read

Maelezo Ya Majadiliano Kati Ya Ma'mun Na Wanachuoni Kuhusu Sifa Za Ali Bin Abi Talib

Is-haq bin Ibrahim bin Ismail bin Hamad bin Zayd amesimulia kwamba siku moja Yahya bin Aktham Qadhil ­Qudhat (Kadhi mkubwa) alinitumizia mimi na baadhi ya sahibu zangu katika wanachuoni, kusema, "Kuwa Ameerul Mumineen ameniamrisha kesho alfajiri niwachukue watu arobaini, wote wawe Faqeeh wenye elimu ya kutosha, wanachuoni wa Fiqhi wawe na uwezo wa kufahamu wanachoambiwa na kujibu vizuri", basi wataje hao ambao unadhani kama watafaa kwa yale anayoyataka Ameerul Mumineen." Tukamtajia idadi maalum na yeye pia akawataja idadi maalum, hata wakatimia arobaini (40) kiasi alichotaka, na wakaandikwa majina yao, na akaamrisha kuamka mapema alfajiri, na akawatumizia wasiohudhuria kuwaamrisha wahudhuriye kwake.

Sote tulioalikwa tukafika kwake kabla ya mapambazuko ya alfajiri, tukamkuta amevaa nguo zake amekaa tayari anatungoja; akampanda mnyama wake nasi pia tukapanda tukaenda hata tukafika mlangoni mwa jumba la mfalme; mara tukamkuta mtumishi amesimama. Alipotuona tu akasema "Ewe baba wa Muhammad; Ameerul Mumineen anakungoja", tukapelekwa ndani; tukaambiwa tusali (sala ya asubuhi) tukasali, hata bado hatujamaliza akaja mjumbe akasema, "Ingieni ndani, tukaingia, mara tukamkuta Ameerul Mumineen amekaa kwenye firashi (tandiko) lake, na amevaa nguo za kifalme (amevaa nguo nyeusi, amejitanda na shuka ya kijani, na amevaa kilemba). Sote tukasimama mbele yake tukamwamkia; na yeye akaitikia Salamu, na akatuamrisha kukaa.

Tulipokwisha sote kukaa kwa uzuri, yeye (Ma'mun) akateremka kwenye tandiko lake, akavua kilemba na shuka aliojitandia, na akavaa kofia ya kidasturi. Baadaye akaja upande wetu akasema, "Nimefanya vile (kuvua yale mavazi) ili ninyi pia mfanye vivyo hivyo na mkae kienyeji." Lakini viatu hatukuvua, tena yeye (Ma'mun) akanyosha miguu yake, na baadaye akatuambia tuvuwe kofia na viatu na shuka ya kujitandia. Sisi tukasita kufanya hivyo. Basi Yahya akatuambia tufuate tulivyoamrishwa na Ameerul Mumineen. Tukaona ajabu basi tukaenda tukavua viatu, shuka na kofia na tukarejea mahali petu.

Tulipokwisha kaa sawa hapo, Mfalme Ma'mun akatuambia kwamba ametuita kwa ajili ya majadiliano, kwa hivyo mwenye kushikwa na choo kidogo au kikubwa na aende, kwani akiwa hakwenda haja atakuwa hana raha kukaa, kusema na kufahamu. Basi mwenye kushikwa na haja, basi kile pale choo (akaonyesha kwa mkono). Tukamshukuru.

Baadaye akatoa swali kuhusu fiqhi (kanuni za Ki-islamu) na akasema, "Ewe Abaa Muhammad! jibu wewe, na baadaye wajibu wengine (watoe ufafanuzi wao). Yahya akajibu na wengine mmoja baada ya mmoja tukajibu na kutoa fafanuzi, hali yeye (Ma'mun) kimya anasikiliza macho chini; hata yalipokwisha maneno, akaelekea kwa Yahya akasema, "Ewe Abaa Muhammad, jibu lako lilikuwa sahihi, lakini hukutumia ukweli katika hoja zako." Baadaye alikuwa akiwajibu kila mmoja na kukataa hoja zao na wengine akazikubali hoja zao hadi wote tukaisha. Baadaye akasema, "Mimi sikukwiteni mje hapa kwa ajili ya jambo hili tulilozungumza, lakini nilipenda kufanya hivyo ili mchangamuke na muwe huru bila ya wasiwasi katika mazungumzo; hasa lengo langu kukwiteni ninyi hapa tujadiliane kwa yale ninayoitakidi na ninayoamini."

