read

Aya Ya Mut'a Imefutwa?

Wanasema:- "Aya isemayo: Na ambao kwa tupu zao ni wenye kujilinda, isipokuwa kwa wake zao au kwa (wanawake) wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, basi hakika hao ndio wasiolaumiwa. Lakini anaetaka kinyume cha haya basi hao ndio warukao mipaka" 23: 5-7. Aya hizi zimeiondoa Mut'a. Jawabu: Aya hizi haziwezi kuiondoa ndoa ya Mut'a kwa sababu, Aya hizi zimeshuka Makka, na Aya ya Muta imeshuka Madina. Kwa mujibu wa misingi va Nasikh na Mansukh dai hili limeanguka, litupe nje.

Wanasema:- "Aya isemayo: Na nyinyi (wanaume) mtapata nusu ya (mali) walizoacha wake zenu" 4:12 inaonyesha kwamba:

Mume atamrithi mke na mke atamrithi mume, jambo ambalo halipatikani kabisa kwenye ndoa va Mut'a.

Jawabu:- Kukosa kurithiana baina ya mume na mke si jambo linaloweza kuzuia kuthibiti ndoa. Bali ndoa inasihi bila ya kuweko kurithiana.

TAZAMA:

Bidayatul Mujtahid J. 2 uk. 381

Sublus Salami J.3 uk. 954

Fiq'hus Sunna J.3 uk. 427

Wanasema:- "Aya isemayo: Ewe Mtume! mnapowaacha wanawake, waacheni katika wakati wa eda zao" 65:1 Aya hii inataja hukumu za talaka kumwacha mwanamke wakati wa eda yake ni kumwacha wakati yuko katika tohara, hana hedhi ambayo hukumwingilia.

Lakini kwa ndoa ya Mut'a hulipati hili, muda ukimalizika waliokubaliana basi, mwanamke anakwenda zake bila ya talaka wala habari ya kukaa eda hakuna.

Jawabu: Zifuatazo ni hukumu za ndoa ya Mut'a, kama ilivyothibiti kwa mujibu wa Sharia:-

1) Ijabu na Qabul:

Mwanamke atasema nimekuoza nafsi yangu kwa muda fulani kwa mahari kiasi fulani. Mume aseme nimekubali.

2) Kutajwa Mahari:

Ni lazima katika ndoa ya Mut'a kitajwe kiwango cha mahari walichokubaliana. Na isipotaiwa ndoa haisihi.

3) Kutajwa Muda:

Katika ndoa ya Mut'a lazima utajwe muda wa kuowana vinginevyo ndoa haitasihi.

4) Mashahidi:

Ndoa ya Mut'a haina haja ya walii wala shahidi.

5) Haifai kuoa Mut'a mwanamke kafiri wala mwanamke malaya.

6) Inafaa kuoa Mut'a mwanamke Ahlul kitabi na Majusi.

7) Mwanamke Bikra:

Hapa wamekhtilafiana, wako waliosema kuwa, mwanamke bikra anaweza kuolewa Mut'a bila ya idhini ya walii wake. Na wako waliosema: Mwanamke bikra lazima asimamiwe na walii wake iwe ni ndoa ya Mut'a au ya daima. Na hii ndiyo Fat'wa ya Asayyid Abdul'qasim Al'musawy Al,khui.

8) Masharti:

Mume na mke wana haki ya kuwekeana sharti, kwa mfano, mume hataki wazae na mkewe muda huu. Au mume na mke wamekubaliana kuwa watarithiana pindi mmoja wao atafariki.

9) Mtoto wa Mut'a:

Mtoto anaezaliwa katika ndoa ya Mut'a ana haki zote sawa na mtoto wa ndoa ya daima.

10) Eda:

Mke wa ndoa ya Mut'a hana talaka, umalizikapo muda waliokubaliana kuoana basi ndoa hukatika. Na kuanzia hapo atakaa eda kwa muda wa hedhi mbili, ikiwa ni mwanamke asiyepata hedhi, basi atakaa eda siku arobaini na tano.

11) Idadi ya Wake:

Inajuzu katika ndoa ya Mut'a kuoa wake wengi, kwa sababu wake wa Mut'a hawaingii katika idadi ya wake wa ndoa ya daima. Kwa hivyo unaweza kuoa wake alfu moja wa Mut'a. Amesema Shafii kuwa:- "Ibnu Jurayhi aliowa Mut'a wake tisini."

TAZAMA:

Tahdhibut Tahdhibi J. 6 uk. 406

Mizanul Itidal J. 2 uk. 151