read

Mwaka Mpya Wa Kiislaam

Inasemwa kuwa, katika mwaka wa kumi na sita Hijra, masahaba walikutana kujadili juu ya tarehe ya Kiislaamu itakayojulisha mwanzo wa mwaka.

Imam Ali (a.s.) Alisema kuwa: "Ifanywe kuwa ni mwanzo wa mwaka mpya, ile siku Aliyohama Mtume (s.a.w) akaacha ardhi ya shirki"

Taz: Fat'hul Bari J. 7 Uk. 209

Tarikhut Tabari J. 2 Uk. 112

Tarikh Ibn Athir J. 2 Uk.526

Alkhutat wal'athar J. 1. Uk. 284

Kwakuwa maafikiano yamepita kuwa mwanzo wa mwaka wa Kiislaamu uanze kwa kufuata tukio la Hijra, na kwamba Hijra imetokea mfungo sita, basi mfungo tano ni mwezi wa kumi na mbili na mfungo sita ni mwezi wa kwanza wa mwaka mpya wa Kiislaamu.

Muharram Si Mwanzo Wa Mwaka

Baada ya kujua mwaka wa Kiislaam unaanza tarehe gani ya mwezi gani, kisha umeingia utata juu ya jambo hili kuwa: Muharram ndiyo mwanzo wa mwaka wa Kiislaamu kwa maana ya Hijra! Ndiyo maana unaona kila uingiapo Muharram baadhi ya Waislam hufanya hafla kubwa kuadhimisha, wakidhani kuwa umeingia mwaka mpya!!! Ukisoma tarikh utaona kuwa:

Imam Ali (a.s.) alisema mwaka mpya uanze ile siku aliyofukuzwa Mtume (s.a.w.) Makka akaenda Madina.

Imam Ali aliwaandikia watu wa Najran akasema.... "Na aliandika Ubeidullah bin Abi Rafii tarehe kumi mfungo tisa mwaka wa thalathini na saba kutoka Mtume (s.a.w.) aingie Madina".

Taz: Alkharaj Uk. 81

Jamharatu Rasailil ar'b J. 1 Uk. 82.

Imam Malik bin Anas anasema: Mwanzo wa mwaka wa Kiislaamu ni mfungo sita, kwa sababu ni mwezi ambao Mtume (s.a.w.) amehama (kutoka Makka kwenda Madina).

Taz: Albidayatu Wannihaya J. 3 Uk. 207.

Assakhawy amepokea kwa Al'Asmai kuwa wao walikuwa wakiandika mfungo sita, ni mwezi aliohamia Madina Mtume (s.a.w.).

Taz: AI'i'lanu Uk. 78

Amesema Assahib bin U'bbad kuwa: Mtume (s.a.w.) aliingia Madina tarehe kumi na mbili mfungo sita, na tarehe ikaanzia hapo. Kisha baadae jambo hili liligeuzwa likarudishwa mwezi wa Muharram".

Taz: U'nwanul Maa'rif Uk. 11

Kuonekana Kwa Mwenyeezi Mungu

Suala la kuonekana Mwenyeezi Mungu, Waislaamu wamegawanyika makundi mawili, kuna wanaosema kuwa: Mwenyeezi Mungu anonekana hapa duniani na huko akhera. Na kuna wanaosema kuwa: Mwenyeezi Mungu haonekani hapa duniani wala huko akhera. Kila kundi lina hoja zake. Wasemao ataonekana wanategemea hoja mbili: Dalilul a'qly, Dalilun naqly.

Dalilul a'qly - Kwa kupitia mantiq akili inaona kuwa: kwa kuwa chochote chenye kuwapo lazima uwiano wa kuonekana uwepo.