Tukasema, "basi na afanye Ameerul Mumineen, Mwenyezi Mungu amuafikishe."

Ma'mun: Imani yangu ni kwamba baada ya Mtume, Hazrat Ali bin Abi Talib ni bora kuliko watu wote, na yeye ndiye mwenye kustahili, na Ukhalifa ni haki yake, mnasemaje?

Allama: Sioni uthabiti wowote juu ya haya uliyoyasema. Kwa sababu gani H. Ali akawa bora na mwenye kustahili Ukhalifa kuliko wote baada ya Mtume (s.a.w.w)?

Ma'mun: Hebu kwanza niambie kwa kitu gani mtu akawa bora kuliko mwenzake, na kwa sababu gani husemwa fulani ni bora kuliko fulani?

Allama: Kwa vitendo vyake vizuri.

Ma'mun: Hakika kweli, sasa niambie kama ikiwa mtu mmoja katika zama za Mtume (s.a.w.w) kwa vitendo vyake akawa bora kuliko wote, lakini baada ya Mtume (s.a.w.w) watu wengine wakatokea wenye kutenda vitendo vizuri zaidi kuliko vitendo vyake, je, hawa watu watakuwa sawa na yeye?

Allama: (Akababaika kulijibu swali hili na akaanza kufikiri; hapo Ma'mun akamwambia).

Ma'mun: Nina hakika kwamba hutaweza kusema ndio, kwani mimi ninaweza kukuonyesha zama hizi hizi, wapo watu ambao kuliko hao wanapigana jihadi, wanahiji (Hija), wanafunga saumu, wanasali na wanatenda mambo mengi mengine ya kheri. Basi kwa hivyo watu wa zama zetu hizi pia watakuwa bora kuliko masahaba.

Allama: Bila shaka, aliyekuwa bora katika zama za Mtume (s.a.w.w), mtu mwingine yeyote hataweza kuupata au kuufikia ubora huo wakati mwingine wowote hata kama amefanyaje.

Ma'mun: Vizuri kabisa, sasa hebu watazame masahaba watukufu wa Mtume, Tabieen, Muhad-ditheen (wapokeao Hadithi) na wale wanavyuoni ambao ndio mnawakubali kuwa ni viongozi wenu wa dini; basi angalia zile daraja za juu za Hadithi walizozipokea katika sifa ya H.Ali wanahadithia. Baadaye hadithi hizi na hadithi zile za wema wa H. Abu Bakr mlizozipokea ninyi mzilinganishe; ikiwa hadithi zote hizo ni sawa na H. Ali, basi bila shaka ninyi mnaweza kudai kwamba H. Abu Bakr alikuwa bora kuliko H.Ali.

Wallahi si hivyo tu, nasema hata mkizikusanya hadithi za wema wa H. Abu Bakr na H. Umar wote wawili pia; na mkazilinganisha na za H. Ali tu, na zikiwa sawa na za H. Ali peke yake, hapo kwa furaha H. Abu Bakr na H. Umar mwakubali kuwa ni bora kuliko H. Ali. La, naapa yamini! hata mkizikusanya hadithi za wema wa H. Abu Bakr na H. Umar na H. Uthman na mkazilinganisha hadithi za watatu hao na kwa jumla zikawa sawa na za H. Ali peke yake, basi ninyi pasipo taabu mabwana watatu hao muwaridhie kuwa bora.

Sivyo wallahi! hata "Ashara Mubash-shara (wale masahaba wapenzi kumi ambao Mtume ameshuhudia kwamba ni watu wa peponi) mkiwachukua wote hawa mkizikusanya sifa zao kwa umoja na mkilinganisha hizo sifa zao na sifa za H. Ali peke yake hapo ninyi mnayo haki ya kusema kuwa ni bora kuliko H. Ali. Lakini haiyumkiniki kabisa, kwa sababu sifa za H Ali zimezidi sifa za H. Abu Bakr; Umar, Uthman, sio hivyo tu bali zimezidi za hao Ashara- Mubashara pia. Vizuri, Ee Is-haq hebu sasa eleza; tangu Mtume (s.a.w.w) alipodhihirisha utume wake wakati ule amali bora kuliko yote ilikuwa nini?

