read

Mkutano Wa Pili, Ijumaa Usiku 24 Rajab, 1345 A.H.

Hafidh: Nilivutiwa mno na mazungumzo yako yenye maelekezo kuhusu mtiririko wa jadi yako. Nakiri kwamba wewe ni kizazi (dhuria) cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), lakini nashangaa ni vipi mtu mwenye elimu kama wewe unakuwa chini ya ushawishi wenye ushusha hadhi wa maadui.

Ukiwa mwenye kuziacha njia za jadi wako Maarufu, umefuata njia za makafiri wa Iran. Ninachomaanisha hapa kwa njia za maadui wapumbavu ni yale mambo mapya ya uzushi (Bid’a) yaliyoingizwa katika Uislamu kupitia kwa Mayahudi.

Muombezi: Tafadhali hebu elezea ni nini unachomaanisha.

Dhana Potofu Kuhusu Asili Ya Madhehebu Ya Shia.

Hafidh: Historia yote ya Mayahudi imeharibiwa na hila. Abdullah bin Saba ‘San’a’i, Ka’bu’l-Ahbar, Wahhab Ibn Munabba, na wengine waliukiri Uislamu, na wakajifanya wanakubali hadith za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na hivyo kusababisha ghasia miongoni mwa Waislamu.

Khalifa wa tatu Uthman bin Affan, aliwaandama na wakakimbilia Misri, ambako walianzisha madhehebu yajulikanayo kama Shia. Walieneza taarifa za uongo kuhusu Khalifa Uthman na kuandika hadith za uongo za kumaanisha kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimteuwa Ali kuwa Khalifa na Imamu.

Kwa kuanzishwa madhehebu haya vurugu zilienea, ambazo zilipelekea kuuwawa kwa Khalifa Uthman na kuchukuliwa kwa cheo cha ukhalifa na Ali. Kikundi kilichokuwa na uadui kwa Uthman kikasimama juu kumpendelea Ali. Wakati wa Ukhalifa wa Bani Umayya, wakati watu wa familia ya Ali na wafuasi wake walipokuwa wanauwawa, kikundi hiki kilijificha.

Bado, baadhi ya watu, kama Salman Farsi, Abu Dharr Ghifari, na Amar Yasir, waliunga mkono mwenendo wa Ali. Mashindano haya yaliendelea mpaka wakati wa Harun’ar- Rashidi, na hasa mwanae Ma’mun-ar-Rashidi Abbas, ambaye alimshinda ndugu yake kwa msaada wa wa-Irani, na kisha wakaeneza wazo la kwamba Ali alikuwa ni bora kuliko makhalifa wengine, Wa-Irani, wakiwa na uadui na Waarabu ambao waliwashinda, wakapata fursa ya kuwapinga Waarabu kwa kutumia jina la dini. Mashi’a wakapata nguvu katika kipindi cha Wadailami na Wafalme wa Ki-Safavid na hatimaye wakatambuliwa.

Basi wakajulikana rasmi kama madhehebu ya Shia. Wazoroasta wa Iran bado wanajiita Mashia. Kwa ufupi, madhehebu ya Shia yalianzishwa na Myahudi, Abdullah bin Saba. Vinginevyo kusingekuwa na neno kama Shia katika Uislamu. Babu yako, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alilichukia neno hilo.

Kusema kweli madhehebu ya Shia ni sehemu ya imani ya Kiyahudi. Nashangaa kwa nini umeacha njia za haki za jadi wako na ukafuata njia ya waliokutangu lia, ambao wamefuata njia za Kiyahudi. Ilikupasa ufuate Qur’ani Tukufu na mfano wa babu yako, Mtume (s.a.w.w.).

Ni Upuuzi Kumhusisha Abdullah Bin Saba’ Na Mashi’a

Muombezi: Ni kitu kisicho cha kawaida kwa mtu msomi kama wewe kutegemeza hoja zake katika misingi ya uongo kabisa. Hakuna maana kwako wewe kulihusisha jina la Abdullah bin Saba na Mashia. Abdullah bin Saba alikuwa Myahudi, na kutegemeana na vyanzo (rejea) vya Shia, yeye ni mnafiki na analaaniwa vikali. Ikiwa kwa wakati fulani alitokea kuwa rafiki wa Ali, ni uhusiano gani aliokuwa nao na Mashia? Kama mwizi atavaa guo ya Mwanachuo, akapanda juu ya mimbari, na akasababisha madhara kwa Uislamu, utayachukia mafundisho na kuwaita Wanachuoni wezi? **

** Huu ulikuwa mwaka wa 1927 (1345 A.H.), katika miaka ya hivi karibuni imebainika kwamba kulikuwa hakuna mtu anayeitwa Abdullah Ibn Saba, huu ulikuwa ni ubunifu wa mtu aliyekuwa akiitwa Seif. Ukweli huu umetokana na utafiti uliofanywa na mwanachuoni mtafiti, Al-Askari. Soma kitabu chake: “Abdallah bin Saba’ na ngano nyinginezo

Kwa kweli Waislamu wa Madhehebu ya Shia kamwe hawajakuwa ni kikundi cha Siasa tu. Walikuwa wakati wote wanaunda madhehebu ya dini, ambayo hayakuanzishwa, kama unavyosema, katika wakati wa Ukhalifa wa Uthman, lakini lililinganiwa kutokana na maneno na maamrisho ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika wakati wake mwenyewe.

Wakati ambapo wewe unajadili kwa msingi wa ushahidi wa kubuni wa maadui, mimi nitanukuu kwa ajili yako Aya kutoka Qur’ani Tukufu na similizi za waandishi wenu wenyewe kuonyesha hali ya ukweli halisi.

Maana Ya Neno Shi’a

Muombezi: Shi’a kama ujuavyo, kilugha ina maana ya “Mfuasi.” Mmoja wa maulamaa wenu mkubwa, Firuzabadi katika kitabu chake “Qamusu’l-lughat,” anasema:

Jina la Shi’a kwa kawaida lina maana ya kila mtu ambaye ni rafiki wa Ali na Ahlul-Bait wake. Jina hili ni lao peke yao.” Maana hii hii hasa inatolewa na Ibn Athir katika “Nihayatul’l-Lugha.” Kutokana na Sharh zenu wenyewe, neno Shia lina maana ya “wafuasi wa Ali ibn Abu Talib,” na lilikuwa likitumika katika njia hii katika wakati wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Kwa kweli alikuwa ni Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe ambaye alilitambulisha neno Shi’a kwa maana ya “Mfuasi wa Ali bin Abu Talib.” Na neno hili lilikuwa likitumiwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ambaye kuhusu yeye Allah (s.w.t.) Anasema:

وَمَا يَنْطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ {3}

إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ {4}

Wala hasemi kwa matamanio (ya nafsi yake). Hayakuwa haya ila ni Wahyi uliofunuliwa.” (53: 3-4)

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliwaita wafuasi wa Ali “Shia,” “waliokombolewa” na “waliookolewa.”

