inasema: “Hatutofautishi baina ya yeyote kati ya Mitume.” (2:285). Basi kwanini umetofautisha baina yao na ukagawa Utume katika makundi mawili; kawaida na maalumu?

Muombezi: Hakika, Aya hii ni kweli iko sawa sawa katika fuo lake. Yaani, kwa kiasi kufanikisha lengo la Utume kuhusikavyo (ambako kuna maana ya kufundisha watu kuhusu kuwepo kwa Allah. Siku ya Malipo na kuzifunza akili zao), Mitume wote kutoka Adamu mpaka mwisho wa Mitume, wako sawa. Lakini wanatofautiana katika sifa, mafanikio na cheo.

Tofauti Katika Daraja Za Mitume.

Je, Mtume ambaye ametumwa kuongoza watu 1,000 ni sawa na yule aliyepelekwa kuongoza watu 30,000, au kwa yule aliyetumwa kuongoza wanadamu wote? Hebu tuchukue mfano. Hivi, Mwalimu wa wanafunzi wa darasa la kwanza ni sawa na Mwalimu wa darasa la nne?

Je, Walimu wa madarasa ya juu ni sawa na Maprofesa au Walimu wa Chuo Kikuu? Wote wako katika Utawala mmoja na kufanya kazi chini ya mpango mmoja wa jumla, lengo lao likiwa kuelimisha wanafunzi. Bado, kwa kuzingatia elimu ya Walimu hao, hawako sawa.

Kila mmoja yuko tofauti na mwingine kwa mujibu wa kisomo, uwezo, na mafanikio yake. Kwa mtazamo wa lengo la Utume, Mitume wote wa Allah wako sawa sawa. Walakini, kwa sababu ya tofauti katika daraja na elimu, wako tofauti. Qur’ani Tukufu inasema:

تِلْكَ الرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۘ مِنْهُمْ مَنْ كَلَّمَ اللَّهُ ۖ وَرَفَعَ بَعْضَهُمْ دَرَجَاتٍ ۚ{253}

Tumewafanya baadhi ya Mitume kuwazidi wengine; Miongoni mwao wako ambao Allah amesema nao, na baadhi yao Amewatukuza kwa (vyeo vingi) daraja.” (2: 253).

Mwanachuo wenu wenyewe Jarullah Zamakshari anasema katika kitabu chake, “Tafsir-e- kush-Shaf” kwamba, Aya hiyo hapo juu ina maana Mtume wetu alikuwa bora katika daraja kwa wengine wote kwa sababu ya sifa zake maalumu, muhimu zaidi ni ambayo kwamba alikuwa wa mwisho wa Mitume.

Nawab: Nimefurahi umelitatua tatizo hili, lakini nina swali lingine, ingawa kwa namna nyingine halihusiki hapa. Tafadhali tueleze kwa ufupi sifa makhususi za Utume maalumu.

Muombezi: Kuna sifa nyingi za pekee kwa Utume Maalumu, na kuna sababu nyingi mno zinazothibitisha vipi Mtume mmoja kati yao wote ndiye Mtume maalum wa Allah. Kwa hakika hatua hiyo huishiliza duru la Utume.

Lakini mikutano hii haikupangwa kuthibitisha Utume wa Allah kwa Waislamu. Kama ingekuwa tuijadili nukta hii kikamilifu, tungetoka nje ya nukta yetu ya Uimamu. Walakini kwa ufupi hata hivyo, nitajadili nukta hii.

Sifa Za Utume Maalum:

Ukamilifu wa ubinadamu umo katika ukamilifu wa nafsi. Ukamilifu wa kimaadili na kiroho hauwezi kufikiwa bila kutakasa nafsi. Ukamilifu huu hauwezekani mpaka mtu aongozwe kwa uwezo wa hekima. Hapo ndipo mtu ataweza kupanda juu na juu zaidi pamoja na nguvu ya elimu na utendaji sahihi mpaka anafikia kilele cha ubinadamu, kama ilivyoelezwa na Ali.

Yeye alisema: “Mtu aliumbwa na uwezo wa kuongea ambayo ni asili ya ubinadamu. Kama mazungumzo yamepambwa na elimu na vitendo, hufanana na kuwepo ufalme wa ki-mbinguni ambao ndiyo asili ya kuumbwa kwa mwanadamu.

Wakati mazungumzo yake yanapofikia pahala pa kujizuia na yanaondokana na mata yote ya maumbile, inakuwa moja pamoja na ufalme wa ki-mbinguni. Kisha huachana na ulimwengu wa kihayawani na kufikia hatua ya juu sana ya ubinaadamu.”
Uwezo wa mtu wa kuzungumza humfanya bora kwa viumbe vyote. Lakini kuna sharti moja lililoambatanishwa kwalo, kwamba uisafishe nafsi yake na uchafu wote kwa elimu na matendo sahihi. Sehemu hizi mbili ndani ya mtu ni kama mbawa mbili za ndege, ambaye huruka juu angani kutokana na nguvu za mbawa zake.

Hivyo hivyo kiwango cha mtu cha mafanikio ya ubinadamu hupanda kutokana na elimu yake na matendo sahihi. Kuvuka mipaka ya hali ya kinyama na kufikia nyanja ya matendo ya kibinadamu hutegemea juu ya ukamilifu wa nafsi. Mtu ambaye hukusanya ndani yake stadi za elimu na matendo sahihi na akafikia thuluthi ya tabaka tatu za watu (watu wa kawaida, watu bora na watu bora zaidi), hufikia daraja la chini kabisa la Utume. Wakati mtu kama huyo anapokuwa shabaha ya hisani maalumu za Allah, anakuwa Mtume.

Naam, kwa kweli Utume vilevile una daraja tofauti. Mtume anaweza kufikia daraja ya juu zaidi katika tabaka hizi tatu. Cheo hiki ni cha juu sana katika nyanja ya uwezekano, ambayo wenye busara (wataalamu) huiita Hekima ya Kwanza, na ambayo ni Athari ya Kwanza au Matokeo ya Mwanzo. Hakuna cheo cha juu kama hiki katika miliki ya viumbe.

Nafasi hii imeshikwa na wa mwisho wa Mitume, ambaye ni wa kwanza, hakuna kama yeye isipokuwa kile Chanzo cha Awali. Wakati Mtume alipopandishwa kwenye daraja hii ya juu zaidi, Utume ulikomelezwa. Uimamu ni daraja la chini kuliko daraja ya juu zaidi ya utume, lakini ni hatua ya juu kuliko daraja zote nyingine za Utume. Kwa vile Ali alipandishwa kwenye hatua ya juu kuliko ya Utume na alikuwa mmoja katika nafsi pamoja na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), aliaminishwa kazi ya Uimamu na hivyo kuwa mbora kwa Mitume wote waliopita.

