read

Israa Na Miiraji

Israa ni: Mwendo wa usiku, kama ilivyokuja katika Qur'an: "Utukufu ni wa yeye ambaye alimpeleka Mja wake usiku, kutoka Msikiti mtukufu (wa Makka) mpaka Msikiti wa mbali (Falastin) ambao tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake, ili tumuonyeshe baadhi ya ishaara zetu" 17:1

Miiraji ni: Msafara ulioanzia katika Msikiti wa Falastin kwenda juu. Tukio la Israa limepokewa na waandishi wa Tarikh kwa njia tofauti, kuna wanaosema kuwa Israa ilitokea mwaka wa kumi na mbili baada ya kupewa Utume, Wengine wanasema ilikuwa mwaka wa kumi na moja, wengine mwaka wa kumi, wengine mwaka wa tano, wengine mwaka wa tatu na wengine mwaka wa pili.

Taz: Albidayatu Wannihaya J. 3 Uk. 108

Tarikhul Khamisi J. 1 Uk. 307

Assahihu Minsiiratin Nabi J. 1 Uk. 269

Kauli ya sawa katika mjadala huu ni: Israa imetokea katika mwaka wa tatu kwa sababu zifuatazo"

Mtume (s.a.w.) alikuwa akipendelea sana kumbusu binti yake Mwana Fatima (a.s) mpaka Mwana Aisha (mkewe Mtume) likamuudhi sana hilo, akasema: "Ewe Mtume wa Mwenyeezi Mungu! Una nini? Kila mara ninakuona sana unambusu Mwana Fatima kama unayekula asali!! Mtume (s.a.w.) akamjibu: "Ni kweli, ewe Aisha! Mimi nilipopelekwa juu (Miiraji) Malaika Jibril (a.s.) aliniingiza Peponi humo nilikula Tunda fulani, likabaki mgongoni, niliposhuka nilimwingillia Khadija (mkewe) mara akapata ujauzito wa Mwana Fatima kutokana na hilo tunda. Na yeye ndiye Tunda bora, kila ninapokumbuka Peponi, humbusu Fatima".

Taz: Tarikh Bughdad J. 5 Uk. 87

Mizanul'itidal J. 2 Uk. 297

Mustadrakul Hakim J. 3 Uk. 156

Majmauz Zawaid J. 9 Uk. 202

Kanzul Ummal J. 14 Uk. 97

Dhakhaairul U'qbaa Uk. 36

Katika hadithi hii tunajifunza kuwa: Mwana Fatima (a.s.) amezaliwa mwaka wa tano baada ya Biitha (kupewa Utume) kwa hiyo, Israa na Miiraji ilikuwa kabla ya kuzaliwa Mwana Fatima, kwa sababu Mwana Fatima ni Tunda la peponi alilokula Mtume siku aliyopelekwa Miiraji. Tunda lililobaki mgongoni kwake hata baada ya miaka miwili akazaliwa Fatima, Bibi bora kabisa katika mabibi wa Peponi - Hadithi.

Mtume (s.a.w.) alipopelekwa juu (Miiraji) Malaika walikuwa wakiuliza kila mahala Je! Muhammad amekwisha pewa Utume? Hili linaonyesha kuwa Tukio la Israa na Miiraji lilitokea katika miaka ya awali ya Utume, wala siyo baada ya miaka kumi na mbili. Kwa sababu ingekuwa hivyo bila shaka suala la Utume lingekwisha eleweka zamani pasingekuwepo haja ya kuliuliza. Israa na Miiraji ilitokea kabla ya kusilimu Abubakr bin Abi Quhafa, kwa sababu, Abubakr amesilimu baada ya miaka mitano ya biitha.

Taz: Assahihu Minsiiratin Nabii J. 1 Uk. 274

Usudul Ghaba J. 4 Uk. 18

Ikiwa Israa na Miiraji imetokea kabla ya kusilimu Abubakr, basi madai ya Laqabu isemwayo kuwa alipata Abubakri ya "SIDDIQ" yanatupwa: Kwa sababu ikiwa laqabu hiyo (kama inavyodaiwa) alupata baada ya kusadikisha msafara wa Mtume (s.a.w.) aliopelekwa katika Israa na Miiraji. Litawezekanaje hilo, ilihali wakati wa tukio la Israa na Miiraji Abubakri alikuwa kafiri! Hapo tasdiq itapatikana?!

Mtume Alikwenda Mwenyewe Au Ni Njozi?

Tukio la Israa, wako baadhi ya Waislamu wanao ona kuwa Mtume (s.a.w.) alioteshwa na wala hakwenda mwenyewe akiwa macho. Na mategemeo yao ni ile habari aliyoisimulia Mwana Aisha kuwa: "Siku hiyo hakukikosa kiwiliwili cha Mtume".

Taz: Tarikhul Khamisi J. 1 Uk. 308

Al' mawahibul laduniyya J. 2 Uk.2

Majibu Yetu

Mwana Aisha wakati wa tukio hilo alikuwa hajaolewa na Mtume, bali yaelekea hata kuzaliwa alikuwa bado!!

Mwenyeezi Mungu anasema: "Utukufu ni wa yeye ambaye alimpeleka Mja wake usiku, kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa mbali" 17:1. lliposemwa: "ASRAA BIA'BDIHI" tamko la "A'BD" hutumiwa kwa roho na kiwiliwili pamoja. Kwa hiyo, Mtume (s.a.w.) alikkwenda mwenyewe akiwa macho.

Kama Israa ingelikuwa kwa njozi, basi kusingekuwako na upinzani mkubwa hivyo, na watu wasingeritarddi.

Taz: Tafsir ibn Kathir J. 3 Uk. 24

Tarikhul Khamisi J. 3 Uk. 308

Almuswannaf J. 5 Uk. 327

Kama Israa ingelikuwa kwa njozi, basi Abu Talib na Bani Hashim wasingetoka kumtafuta, kwa sababu Bani Hashim walitoka kumtafuta siku hiyo.

Taz: Assahihu Minsiiratin Nabii J. 1 Uk. 276