Hafidh: Kiko wapi kitu kama hicho? Sisi hatujakiona kamwe.

Muombezi: Sisi tumekiona na hatufikirii kuwa ni sawa kuficha ukweli. Allah (s.w.t.) Amewalaani wafichaji na hao akawaita ni watu wa motoni. Allah (s.w.t.) Anasema:

“Hakika wale wanaficha hoja zilizo wazi na uongozi ambao tumeuteremsha baada ya kuzibainisha kwa watu kitabuni, hao anawalaani Allah na wanawalaani wenye kulaani.” (2:159) “Hakika wale wafichao aliyoyateremsha Allah katika Kitabu wakafadhilisha thamani ndogo, hao hawali matumboni mwao isipokuwa moto, wala Allah hatawasemeza Siku ya Kiyama wala hatawatakasa, na watapata adhabu iliyo kali.”

Hafidh: Kama tunaijua kweli na tukaificha nakubali kwamba tunastahili laana kama ilivyofunuliwa katika aya hizi tukufu.

Muombezi: Natumaini utaziweka akilini Aya hizi mbili ili kwamba usije ukashindwa nguvu na tabia au kutovumilia. Hafidh Abu Nu’aim Isfahani ni moja wa watu wenu maarufu sana katika wasimuliaji wa hadith. Ibn Khallikan amemsifu katika kitabu chake “Wafayatu’l Aayan” kama Huffadh mkubwa (Mtu wa hikma) na mmoja kati ya wasimuli- aji wa hadith aliyeelimika sana.

Vile vile anaelezea kwamba jalida kumi za kitabu chake “Hilyatu’l–Aulya” ni miongoni mwa vitabu vizuri mno vya kufundishia. Salahu’d-din Khalil bin Aibak Safdi anaandika katika “Wafiy bi’l-Wafiyat” kuhusu yeye: “Mfalme wa wasimuliaji wa hadith, Hafidh Abu Nu’aim, alikuwa wa mbele sana katika ilmu, uchamungu, na uaminifu.

Alikuwa na nafasi ya hali ya juu katika usimuliaji na uelewaji wa hadhith. Kitabu chake kilicho bora sana ni “Hiliyatul’-Auliya” katika jalida kumi, zikiwa na chimbuko kutoka Sahih mbili (Bukhari na Muslim).” Muhammad bin Abdullah al- Khatab amemsifu katika “Rijali’l-Mishkati’l-Masabin.” akisema kwamba ni miongoni mwa wasimuliaji hadith wa mbele ambaye simulizi zake ni za kuaminika kabisa.

Kwa ufupi, Mwanachuo na Muhadithina huyu mwenye kuheshimika na fahari ya Maulamaa wenu, anasimulia kutoka kwa Abdullah ibn Abbas kupitia nyororo yake mwenyewe ya wasimuliaji katika Kitabu chake “Hilyatu’l-Auliya” kama ifuatavyo: “Wakati aya ifuatayo ya Qur’ani Tukufu ilipoteremshwa:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَٰئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ {7}

جَزَاؤُهُمْ عِنْدَ رَبِّهِمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۖ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ۚ ذَٰلِكَ لِمَنْ خَشِيَ رَبَّهُ {8}

‘(Na kwa) wale ambao wanaamini na kufanya mema, hakika hao ndio wabora wa viumbe. Malipo yao kwa Mola wao ni bustani zipitazo mito chini yake, watakaa humo milele. Allah yuko radhi nao na wao wako radhi Naye, na hayo ni kwa yule amchae Mola.’” (98: 7– 8)

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), akizungumza na Ali, alisema: “Ewe Ali, wabora wa viumbe (khairi’l-Bariyya) katika Aya hii tukufu inakuashiria wewe na wafuasi (Shi’a) wako. Katika siku ya ufufuo, wewe na wafuasi (Shi’a) wako mtapita daraja ambayo kwamba Allah atakuwa radhi nanyi na ninyi mtakuwa radhi Naye.”

Sifa Zaidi Za Shi’a

Halikadhalika, Abu’l-Muwayyid Muwafiq Bin Ahmad Khawarizmi katika sura ya 17 ya Manaqib yake; Hakim Abu’l-Qasim Abdullah Bin Abdullahi’l-Haskani, katika Shawahidut-Tanzil; Muhammad Bin Yusuf Ganji Shafi’i katika Kifayatut-Talib, uk. 119, Sibt Ibn Jauzi katika Tadhkira, uk. 31, Munzir Bin Muhammad Bin Munzir, na hususan Hakim, wamesimulia kwamba Hakim Abu Abdullah Hafidh (mmoja wa maulamaa wenu wakubwa) alisema, akitegemea juu ya ushahidi wa wasimuliaji kurudi nyuma hadi kufikia kwa Yazid Bin Sharafi’l-Ansari, mwandishi wa Amiru’l-Mu’minin Ali Bin Abi Talib kwamba Ali alisema kwamba wakati wa kifo cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), Mtume aliegema kwenye kifua cha Ali na akasema: “umeisikia ile aya tukufu: Wale ambao wameamini na wakafanya matendo mema, hao ndio bora wa viumbe.’ (98:7)

Hawa ni Shi’a wako. Sehemu yangu ya kukutania na wewe itakuwa ni kwenye Chemchemu ya Kauthar (katika Pepo). Wakati viumbe wote watakapokusanyika kwa ajili ya hesabu, uso wako utang’ara, na utatambulishwa siku hiyo kama kiongozi wa watu wenye nyuso angavu.”

Jalalud-Din Suyuti katika Durru’l-Mansur anamnukuu Abu’l-Qasim Ali Bin Hasan (anayejulikana zaidi kama Ibn Asakir Damishqi) ambaye anamnukuu Jabir Bin Abdullah Ansari, mmoja wa masahaba wakubwa wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), akisema kwamba yeye na watu wengine walikuwa wamekaa pamoja na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) wakati Ali Bin Abi Talib alipoingia ndani. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Naapa kwa Yule ambaye anamiliki uhai wangu kwamba mtu huyu (Ali) na wafuasi wake watapata wokovu katika Siku ya Ufufuo.” Wakati huo huo aya hiyo hapo juu ilishushwa.

Katika sharhe hiyo hiyo, Ibn Adi anamnukuu Ibn Abbas akisema kwamba wakati aya hiyo hapo juu iliposhuka, Mtume akasema kumuambia Amiru’l-Mu’minin, Ali: “Wewe na waafuasi wako mtakuja Siku ya Ufufuo katika hali ambayo kwamba wote mtaridhia juu ya Allah, na Allah ataridhika nanyi.”

