read

Utangulizi

Alhamdulillah, Rehma na Amani zimshukie Mtume wetu na Muombezi wetu Muhammad (s.a.w.) na Aali zake watukufu waliotakaswa. Ninamshukuru zaidi Mwenyeezi Mungu kwa kuniwafiqisha kuchapisha kitabu: Muongozo wa Wasomao, kama alivyoniwafiqisha kabla ya hiki kuchapisha vitabu: Mut'a ndoa sahihi na Meza ya uchunguzi na vingine vingi, Alhamdulillah, Muongozo wa Wasomao, ni kitabu kilichokusanya maudhui nyingi tofauti kwa muhtasari.

Ndani yake tumejaribu kufafanua baadhi ya mambo yaliyoeleweka kimakosa, kwa kuonyesha ushahidi na rejea zake. Nataraji hili litakuwa ni kichocheo cha wasomi (masheikh) kutufunulia yaliyofichikana au kufahamika kimakosa katika tarikh ili waislamu wapate ufahamu vyema Uislamu wao.

Ee Mola weta! Tuonyeshe Haki tuifahamu kuwa ni haki uturuzuku kuifuata. Na tuonyeshe batil tuifahamu uwa ni batil uturuzuku kuiepuka.

Omar Jumaa Mayunga
9 Shaaban 1413
1 Februari 1993
DAR ES SALAAM

Mwanzo Wa Wahy

Amesema Bukhari na Muslim na wengineo kuwa: Imepokewa kutoka kwa Azzuhry naye amepokea kwa U'rwa bin Zubeir naye amepokea kwa Mwana Aisha (mkewe Mtume) kwamba: Malaika Jibril (a.s) alikuja kwa Mtume (s.a.w.) naye akiwa katika pango la Hiraa akamwambia: Soma, Mtume akajibu: Mimi sijui kusoma. Mtume anasema: Malaika akanikaba kwa nguvu mpaka nikazidiwa kisha akaniambia: Soma, Mtume akajibu: Mimi sijui kusoma. Kisha ndipo Malaika alipomsisitiza kwa nguvu akisema:

"Soma kwa jina la Mola wako, ambaye ameumba. Amemuumba mwanadamu kutokana na damu iliyoganda. Soma na Mola wako ni Mtukufu kuliko wote". Qur'an, 96:1-3

Baada ya hapo, Mtume (s.a.w.) alirudi kwa mkewe mwana Khadija (a.s.) akiwa amejawa khofu kubwa. Alipoingia ndani alijitupa chini na huku akilalamika: "Nifunikeni, nifunikeni!!" Alipotulia akasema: "Ninaogopa sijui kitanipata nini?!" Khadija akamtuliza: "Sivyo! Wallahi Mwenyeezi Mungu hatakuangamiza abadani, wewe unaunga udugu, unavumilia matatizo, unasaidia wanyonge, unasaidia kuleta haki." Hapo Khadija akamchukua Mtume akampeleka kwa Ibnu ammi yake Waraqa bin Nawfal (alikuwa mnasara, mwandishi wa Injili kwa lugha ya kiibrania).

Walipofika kwa Waraqa, Khadija akamwambia: "Ewe Ibnu ammi! Msikilize Muhammad aliyo nayo." Waraqa akamuuliza, "una nini?" Muhammad akamwelezea yote kama aliyoyaona, Waraqa akamwambia: "Huyu ni Malaika ambaye amepata kumteremkia vilevile Nabii Musa (a.s.) Ee!!!" Natamani kama nitakuwa hai wakati watakapokufukuza watu wako!!! Muhammad (s.a.w) akashituka: "Watanifukuza??" Waraqa akajibu: "Ndiyo, hakuna mtu yeyote anayeleta jambo kama hili uliloleta wewe isipokuwa atapigwa vita na watu wake".