Hafidh: Sehemu ya mwisho ya maneno yako inachanganya. Kwanza, unasema Ali alikuwa katika ngazi ya Utume, pili, kwamba alikuwa nafsi moja na Mtume Muhammad, tatu, kwamba alikuwa bora kwa Mitume mingine. Nini hoja zako kuthibitisha ukweli wa maneno yako?

Hoja Za Cheo Cha Utume Kwa Ajili Ya Ali Kutoka Kwenye Hadith Manzila.

Muombezi: Kwamba Ali amepata cheo cha Utume yaweza kuthibitishwa kwa kurejea kwenye hadith ya Manzila (Hadith inayohusu vyeo), ambayo imesimuliwa kwa kauli moja kwa kadri ya maneno yanayofanana. Wa mwisho wa Mitume watukufu amerudia mara nyingi na katika mikusanyiko tofauti. “Je, huridhiki kwamba kwangu wewe ni kama Harun alivyokuwa kwa Musa, isipokuwa tu kwamba hakutakuwa na Mtume baada yangu?” Na wakati mwingine aliwaambia wafuasi wake. “Ali kwangu mimi ni kama alivyokuwa Hauna kwa Musa.”

Hafidh: Usahihi wa hadith hii haukuthibitishwa. Hata kama ingethibitishwa kuwa ni kweli itakuwa ni simulizi pekee na kwa hiyo haikubaliki.

Usahihi Wa Hadith Ya Manzila Kutoka Kwenye Rejea Za Kawaida.

Muombezi: Katika kutoa taarifa kuhusu usahihi wa hadith hii, nitarejea kwenye vitabu vyenu. Hii sio simulizi ya pekee. Imethibitishwa na maulamaa wenu mashuhuri, kama Suyuti, Hakim Nishapuri, na wengine, ambao wamethibitisha kutegemeka kwake kwa vyanzo vinavyokubaliwa kwa pamoja. Baadhi yake ni hivi vifuatavyo:

(1) Abu Abdullah Bukhari katika Sahih yake Juz. 111, Kitab Ghazawa, gahazawa Tabuk; uk. 54, na ndani ya kitabu chake “Bida’u’l-Khalq”, uk. 180;
(2) Muslim bin Hajjaj katika Sahih yake iliyochapishwa Misri, 1290 A.H. Juz. 11, chini ya kichwa cha habari, “Ubora wa Ali;” uk. 236-7;
(3) Imam Ahmad bin Hanbal katika Musnad Juz. 1 “Sababu za kutoa jina la Husain”, Uk. 98, 118, 119 na maelezo chini ya kurasa ya kitabu hicho hicho, Sehemu ya 5 uk. 31;
(4) Abu Abdu’r-Rahman Nisa’i katika “Khasa’isi’l-Alawiyya” uk. 19;
(5) Muhammad bin Sura Tirmidhi katika Jami’ yake;
(6) Hafidh Ibn Hajar Asqalani kati- ka “Isaba.” Juz. 11, uk. 507;
(7) Ibn Hajar Makki katika “Sawa’iq Muhriqa” Sura ya 9, Uk. 30& 34;
(8) Hakim Abu Abdullah Muhammad bin Abdullah Nishapuri katika “Mustadarak”, Juz. 11, Uk. 109;
(9) Jalalu’d-Din Suyuti katika “Tarikhu’l-Khulafa” uk. 65;
(10) Ibn Abd Rabbih katika “Iqdu’l-Farid” Juz. 11, uk. 194;
(11) Ibn Abdu’l-Birr katika “Isti’ab”, Juz. 11, uk. 473;
(12) Muhammad bin Sa’d Katib Waqidi katika “Tabaqatu’l-Kubra;”
(13) Imam Fakhru’d-Din Radhi katika “Tafsir Mafatihu’l-Ghaib”;
(14) Muhammad bin Jarir Tabari katika “Tafsir” yake, na pia katika “Tarikh” yake;
(15) Seyyed Mu’min Shablanji katika “Nuru’l-Absar”, uk. 68;
(16) Kamalu’d-Din Abu Salim Muhammad bin Talha Shafi’i katika “Matalibus-Su’ul”, uk. 17;
(17) Mir Seyyed Ali bin Shahabu’d-Din Hamadani katika “Mawaddatu’l-Qubra”, kuelekea mwisho wa Mawadda 7;
(18) Nuru’d-Din Ali bin Muhamma Maliki Makki, ajulikanaye kwa jina la Ibn Sabbagh Maliki katika “Fusulu’l Muhimma” uk. 23 na 125;
(19) Ali bin Burhanu’d-Bin Shafi’i katika “Siratu’l-Halabiyya” Juz. 11, uk, 49;
(20) Sheikh Sualyman Balkh Hanafi katika “Yanabiu’l-Mawadda”,
(21) Mulla Ali Muttaqi katika “Kanzu’l-Ummal”, Juz. VI, uk. 152 –153;
(22) Ahmad bin Ali Khatib katika “Ta’rikh Baghdad”;
(23) Ibn Maghazili Shafi’i katika “Manaqib”;
(24) Muwaffaq bin Ahmad Khawarizmi katika “Manaqib”;
(25) Ibn Jazari Ali bin Muhammad katika “Usudu’l-Ghaiba”;
(26) Ibn Kathir Damishqi katika “Tarikh” yake;
(27) Ala’u’d- Daula Ahmad bin Muhammad katika “Urwatu’l-Wuthqa”;
(28) Ibn Athir Mubarak bin Muhammad Shaibani katika “Jami’ul’-Usul”;
(29) Ibn Hajar Asqalani katika “Tahdhibut- Tahdhib”;
(30) Abu’l-Qasim Husain bin Muhammad Raghib Isfahani katika “Muhadhiratu’l-Udaba”; Juz. 11, uk. 212.

Maulamaa wenu wengi wengine wakubwa wameisimuliwa hadith hii muhimu pamoja na tofauti kidogo ya maneno kutoka kwa Masahaba wengi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kama vile:

(1) Umar bin Khattab,
(2) Sa’d bin Ali Waqqas
(3) Abdullah bin Abbas;
(4) Abdulllah bin Mas’ud;
(5) Jabir bin Abdullah Ansari,
(6) Abu Huraira;
(7) Abu Sa’id Khurdri;
(8) Jabir bin Sumra;
(9) Maliki bin Huwairi’s,
(10) Bara’a bin Azib;
(11) Zaid bin Arqam;
(12) Abu Rafi;
(13) Abdullah bin Ubai;
(14) Abu Suraiha,
(15) Hudhaifa bin Assad,
(16) Anas bin Malik,
(17) Abu Huraira Aslami,
(18) Abu Ayyub Ansari,
(19) Sa’id bin Musayyab
(20) Habib bin Abi Thabit,
(21) Sharhbil bin Sa’d;
(22) Ummi Salma (Mke wa Mtume);
(23) Asma bint Umais, (Mke wa Abu Bakar);
(24) Aqil bin Abi Talib
(25) Muawiyya bin Abu Sufyan, na wengi wa Sahaba wengine.