Katika Manaqib ya Khawrizmi, ifuatayo ilisimuliwa kutoka kwa Jabir Bin Abdullah Ansari: “Nilikuwa kwenye hadhara ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) wakati Ali alipoungana nasi, na wakati ule Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: ‘Huyu ambaye amekujieni ni ndugu yangu.’ Kisha, akaelekea Ka’ba, Mtume akachukua mkono wa Ali na akasema: “Naapa kwa Yule ambaye anamiliki uhai wangu, huyu Ali na wafuasi wake watakuwa wamepata wokovu katika Siku ya Hukumu.’

Kisha akasema: ‘Ali ndiye wa mbele zaidi yenu wote katika imani, mwenye kuzingatia mno kuhusu dhamana za Allah, mwadilifu kupita wote katika kuamua mambo ya watu, na mwadilifu kupita wote katika kugawa masurufu miongoni mwa watu, na aliye juu zaidi ya wote kwa cheo mbele ya Allah.’” Katika wakati huo aya hiyo hapo juu ilishushwa.

Katika Sura ya 11 ya Kitabu chake “Sawa’iq” Ibn Hajar anamnukuu Hafidh Jamalu’d-Din Muhammad Bin Yusuf Zarandi Madani (Mwanachuo mkubwa wa madhehebu yenu) akisema kwamba: Wakati Aya hiyo hapo juu ilipoteremshwa, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Ewe Ali, Wewe na Shi’a wako ndio wabora wa viumbe walioumbwa.

Wewe na Mashi’a wako mtakuja Siku ya Hukumu katika hali ambayo nyote mkiwa mmeridhia kwa Allah, na Allah atakuwa radhi nanyi. Maadui zako watakuwa wamechukizwa mno, na mikono yao itakuwa imefugwa kuzunguuka shingo zao.” Kisha Ali akauliza, ni nani maadui zangu. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akajibu, “Yule ambaye ana uadui kwako na ambaye anakutukana.”

Allama Samhudi, katika Jawahiru’l-Iqdain, kwa idhini ya Hafidh Jamalu’d-Din Zarandi Madani na Nuru’d-Din Ali bin Muhammad bin Ahmad Maliki Makki, ajulikanaye kama Ibn Sabbagh, ambaye anaheshimiwa kama mmoja wa Wanachuo wenu Mashuhuri na mnadharia mkubwa wa mambo ya dini, katika kitabu chake “Fusulu’l-Muhimma” anasimulia kutoka kwa Abdullah bin Abbas, kwamba wakati Aya hii iliyo kwenye mjadala ilipoteremshwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema kumuambia Ali; “Ni wewe na Mashi’a wako. Wewe na wao mtakuja Siku ya Hukumu mkiwa mmefurahi mno na mmeridhia, ambapo maadui zako watakuja na huzuni kubwa na mikono iliyofungwa.”

Mir Seyyed Ali Hamadani Shafi’i, mmoja wa wanachuo wenu mashuhuri katika kitabu chake “Mawaddatul’l-Qurba” na mwanachuo anayejulikana vizuri sana kwa upinzani wake juu ya Shia, Ibn Hajar katika kitabu chake “Sawa’iq-e-Muhriqa”, anasimulia kutoka Ummu’l-Mu’minina Umm Salma, mke wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), kwamba Mtume alisema:

“Ewe Ali, wewe na Mashia wako mtaishi Peponi; wewe na Mashia wako mtaishi katika Pepo.” Mwanachuo anayejulikana sana wa Khawarizm, Muwaffaq bin Ahmad, kati- ka kitabu chake “Manaqib” Sura ya 19, anasimulia kutoka rejea zinazoaminika kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema kumuambia Ali: “Katika umma wangu wewe ni kama Masihi Isa Mwana wa Mariamu.”

Taarifa hii inaonyesha kwamba, kama vile wafuasi wa Mtume Isa (A.S.) walivyogawanyi- ka katika makundi: Waumini wa kweli wajulikanao kama Hawari’in, Mayahudi, na wapi- ga chuku (wenye kutia maneno chumvi) ambao wanamshirikisha yeye na Allah; katika njia hiyo hiyo Waislamu watakuja kugawanyika katika makundi matatu. Mojawapo litakuwa Shi’a, waumini wa kweli. Kundi lingine litakuwa la maadui wa Ali, na kundi la tatu litakuwa la wenye kukuza cheo chake.

Sifa Za Shia Zathibitishwa Kutoka Kwenye Vitabu Vya Sunni.

Kufikia hapa watu walitawanyika katika kuitikia mwito wa Swala ya Isha. Baada ya Swala Mulla Abdu’l-Hayy alirudi na Sherhe ya Suyuti, Mawaddatu’l-Qurba, Musnad ya Imam Ahmad bin Hanbal, na Manaqib ya Khawarizmi. Alisoma kutoka kwenye vitabu hivyo hadith alizokuwa amezinukuu Muombezi katika mijadala yake kwa njia ya uthibitisho. Kwa vile rejea zangu zilikuwa sawa sawa, muonekano wa nyuso za wale wote ambao wako katika kambi ya upinzani ulibadilika. Wakati huo huo walikuta hadith nyingine katika Mawaddatu’l-Qurba.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema, “Ewe Ali, Siku ya Hukumu wewe na Mashi’a wako mtakuja mbele za Allah mkiwa mmefurahi mno na kuridhia, ambapo adui yako atakuja na huzuni kubwa na mikono ikiwa imefungwa.”
Muombezi: Hizi ni hoja zilizo wazi zinazoungwa mkono na Kitabu cha Allah, na hadith sahihi, na Ta’arikh. Kuungwa mkono kwa upande wangu kunakuja kutoka kwenye vitabu vya wanachuo wenu mashuhuri. Haya ni kwa nyongeza juu ya simulizi nyingi ambazo zimo katika vitabu na Sherhe za Shi’a. Kwa kutumia vitabu hivivilivyoko mbele yenu sasa, ninaweza kuendelea kuwasilisha hoja ziungazo mkono nukta iliyo kwenye mjadala mpaka kesho asubuhi, kwa rehema za Allah; lakini nafikiri kwamba hoja nilizowasilisha zipaswe kuwa zinatosha kuondoa mashaka yenu kuhusu Mashi’a. Watukufu mliohudhuria, sisi Mashia sio Mayahudi. Sisi ni wafuasi wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.).

Mwanzilishi wa neno Shi’a kwa maana ya “Wafuasi wa Ali” hakuwa mlaaniwa huyu Abdullah bin Saba, bali ni Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe. Kamwe hatumfuati mtu binafsi bila rejea zenye hoja za kumuunga mkono. Mmesema kwamba ilikuwa ni baada ya Uthman ndio neno “Shi’a” lilipoanza kutumika kuashiria wafuasi wa Ali. Kwa kweli, hata wakati wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) Masahaba kadhaa maarufu wenye kutajika walikuwa wakiitwa Mashi’a.