Taz: Sahihi Bukhari J.I uk, 5-6

Sahihi Muslim J. I uk, 97

Almuswannaf J. 5 uk, 322

Tarikhut Tabari J. 2 uk, 47

Madda hii (mwanzo wa Wahy) waandishi wameieleza kwa njia nyingi tofauti zenye kugongana. Hapa tutajaribu kuzitaja chache tu:

Khadija na Abubakr walimpeleka Muhammad (s.a.w.) kwa Waraqa bin Nawfal baada ya kuelezwa Waraqa kuwa Muhammad amepata matatizo, Waraqa akamuuliza Muhammad ana nini? Muhammad (s.a.w.) akamwambia:

"Ninasikia ninaitwa nyuma yangu, ewe Muhammad ewe Muhammad, nikisikia hivyo mimi hukimbia ovyo." Waraqa akamkataza asiwe anakimbia bali akaze roho ili ayasikie anayoambiwa..." Muhammad alishika maelekezo hayo, mara aliposikia akiitwa: Ewe Muhammad! Sema, Bismillahir Rahmanir Rahim, Alhamdulillahi rabbil a'lamina.... mpaka mwisho wa suratul Fatiha. Akaambiwa: Sema: "Laa ilaha illallahu" Muhammad (s.a.w.) baada ya hapo alikwenda kwa Waraqa bin Nawfal, akamjulisha hali hiyo. Waraqa akambashiria habari njema yakuwa: "Hali kama hiyo alipewa pia Nabii Isa bin Maryam".

Taz; Albidayatu Wannihaya J. 3 Uk. 9

Assiratun Nabawiyya J. 1 uk 83

Assiratul Halabiyya J. 1 uk 250

Siiratu Mughlataya uk, 15

Khadija alipompeleka Muhammad (s.a.w.) kwa Waraqa na akamweleza yaliyomtokea. Waraqa alisema: "Huyu ni Nabii wa Umma huu, mwambie atulize moyo."

Taz: Albidayatu Wannihaya J.3 uk, 12

Siiratu Ibn Hisham J. 1 uk, 238

Assiratul Halabiyya J. 1 Uk. 239.

Khadija alimwambia Muhammad (s.a.w.) atakapokufikia huyo anayekusomesha, unambie, Mtume (s.a.w.) alipofikiwa na hali hiyo akamjulisha mkewe. Khadija akampakata katika mapaja yake, kisha akavua shungi yake, mara Mtume (s.a.w.) akaona yule aliyemjia anaondoka haraka. Mtume akamjulisha mkewe hilo, Khadija akasema, "Huyo ni Malaika, na wala siyo shetani, basi kaza roho na furahi".

Taz: Assiratul Halabiyya J. 1 Uk. 252.

Waraqa bin Nawfal alimwambia Khadija: "Muulize Muhammad (s.a.w.) nani anaemjia! Ikiwa ni Malaika Mikaeli basi amemletea amani. Na ikiwa ni Malaika Jibril basi amemletea vita na mateka. Khadija Alipomuuliza Mtume (s.a.w.) akajibu: "Ni Jibril". Khadija akapiga uso wake.

Taz: Tarikhul Yaa'quby J. 2 Uk. 23.

Khadija alipewa kipande cha karatasi na mganga mmoja ili ampe Muhammad (s.a.w.) kama hali hii (iliyomfikia Muhammad) inasababishwa na ugonjwa wa kichaa, basi atapona... Khadija aliporudi kwa mumewe akamkuta anasoma Qur'an, Khadija akamchukua akaenda naye kwa yule mganga, walipofika kwa mganga, akafunua mgongo wa Mtume akaona muhuri wa Utume uko kati ya mabega mawili!!!

Taz: Tarikhul Khamisi J. 1 Uk. 284

Assiratul Halabiyya J. 1 Uk. 243

Assiratun Nabawiyya J. 1. Uk. 83

Muhammad (s.a.w.) alipofikiwa na hali hiyo (ya kujiwa na Malaika) alikuwa akipanda katika kilele cha mlima mrefu na akitaka kujitupa chini (ili afe).

Taz: Almuswannaf J. 5 Uk. 323

Muhammad (s.a.w.) alirudi kwa mkewe (kutoka katika pango) akiwa nafuraha kubwa akamwambia mkewe: "Nataka kukueleza habari njema, mimi nimeona katika ndoto kuwa Jibril amenijulisha kwamba ametumwa na Mola wangu aje kwangu... Khadija akamwambia: "Furahi, wallahi Mwenyeezi Mungu hatakufanyia lolote ila lililokuwa la kheri... kisha Khadija akaenda kwa mganga wa kinasara, kuuliza uwezekano wa kumuona Jibril. Mganga alishangaa sana kusikia jina la Jibril katika nchi hiyo, kisha akasema kuwa: "Huyo ni Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu..."