Kwa ufupi wote hawa wameisimuliwa pamoja na tofauti kidogo ya maneno kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Ewe Ali, wewe uko kwangu mimi kama Harun alivyokuwa kwa Musa, isipokuwa kwamba hakutakuwa na Mtume baada yangu.”
Je, Maulamaa wote hawa wakubwa – na kuna wengi sikuwataja – hawatoshi kuthibitisha kwamba hadithi hii imekubaliwa kwa pamoja kuwa ya kweli? Je, utathibitisha sasa kwam- ba ulikuwa katika kutokuelewa?

Kwa vile unachukua mwelekeo wa wasiwasi kuhusu ukweli wa hadith hii, yakupasa uangalie katika Kitabu “Kifayatut-Talib fi Manaqib-e-Ali Bin Abu Talib,” Sura ya 7, kilichoandikwa na Muhammad bin Yusuf Ganji Shafi’i, ambaye ni mmoja wa Maulamaa wenu Maarufu mno wa madhehebu yenu. Baada ya kunukuu hadith sita zenye kumtukuza Ali, mwandishi huyu akaisherehesha (uk.149) hadith hii kama ifuatavyo:

“Hii ni hadithi ambayo usahihi wake umekubaliwa na wote. Imesimuliwa na Maimamu wenye elimu zaidi na Huffadh (wajuao Qur’ani Tukufu kwa moyo), kama vile Abu Abdullah Bukhari katika Sahih yake, Muslim bin Hajjaj katika Sahih yake, Abu Dawud katika Sunan yake, Abu Isa Tirmidhi katika Jami’ yake, Abu Abdu’r-Rahman katika Sunan yake, Ibn Maja Qazwini katika Sunan yake. Wote hawa kwa pamoja wamekubali usahihi wake. Hakim Nishapuri amesema kwamba hadith hii imeingia katika hatua ya Mutawatir.”

Nina hakika kwamba sihitaji kutoa ushahidi zaidi kuonyesha kwamba hadith hii ni Sahihi.

Hafidh: Mimi sikukosa maadili ya kidini, hivyo siwezi kukataa mantiki yako ya kiakili, lakini hebu vuta mazingatio kwenye kauli ya mwanachuo na mwana itikadi mkubwa, Abu’l-Hasan Amadi, ambaye ameikataa hadith hii.

Muombezi: Nashangaa kwa nini mtu mwenye elimu kama wewe, baada ya kusikia maoni ya Maulamaa wako mashuhuri, utaamini taarifa ya mtu muovu ambaye alikuwa hata kuswali haswali.

Sheikh: Mtu yuko huru kuelezea imani yake. Kama mtu akielezea maoni yake, haitupasi sisi kumkashifu. Haipendezi kwa wewe kumzulia uongo badala ya kutoa majibu yenye mantiki kwenye maelezo yake.

Muombezi: Umenielewa vibaya. Simlaumu mtu yeyote kinyume cha haki. Si kuwa ninaishi katika wakati wa uhai wa Amadi. Maulamaa wenu wenyewe wameelezea kwamba alikuwa ni mtu aliyekuwa hana dini.

Sheikh: Ni wapi ambapo Ulamaa wetu wamesema kwamba alikuwa ni mtu asiyekuwa na dini?

Amadi Haaminiki Kama Msimuliaji Wa Hadithi.

Muombezi: Ibn Hajar Asqalani ameandika katika Lisanu’l-Mizan: “Saif Amadi Mutakallim Ali bin Abi Ali, mwandishi, alifukuzwa kutoka Damascus kwa sababu ya maoni yake yasiyokuwa ya kidini, na ni kweli kwamba alikuwa hasali.”

Na Dhahabi, ambaye pia ni mmoja wa Maulamaa wenu Maarufu, ameandika hivyohivyo katika “Mizanu’l-Itidal.” Amesema kwamba Amadi alikuwa mzushi. Kama Amadi asingekuwa muovu na mzushi asiyekuwa na dini, asingeweza kutoa maneno ya kashfa kuhusu Sahaba wote wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.), ikiwa ni pamoja na Khalifa wenu wenyewe, Umar bin Khatab (mmoja wa wasimuliaji wa hadithi hii). Sio haki kabisa kwamba mnawaona Mashi’a kuwa na taksiri kwa sababu ya kutokubali hadith zilizoandikwa katika “Sihah.” Kama hadithi imetolewa kutoka vyanzo sahihi, inakubaliwa hata kama iko kwenye “Sihah.” Lakini hadithi iliyothibiti, ambayo imeandikwa na Bukhari, Muslim, na waandishi wengine wa “Sihah” inakataliwa na Amadi, hamuoni taksiri kwayo.

Kama unataka kujua kwa ukamilifu hoja zinazohusu usahihi na vyanzo vya hadith hii kutoka kwenye maandishi ya Maulamaa wenu, na kama uko tayari kuwalaumu watu kama Amadi, unaweza ukaangalia jalada za “Abaqatu’l-Anwar”, zilizoandikwa na mwanachuo mkubwa na mfasiri, Allama Mir Seyyed Hamid Husain Dihlawi.

Yakupasa uangalie hususan hadith ya Manzila ili uweze kujua kwamba vipi mwanachuo huyu mkubwa wa Kishi’a alivyokusanya vyanzo kutoka kwa wanachuo wenu wa Shariah na wakathibitisha kutegemeka kwa hadhi hii.

Hafidh: Umesema kwamba mmoja wa wasimuliaji wa Hadithi hii alikuwa Umar bin Khattab. Ningetaka kujua zaidi kuhusu habari hii.

Kuthibitishwa Hadith Ya Manzila Na Umar Bin Khattab.

Muombezi: Abu Bakar Muhammad bin Ja’afaru’l-Mutiri na Abu’l-Laith bin Muhammad Samarqandi Hanafi, katika vitabu vyao, Majalis, Muhammad bin Abdu’r-Rahman Dhahabi katika “Riadhu’n-Nadhara”, Mulla Ali Muttaqi katika “Kanzu’l-Ummal” na wengine, wamesimulia kutoka kwa Ibn Abbas akisema kwamba siku moja Umar bin Khattab alisema: “Liache jina la Ali (yaani usimzungumze Ali sana kwa ubaya) kwa sababu nimesikia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akisema kwamba Ali alikuwa na sifa tatu.