Hafidh Abu Hatim Razi katika kitabu chake “Az-Zainat” ambacho amekiandika kwa ajili ya kufafanua maana ya maneno fulani na Semi zinazotumika miongoni mwa Wanachuo, anasema kwamba neno la kwanza jipya ambalo lilikuja kukubaliwa na wote katika Uislamu wakati wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) lilikuwa ni “Shia.” Neno hili lilitumika kwa masahaba maarufu wanne: Abu Dharr Ghifar, Salman Farsi, Mikdadi bin Aswad Kindi, na Ammar Yasir. Hadith nyingi zaidi zilinukuliwa katika kuunga mkono nukta hii hii.

Sasa ni juu yenu kufikiria vipi iliwezekana kwamba wakati wa Mtume (s.a.w.w.) Wanne kati ya masahaba wake wakubwa waliitwa Shi’a. Kama Mtume (s.a.w.w.) alifikiria kuwa neno hilo ni la uzushi (bida’a), kwanini hakuwakataza watu kulitumia? Ukweli ni kwamba watu walisikia kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) mwenyewe kwamba wafuasi (Mashi’a) wa Ali walikuwa ni wakazi wa Peponi. Walikuwa na fahari nalo na kwa uwazi wakajiita wenyewe Mashi’a.

Cheo Cha Salman, Abu Dharr, Mikdadi Na Ammar

Umesimulia Hadith kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) isemayo: “Hakika masahaba wangu ni kama nyota; yeyote katika wao mtakayemfuata, mtakuwa mmeongozwa sawa-sawa.

Abu’l-Fida anaandika katika kitabu chake cha Tarikh kwamba watu hawa wanne, ambao walikuwa masahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) walijitenga, pamoja na Ali kula kiapo cha utii kwa Abu Bakar, siku ile ya Saqifa. Kwa nini hamchukulii kukataa kwao kula kiapo kuwa kunafaa kuigwa?

Maulamaa wenu wenyewe wameandika kwamba walipendwa na Allah na Mtume Wake. Sisi tunawafuata kama walivyomfuata Ali.

Kwa hiyo kutokana na hadith yenu wenyewe, sisi tuko katika njia ya Mwongozo. Kwa ruksa yenu, na kutilia maanani uchache wa muda, ninawasilisha kwenu simulizi chache katika kuunga mkono hoja yangu kwamba watu hawa wanne walipendwa na Allah na Mtume (s.a.w.w.).

Abu Nu’aim Isfahami katika “Hilyatu’l-Auliya”, Juz. 1, uk. 172 na Ibn Hajar Makki katika hadith ya tano ya hadith arobaini zilizosimuliwa katika “Sawa’iqul- Muhriqa” kwa kumtukuza Ali, iliyosimuliwa kutoka kwa Tirmidhi, na Hakim kutoka kwa Buraida, kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.)) alisema: “Hakika, Allah ameniamuru mimi kuwapenda watu wanne na amenijulisha kwamba Yeye mwenyewe anawapenda.”

Wakati watu walipomuuliza ni kina nani watu hao wanne, alisema: “AIi ibn Abu Talib, Abu Dharr, Mikdadi na Salman.” Tena, Ibn Hajar katika Hadithi ya 39 amesimulia kutoka kwa Tirmidhi na Hakim kutoka kwa Anas bin Malik kwamba Mtume amesema: “Pepo inashauku juu ya watu watatu, Ali, Ammar, na Salman.”

Je, vitendo vya Sahaba hawa Mashuhuri wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) sio vya mfano wa kuigwa na Waislamu wengine? Je, sio aibu kwamba kwa maoni yenu Sahaba wamewekewa mpaka kwa wale tu waliocheza mchezo wa Saqifa, au ambao wameukubali mpango wake bila kupinga, ambapo wengine ambao wamepinga hila za Saqifa wanaonekana kama wasiokuwa waaminifu? Na ikiwa ni hivyo, basi hadith uliyoinukuu ingekuwa na maneno haya: “Hakika wachache kati ya Sahaba wangu ni kama nyota .”

Sababu Za Wa-Irani Kuupokea Ushi’a.

Umekuwa sio mwema katika kusema kwamba, “Ushia ni Dini ya kisiasa, na kwamba Mazoroasta wa Iran wameukubali kwa ajili ya kujiokoa kutoka umiliki wa Waarabu, umesema hivyo katika upofu wa kufuata watangulizi wako. Nimekwishathibitisha kwamba ni dini ya Uislamu, dini ambayo Mtume (s.a.w.w.) ameiweka amana mikononi mwa wafuasi wake. Kwa kweli, wale ambao bila kibali chochote kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.), wakaweka msingi wa Saqifa, walikuwa ndio wenyewe wanasiasa na sio wafuasi wa famil- ia Tukufu ya Mtume (s.a.w.w.).

Ni tabia ya Wa-Iran kwamba wao hutazama mambo kwa kuyachunguza. Wakati watakaposadikishwa na ukweli wake, wanayakubali, kama ambavyo waliukubali Uislamu wakati Iran iliposhindwa na Waarabu. Hawakulazimishwa kufanya hivyo. Waliuacha Uzoroasti na kwa uaminifu kabisa wakaushika Uislamu.

Halikadhalika, wakati waliporidhishwa na mantiq na huduma za Ali zenye thamani isiokadirika, wakaukubali Ushi’a. Kinyume na maelezo ya waandishi wenu wengi,Wairani hawakumkubali Ali wakati wa Ukhalifa wa Harun-r-Rashid au Maamunu’r-Rashid. Walimkubali Ali wakati wa uhai wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Salman Farsi alikuwa mmoja wa wafuasi waaminifu kabisa wa Ali.

Alifikia kiwango cha juu cha Imani. Maulamaa wa Madhehebu zote kwa makubaliano ya pamoja wameandika kwamba Mtume amesema: “Salman anatokana na Ahlul Bait wetu (yaani ni mmoja wa watu wa Nyumba yangu).” Kwa sababu hii aliitwa “Salman Muhammad” na yeye inakubalika kabisa kuwa ni mfuasi thabiti mwenye kumuunga Ali, na mpinzani mkali wa Saqifa.

Kama, kutegemeana na vitabu vyenu wenyewe, sisi tukimfuata yeye, basi tuko katika njia iliyonyooka. Alizisikia aya za Qur’ani na maneno ya Mtume (s.a.w.w.) kuhusu Ali na kiwazi kabisa akaelewa kwamba utii kwa Ali ulikuwa ni utii kwa Mtume (s.a.w.w.) na kwa Allah (Swt). Alimsikia mara kwa mara Mtume akisema: “Mwenye kumtii Ali ananitii mimi; na mwenye kunitii mimi anamtii Allah (Swt); ambaye ana uadui kwa Ali ni adui kwangu; na ambaye ana uadui kwangu ni adui kwa Allah (Swt).

