read

Hadithi Zisemazo Kuwa Ataonekana

Anasimulia Abu Huraira katika Hadithi aliyoipokea kuwa: (siku ya kiyama) "Mwenyeezi Mungu atawaijia (watu) akiwa na sura tofauti na ile wanayomjua, awaambie: Mimi ndiyo Mola wenu. (Watu) watajibu:

Mwenyeezi Mungu atuepushe nawe, sisi tutabaki hapa hapa mpaka Mola wetu (tunayemjua) atufikie, na akija sisi tutamjua. Mara Mwenyeezi Mungu atawafikia kwa sura yake ile wanayomjua atasema: Mimi ni Mola wenu. Nao watajibu: (kweli) wewe ndiye Mola wetu, na watamfuata".

Taz: Sahihi Bukhari J. 4 Uk. 92

Sahihi Muslim J. 1 Uk. 86

Tafsirul Khazin J. 7 Uk. 137

Abu Huraira anaendelea kusimulia: "Watu walimuuliza Mtume (s.a.w.) 'Ewe Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu! Hivi tutamuona Mola wetu siku ya kiyama?' Mtume (s.a.w.) akajibu: 'Hivi mnapata pingamizi gani kwa kutazama mwezi wa siku kumi na tatu?'

Wakajibu: 'Hatupati pingamizi yoyote.' Mtume (s.a.w.) akauliza tena: 'Mnapata kizuizi gani kutazama jua ambalo halina mawingu?' Wakajibu: 'Hakuna kuzuizi chochote.' Mtume (s.a.w.) akawaambia: 'Basi ndivyo matakavyomuona".

Suhaybu anasimulia kuwa: Amesema Mtume kuwa:

"Watu wa peponi watakapoingia Peponi, Mwenyeezi Mungu atawauliza: 'Mnataka niwaongeze kitu gani?'

Watasema: 'Oh, umekwisha ng'arisha nyuso zetu, umetuingiza peponi na umetuepusha mbali na moto.' (Hapo) Pazia litaondolewa, eeh, hawajapewa kitu kilicho bora zaidi kuliko kumuona Mola wao. Kisha Mtume (s.a.w.) akasoma aya:
"Wale waliofanya wema watapata wema na zaid". 10:26
Iliposemwa: (katika Aya iliyotangulia), "WAZIYADAH" maana yake, KUMUONA MWENYEEZI MUNGU"

Taz: At'targhib Wat'tarhib J. 4 Uk. 551

Majibu Yetu

Tamko la "AZZIYADAH" katika sura ya kumi aya ya ishirini na sita ni: MUB'HAM halionyeshi chochote kuhusu kuona. Kwa hiyo, huwezi kwa tamko hilo kuthibitisha kuwa Mwenyeezi Mungu anaonekana. Bali lililothibiti waziwazi ni hivi asemavyo Mwenyeezi Mungu kuwa

"Maono hayamfikii bali yeye anayafikia "Maono", 6:103.

Kwahiyo, zile hadithi zisemazo kuwa Mwenyeezi Mungu anaonekana ni batili kwa sababu zinapinga Aya. Mwenyeezi Mungu anakataa kuwa: "Maono hayamfikii" na maono ni zaidi kuliko macho!!