Kama ningekuwa na moja kati ya sifa hizi, ningeihifadhi zaidi kuliko kitu chochote kifikiwacho na mwanga wa jua juu yake. Siku moja mimi; Abu Bakar, Abu Ubaida Jarra na baadhi ya Sahaba wengine tulikuwepo, na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa amepumzika kwa kumuegemea Ali bin Abu Talib. Alipiga bega la Ali na kusema: “Ali! Kiasi imani inavyohusika, wewe ni wa kwanza wa Waumini wote, na kiasi Uislam unavyohusika, wewe umechukua nafasi ya kuongoza!’

Kisha akasema: ‘Ali! Uko kwangu mimi kama alivyokuwa Harun kwa Musa. Na ni muongo ambaye anafikiri ni rafiki yangu kama yeye ni adui yako.”

Je, inaruhusiwa katika imani yenu kukataa maneno ya Khalifa Umar? Kama hairuhusiwi, kwa nini unaamini taarifa za ajabu za mtu kama Amadi?

Nafasi Ya Simulizi Pekee Katika Madhehebu Ya Sunni.

Ningali bado sijajibu moja ya madai yako. Umesema kwamba hadith hii ni simulizi pekee, na kwa ajili hiyo haikubaliki. Kama tukisema kitu hicho kwa mujibu wa mtindo wa watu ambao tunao katika maoni, tutakuwa wenye haki. Lakini inanishangaza kusikia kitu hiki kutoka kwako, kwa sababu katika madhehebu yenu hata simulizi pekee inatosha kuthibitisha ukweli wa jambo.

Kama mtu akikataa kukubali usahihi wa simulizi pekee, kwa mujibu wa maulamaa wenu atakuwa si muumini. Maliku’l-Ulama Shahabu’d-Din Daulatabadi amesema katika “Hidayatu’S-Sa’da”: “Kama mtu anakataa kukubali riwaya pekee au rai na akasema kwamba haikubaliki, huyo ni kafir.

Kama akisema simulizi pekee hii sio sahihi, na rai hii haikuthibiti, atakuwa mtenda kosa, sio kafir.

Hafidh: Tumetoka kwenye mada yetu ya msingi. Tafadhali hebu tueleweshe ni vipi utaweza kuthibitisha kwa Hadith hii ya Manzila kwamba Ali alishika cheo cha Utume.

Sifa Za Ali.

Muombezi: Hadith hii inathibitisha kwamba Ali anazo sifa tatu:

(1) Cheo cha Utume.
(2) Cheo cha Mrithi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.); na
(3) Nafasi yake ya juu miongoni mwa Sahaba wote wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Kama alivyo Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), wafuasi wa Ali walimfananisha na Harun, ambaye alikuwa Mtume, aliwekwa kuwa Khalifa wa Musa, na alikuwa mbora juu ya Bani Israel wote.

Nawab: Harun alikuwa Mtume?
Muombezi: Ndiyo.
Nawab: Unaweza kuonyesha Aya kutoka kwenye Qur’ani yenye kuunga mkono nukta hii?

Muombezi: Allah ameutaja Utume wake katika Aya nyingi. Anasema: “Hakika tumekuletea wahyi kama tulivyompelekea wahyi Nuh na manabii baada yake. Na tulimpelekea Ibrahim na Ismail na Is’haq na Yakub na makabila; na Isa na Ayub na Yunus na Harun na Suleiman na Daud tukampa Zaburi.” (4:163)

Na halafu tena Anasema: “Na mtaje Musa katika Kitabu, hakika yeye alikuwa mwenye kusafishwa, na alikuwa Mtume, Nabii. Na tukamwita upande wa kulia wa mlima, na tukamsongeza kuzungumza naye kwa siri. Nasi tukampa katika rehema zetu nduguye Harun, Nabii.” (19:51-53)

Hafidh: Hivyo kwa mujibu wa hoja yako, Muhammad na Ali wote walikuwa Mitume.
Muombezi: Mimi sikuelezea katika njia unayoelezea wewe. Kwa kweli wewe mwenyewe unajua kwamba kuna tofauti kubwa ya maoni kuhusu ni Mitume wangapi walikuwepo. Baadhi wanadai kwamba walikuwepo 120,000 - au hata zaidi.

Lakini wote hao katika nyakati zao husika walikuwa wamegawanyika katika makundi na walikuwa (daraja ya) chini kwa Mtume mkuu ambaye kwake kilifunuliwa kitabu kitukufu kikiwa na sheria mpya za dini. Watano miongoni mwao walikuwa ni Mitume wakuu: Nuh, Ibrahim, Musa, Isa, na mwisho wa Mitume wote, Muhammad, ambaye cheo chake kilikuwa ndio cha juu zaidi.

Harun alikuwa mmoja wa wale Mitume ambao hawakuwa wa kudumu au wa kujitegemea. Alikuwa chini ya Sharia (mfumo wa kidini) ya ndugu yake Musa. Ali alifikia cheo cha Utume lakini hakupandishwa kwenye cheo hicho cha Mtume kwa asili yake yenyewe kwa vile alikuwa chini ya Shari’a ya Muhammad.

Katika hadith hii ya Manzila, madhumuni ya Mtume yalikuwa ni kuwaambia watu kwamba, kama vile ambavyo Harun amefikia Cheo cha Utume lakini alikuwa chini ya Musa, Ali alifikia cheo cha Utume. Uimamu ulipasishwa kwake, lakini alikuwa chini ya Muhammad (s.a.w.w.).

Umuhimu Wa Cheo Cha Ali.

Katika Sharhe yake juu ya Nahju’l-Balagha, Ibn Abi’l-Hadid anasema kuhusiana na hadith hii kwamba kwa kutaja cheo cha Harun katika kumlinganisha na Musa, Mtume alionyesha kwamba Ali bin Abu Talib alishika cheo hicho. Vivyo hivyo, Muhammad bin Talha Shafi’i, katika “Matalibus-Su’ul”, uk. 19, baada ya kuelezea cheo na nafasi ya Harun, anasema: “Maana hasa ya jambo hili ni kwamba, nafasi ya Harun katika kuhusiana na Musa ilikuwa kwamba Harun alikuwa ndugu yake, muwakilishi wake, mshirika katikaUtume, na wasii wake au Mshika Makamu wakati Musa alipokuwa safarini.