Kila Mu-Iran, hata hivyo, ambaye alikwenda Madina na kusilimu, iwe wakati wa Mtume au baadae, alizitii amri za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Kwa sababu hii Khalifa wa pili akashindwa kuvumilia na akaweka vikwazo vingi juu ya Wairan. Shida hizi na taabu zilizaa uadui ndani ya nyoyo zao. Walihoji ni kwanini Khalifa awanyime haki za Uislamu kinyume na amri zilizowekwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Shukurani Za Wa-Iran Juu Ya Huruma Za Ali.

Mbali na hali hizi, Wa-Irani walikuwa na shukurani sana kwa Ali kwa huruma zake kuhu- siana na matendo waliyofanyiwa mabinti wa kifalme waliotekwa na Waarabu. Wakati wafungwa wa Mada’in (Taisfun) walipoletwa mjini Madina, Khalifa wa pili aliamuru kwamba wafungwa wote wa kike wafanywe kuwa watumwa wa Waislamu. Ali alilikataza hili na akasema kwamba mabinti wote wa kifalme ni wafungwa wa kipekee na wanapaswa wapewe heshima.

Wawili kati ya wale wafungwa walikuwa ni mabinti wa mfalme Yazdigerd wa Iran na hawakuweza kufanywa watumwa. Khalifa akauliza ni nini kifanywe. Ali akasema kwamba kila mmoja yapasa aruhusiwe kuchagua mume miongoni mwa Waislamu. Kwa ajili hiyo, Shahzanan alimchagua Muhammad ibn Abu Bakar (ambaye alilelewa na Ali), ambapo yule binti mfalme mwingine, Shahbanu alimchagua Imam Husain, mjukuu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Wote walikwenda kwenye nyumba za watu hawa baada kufungishwa ndoa kisheria. Shahzanan alizaa mtoto wa kiume, Qasim Faqih, baba wa Ummi Farwa, ambaye alikuwa mama wa Imam wetu wa Sita, Ja’afar as- Sadiq. Imam Zainu’l-Abidin, Imam wetu wa nne alizaliwa na Shahbanu.

Hivyo mwanzo wa Ushia haukuwa na uhusiano wowote na wakati wa Harun na Ma’amun au na Utawala wa Ufalme wa Safavid katika Iran, kama ulivyosema mapema. Ulitangazwa wazi karne saba kabla ya Ufalme wa Safavid (yaani karne ya 4 A.H) wakati wa-Dailami (wa-Buwayyid) walipokuwa watawala. Katika mwaka wa 694 A.H. Falme ya Iran ilikuwa ikitawaliwa na Ghazan Khan Mughal (ambaye jina lake la Kiislamu lilikuwa Mahmud). Tokea wakati huo, Imani juu ya Ahlul Bait wa Mtume (s.aw.w.) ilidhihirisha kama jambo la kawaida, Ushia ulikua kwa uimara kabisa.
Baada ya kifo cha Ghazan Khan Muqhal mnamo mwaka wa 707 A.H., ndugu yake, Muhammad Shah Khuda Bandeh akawa mtawala wa Iran. Aliandaa mjadala wa kidini (Mdahalo) kati ya Alama Hilli, Mwanachuo msomi wa Kishia, na Khwaja Nidhamu’d-Din Abdul’l-Maliki Maraghe’i, Kadhi Mkuu wa (Madhehebu) Shafii na Mwanachuo mkubwa wa Kisunni wa wakati huo.

Midahalo Kati Ya Allama Hilli Na Kadhi Mkuu Kuhusu Uimamu.

Nukta ya mdahalo huu ilikuwa ni Uimamu. Allama Hilli alitoa hoja zenye nguvu sana kuthibitisha kwamba Ali alikuwa ndiye mrithi alitemfuatia mara moja Mtume (s.a.w.w.) bila mwanya, na kwa kuridhisha kabisa akabainisha uwongo wa madai ya ule upande mwingine, kiasi kwamba wale wote waliohudhuria walitosheka kabisa na jinsi ya ukweli wa Allama. Khwaja Nidhamu’d-Din alikubali kwamba hoja za Allama haziwezi kukanushwa. Lakini akasema kwamba, kwa vile alikuwa akifuata njia za wakubwa wake waliomtangulia, haikuwa vizuri kuiacha. Aliona kwamba ilikuwa ni muhimu kudumisha mshika- mano miongoni mwa Waislamu.

Mfalme Wa Irani Aliikubali Iman Ya Kishi’a.

Mfalme alisikiliza hoja hizo kwa usikivu makini, mwenyewe akaukubali msimamo wa Shi’a, na akatangaza uhalali wa Ushia katika Iran. Hatimaye alitangaza kwa nagavana wa mikoa kwamba Khutuba za kila juma (zinazotolewa misikitini) zinapaswa zitangaze haki ya Ali kama mrithi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Vile vile aliamuru kwamba Kalimah iandikwe kwenye dinari (Sarafu za dhahabu) katika njia hii: “La ilaha illa llah Muhammad Rasulullah, Aliyan Waliyyullah,” maana yake, “Hakuna Mungu ila Allah; Muhammad ni Mtume wa Allah na Ali ni Walii wa Allah.” (makamu au mlezi wa watu aliyeteuliwa kiungu). Katika njia hii mizizi ya Ushi’a ilisimama kwa umadhubuti kabisa.

Karne saba baadae, wakati wafalme wa Ki-Safavid walipoingia madarakani, utando wa ujinga na ushabiki usio na maana katika dini viliendelea kuondolewa, Ushi’a ukashamiri kila mahali katika nchi ya Iran. Ndio, wako Mazoroasti katika Iran na wale wanaotia chimvi cheo cha Ali na kumfikiria yeye kuwa ni Mungu. Lakini haipasi kuwahusisha na watu wa kawaida wa Iran, ambao wana imani katika Allah na Mtume Muhammad kama Mtume wa mwisho. Hawa wanamfuata Ali na watoto wake kumi na moja kama ilivyoamrishwa na Mtume (s.a.w.w.).

Hafidh: Ni kitu cha kushangaza kwamba ingawa kiasili umetokea Hijaz (Arabia) na umeishi Iran kwa muda mfupi, bado unawaunga mkono Wairani, na kuwaita wafuasi wa Ali, ambaye yeye mwenyewe alikuwa mtiifu kwa Allah. Lakini Mashia wa Iran wanamchukulia Ali kama ni Mungu.