Taz: Albidayatu Wannihaya J. 3 Uk. 13.

Mjadala Wa Riwaya Za Wahy

Kwa kweli tukitaka kuijadili mada hii kwa undani zaidi, itatulazimu tutumie muda mrefu katika kuchambua kifungu kimoja baada ya kingine. Na hilo litahitaji kuchukua nafasi ya kitabu kizima ili kujaribu kutatua utata huo. Lakini, kama wasemavyo wataalamu: "Maa Laa yudraku kulluhu laa yutraku kulluhu" yaani, "Yasiyowe za kupatikana yote, hayaachwi yote". Kwa hiyo nasi hatutaacha kutaja japo kidogo:

Kutokana na sanad ya Hadithi, ambapo mategemeo yake yamepokelewa katika sahihi mbili (Bukhari na Muslim) na zingine, ambazo zinaonyesha kama:

Imepokewa kutoka kwa Az Zuhry kutoka kwa U'rwa bin Zubeir kutoka kwa Mwana Aisha. Sasa: hapa tutaangalia mambo ya fuatayo:

Az Zuhry na U'rwa hawa walikuwa wapinzani wa Imam Ali (a.s.) na wakimtukana.

Taz: Qamusir Rijal J. 6 Uk. 300

Algharat J. 2 Uk. 558-560

Na Mtume (s.a.w.) amesema juu ya Imam Ali (a.s.) kuwa: "Yeyote mwenye kumtukana Ali basi amenitukana mimi na mwenye kunitukana mimi amemtukana Mwenyezi Mungu".

Taz: Mustadrakul Hakim J. 3 Uk. 121

Musnad Ahmad J. 5 Uk. 30

Alfusulul Muhimma Uk. 111

Tarikh Ibn Asakir J. 2 Uk. 184

Manaqibu Ali Uk. 394

Kwa hiyo, mtu mwenye kumtukana Mtume (s.a.w.) hawezi kuwa mwema hata kidogo, licha ya kupokea mafunzo ya dini kutoka kwake.

Amma kuhusu Mwana Aisha (mkewe Mtume) ambae katika mwaka wa thelathini na sita Hijra, alitoka nyumbani mwake Madina kwenda Basra ili kumpiga Ali bin Abi Talib (a.s.) na akafanya hivyo.

Kitendo cha mke wa Mtume cha kutoka nyumbani mwake kwenda nje, ni jambo lililokatazwa na Mwenyeezi Mungu:
"Na kaeni majumbani mwenu" 33:33
Mwana Aisha ameipuuza hukumu hii! Aidha, kitendo cha kumpiga Imam Ali (a.s.) ni jambo linalomuweka mtu mahala pabaya. Imepokewa kutoka kwa A'diyyi bin Thabiti kutoka kwa Zuhry amesema: "Amesema Imam Ali kuwa: "Ninaapa kwa ambaye ameumba mbegu na akaumba upepo, hiyo ni ahadi ya Mtume kwangu mimi kuwa: Hanipendi mimi isipokuwa mu'umin na hanibughudhi (hanichukii) mimi isipokuwa mnafiki".

Taz: Sahihi-Muslim katika kitabul Iman

Sahihit Tirmidhi J. 2 Uk. 301

Musnad Ahmad J. 1 Uk. 84

Tarikh Bughdad J. 2 Uk. 255

Hilyatul Awliyaa J. 4 Uk. 185

Kanzul Ummal J. 6 Uk. 394

Mustadrakul Hakim J. 3 uk 129

Al Istiab J. 2 Uk. 214

Addurrul ManthurAya ya 25 sura 47.

Mwana Aisha ameipuuza hukumu hii! Nanikweli Mwana Aisha hampendi kabisa Imam Ali (a.s.). Hilo linathibitishwa na hali halisi, kwanza, amepigana na Imam Ali (a.s.) na kupiga hakuanzi kabla ya kuchukia. Na alipopata habari Mwana Aisha kuwa Imam Ali ameuliwa, alisujudu kumshukuru Mwenyeezi Mungu!!!