AlIama: Kuamini kwa moyo safi na ukamilifu.

Ma'mun: Kuamini dini ya lslamu kwa kutangulia mbele ya watu wote si amali bora kabisa?

Allama: Kwa nini isiwe hivyo? Bila shaka ni bora.

Ma'mun: Isome Aya hii katika Qur’ani (56:10&11) "Was-saabiqun as-Saabiqun, Ulaikal – muqar- rabuuun" (Na waliyotangulia kabisa katika heri hao ndio walioko mbele. Hao ndio vipenzi zaidi kuliko wote (Kwa Mwenyezi Mungu ). Hapa Mwenyezi Mungu amewakusudia wale ambao katika kuamini Uislamu walikuwa mbele kwa haraka. Je! mnamjua mtu, ambaye aliamini mbele kuliko H. Ali?

Allama: Bwana, H. Ali ameamini utotoni wakati ambapo haikumlazimu sheria juu yake, lakini H. Abu Bakr alikuwa mzee na akaukubali Uislamu ambapo kila kitu cha sheria kilikuwa wajib juu yake.

Ma'mun: Nataka kwanza uniambie ni nani wa kwanza wa mbele kuukubali Uislamu, baadaye tutajadiliana juu ya uzee au utoto.

Allama: Bila shaka mbele kuliko H. Abu Bakr ameamini H. Ali lakini alikuwa mtoto.1

Ma'mun: Kweli H. Ali utotoni ameamini; sasa tuafikiwa kuwa yapo mambo mawili, la kwanza ni kuwa H. Ali ameamini kwa kuwa Mtume amemwambia aamini; la kwamba Mwenyezi Mungu amemwongoza kwa "Ilham" Ali auamini Uislamu; sasa niambie ni njia gani mnaikubali?

Allama: (Anahadithia kama swali hili la Ma'mun lilinibabaisha mno, na nikafikiri sana mwishowe sikuweza kumjibu, hapo Khalifa mwenyewe akasema.)

Ma'mun: Is-haq! ninyi hamwezi; hamtakubali kusema kwamba H. Ali aliletewa "Ilham" (ameongozwa na Mola) kwa sababu mkikubali hivyo itakuwa ninyi daraja ya H.Ali mmeitukuza kuliko ya Mtume, kwani Mtume kwa kuletewa "Ilham" (Uongozi) na Mwenyezi Mungu hakuujua Uislamu, bali Mwenyezi Mungu alimpeleka Jibrili kwa Mtume.

Allama: Bila shaka H. Ali hakushushiwa Ilham, bali Mtume binafsi alimwita na akamtaka auamini Uislamu.

Ma'mun: Kadhia hii itakuwa hali mojawapo ya mbiIi: Mtume kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu amemwambia H. Ali kuukubali Uislamu (Kuamini), au Mtume kwa matamanio yake mwenyewe tu amemtaka H. Ali aamini.

Allama anasema, swali hili la Khalifa Ma’mun vile vile lilimfadhaisha na akafikiri amjibu nini. Hakuweza kumjibu basi hapo Khalifa mwenyewe akasema.

Ma'mun: Ee, Is-haq, ninyi hamwezi kumtuhumu na kumsingizia Mtume (s.a.w.w) kwamba yeye hufanya kitu cho chote kwa matamanio yake, kwani mkisema hivyo itakuwa ninyi mnamghadhibisha Mwenyezi Mungu ambaye alimwamrisha Mtume wake awaambie watu hivi, "Wamaa Yantiqu Anil-hawaa, In huwa illaa Wahyun Yuuhaa" (53: 3&4) (Hatamki neno lolote kwa matamanio yake; ila kama anavyoamrishwa na Mwenyezi Mungu).

Allama: Bila shaka Mtume hakufanya hivyo kwa matamanio yake binafsi bali kwa amri ya Mwenyezi Mungu alimwambia H. Ali aamini.