Hapa kuna baadhi ya beti kutoka kwa washairi wa Kiiran wakiashiria hoja hii, ambapo Ali mwenyewe alilaani imani kama hizi. Mwisho wa beti hizi unaonyesha Ali akisema: “Nani anasaidia wakati wa matatizo! Ni mimi ambaye ni Mungu! Ni mimi.” Ubeti wa mshairi mwengine unasema: “Kulingana na iman ya wale ambao wana akili na wanamtambua Mungu, Mungu ni Ali na Ali ni Mungu.”

Muombezi: Nashangaa kwanini, bila kufanya uchunguzi, uweze kuwatuhumu Wairani wote kuwa wanamchukulia Ali kama Mungu. Wanachuo wenu wenyewe wamefanya madai ya kishabiki kama haya. Wamesema kwamba Mashi’a wanamwabudu Ali na kwa ajili hiyo wao ni Makafiri. Kwa hiyo kuwaua wao ni wajib. Matokeo yake Waislamu wa Uzbekistan na Turkistan kwa ukatili mkubwa wakamwaga damu za Waislamu wa Iran.

Watu wa kawaida miongoni mwa Masunni mara kwa mara wanapotoshwa na baadhi ya Ulamaa wenu, na watu wenu wanawachukulia Wairani kuwa ni Makafiri.
Katika wakati uliopita, watu wenu Wa-Turkomania wameshambulia msafara wa Wairani karibu na Khorasan, wakawanyang’anya na kuwaua watu, na kusema kwamba, yeyote atakayeua marafidh saba (yaani Shi’a) atakuwa na uhakika wa kwenda peponi.

Yakupasa uweke akilini kwamba lawama za kuhusika na mauaji haya zinakuwa moja kwa moja juu ya viongozi wenu, ambao huwaambia Masunni wasio na elimu kwamba Mashi’a wanamuabudu Ali.

Uislamu Unakataza Kujigamba Kuhusu Nasaba.

Nikirejea kwenye nukta yako ya kwanza kwamba, kwa kuwa mwanzoni nilihusiana na Arabia, Makka ma Madina, kwanini niwaunge mkono Wairani. Nakuambia kwamba mimi sina tabia ya ushabiki wa kitaifa.

Mtume wetu (s.a.w.w.) amesema: “Waarabu wasijigambe kwamba wao ni bora kwa wasio Waarabu na kinyume chake; na weupe wasijigambe kwa ubora kwa weusi na kinyume chake. Ubora uko tu katika elimu na uchaji. Katika Qur’ani Tukufu Allah (swt) anasema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُمْ مِنْ ذَكَرٍ وَأُنْثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِنْدَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ {13}

“Enyi watu! Hakika tumekuumbeni ninyi mume na mke; na tumekufanyeni mataifa na makabila ili kwamba mpate kujuana; hakika aliye mbora sana miongoni mwenu mbele ya Allah ni yule amchae Allah zaidi…” (49:13).

Vile vile katika Sura hiyo hiyo ndani ya Qur’ani Anasema:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ {10}

“Kwa hakika Waumini wote ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu na mcheni Allah ili mrehemiwe.” (49:10).

Kwa hiyo, watu wote, Waasia, Waafrika, Wazungu, Waamerika weupe, weusi, wekundu au manjano, makabila yote ambayo ni Waislamu ni ndugu, na hakuna hata mmoja anayeweza kudai ubora juu ya mwingine. Kiongozi mkubwa wa Waislamu, Mwisho wa Mitume, alitenda juu ya msingi huu. Alionyesha mapenzi yake makhususi kwa Salman Farsi wa Iran, Suhaib wa Asia ndogo, na Bilal wa Abysinia (Uhabeshi – Ethiopia ya sasa).

Na kwa upande mwingine alimpuuza Abu Lahab (ambaye jina lake lina maana ya Baba wa Miali ya Moto), ami yake mwenyewe ambaye amelaaniwa katika Sura ya Qur’ani Tukufu ambayo inasema:

تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ {1}

“Imeangamia mikono miwili ya Abu Lahab! Naye amekwisha angamia…” (111:1).

Uislamu Vile Vile Unakataza Ubaguzi (Wa Aina Zote).

Ulimwengu umeshuhudia matatizo ya taratibu mbaya mno katika nchi za Maghribi ambayo yalikuwa ni matokeo ya ubaguzi wa rangi. Katika nchi hizo weusi hawaruhusiwi kwenye mahoteli, migahawa, makanisa, na sehemu nyingine za mikusanyiko iliyokusudiwa kwa weupe tu. Uislamu ulipiga marufuku taratibu hizo za kikatili miaka 1300 iliyopita na kutangaza kwamba Waislamu, bila kujali kabila, rangi, au utaifa wote ni ndugu. Hivyo Waarabu wakienda kombo, nitawalaumu, na nitakuwa rafiki wa Mashi’a wa Iran.

Pili, umewahusisha Mashabiki (wakereketwa) wa Kiiran (Maghullat) na Mashi’a ambao ni Madhubuti, wenye kuabudu Mungu Mmoja (yaani Allah) na kumfuata Ali kutokana na Maamrisho ya Mtume (s.a.w.w.) Tunamchukulia Ali kama mja mcha Mungu wa Allah na aliyechaguliwa na Allah kuwa mrithi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Lawama Kwa Mashabiki Washupavu (Maghullat).

Aidha, tunawapuuza wale ambao iman zao ni kinyume na sisi, kama Saba’iyya, Khitabiyya, Gharabiyya, Allawiyya, Mukhammasa, Bazighiyya, Nussairiyya, ambao wametawanyika nchini Irani kote, Mosul, na Syria. Sisi Mashi’a tuko tofauti nao na tunawaona wao kuwa ni Makafir.

Katika vitabu vyote vilivyoandikwa na Maulamaa wa Kishi’a na Wanachuo wa Shari’ah, Maghulamu wamechanganywa pamoja miongoni mwa Makafir, kwa vile imani yao ni kinyume na misingi ya Ushi’a. Kwa mfano, wanahoji kwamba, kwa vile kuingia kwa roho katika umbo la mwili inawezekana (kama Jibril alivyoweza kujitokeza mbele ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika umbo la Dahiyya-e-Kalbi), ilikuwa ni Mapenzi ya Allah kwamba Nafsi yake tukufu ionekane katika umbo la mwanadamu, katika mwili wa Ali.

Kwa sababu hii wanakiona cheo cha Ali kuwa ni kikubwa kuliko cha Mtume. Jambo kama hilo lilijitokeza wakati wa Ali mwenyewe. Baadhi ya watu kutoka India na Sudan walikuja kwake na kutamka kwamba yeye alikuwa Mungu. Mara kwa mara Ali aliwakataza kushikilia itiqadi hii, lakini hakuna athari iliyotokea (hawakuacha).

