read

Kisa Cha Kujitolea H. Ali Roho Yake, Usiku Wa Kuhama Mtume Makka

Ma'mun: Hebu kidogo nieleze kuwa yule mwenzi ambaye alikuwa na Mtume (s.a.w.w) katika pango, au bwana yule ambaye alijitolea roho yake na kumhifadhi Mtume, na akalala mahala pa Mtume hadi akaweza kuhama; bora yupi?

Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume (s.a.w.w) amtake H. Ali alale mahala pake kwa kujiweka hatarini roho yake ili amwokoe (Mtume). Basi Mtume alipomfikishia maneno ya Mola; Ali akalia, Mtume akamwuliza, "unalia nini, unalia kuogopa mauti?" H. Ali akajibu, "Siyo bwana. Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu silii kwa haya, bali ninao wasiwasi kuhusu wewe, kwamba kwa kuhama utaingia taabuni. Je, nikilala mahala pako wewe roho yako itasalimika?" Mtume (s.a.w.w) akasema, "Bila shaka itasalimika."

Hapo H. Ali akafurahi na akasema, "Bwana kwa hiyo basi nina hofu gani? Mimi mzima wako ni tayari, kwa utulivu mno, bila wasiwasi, na kwa furaha nitafidia roho yangu ili nikusalimishe." Baadaye akaenda kulala mahala pa Mtume (s.a.w.w) na akajifunika shuka la Mtume lenye rangi ya kijani kibichi, akalala kwa raha kabisa. Punde baadaye makafiri wa Kikureshi wakafika na wakaizunguka nyumba kwa kumfikira H. Ali kuwa ndiye Mtume aliyelala; hapakuwa na shaka kwa mtu hata mmoja katika wao. Kabla ya hapo Makureshi walikwisha kata shauri kwamba katika kila kabila mtu mmoja atampiga Mtume pigo moja kwa upanga, wote kwa mara moja.

Madhumuni ya kufanya hivyo ni kuwa Bani Hashim wasiweze kuchukuwa kisasi kwa kabila fulani tu, ijapokuwa H. Ali alikuwa akisikia na akijua mashauri yao yote yakifanywa kuwa tayari kumwua, hakukunja uso hata kidogo, wala kuingiwa na wasiwasi, bali kwa utulivu kamili akalala kwa kujitolea. Kinyume cha hayo H. Abu Bakr (kwa neno dogo tu) kule pangoni akaingiwa na hofu na akalia na kubabaika. Huku H. Ali kwa utulivu kamili bila hofu wala wasiwasi akalala vivyo hivyo muda mrefu. Kwa kujitolea na mhanga huo wa H. Ali, Mwenyezi Mungu (alifurahiwa) akawapeleka malaika wake watukufu ambao mpaka asubuhi walimlinda.
Asubuhi alipoondoka hapo alipolala pahala pa Mtume, makafiri wa kikureshi wakawa wanamtazama na wakasema, "Ala ulikuwa wewe umelala? Basi Mtume yuko wapi?" Na Ali akawajibu "Ninajuwaje Mtume aliko?” Ndipo wale wakasema "Ewe Ali, inaonyesha tangu usiku, ulijifanya adui wa roho yako (kwa kulala juu ya mahala hapa) na ukamwokoa Mtume wenu. Kwa ufupi hivyo mpaka kufa kwake H. Ali katika kila jambo alithibitisha utukufu wake juu ya watu wote, na utukufu wake na fadhila yake unazidi. Hakuna utukufu kama ya H. Ali.1

 • 1. Ukitaka kujua zaidi vitazame vitabu vifuatavyo:­
  Tareekhul Khamees juzuu ya kwanza Uk. 367
  Ibn Jaree Tabaree katika kitabu chake tareekhul umam, juzuu ya pili, Uk. 244
  Ibn Hisham katika kitabu chake Seeratun Nabi, juzuu ya pili Uk. 94
  Abul Fida katika Tareekh, juzuu ya kwanza Uk. 133
  Ibn Atheer katika Tareekh, juzuu ya pili, Uk. 38
  Ibn Khalduun katika tareekh, juzuu ya pili, Uk. 15
  Al-Hakim katika Mustadrak juzuu ya tatu, Uk. 133
  Suyootee katika Durre Manthoor, juzuu ya tatu, Uk. 180
  Imam Hanbal katika Musnad, juzuu ya kwanza, Uk 331 na 348

  Viko vitabu vingi vingine vya kuthibitisha hivyo lakini kwa muhtasari tumeandika hivyo tu