Ma'mun: Ni ajabu mno! Hii ndio shani ya Mwenyezi Mungu! kuwaambia Mitume wake kumtaka mtu ambaye si halali (si wajibu juu yake) kumwambia kufanya jambo?

Allama: Ma'adhallah! Toba! sivyo hivyo kabisa.

Ma'mun: Wewe ulivyosema kwamba H. Ali ameamini utotoni, ambapo wakati ule haiumjuzia kuamrisha cho chote, basi kwa kusema kwenu hivi ni maana yake kwamba Mtume amewaita watoto kuamini jambo lililokuwa si uwezo wao. Na ikiwa wale watoto kwa kutakwa na Mtume wangeamini, je, nini hukumu ya mtoto mmojawapo baadaye akikufuru utotoni, hatapewa adhabu ya kukufuru kwake? Je, isingemjuzia Mtume kuwaamrisha jambo lolote? Mwaridhia kumsingizia Mtume kwamba amefanya mambo kama haya?

Allama: Toba! sivyo kabisa.

Ma'mun: Nafahamu kwamba madhumuni ya maneno yako ni kuwa, hiyo ilikuwa sharafa mahsusi ya H. Ali, hata iwe H. Ali kwa cheo (Sharafa) hicho na fadhila hii (ambayo imezidi zote) awe bora kuliko wote. Ndio sababu watu wote wazijue sifa na vyeo vyake vyote. Kinyume chake ikiwa Mwenyezi Mungu alimwamuru Mtume kuwataka kwa jumla kila mtoto aamini, basi Mtume kama alivyomtaka H. Ali waamini, angewataka watoto vile vile waamini.

Allama: Bila shaka bwana! uliyoyasema yote ni kweli.

Ma'mun: Je, Mtume alipata kuwaambia watoto wa jamaa zake mmojawapo kuamini? Makusudio ya kuuliza kwangu hivi, ni kwamba msije mkasema kuwa H. Ali alikuwa bin Ammi wa Mtume ndipo akamtaka aamini kama alivyowataka watoto wa jamaa zake wengine waamini; basi ikiwa ndivyo hivyo, hapatakuwa na sifa wala kufadhilika kwa H. Ali mahsusi yake.

Allama: Sijui mimi kama Mtume alipata au hakupata kumwamkia mtoto yeyote.

Ma'mun: Ee, Is-haq! unadhani wewe kwamba kesho Kiyama, Mwenyezi Mungu atakuuliza kuhusu mambo usiyoyajua?

Allama: La, jambo nisilolijua kwa nini niulizwe?

Ma'mun: Kwa hiyo, jambo ambalo Mwenyezi Mungu ametuondolea takalifu yake, kwa nini unalitaja? (itapokuwa hujui) kwamba Mtume (s.a.w.w) alipata kumwambia mtoto mmoja yeyote katika ukoo (jamaa) wake kukubali Uislamu, basi kuna dharura gani ya kudhania? Sema kwa mujibu wa elimu yako, kwamba Mtume hakumwambia mtoto mwingine yeyote. Hiki ni cheo kilicho mahsusi cha H. Ali. Niambie sasa, baada ya mtu kuamini, jambo (amali) gani bora ili kuitenda?

Allama: Kufanya jihadi (kupigana) katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Ma'mun: Hakika, ni kweli, jinsi H. Ali alivyopigana na kuweka ukumbusho wa uhodari na ushujaa wake. Je, yupo sahaba mwingine ambaye amefanya hivyo?

Allama: Vita gani na wakati gani?

Ma'mun: Chukuwa wakati wo wote, au vita vyo vyote utakavyopenda kutaja (Wakati wo wote au vita vyo vyote sahaba yeyote amepigana na kufanya kazi kama H. Ali?

Allama: Na tutazame vita vya Badr.

Ma'mun: Ndio hasa tazama humu. Mimi vile vile ninavipenda vita hivi. Katika vita vya Badr pia (ambavyo vilikuwa katika mwaka wa pili, A.H., mwezi wa Ramadhani) mambo aliyoyafanya H. Ali na mambo waliyoyafanya masahaba wengine si tofauti sana? Hebu sema katika vita hivi watu wangapi wameuawa?