Hatimaye, kama ilivyoandikwa katika vitabu vingi vya Tarekh, Ali aliamrisha wauwawe ndani ya visima vya moshi. Maelezo ya habari hii yameandikwa katika Baharu’l-Anwar, Juz. 7, na mwanachuoni mkubwa, Agha Muhammad Baqir Majlis. Amir’l-Mu’miniina na Maimam wengine waliwalaumu vikali sana watu kama hawa. Ali alisema: “Ee Allah ninakibeza kikundi cha Ghulat, kama vile Isa alivyowabeza Wakristo.

Ikiwezekana uwatelekeze hao daima.” Katika wakati mwengine alisema: “Kuna makundi mawili ambayo yatapatwa na vifo vya kufedhehesha, na mimi siwajibiki nao (kwa vile ninavidharau vitendo vyao): Hao ni wale wanaozidisha mipaka halali ya mapenzi kwangu, na hao ni Ghullat, na wale ambao bila sababu yoyote ile, wana uadui juu yangu. Nawachukia wale ambao wanatukuza cheo changu kupita mipaka yake halisi.”

Vilevile alisema: “Kuna makundi mawili yaliyojihusisha na mimi yatapata shida ya kifo cha aibu: Moja ni lile lililo na watu ambao wanasema ni marafiki na kunitukuza kupita mipaka ya halali; jingine lina maadui ambao wanatweza hadhi yangu.”

Mashi’a wanawalaumu wale ambao wanamtukuza Ali na Ahlul Bait wake kupita mipaka iliyoamriwa na Allah na Mtume (s.a.w.w.). Maulamaa wetu kwa pamoja wamewachukulia wote hao kwamba ni Makafir. Hairuhusiwi kuhudhuria mazishi yao au koleana nao. Vilevile wananyimwa kurithi mali ya Waislamu; sadaka na kodi za kidini haziwezi kupewa wao. Qur’ani Tukufu inawalaumu katika maneno haya:

“Sema: Enyi watu wa Kitabu msipite kiasi katika dini yenu bila ya haki. Walamsifuate matamanio ya watu waliokwisha potea toka zamani, na wakapoteza wengi, na wenyewe wakapotea njia iliyo- sawa.” (al-Maidah; 5:77).

Allama Majlisi katika Kitabu chake “Baharu’l-Anwar” Juz. 3 ambacho ni ensaklopidia (kitabu cha maarifa yote) ya itiqad ya Shi’a, ameandika hadith nyingi kuwalaumu Ghullat. Imam Ja’far Sadiq (a.s.) ananukuliwa akisema, “Sisi ni waja wa Allah, ambaye ametuumba na akatufanya sisi kuwa bora kwa viumbe wake wengine. Hakika sisi tutakufa na tutasimama mbele ya Allah kwa ajili ya hesabu. Yule ambaye ni rafiki ya Ghullat ni adui yetu; na yule ambaye ni adui yao huyo ni rafiki yetu. Maghullat ni makafir na Washirikina; laana naiwe juu yao.”

Kiongozi mkubwa wa dini wa Mashia vilevile amemnukuu Imam huyu huyu akisema: “Laana ya Allah iwe juu ya wale ambao wanadai Utukufu na Umungu kwa Ali. Kwa jina la Allah, Ali alikuwa ni mja mtiifu wa Allah. Laana iwe juu ya wale waliotukashifu sisi; baadhi ya watu wanasema mambo kuhusu sisi ambavyo sisi wenyewe hatuyasemi. Tunasema wazi kwamba hatuna uhusiano nao.”

Sheikh Saduq (Abu Ja’far Muhammad bin Ali) Faqih mwenye kuheshimiwa sana (Mwanachuo Shari’ah) wa Mashia, anamnukuu Zarara bin A’yun, mwandishi wakuamini- ka wa Kishia, ambaye alikuwa Hafidh na Sahaba wa Imam Muhammad Baqir na Imam Ja’far Sadiq, akisema: “Nilimueleza Imam Ja’far Sadiq kwamba mmoja kati ya watu anayejulikana kwake, huamini katika Tufiidh (uwakilishi wa mamlaka ya Mungu). Imam akasema: ‘Ina maanishwa nini kwa Tufwidh?,’
Nikajibu. ‘Yule mtu anasema kwamba, Allah alimuumba Muhammad na Ali na kisha akakabidhi Mamlaka yake kwao juu ya mambo ya watu. Hivyo wao ndio waumbaji, watoaji wa chakula, wao wahuishaji na wao ndio wenye kufisha.’

Mtukufu Imam akasema: “Adui huyo wa Allah, anaongopa. Wakati utakaporudi kwake, msomee Aya hii kutoka katika Qur’ani Tukufu “…… au wamemfanyia Allah washirika ambao wameumba kama alivyoumba Yeye, kwa hiyo alivyoviumba vikawababaisha (akili)? Sema Allah ndiye Muumbaji wa kila kitu na ni mmoja tu, Mwenye Enzi Kuu.” (13:16).

Mashi’a Wako Tofauti Na Ghullat.

Sisi Shi’a ni tofautli na Ghullat. Waache wadai kwamba wao ni Mashi’a, Mwenyezi Mungu, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), Ali, na kizazi chao wanawachukia.

Ali alimuweka mkubwa na Ghullat jela kwa muda wa siku tatu, na akamuamuru atubie kwa uovu wake.

Alipokataa Ali alimfanya achomwe mpaka akafa. Kama huwezi kutoa angalau kitabu kimoja ambacho ndani yake Ghullat wametukuzwa, basi angalau uwalaumu Maulamaa wasio wavumilivu ambao wanawapotosha Masunni kuhusu Mashi’a.

Ufafanuzi Kuhusu Heshima Kwa Maimam.

Hafidh: Ushauri wako wa Kindugu unafaa kufikiriwa. Lakini tafadhali, je unaweza kufafanua nukta nyingine zaidi? Umesema muda wote kwamba hamuwatukuzi Maimam wenu kupita kiasi. Mnawaona Ghullat kama watu duni (wasiostahili heshima) na wanaofaa kwenda jahannamu, lakini unatumia maneno yasiyostahili kwa mintarafu ya Maimam wenu.

Umesema “Rehema za Allah ziwe juu yao”, ingawa unajua kwamba, kwa mujibu wa Qur’ani, neno hili limetengwa kwa ajili ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) tu. Qur’ani inasema:

إِنَّ اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ {56}

“Hakika Allah na Malaika wake wanamtakia Rehema Mtume. Enyi ambao mmeamini mtakieni rehema juu yake na Msalimuni kwa (uzuri) wa Salamu.” (33:56).

Mwendo wako huo unakiuka kiwazi kabisa hukumu ya Qur’ani. Neno lako hilo ni Uzushi (bida’a).