Mtukufu Mtume wa Allah (s.a.w.w.) alikuwa vilevile katika hadith hii alionyesha kwamba, Ali alikuwa nayo nafasi ile ile kama aliyokuwa nayo Harun, isipokuwa Utume, ambao umeondolewa kwa kusema kwake: “Hakutakuwa na Mtume baada yangu.”

Kwahiyo, imethibitishwa kwamba Ali alikuwa ndugu yake Mtume, waziri (msaidizi) muwakilishi, na mrithi au Makamu wake, kama ilivyoelezewa na Mtume katika safari yake ya Tabuk. Hadith hii kwa umoja inakubaliwa kuwa ni ya kweli. Maoni kama haya yameelezewa na Ibn Sabbagh Maliki katika “Fusulu’l-Muhimma” uk. 29, na wengine wengi wa Maulamaa wenu mashuhuri.

Hafidh: Nafikiri madai yako kwamba kama Mtume wetu asingekuwa Muhuri (mwisho) wa Mitume,
Ali angeishika nafasi hiyo, ni (madai) ya kipekee kwako wewe mwenyewe. Hakuna mtu mwingine
aliyesema hivyo.

Muombezi: Madai haya hayakuishia kwangu na kwa Maulamaa wa Kishi’a tu. Maulamaa wenu wenyewe wamekuwa na maoni kama haya. Mmoja wa Maulamaa wenu wakubwa ni Mulla Ali bin Sultan Muhammad Harawi Qari.

Katika kitabu chake “Mirqat- e-Sharh bar Mishkat”, yeye anasema, akitoa maoni juu ya hadith ya Manzila; “Kuna dalili katika Hadith hii kwamba, kama kungekuwa na Mtume wa Allah baada ya mwisho wa Mitume, basi angelikuwa ni Ali.” Mwingine katika ulamaa wenu mashuhuri ambaye ameitafsiri Hadith hii kwa njia hii hii ni yule mwanachuoni ajulikanaye sana, Jalalu’d-Din Suyuti.

Anaandika kuelekea mwisho wa kitabu chake “Baghiatu’l’-Wu’az fi Tabaqatu’l- Huffadh”, akitoa Sanad (nyororo) ya wapokezi mpaka kufikia kwa Jabir Abdallah Ansari, kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimwambia Amiru’l-Muuminiina Ali. “Angelikuwepo Mtume yoyote baada yangu, basi angelikuwa ni Wewe!”
Kwa nyongeza, Mir Seyyed Ali Hamadani Faqih Shafi’i anasema katika Mawaddad ya Pili ya Mawadda Sita katika kitabu chake “Mawaddatu’l-Qurba,” akinukuu riwaya kutoka kwa Anas bin Malik, kwamba Mtume alisema: “Hakika, Allah amenifanya mimi Mkuu kwa Mitume wote, akanichagua mimi kwa ubora, na akanifanyia mimi wasii, binamu yangu Ali.

Kupitia kwake yeye akaimarisha mabega yangu, kama vile mabega ya Musa yalivyoimarishwa na Harun. Yeye (Ali) ni makamu wangu na msaidizi wangu.

Kama kungelikuwepo na Mtume yoyote baada yangu, angelikuwa ni Ali, lakini hakutakuwa na Mtume baada yangu.”

Hivyo unaona kwamba siko peke yangu katika kudai cheo cha Utume kwa Ali. Mtume na Maulamaa wenu wamelikubali hilo. Kwa vile alikuwa na cheo cha Harun na kwa vile muda wa Utume ulikuwa umefikia kikomo Ali alikuwa mwenye kufaa zaidi kwa Ukhalifa. Moja ya dalili za utukufu wa cheo cha Ali ilikuwa kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliruhusu mlango wa nyumba ya Ali kubakia kufunguka kuelekea Msikitini.

Maneno haya yalisababisha mshangao na bumbuazi miongoni mwa Masunni. Muombezi akauliza kwa nini inakuwa hivyo.

Nawab: Ijumaa iliyopita tulikwenda Msikitini kusali. Hafidh Sahib akatueleza kuhusu ubora wa khalifa Abu Bakar. Alisema kwamba yeye aliruhusiwa kuweka mlango wa nyumba yake kuelekea Msikitini. Tunashangaa kusikia wewe ukisema kwamba ruhusa hii ilikuwa kwa Ali pekee. Tafadhali hebu ifafanue nukta hii.

Muombezi: (Akimgeukia kwa Hafidh Sahib) Ulitoa kauli hii?

Hafidh: Ndio Imesimuliwa kwenye hadith Sahih zetu, kama iliyoelezwa na Sahaba mchamungu na mwadilifu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), Abu Huraira. Mtume aliagiza kwamba: “Milango yote ifunguliwayo kuelekea Msikitini ifungwe isipokuwa mlango wa nyumba ya Abu Bakr, kwani Abu Bakr anatokana na mimi na mimi ninatokana na Abu Bakr.”

Muombezi: Hakika unajua kwamba kwa sababu ya ubora wa Amiru’l-Mu’minina, Ali, Bani Ummaya walifanya juhudi endelevu kwa kupitia njia za siri na hususani kupitia kwa watu wenye kujipendekeza na kumsifu sifu mno Mu’awiya, kama Abu Huraira na Mughira ili kubuni hadith kama hizo. Aidha, wafuasi wa Abu Bakr, kwa sababu ya kumuunga mkono kwao yeye, waliziimarisha hadith hizi za kughushi.

Ibn Abi’l-Hadid, katika Sherhe yake ya Nahju’l-Balagha Jz. 1, na tena katika Jz. 3, uk. 17, anaeleza kwa urefu kwamba miongoni mwa hadith nyingi za kughushi ni hii ielezeayo kuhusu kufungwa kwa milango ya nyumba zote inayoelekea Msikitini isipokuwa ule wa Abu Bakr.

Kinyume na hadith hii ya kughushi, ziko hadith nyingi sahihi, ambazo zimesimuliwa sio tu katika vitabu Sahih vya Shi’a, lakini vilevile katika vitabu vya kutegemewa vya Mualamaa wenu wenyewe, kama “Sahih.”

Nawab: Kwa vile ni suala la ubishani, huku Hafidh Sahib akisema ni pekee kwa Abu Bakr, na wewe ukisema ni pekee kwa Ali, tungefurahia kama ungenukuu kutoka vitabu vyetu ili kwamba tuweze kulinganisha rejea zako na zile za Hafidh Sahib.

Hadith Ambayo Kwa Amri Ya Mtume Milango Ya Nyumba Inayoelekea Msikitini Ilifungwa Isipokuwa Mlango Wa Nyumba Ya Ali.

