read

Mabishano Juu Ya Kisa Cha Ghadeer

Ma'mun: Ewe, Is-Haq, sasa niambie hadithi ya Ghadeer, Je, mnasimulia?

Allama: Ndiyo bwana.

Ma'mun: Hebu eleza kidogo.

Allama Is-haq anasema, "Nikaeleza kisa cha ghadeer mbele ya Ma'mun. Baadaye Ma'mun akasema:
Ma'mun: Ewe Is-haq! Hebu sema, yaweza kuingia akilini mwako maneno haya, kwamba kwa jinsi ilivyombidi H. Abu Bakr kuiamini na kuifuata hadithi inayomhusu H. Ali itampasa H. Ali vile vile hadithi inayowahusu H. Abu Bakr na Umar kuifuata? (Yaani Mwenyezi Mungu alifanya faradhi (lazima) juu ya H. Abu Bakr na Umar kwa kuwa wamekubali kwamba H. Ali ndiye bwana na mwongozi wao, lakini haikuwa lazima bali hata haikumjuzia H. Ali kuwakubali H. Abu Bakr na Umar kuwa mabwana wake).

Allama: Bwana! Watu wanasema kwamba sababu ya kisa hiki ni Zayd bin Haritha, kwani kati yake na H. Ali ilikuwa baadhi ya kutopatana: ambao juu ya hayo akaacha usuhba (urafiki) na H. Ali. Kwa hiyo Mtume akasema, "Mwenye kuamini mimi ni bwana (rafiki) wake, basi Ali vile vile bwana (rafiki) wake. Ee, Mwenyezi Mungu, Mpende ampendaye Ali; na mfanye adui mwenye kumfanya Ali adui yake."

Ma'mun: Kwanza nieleze Mtume amesema hadithi hii wakati gani? Hakusema wakati alipokuwa akirudi kwenye hija yake ya mwisho, (alipofika Ghadeer-e-khum) wakati ule ndiyo?

Allama: Ndiyo, wakati ule ndiyo akasema.

Ma'mun: Ikiwa muda mrefu kabla ya kisa cha Ghadeer-e-Khum huyo Zayd bin Haritha ameshakuwa Shaheed (ameuawa) basi vipi nyie mnasingizia kuwa kisa cha Ghadeer ni sababu ya kutopatana na Zayd? (Kwa sababu Wanahistoria wote kwa ujumla wanaafikiana kwamba katika vita vya Mutah ambavyo vilikuwa katika mwaka wa nane (Hijria) ndiyo Zayd kawa Shaheed (ameuawa), ambacho ni kisa mashuhuri.
Na kisa cha Ghadeer kimekuwa mwezi kumi na nane (Mfungo tatu) Zilhaj, mwaka wa kumi wa Hijria. Hebu sasa niambia, ikiwa mtoto mmoja wako aliyefikia umri wa miaka kumi na tano (15) ukamwona anamwambia watu hivi, "kila aliyekuwa rafiki yangu, basi yule vile vile atakuwa rafiki wa binamu wangu; enyi watu kumbukeni maneno haya vizuri na msije mkayasahau." Je, wewe hutaona vibaya, kwa vile mwanao kuwaambia watu maneno ya upuuzi kama hayo, ambayo yanajulikana na kila mtu, na hapana aliyeyakataa?

Allama: Shahidi Mungu, nasema hakuna budi nitaona vibaya.

Ma'mun: Basi, haya! Maneno ambayo hupendi hata mwanao ayaseme, basi vipi utampenda Mtume? (Yaania Mtume (s.a.w.w) alikuwa anajua kwamba aliyekuwa rafiki yake, basi vile vile ni rafiki wa H. Ali, au tuseme anayependa Mtume, hakuna shaka anampenda H. Ali vile vile. Kwa hivyo, kitu gani kilimfanya Mtume kufanya bidii na usimamizi wote ule na kuwapa habari masahaba na Waislamu? Hapana budi itakulazimu kukiri na kusema kwamba shabaha na lengo la Mtume ni kuwafahamisha kwamba mwenye kumkubali yeye kuwa ni bwana na mwongozi wake, basi vile vile amemkubali H. Ali kuwa ni bwana na mwongozi wake).1

Nina majonzi kuona hali yenu hiyo. Msiwe watumwa wa wanavyuoni wenu, na hawa waongozi wenu wa dini msiwafikiri kuwa miungu wenu. Kwa hakika ninyi mnalelewa kwamba Mwenyezi Mungu katika Qur’ani amesema: "Ittakhadhuu - Ahbaa-rahum." (wamefanya wanavyuoni wana watawa wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu, (9:31). Ijapokuwa (Mayahudi na Manasara) hawakusali sala za waongozi wa dini yao, wala hawakufunga wala hawakuitakidi kwamba waongozi wa dini yao hakika ni miungu wao; lakini kila waliyoyasema hawa wanavyuoni wao, waliyakubali bila ya kutumia akili yao (na ndivyo Mwenyezi Mungu akasema hivyo).

 • 1. Ukitaka kujua zaidi vitazame vitabu vifuatavyo:­
  Imam Hanbal katika Musnad, Juzuu ya nne, Uk. 372
  Ibn Katheer katika Tarehe yake al-Bidaya wa-Nihay, juzuu ya tano uk. 208/214, anaeleza kwamba Bwana Abul Maali Juwayni anahadithia kuwa, “Naliona kwa mfunga kitabu, kitabu kilichoandikwa hadithi ya Mtume na jina la kitabu hicho ni ‘kitabu cha ishirini na naen kuhusu hadithi hii ya man kuntu Mawla Fa Aliy-yun Mawla’ na tutaanza kitabu cha ishirini na tisa.”
  Ibn Jareer Tabari katika Tarehe yake
  Sibt ibn Jawzi katika tadhkira Khawasul-Umma, mlango wa pili Uk. 18
  Sheikh Ahmad bin al-Fadhil Bakatheer katika Waseelatul Maal
  Suyooty katika Azhaarul Mutanaathira, NA Durri Manthoor, juzuu ya pili, Uk. 293/294
  Hakim katika Mustadrak, juzuu ya tatu, Uk. 110/111.
  Imam Ghazali katika Sirrul Alameen
  Imam Nasai katika Khasais Alawiya
  Muhamad bin Isa Tirmidhi katika kiabu chake cha Sunan
  Viko vitabu vingi vingine vya kuthibitisha hiyo lakini kwa muhtasari tumeandika hivyo tu