Allama: Zaidi ya sitini.

Ma'mun: Katika hao sitini H. Ali peke yake kawauwa wangapi?

Allama: Mimi sijui.

Ma'mun: Basi nisikie mimi, ishirini na tatu au chache yake ishirini na mbili, na arobaini waliobaki katika makafiri wameuwawa na Waislamu wengine.2

Allama: Bwana angalia vile vile haya, kuwa H. Abu Bakr Radhiyallah, alikuwa amekaa katika Jukwaa (Areesh) pamoja na Mtume.

Ma'mun: Hapana shaka alikuwa! Lakini kule akifanya nini? (kwani huku akimuua adui? Au akipigana na adui?).

Allama: Alikuwa amekaa na akifikiria njia ya kushinda vita.

Ma'mun: Inasikitisha mtu kama wewe kusema hivyo! Niambie yeye akifikiri hayo mbali na Mtume, au pamoja na Mtume? Ikiwa walikuwa pamoja basi yaonyesha kwamba Mtume alimfanya kushirikiana katika fikra zake? Katika mambo haya matatu ni jambo lipi unalikubali?

Allama: Ma'adhallah hakushiriki katika fikra, wala hakuwa mshiriki wake wala Mtume (s.a.w.w) hakuhitajia fikra zake.

Ma'mun: Ikiwa si hivyo basi hapo kwenye jukwaa amekaa akifanya nini? Ikiwa katika vita vya Badri hakutenda jambo lolote ila kukaa jukwani tu, basi itakuwa vipi yule ambaye katika kumhifadhi Mtume, kajitumbukiza vitani, na kupigana kwa upanga, roho mikononi asiwe bora kuliko yule aliyekaa kwenye jukwaa raha mstarehe?

Allama: Bwana Jihadi (vita) jeshi zima la Ki-islamu lilikuwa likipigana. H. Ali alikuwa na halisi gani?

Ma'mun: Ndio hii ni kweli kwamba wote walikuwa wakipigana, lakini je, yupi bora? Yule aliyekuwa anapigana na kumhifadhi Mtume; au yule aliyekaa naye kwa utulivu na amani? Kwani wewe aya hii katika Qur'ani hukusoma ambayo inasema:

"La yas-tawil qaa-iduuna minal-mu’mineena ghayru ulidh-dha-rari wal-mujaa hiduu-na fi sabee-lil-Laahi biamwaa-lihim wa-an-fusi-him, Fadh-dha-lal-laa-huI mujaa-hideena biam-waa-lihim wa-an-fusi-him alal qaa­idee-na darjah; wa-kul lan wa-adal-laa- hul hus-naa; wa fadh-dha-lal laa-hul mujaa hidee-na al-qaa-ideena ajran adhee-ma." (4:95)

(Hawawi sawa Waislamu wanaokaa wasiende vitani, isipokuwa wenye udhuru (Hawawi sawa) na wale wapiganao katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na kwa nafsi zao. Mwenyezi Mungu amewafadhilisha katika cheo wale wapiganao katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na kwa nafsi zao kuliko wakaao (wasiende kupigana) Ingawa Mwenyezi Mungu amewaahidi wote (kupata) wema, lakini Mwenyezi Mungu amewafadhilisha kwa ujira mkuu wale wapiganao kuliko wakaao).3

Allama: Lakini H. Abu Bakr na Umar pia walikuwa vitani (kwa sababu ya nia hiyo walikuja vitani).

Ma'mun: Basi kwa hivyo, H. Abu Bakr na Umar (ambayo walikuja) itakuwa wanao ufadhili juu ya wale wasioenda kabisa vitani, ndiyo au siyo?

Allama: Hapana budi ndiyo.

Ma'mun: Basi kwa sababu hiyo, bwana mkubwa yule ambaye roho yake aliweka hatarini, na akapigana na maadui, vile vile atakuwa bora kuliko H. Abu Bakr na Umar (kwa sababu wawili hawa ijapokuwa walifika vitani, lakini hawakufanya kitu, bali walikaa tu kwa utulivu).

Allama: Ndiyo maneno yako kweli.

Ma'mun: Sina shaka, Qur’ani unasoma?