Dalilun naqly: Mwenyeezi Mungu anasema:

Na alipofika Musa kwenye miadi yetu, na akazungumza na Mola wake akasema: "Mola wangu! Nionyeshe ili nikuone." Akasema "Huwezi kuniona, lakini tazama jabali, kama litakaa mahala pake ndipo utaweza kuniona" 7:143

"Nyuso siku hiyo zitang'aa zikitazama kwa Mola wao" 75: 22-23

MAJIBU YETU

Kwanza, ni muhimu kuangalia maana ya tamko la "ARRU-UYA" yaani "KUONA". Taqriban tamko hili linatumika katika nyanja zifuatazo,

(a) Kuona kwa mboni za macho.

(b) Kuona kwa dhana.

(c) Kuona kwa yaqin.

Sasa: Inaposemwa: Mwenyeezi Mungu anaonekana, ni kwa kupitia kigezo gani kati ya vigezo vilivyotajwa hapo juu au chochote kingine. Ikiwa kuwepo kwa kitu ni sharti ya kuonekana, ni nani basi aliyethibitisha mpaka sasa kuwa ameiona Roho, Akili, Nguvu, Sauti, na kadhalika?!

Kuhusu aya zilizosomwa kuthibitisha kuwa Mwenyeezi Mungu anaonekana, majibu yake ni kama ifuatavyo:

Nabii Musa (a.s.) alikuwa akijua vyema kuwa Mwenyeezi Mungu haonekani duniani wala huko akhera. Wala hilo ombi lake hakukusudia kuomba jambo lisilo wezekana, isipokuwa Nabii Musa hapa ametumia uslub (njia) ya kukomesha madai ya watu wake ambao waling'ang'ania kumtaka awaonyeshe Mwenyeezi Mungu waziwazi kama tunavyo soma katika Qur'an: "Ewe Musa, hatutakuamini mpaka tumuone Mwenyeezi Mungu waziwazi". 2:55

Kwahiyo, Nabii Musa (a.s.) alitaka kumaliza ubishi wao, akatumia ibara kati yake na Mola wake ili afute kabisa matumaini ya ombi la watu wake. Qarina ya nukta hii ni pale aliposema Mwenyeezi Mungu kuwa:

"Hakika walimuomba Musa makubwa kuliko hayo, na wakasema: Utuonyeshe Mungu wazi wazi." 4:153

Iliposemwa: "FASAWFA TARAANI" yaani "UTANIONA" ibara hii imetanguliwa na tamko la: "LAN TARAANI" yaani, "HUTANIONA ABADANI" silabi ya "LAN" imekuja katika "NAFYU TAABID" "HUTANIONA ABADAN" matumaini ya kumuona Mwenyeezi Mungu hayako aslan, kwa mujibu wa maweko ya silabi na matumizi yake yaliyokuja katika Aya hii.

Iliposemwa: "ILA RABBIHA NADHIRA". yaani, ZIKINGOJA MALIPO KWA MOLA WAO" na wala si ZIKITAZAMA KWA MOLA WAO, hiyo ni tasfiri ya kimakosa kama tutakavyoonyesha. Ku'unganishwa silabi ya "ILA" na silabi ya "NADHAR" hapa kunafidisha maana yaa "KUNGOJEA"

Tutaonyesha mfano hapa kuthibitisha hilo kama ifuatavyo: katika kitabu: Lisanul A'rab juzu ya saba ukurasa 72 imeandikwa hivi:- "INNAMAA NANDHURU ILA LLAHI THUMMA ILAYKA" akafafanua hapo hapo: "INNAMAA ATAWAQQAU FADHLALLAHI THUMMA FADHLAK" Maana ya msitari wa kwanza "Kwa hakika tunangojea fadhila za Mwenyeezi Mungu, kisha fadhila zako" katika msitari wa pili, alikusudia kufafanua ibara isemayo: "NANDHURU ILA LLAHI" akasema;

"ATAWAQQAU FADHLA LLAHI" yaani, "Ninangojea Fadhila za Mwenyeezi Mungu". Hivi ndivyo yalivyo matumizi ya silabi ya "ILA" inapokutana na silabi ya "NADHAR" mara nyingi.