Taz: Magatilut Talibina Uk. 27

Aljamal Uk. 83-84

Mwenyeezi Mungu anasema: "Haiwi kwa mwanamume aliyeamini, Mwenyeezi Mungu na Mtume wake wanapohukumu jambo wawe na hiari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotovu ulio wazi" 33:36.

Riwaya za tukio hilo zinagongana kama unavyoziona - kama utarejea kuzisoma utaliona hilo. Lakini, kwanini Jibril amkamate Mtume kisha amkamuekamue mpaka akaribie kuzimia!? Kwanini Mtume akubali kusoma baada ya kukamuliwa kwa nguvu mara ya tatu? Kwanini asikubali tu kusoma mara ya kwanza kabla ya mateso haya? Na, vipi Mtume arudi kwa mkewe akiwa na khofu kubwa kiasi hiki!! Je! Muhammad (s.a.w.) hakuwa na uwezo wa kumpiga kofi malaika huyo?! Kama alivyofanya hivyo Nabii Musa (a.s.) alipoijiwa na Malaika I'zrail ili achukue roho yake, Musa alimpiga kofi moja tu mpaka jicho likang'oka!!

Taz: Sahihi Bukhari J. 1 Uk. 152

Sahihi Muslim J. 7 Uk. 100.

Musnad Ahmad J. 2 Uk. 315

Almuswannaf J. 11 Uk. 274

Sunannun Nasai J. 4 Uk. 118

Albidayatu Wannihaya J. 1 Uk. 317

Tarikhut Tabari J. 1 Uk. 305.

Haiwezekani kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.) alikuwa mwoga hivyo, na Nabii Musa tu peke yake awe shujaa wa kuwang'oa macho malaika!!

Kwamba, Mtume (s.a.w.) aliingiwa khofu kubwa, Khadija na Waraqa walimtuliza mpaka akatulia. Sasa, tuangalie hali hii kama ifuatavyo:

Inawezekana kwa Mwenyeezi Mungu, kumpeleka Mtume ambaye hajui Utume wake yeye mwenyewe! Ila kwa Kuthibitishiwa na mwanamke na mnasara? Vipi jambo nyeti hili agundue mwanamke kuwa huo ni Utume na wala si kichaa (kama alivyodhani Muhammad) pia mnasara ajue yaqini kuwa huo ni Utume?! Hili linatupa kufikiri kuwa hawa (mwanamke na mnasara) ni wajuzi na watukufu zaidi kuliko Muhammad (s.a.w.).

Mwenyeezi Mungu anasema: "Na wakasema waliokufuru: mbona haikuteremshwa kwake Qur'an yote mara moja? Ndivyo ilivyo, ili tukuimarishe kwayo moyo wako na tumeipanga kwa mpango." 25:32

"Waambie (Muhammad) roho takatifu ameiteremsha kutoka kwa Mola wako kwa haki, ili kuwaimarisha wale walio amini, na kuwa muongozo na habari njema kwa waliosilimu." 16:102
katika aya hizi timachunguza ibara isemayo: "ILU TUKUIMARISHE KWAYO MOYO WAKO". Kwa hiyo, moyo wa Muhammad uliimarishwa na Mwenyeezi Mungu sikiliza Mwenyeezi Mungu analifafanua hili:

"Waambie (Muhammad) hakika mimi ninayo dalili ya wazi itokayo kwa Mola wangu" 6: 57

"Waambie (Muhammad) Hii ndiyo njia yangu, ninaita kwa ujuzi hasa, mimi na wanaonifuata." 12:108

Katika Aya hizi tunaangalia maneno: "MIMI NINAYO DALILI YA WAZI ITOKAYO KWA MOLA WANGU" "NINAITA KWA UJUZI HASA" kwahiyo, Mtume Muhammad (s.a.w.) anajua kuwa anayo dalili (ushahidi) ulio wazi, na kwa ajili hiyo, anawaita watu kwa ujuzi kamili. Hii si sawa na kusema: Muhammad (s.a.w.) uliimarishwa moyo wake na mnasara (Waraqa bin Nawfal).