read

Majibu Yetu

Kabla ya kuingia katika majadiliano hayo ni vyema kuzingatia jambo mmoja, nalo ni "NINI QUR'AN"? Taarif ya Qur'an ni: "Maneno ya Mwenyeezi Mungu aliyoyateremsha kwa Mtume wake Muhammad (s.a.w.) hali yakuwa ni muujiza wake" sasa, Ikisemwa kuwa: Mtume (s.a.w.) hakuwasomea Qur'an maiti wake, huwa inakusudiwa Qur'an gani?? Kwa sababu, katika salatiil maiti mna Suratul Fatiha, na Mtume (s.a.w.) aliwasalia mauti wake. Isipokuwa, ikithibitishwa kwa dalili kuwa: Suratul Fatiha si Qur'an1

Kuhusu Aya iambiwayo kuwa inazuia thawabu za Qur'an kumfikia maiti 53:39 tuangalie matni yake: "WA AN LAYSA LIL'INSANI ILLA MASAA", yaani, "Na yakwamba mtu hatapata isipokuwa aliyo yafanyia juhudi." Hivi ndivyo ananyosema Mwenyeezi Mungu na wala hasemi: "LA YANTAFIU'UL INSANU ILLA MASAA", yaani, "Hanufaiki mwanadamu isipokuwa kwa yale aliyoyafanyia juhudi". Hapa pana tofauti kubwa kati ya ibara ya kwanza na hii ya pili. Ibara ya kwanza inafidisha kuwa: "Mwanadamu atalipwa thawabu kwa mujibu wa matendo yake". Na ibara ya pili inafidisha kuwa: "Mwanadamu hanufaiki kwa chochote isipokuwa kwa matendo aliyoyatenda mwenyewe."

Kwa ibara hizi ni sawa na kusema kuwa: "Athumani ana kibanda kidogo cha makuti, na humo ndimo anamoishi. Kwa hiyo, Athumani hana nyumba nyingine yoyote atakayoishi isipokuwa katika kipanda hicho.

Lakini hali hii haizuii yeyote mkarimu kumjengea Athumani nyumba kubwa na bora.

Mkarimu kama atajenga nyumba iliyo bora na kubwa, kisha akampa Athumani, haiwezi kusemwa: Athumani hawezi kukaa katika nyumba hiyo eti kwa sababu hakuijenga yeye.

Amma Hadithi iamiwayo kuwa iazuia thawabu ya Qur'an kumfikia maiti isemayo: "IDHA MATA IBNU ADAMA IN'QATAA A'MALUHU ILLA MIN THALATHA..." yaani, "Anapokufa Mwanadamu matendo yake yote hukatika isipokuwa mambo matatu...." wala Hadithi haisemi: "IDHA MATA IBNU ADAMA IN'QATAA INTIFAU'HU" yaani, "Anapo kufa Mwanadamu humalizika kunufaika kwake". Ibara ya kwanza inafidisha kuwa: "Kinachomalizika ni matendo yake". Na ibara ya pili inafidisha kuwa: "Kinachomalizika ni kunufaika". Kwa mizani ya somo hili, natija inaonyesha kuwa Qur'an ikisomwa kwa ajili ya maiti, lazima thawabu ya kisomo hicho zitamfikia maiti, na hapa tutaonyesha hali tatu zilizo hai:

Mtume (s.a.w.) amesema:- "MAN MATA WA A'LAYHI SIYAM SAMA A'NHU WALIYYUHU". yaani, atakae kufa na juu yake kuna saumu atafunga kwa niaba yake walii wake". Hadithi hii imekubaliwa na Waislamu wote na hata Imam Shafi naye ameikubali. Je! Kama mlango wa kunufaika umefungwa, thawabu ya funga anayofanyiwa maiti na walio hai ingemfikiaje?

Mtume (s.a.w.) alimwambia mwanamke mmoja: "Mhijie mama yako". Na akamwambia mwanamume: "Mhijie baba yako". Hadithi hii pia imekubaliwa na Waislamu wote, Je! Thawabu za hija anayohijiwa na walio hai zinamfikiaje maiti, kumbe mlango wa kunufaika umefungwa??