Muombezi: Vyanzo vifuatavyo vimesimulia kwamba, Mtume aliamrisha kwamba ile milango ya nyumba zote inayofunguka kuelekea Msikitini ifungwe isipokuwa mlango wa nyumba ya Ali: Ahmad bin Hanbal katika Musnad. Jz. 1 uk. 175, Jz. 2 uk. 26 na Jz. 4, uk. 369; Imam Abu Abdu’r-Rahman Nisa’i katika “Sunan” na katika “Khasa’isi’l-Alawi” uk. 13 – 14; Hakim Nishapuri katika “Mustadrak”, Jz. 3, uk. 117- 125 na Sibt Ibn Jauzi katika “Tadhkira” uk. 24 – 25 wameshuhudia usahihi wa Hadithi hii juu ya msingi wa Sanad za wasimuliaji wa Tirmidhi na Ahmad.
Halafu, Ibn Athri Jazri katika “Athna’l-Matalib”, uk, 12, Ibn Hajar Makki, katika “Sawa’iq Muhriqa”, uk. 76; Ibn Hajar Asqalani katika “Fathu’l-Bari” Jz. 7, uk. 12, Tibrani katika “Ausat”, Khatib Baghdadi katika kitabu chake cha “Tarikh” Jz. 7, uk. 205, Ibn Kathir kati- ka “Tarikh” Jz. 7, uk. 342, Muttaqi Hindi katika “Kanzu’l-Ummal”, Jz. 6, uk. 408; Haithami katika “Majima’uz-Zawa’id”, Jz. 9, uk. 65; Muhibu’d-Din Tabari katika “Riyadh” Jz. 2, uk, 451; Hafidh Abu Nu’aim katika “Fadha’ilus-Sahaba” na katika “Hilyatu’l-Auliya” Jz. 4, uk. 183; Jalalu’d-Din Suyuti katika “Ta’rikhu’l-Khulafaa”, uk. 116, katika “Jamu’l-Jawami”, katika “Khasa’isul-Kubra” na katika “La’aliu’l-Masunu’a” Jz. 1, uk, 181; Khatib Khawarizmi katika “Manaqib”, Hamwaini katika “Fara’id”, Ibn Maghazili katika “Manaqib”, Munawi Misri katika “Kunuzu’d-Daqa’iq”, Sulayman Balkh Hanafi katika “Yanabiu’l-Mawadda”, uk. 87, alitumia sura yote nzima ya 17 kwa suala hili hasa peke yake, Shahabu’d-Din Qastalani katika “Irshad Bari”, Jz. 6, uk. 81, Halabi kati- ka “Siratu’l-Halabiyya” Jz. 3, uk. 374 na Muhammad bin Talha Shafi’i katika “Matalibus- Su’ul” na wengine wengi, hususan kutoka miongoni mwa masahaba mashuhuri wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) wamesimulia kitu hicho hicho. Kwa mfano Khalifa Umar bin Khattab, Abdulla Ibn Abbas, Abdullah bin Umar, Zaid bin Arqam, na Jabir bin Abdullah Ansari wamethibitisha usahihi wa hadith hii.

Baadhi ya maulamaa wenu mashuhuri, kwa ajili ya kuepusha watu kutokana na kupotezwa na Bani Umayya wamesisitiza ukweli wa hadith hii. Muhammad bin Yusufu Ganji Shafi’i, katika kitabu chake “Kifayatut-Talib” Sura ya 50, ameshughulika na hadith hii chini ya kichwa cha habari maalum. Akinukuu kutoka vyanzo sahihi anasema kwamba, kwa vile idadi ya milango ya masahaba wa Mtume ilifunguka kuelekea Msikitini, na kwa vile Mtume amepiga marufuku watu wote kuingia Msikitini na hali ya janaba au haidh, aliagiza kwamba milango yote ya nyumba ifungwe isipokuwa mlango wa nyumba ya Hadhrat Ali.

Yeye alisema: “Fungeni milango yote bali acheni mlango wa nyumba ya Ali ubakie wazi.” Muhammad bin Yusuph Shafi’i anasema kwamba ni Ali pekee yake ambaye kwam- ba aliruhusiwa kuingia na kukaa ndani ya Msikiti katika hali ya janaba. Aliendelea kusema: “Kwa ufupi, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa kuufanya upendeleo huu wa kipekee juu ya Ali ilikuwa ni heshima kubwa mno. Inaonyesha kwamba Mtume alijua kwamba Ali, Fatima, na dhuria wao walikuwa huru kabisa kutokana na uchafu kama inavyoonyeshwa wazi na ‘aya ya tohara’ katika Qur’ani Tukufu.”

Maneno haya ya mwanachuo wa Ki-Shafi’i yanaweza kulinganishwa na hadith iliyotajwa na Hafidh Sahib. Tukiachilia mbali vyanzo vyote Sahihi tulivyonukuu, kama mnao uthibitisho wowote wa utohara wa Abu Bakr, tafadhali utoeni. Ukweli ni kwamba hata Bukhari na Muslim katika ukusanyaji wao wa hadithi wameonyesha ukweli huu kwamba mtu aliyanajisika hawezi kukaa ndani ya Msikiti. Mtume alisema: “Hairuhusiwi kwa mtu yeyote ambaye sitohara kukaa ndani ya Msikiti isipokuwa kwa mimi na Ali.”

Labda ningeruhusiwa hapa kunukuu hadith kutoka kwa Khalifa wa pili Umar bin Khattab, ambayo imeandikwa na Hakim katika “Mustadrak”, uk. 125, na Sulaiman Balkhi katika. Yanabin’l-Mawadda Sura ya 56, uk. 210, na wengineo, kama Imam Ahmad bin Hanbal, Khatib Khawarizmi, Ibn Hajar, Suyuti, na Ibn Athir Jazri. Yeye alisema: “Hakika Ali bin Abi Talib alikuwa nazo sifa tatu za pekee, kama ningekuwa na mojawapo kati ya hizo, ingelikuwa ni bora zaidi kwangu mimi kuliko ngamia wa manyoya mekundu:-

(1) Mtume alimuozesha binti yake kwake,
(2) Mtume aliagiza kwamba milango ya nyumba zote inayofunguka kuelekea msikitini ifungwe, isipokuwa mlango wa nyumba ya Ali;
(3) Mtume alimpa bendera (ya Uislamu) siku ya vita ya Khaibar.”