Muombezi: Aya hii haitukatazi kumuombea rehema mtu wengine yoyote. Tunaamrishwa kumuombea Rehema Mtume. Katika Aya nyingine ya Qur’ani Tukufu, Allah anasema. “Amani na iwe juu ya watu wa Ya Sin (Ahl Ya Sin),” yenye maana ya kizazi cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Ama kwa Mitume wengine wa Allah, kuombea rehema hakukutolewa pamoja na vizazi vyao popote katika Qur’ani. Kuombea rehema kumetolewa tu kwa Mitume wa Allah.

سَلَامٌ عَلَىٰ نُوحٍ فِي الْعَالَمِينَ {79}

“Amani na Salaam kwa Nuh miongoni mwa Mataifa.” (37: 79).

سَلَامٌ عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ {109}

“Amani na Salaam kwa Ibrahim.” (37:109)

سَلَامٌ عَلَىٰ مُوسَىٰ وَهَارُونَ {120}

Amani na Salaam kwa Musa na Haruni.”(37:120).

Watu Wa Ya Sin Inawahusu Watu Wa Muhammad

Wafasiri wote na Wanachuo wa madhehebu yenu wenyewe wanakiri kwamba Allah amemuita Mtume kwa jina Ya Sin. Hivyo basi Ahli (watu wa) Ya Sin maana yake ni watu wa Muhammad. Miongoni mwa wengine, Ibn Hajar Makki, Mwanachuo wa Kisunni mchungu sana kwa Shia, anasema katika “Sawa’iq Muhriqa” chini ya aya zilizonukuliwa katika kuwasifu Ahlul Bait, kwamba kikundi cha Wafasiri wamemnukuu Ibn Abbas (Mfasiri, na mkubwa wa Waumini) akisema kwamba Ahl Yasin maana yake ni Ahl Muhammad.
Kwa hiyo, Salaam, maamkuzi ya amani kwa Ahli Ya Sin yana maana Salaam kwa Ahli Muhammad. Imam Fakhru’d-Bin Razi anaandika: “Ahli Bait wa Mtume wako sawa naye katika mambo matano:

1) Salaam: Salaam kwa Mtume na Salaam kwa Ahli Ya Sin (Ahli Muhammad) ni kitu kimoja.

2) Salawat (kutakia rehma) katika Swala kwa Mtume na Ahlul Bait wake, ambako ni laz- ima.

3) Tohara: Allah Anasema katika sura ya “Ta Ha” (20:1): “(Ewe Mtume) Msafi na tohara:” Ile aya ya tohara iliteremshwa katika kuwatukuza Ahlul-Bait (33:33).

4) Uharamu wa Sadaka: Sadaka haiwezi kupokelewa imma na Mtume au Ahlul-Bait wake. Mapenzi:

5) Mapenzi: Mapenzi kwa Mtume maana yake nimapenzi kwa Ahlul Bait wake.

Allah Anasema:

قُلْ إِنْ كُنْتُمْ تُحِبُّونَ اللَّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ{31}

“Sema: kama mnampenda Allah, basi nifuateni mimi, Allah atakupendeni ninyi…”(3:31)

Na kuhusu Ahlul Bait Allah Anasema:

ۗ قُلْ لَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا إِلَّا الْمَوَدَّةَ فِي الْقُرْبَىٰ ۗ{23}

“Sema: Sikuombeni malipo yoyote kwa haya bali Mapenzi kwa Ndugu wangu wa karibu” (42:23).

Salawat Juu Ya Muhammad Na Aali - Muhammad Ni Sunna (Iliyokokotezwa),

Na Katika Swala Za Faradhi Ni Wajibu.

Wengi wa wasimuliaji wa Hadith hususan Bukhari katika Sahih yake Juz. 3, na Muslim katika Sahih yake Juz. 1 Sulayman Balkhi katika Kitabu chake “Yanabiu’l-Mawadda”, na hata Ibn Hajar katika Kitabu chake “Sawa’iqi” wanamnukuu Ka’b bin Ajza akisema: “Wakati Aya: ‘Hakika, Allah na Malaika wake wanamtakia rehema (wanamswalia) Mtume” (33:56) ilipoteremshwa, tulimuuliza Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), namna gani tutaomba rehema kwa ajili yako, Ewe Mtume wa Allah,?” Mtume akajibu, “Ombeni juu ya rehema (Swalawat) zenu kwa namna hii. “Ee Allah teremsha rehema kwa (Mtume) Muhammad na Aali Muhammad.’”

Imam Fakhru’d-Din Razi, katika Juzuu ya 6, ya Kitabu chake “Tafsir-e-Kabir” pia anasimulia hadithi kama hiyo. Ibn Hajar, akisherhesha juu ya hadith hiyo, anaonyesha kwamba, ni wazi kutoka katika Hadithi hii kwamba kuomba rehema kwa ajili ya Mtume ni sawa sawa na kuomba rehema kwa kizazi chake pia. Vilevile anamnukuu Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akisema: “Msiniswalie (Msiniombee) Swalawat kigutu.”

Alipoulizwa anamaanisha nini kwa Swalawat kigutu; akasema: “Msiseme, ‘Allahumma swali Ala Muhammad,” (Ewe Allah Mrehemu Muhammad) bali semeni, Allahumma swali Ala Muhammad wa Ala Aali Muhammad.”

Dailami anaandikwa kwamba, Mtume alisema: “Sala zetu hubakia zimezuiliwa mpaka tuombe Swalawat juu ya Mtume na Ahlul (watu) wake” Imam Shafi’i anasema: Enyi Ahlul Bait (watu wa Nyumba ya Mtume) Allah Amefanya mapenzi kwenu kuwa ni wajib (lazima) kwetu sisi katika Qur’ani Tukufu.

Kwa mintarafu ya ubora wenu, Cheo na Sifa zenu, inatosha kujua kwamba kama mtu hakuomba Swalawat (rehema) kwa ajili yenu, Sala yake haikubaliwi.” Kama Swalawat kwa ajili ya Mtume na Dhuria (kizazi) wake inaachwa kwa makusudi, basi swala hiyo ya wajib inakataliwa. Na Mtukufu Mtume amesema: “Sala ya wajib ni nguzo ya iman; kama Sala ikikubaliwa, matendo mengine yote (ya ibada) yanakubaliwa; kama imekataliwa, matendo yote mengine yanakataliwa.”

Kuomba Swalawat kwa ajili ya Ahlul-Bait ni Sunna iliyokokotezwa na ni namna ya ibada ambayo ilikuwa ikifanywa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe. Tunaona fahari kufanya kile ambacho Qur’ani Tukufu na Mtume (s.a.w.w.) wametuarimsha sisi kufanya.