read

Musa Na Sala Tano

Imepokewa katika riwaya kuwa: Sala tano zimefaradhiwa wakati Mtume (s.a.w.) alipopelekwa katika msafara wa Miiraji huko juu Inasemwa kuwa, zilifaradhiwa sala hamsini kwa kila siku, na Mtume (s.a.w.) alipokuwa akirudi na agizo hilo, alipofika mbingu ya sita akakutana na Nabii Musa (a.s.) akamshauri Mtume Muhammad (s.a.w.) arudi kwa Mola wake amuombe ampunguzie Sala hizo.

Mtume alirudi kwa Mola wake na akapunguziwa Sala kumi, aliposhuka katika mbingu ya sita akakutana na Nabii Musa akiwa na sala arobaini. Nabii Musa akamrudisha kwa Mola wake apunguziwe Sala hizo, Mtume akafanya hivyo, Mwenyeezi Muungu akapunguza Sala kumi. Mtume alipofika kwa Nabii Musa, akamrudisha kwa Mola wake akaombe takhfif; Mtume alifanya hivyo, Mwenyeezi Mungu akapunguza sala kumi Mtume akashuka alipofika kwa Nabii Musa akiwa na sala ishirini, Nabii Musa akamtaka arudi kwa Mola wake akampunguzie, kwa sababu umma wake hawawezi hilo.

Mtume (s.a.w.) alifanya hivyo, Mwenyeezi Mungu akapunguza Sala kumi, Mtume akashuka akiwa na sala kumi, alipokutana na Nabii Musa akamrudisha kwa Mola wake ili apunguziwe, Mtume alifanya hivyo, Mwenyeezi Mungu akapunguza Sala tano, Mtume (s.a.w.) aliposhuka kwa Nabii Musa (a.s.) akiwa na sala tano, alipotaka kumrudisha kwa Mola wake, Mtume (s.a.w.) alisema:- "Kwa hakika, nimerudi kwa Mola wangu mara tano, kuomba takhfif mpaka sasa naona aibu kubwa". Ndipo aliposhuka Mtume (s.a.w.) akiwa sala tano, ambazo wanapaswa Waislamu kuzisali kwa kila siku.

Uchunguzi

Tunaamini kuwa: "Mwenyeezi Mungu haweki sheria yoyote isipokuwa ina maslahi ndani yake. Kwa mantiq hii, Mtume (s.a.w.) asingehitaji kurudi mara zote hizo kwa ajili ya kupunguziwa. Kwa sababu kufanya hivyo ni kutaka sheria isiyo na maslahi, kama ambavyo sababu zilizompelekea Nabii Musa kutaka zipunguzwe Sala hamsini ni kushindwa kuzitekeleza sala hizo. Kama kwamba Nabii Musa anaamini kuwa Sheria hii (ya Sala hamsim) inakwenda kunyume na maslahi, na hilo ni muhali (haliwezekani) kwa Mwenyeezi Mungu. Aidha, vipi Mwenyeezi Mungu hakujua kuwa: Umma wa Mtume Muhammad (s.a.w.) hauwezi hilo, bali Musa yeye alijue hilo?? Au tuseme, ni takhfif kwa jambo lisilowezekana, vipi, Mwenyeezi Mungu anatwambia wakati wote:
"Mwenyeezi Mungu huwatakieni yaliyo mepesi wala hawatakieni yaliyo mazito". 2: 185.

"Wala hakuweka juu yenu dhiki katika dini" 22:78.
Na vipi Nabii Ibrahim hakushitushwa na misafara ya nenda rudi ya Mtume Muhammad, asimuulize kuna nini! Maana kwa mujibu wa riwaya zinzosimulia tukio hili zinasema kuwa, Nabii Ibrahim (a.s.) alikuwa katika mbingu ya saba na Nabii Musa (a.s.) mbingu ya sita. Aidha, kwanini Mwenyeezi Mungu asimpe moja kwa moja Mtume wake Sala tano, kuliko usumbufu huu alioupata Mtume wa nenda rudi mpaka akaingiwa na aibu kubwa akashuka kwa shingo upande na sala zake tano!!?