Kutokana na maelezo haya, ni wazi sasa kwamba Ali alikuwa sawa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika sifa zote, kama vile tu Harun alivyokuwa kwa Musa. Hivyo wakati Musa alipomuona anafaa kwa kazi hii, alimuomba Allah kumfanya mshirika katika ujumbe wake, ili kwamba aweze kuwa Waziri wake. Vivyo hivyo, wakati Mtume alipoona kwamba hakuna yoyote miongoni mwa wafuasi wake wote mwenye kustahiki kama Ali, alimuomba Allah amfanye Ali kuwa Waziri na mshirika wake.

Nawab: Kuna hadith zaidi zinazohusu suala hili?
Muombezi: Ndio, nyingi zinapatikana kuhusiana na suala hili katika vitabu vyenu wenyewe.
Nawab: Niko tayari kuzisikiliza mradi ninyi pia (akionyesha upande wa Maulamaa wa upande mwingine) mtataka kusikiliza.
Hafidh: Hakuna ubaya. Kusikiliza Hadith ni tendo la ibada kama simulizi yenyewe hiyo.

Wakati Akiwa Kwenye Rukuu Katika Sala Ali Alitoa Pete Kumpa Masikini.

Muombezi: Ibn Maghazili faqih Shafi’i katika “Manaqib” yake, Jalalu’d-Din Suyuti katika Durrul-Manthur mwana theolojia mashuhuri, Ahmad Tha’labi katika “Kashfu’l- Bayan,” Sibt Ibn Jauzi katika “Tadhkiratu’l-Khawasu’l-Umma”, kuhusiana na Aya ya Wilayat wananukuu kutoka kwa Abu Dharr Ghifari na Asma bint Umais (mke wa Abu Bakr) kwamba, wamesema kwamba siku moja walikuwa wanasali Sala ya Adhuhuri msik- itini wakati Mtume alikuwepo. Akaja masikini akaomba sadaka. Hakuna aliyempa chochote. Ali alikuwa anarukuu (katika Sala). Wakati alipoonyesha kidole chake, masikini alitoa ile pete kutoka kwenye kidole chake.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliyaona yaliyotokea, akanyanyua kichwa chake kuelekea mbinguni akasema: “Ya! Allah, Ndugu yangu Musa alikuomba: ‘Ya! Allah, nifungulie kifua changu na nifanyie wepesi kazi yangu. Chagua kwa ajili yangu msaidizi kutoka kwenye familia yangu, Harun ndugu yangu.’” Ilifunuliwa Aya kumuambia Musa kwamba du’a yake imekubaliwa.

Allah akachagua kwa ajili yake msaidizi na akaimarisha mikono yake na akawapa uwezo na mamlaka kiasi kwamba hakuna hata mmoja aliyeweza kuwashinda nguvu. “na Musa akasema kumwambia ndugu yake Harun: ‘Chukua mahala pangu miongoni mwa watu, na utendee wema wala usifuate njia ya waharibivu’” (7: 142)

Cheo Cha Harun Kama Mtume Kadhalika Kama Khalifa.

Hafidh: Umesema kwamba Harun alikuwa ni mshirika wa Musa katika Utume. Ilikuaje tena akafanywa kuwa Khalifa wake? Mshirika katika Utume hushikilia nafasi ya juu kuliko ile ya ukhalifa au umakamu. Kama mshirika ni Mtume, na akafanywa kuwa Khalifa, huku ni kushusha cheo chake.

Muombezi: Kanuni ya Utume inahusika kwa Musa, na Utume wa Harun ulikuwa chini ya ule wa Musa. Lakini kuhusu kuhubiri alikuwa mshirika wake, kama ilivyo dhahiri kutokana na ombi la Musa, lililoandikwa katika Qur’ani: “Musa akasema: Ewe Mola Wangu! Nikunjulie kifua changu, na unifanyie kazi yangu kuwa nyepesi, na ulifungue fundo lililo katika ulimi wangu, wapate kufahamu maneno yangu.

Na unipe waziri katika watu wangu, Harun, ndugu yangu. Kwake niongeze nguvu zangu, na umshirikishe katika kazi yangu.” (at-Taha; 20: 25-32)

Vivyo hivyo, Ali alikuwa mmoja ambaye mbali na kuwa daraja ya Utume alikuwa ni mshirika wa Mtume katika hatua zote na sifa maalum.

Hafidh: Nimeshangazwa kukusikia unavyoitia chumvi nafasi ya Ali. Wote tumeshitush- wa. Umesema hivi punde tu kwamba Ali alikuwanazo sifa zote za Mtume.

Muombezi: Maelezo haya sio ya kutia chumvi. Ni ya ukweli. Makamu wa Mtume, kutokana na akili ya kuwaida, yapasa awe mfano wa Mtume. Hata Maulamaa wenu wakubwa wameelezea itiqad kama hii hii. Imam Tha’labi, katika Sherhe yake, ali- ithibitisha nukta hii.

Na yule mwanachuo mkubwa wa Kisunni, Alim Fadhili Seyyed Ahmad Shahabu’d-Din, katika Kitabu chake “Tauzihu’d-Dala’il” amerejea kwenye nukta hii kama ifuatavyo: “Sio siri kwamba Amiru’l-Mu’minin alifanana na Mtume wa Allah, katika nyingi ya sifa nzuri, matendo yasiyo ya kibinafsi, tabia, maombi kwa Allah, na njia zote tukufu za maisha. Hii imethibitishwa na riwaya sahihi na vianzo vya kutegemea, na haihitaji uthibitisho wowote au hoja. Baadhi ya Maulamaa wamezihisabu kuwa ni sawa sifa zile ambazo Ali na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) walikuwa nazo.”

Miongoni mwa sifa walizoshirikiana wote ni nasaba yao safi. Na tukihoji kutokana na aya ya tohara, tunaona kwamba Ali ni sawa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika utohara (Aya hii iliteremshwa kwa ajili ya watu watano: Muhammad, Ali, Fatima Hasan na Husain). Ali, kama Mtume alikuwa Mwakilishi wa Allah. Kwa mujibu wa madhehebu zote, aya ifu- atayo iliteremshwa kwa ajili ya Ali.

“Hakika rafiki yenu mlinzi ni Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na walioamini; ambao hushika Swala na hutoa Zaka nao wakiwa wamerukuu.”
Ali alikuwa sawa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika utendaji kazi za Utume na kuhubiri, kama suala la Suratul-Bara’at linavyoonyesha. Mtume alimpa Abu Bakr baadhi ya aya za Sura hii na akamwagiza akazisome kwa watu wakati wa Hija. Mara Malaika Jibril ali- tokea mbele ya Mtume na akamwambia kwamba ni mapenzi ya Allah kwamba jambo la Qur’ani tukufu linapaswa kupelekwa ama na Mtume mwenyewe, au mtu ambaye ana- tokana naye. Ali alikuwa anafanana na Mtume katika wajibu wake kama Muakala wa Allah. Mtume Mwenyewe alisema: “Nimeamrishwa na Allah nitangaze hivi kwenu.”