Mwenyeezi Mungu anasema:
"Zinamtukuza mbingu saba na ardhi (saba) na vilivyomo ndani yake, na hakuna chochote isipokuwa kinamsabihi kwa sifa zake njema lakini nyinyi hamfahamu kutukuza kwao" 17:44. Iliposemwa: "Na hakuna chochote isipokuwa kinamsabihi kwa sifa zake njema". Hii inafidisha kuwa: Vitu vyote vinamsabihi Mwenyeezi Mungu, na kwa kuelewa zaidi hili tumsikilize Mtume (s.a.w.). Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Mtume (s.a.w.) alipita kwenye makaburi mawili akasema: Hawa waliomo katika makaburi haya wanaadhibiwa...
Mara akaagiza kuti la mtende, akalipasua vipande viwili kisha akachimbiaa kimoja katika kaburi hili na kingine akachimbia katika kaburi lile, halafu akasema: Bila shaka vitawapunguzia (adhabu) madam havijakauka". Hiposemwa: "Madam havijakauka" inafidisha kuwa: Wakati wote vitakapokuwa vibichi (vipande vya kuti Ia mtende) vitakuwa vinamsabihi Mwenyezi Mungu. Hapa Mtume (s.a.w.) ana thibitisha kuwa: Tasbihi za kuti zina mpunguzia adhabu maiti, kupunguziwa adhabu ni hatua ya kuingia mtu katika neema (pepo). Mpenzi msomaji! Tasbihi za kuti la mtende zitampa nafuu maiti, lakini Mwislamu akisoma Qur'an kwa ajili ya kumuombea maiti itakosa kumfikia??

Taz: Tafsirul Qurtubi J. 10 Uk. 267

  • 1. Tarehe 18-8-1984 katika mkoa wa Mwanza Tarafa ya Nyakato Kijiji cha Buzuruga, kulitokea tatizo kubwa lililosababishwa najeshi la jadi Ia sungusungu. Jeshi la jadi la sungusungu kwa makusudi kabisa, ililiivamia nyumba ya MwisIamu, likaingia ndani na kuchanachana vitabu vitano vitakatifu vya Kiislamu. YASIN NDOGO (b) MAJMUUL MUBARAK (c) IRSHADUL MUSLIMINA (d) HADITHI ZA MTUME (e) AHLUL BADR.

    Kisha Sheikh Mkuu wa Tanzania alitoa fat'wa kwa kupitia Redio Tanzania kuwa: "Qur'an haikuchanwa" ingawa kwa maelezo yao - kama yalivyo kwenye kitabu: "Taarifa ya ujumbe wa Sheikh Mkuu" ukurasa 14 inasema: "Irshadul Muslimina kilichanwa kwa dharau" mwisho wa kunukuu. Kwa hiyo, Irshadul Muslimina iliyochanwa kwa dharau, ukikifunua kitabu hicho ukurasa wapili katika mlango wa kwanza utaiona Aya ya kumi na nane na ya kumi na tisa nusu yake, za Suratul Jathia.

    Bakwata inasema: Qur'an haikuchanwa lakini aya mbili katika Suratul Jathia zimechanwa kwa dharau!!! Sijui kwa Bakwata Qur'an inathubutu kwa vipi! Kwa kukamilika Sura ngapi au Aya ngapi hata isemwe ni QUR'AN? Kwa nini washutumiwe na kulaniwa watu wanaopendekeza kuwa: Sharia ya Mirathi na ya ndoa zifanyiwe marekebisho?? Katika Mirathi wanachoomba iondolewe ni Aya isemayo

    "LIDH'DHAKARI MITHLU H'ADH'DHIL UNTHAYAYNI" 4:11

    katika Ndoa wanaomba iondolewe Aya: "MATHNA WATHULATHA WARUBAA" 4:4 sasa, unaweza kuhesabu silabi za Aya hizi, kisha uhesabu silabi za Aya zilizomo katika vitabu vilivyochanwa. Ndipo utamjua nani mwenye kosa wakufaa kushutumiwa na kulaaniwa! Kwakuwa sheria ni msumeno, hapa napenda kukumbusha baadhi ya matukio kama haya yalioyofanywa na wakubwa. Baada ya kufariki Mtume (s.a.w.) sheria isemayo kuwa "Katika mafungu manane ya sadaka, fungu moja kati ya haya ni la wale wanaoingia Uislamu. Fungu hili lilifutwa!! Na Aya inasomeka hivi: "WAL'MUALLAFATI QULUBUHUM" Taz: Tafasirut Tabari J. 10 Uk. 113 Hukumu ya Aya hii imefutwa, kwa hiyo, maasi ya kunyanyasa sheria ya Mwenyeezi Mungu hayakuanza juzi katika Tarafa ya Nyakato, bali yameanza mbali huko baada ya kufariki tu Mtume (s.a.w.).