Kisha akakamata mkono wa Ali na kusema: “Jueni nyote, yule ambaye ni mimi ni Maula kwake (yaani, ambaye mimi ni mwenye kutawalia mambo yake). Ali vilevile ni Maula (Bwana) wake.” Aidha, nafsi ya Ali imetangazwa kuwa ni nafsi ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Aya ya kuapizana (Mubahila) inasema:

فَمَنْ حَاجَّكَ فِيهِ مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ فَقُلْ تَعَالَوْا نَدْعُ أَبْنَاءَنَا وَأَبْنَاءَكُمْ وَنِسَاءَنَا وَنِسَاءَكُمْ وَأَنْفُسَنَا وَأَنْفُسَكُمْ ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَلْ لَعْنَتَ اللَّهِ عَلَى الْكَاذِبِينَ {61}

Watakaokuhoji katika haya baada yakukufikia ilmu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake zenu na wanawake zetu, na nafsi zetu na nafsi zenu, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo. (3: 61)

Tukirudi kwenye wakati ule ndani ya Msikiti, wakati Ali alipompa masikini pete yake na Mtume akamuomba Allah, akimuomba Yeye amfanye Ali kuwa mshirika wake katika Utume wake.

Kisha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akaomba: “Ya Allah! Mimi ni Muhammad, mchaguliwa Wako na Mtume Wako. Kifungulie kifua changu. Na nifanyie wepesi kazi yangu na unichagulie msaidizi kutoka kwenye familia yangu, Ali. Imarisha mgongo wangu kupitia kwake.”

Abu Dharr amesimulia: “Kwa jina la Allah! Du’a ya Mtume ilikuwa haijafikia mwisho, Malaika Jibril akatokea na kumfunulia Aya hii: “Hakika rafiki yenu mlinzi ni Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na walioamini, ambao wanadumisha Swala na kutoa Zaka huku wakiwa wamerukuu. (5: 55)

Du’a ya Mtume ilikubaliwa, na Ali aliteuliwa kama waziri wake. Muhammed bin Talha Shafi’i, katika “Matalibus-Su’ul”, uk. 19, amelishughulikia suala hili kwa urefu. Juu ya hayo, Hafidh Abu Nu’aim Isfahan katika “Manaqatu’l-Mutaharin”, Sheik Ali Ja’far kati- ka “Kanzu’l-Barahin”, Imam Ahmad Bin Hanbal katika “Musnad”, Seyyed Shahabu’d- Din katika “Tauzihu’d-Dala’il”, Jalalu’d-Din Suyuti katika “Durrul-Mansur”, na wanachuo wenu wengine mashuhuri wa madhehebu yenu wameisimulia hii katika vitabu vyao. Baadhi yao wamesimulia kutoka kwa Asma bint Umais (Mke wa Abu Bakr), na baadhi kutoka kwa masahaba wengine.

Ifuatayo imesimuliwa na Abdullah Ibn Abbas. “Mtume alitushika mikono mimi na Ali. Alisali rakaa nne, na akiwa amenyoosha mikono yake Mbinguni, akasema: “Ya Allah! Musa mtoto wa Imran, alikuomba umteulie msaidizi na kuifanya nyepesi kazi yake.

Mimi ni Muhammad. Nakuomba ufungulie kifua changu na uifanye nyepesi kazi yangu. Ufanye ulimi wangu kuwa fasaha ili watu wapate kuelewa maneno yangu. Niteulilie msaidizi kutoka kwa familia yangu, Ali. Niimarishe mgongo wangu kupitia kwake, na mshirikishe pamoja nami katika kazi yangu! Nilisikia sauti ikisema: ‘Ewe Muhammad! Nimelikubali ombi lako.’

Kisha Mtume akamshika Ali mkono na akasema: “Nyanyua mikono yako kuelekea juu mbinguni na umuombe Allah ili kwamba ajaalie kitu juu yako.’ Ndipo Ali akanyanyua mikono yake juu na kusema: ‘Ya Allah! Niahidi mimi kwa upande wako kwamba utanichukuwa mimi katika upendo Wako.” Mara Malaika Jibril akatokea na kule- ta Aya ifuatayo katika Suratul-Mariam: “Hakika wale waliomini na wakatenda mema, Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehma atawajaalia mapenzi Yake juu yao.” 19: 96

Wakati masahaba wa Mtume waliposhangazwa na hili, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akase- ma: “Kwa nini mnashangaa? Qur’ani Tukufu ina vigawanyo vinne: Robo moja inatuhusu sisi Ahlul-Baiti, robo moja inahusiana na mambo ya halali; robo moja ni kwa ajili ya mambo ya haramu; na robo moja inahusu maagizo na Sheria. Naapa kwa jina la Allah kwamba, kuna Aya nyingi katika Qur’ani ambazo zimeshushwa kwa kumsifu Ali.”
Sheikh: Hata kama hadith hii itachukuliwa kama ni Sahih, haiashirii cheo maalum kwa Ali. Hadith hiyo hiyo imesimuliwa kuwahusu Khalifa Abu Bakr na Khalifa Umar. Qaz’a bin Suwaid amesimulia kutoka Ibn Malika ambaye anamnukuu Ibn Abbas akisema kwamba, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema; “Abu Bakr na Umar wako kwangu mimi kama alivyokuwa Harun kwa Musa.”

Muombezi: Yakupasa uangalie tabia za baadhi ya wasimuliaji wenu (wa hadith). Wakati mwingine unahoji kutokana na similizi za Amadi na wakati mwingine kutoka kwenye zile za yule mwongo mwenye sifa mbaya na mzushaji; Qaz’a bin Suwaid, pamoja na kwamba mualamaa wenu mashuhuhuri wamempuuza.

Allama Dhahabi, katika “Mizanul-ltidal”, katika maelezo ya habari za Qaz’a bin Suwaid na Ammar bin Harun, wanaipuuza hadith hii na kusema kimkato tu: “Huu ni uwongo.” Wakati Maulamaa wenu wanampuuza Qaz’a, hadith anazosimulia inapasa zipuuzwe. Linganisha Hadith hii ya Qaz’a bin Suwaid na Sanad ya Hadith ambayo nimenukuu kutoka kwa maulamaa wenu mashuhuri mno wa madhehebu yenu na uamue mwenyewe ni hadith ipi unaikubali.