Allama: Ndiyo bwana ninasoma.

Ma'mun: Hebu isome sura ya Hal Ata’ ambayo ndani yake Mwenyezi Mungu anasema, "Hal Ata Alal Insani Hiynum Minad Dahri Lam yakun Shay-am-Madh-kuura." (hakika ulimfika mtu wakati fulani wa dahari ambapo hakuwa kitu kinchotajwa).

Allama Is-haq anasema nikaanza kuisoma hiyo sura, lakini nilipofika kwenye kuanzia aya hii: "Yashrabuna Min Ka’sin Kana Mizaa-Juha ka-fuura mpaka Wayut-imuunat-ta-ama Ala Hub-bihi Misky-Naw-waya-tiyamaw-wa-asiyra." (…Watakunywa katika kikombe kilichochanganyika na kafuri… Na huwalisha chakula maskini na yatima na mfunguwa kwa mapenzi yake. Qur'ani 76:5-8) Ma'mun akauliza, akasema:

­Ma'mun: Ngoja kidogo, hebu nifahamishe aya hizi, zimeshushwa katika shani ya nani?

Allama: Katika ukubwa na cheo cha H. Ali.

Ma'mun: Kwa njia ipi maneno haya yamekufikia kwamba H. Ali alipokuwa akiwapa chakula maskini, yatima na mfungwa, na huku kwa ulimi wake akisema hivi: "Innamaa Nut-imukum Liwaj-Hillah.." (Tunakulisheni nyie kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu tu, hatutaki kwenu malipo wala shukrani!).
Ikiwa si hivyo, na bila shaka sivyo; basi inathibitisha kwamba Mwenyezi Mungu akijua nia ya H. Ali, na baadhi yake Mwenyezi Mungu Mwenyewe ametambulisha na kudhihirisha kwa kusema vile, "sisi tunakulisheni kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu tu." Hebu sasa, niambie jinsi Mwenyezi Mungu kwa sifa hii ya H. Ali aliyomsifu. Unaweza kumtaja sahaba mmojawapo ambaye alikuwa amefanya jambo fulani, na Mwenyezi Mungu juu ya nia yake, badala yake akatia maneno yake na akaileta kwa namna ya aya?

Allama: H. Ali bila shaka hakuyasema kwa ulimi wake haya 'Innamaa Nut-imukum Liwaj-hil-laah', wala hakuna sahaba yeyote sifa kama hii kuteremshiwa katika Qur’ani.4

Ma'mun: Ndiyo unasema kweli, na sababu yake ni hii, kwamba Mwenyezi Mungu anajua tabia na nia ya vitendo vya H. Ali, kwamba H. Ali kila jambo alifanyalo huwa kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu tu, hana makusudio mengine. Ewe Is-haq, hebu sasa niambie wewe unashuhudia na kukiri au la, kwamba Ashra Mubash-shara ni watu wa peponi?

Allama: Bila shaka! Na mimi vile vile ninashuhudia pia.

Ma'mun: Je, sasa ikiwa mtu kasema hivi: "Naapa kwa Mwenyezi Mungu sijui hadithi hiyo ni kweli au uwongo, na pia sijui kwamba Mtume (s.a.w.w) amehadithia hiyo hadithi au la." Je, mwenye kusema hayo yote, utamfikiri kuwa ni kafiri?

Allama: Ma’adhallah kabisa siyo!

Ma'mun: Hebu sasa tutazame ikiwa mtu, yule yule akisema, "Mimi sina hakika kwamba sura ya Hal Ata’ ni maneno ya Qur'ani (Mwenyezi Mungu) au siyo, basi huyo atakuwa kafiri au sivyo?

Basi nini tofauti na sababu ya maneno haya mawili? Tofauti hii ipo, kuwa fadhila ya H. Ali Qur'ani ni ushuhuda wake, ambao mwenye kukanusha huwa kafiri; na fadhila ya masahaba ni maneno ya hadithi ambayo huwa kila namna sahihi au si sahihi, na akiyakanusha imani imekwisha; Vema, je, Ee Is-haq wewe unahadithia hadithi za Mtume?

Allama: Ndiyo bwana, ninafanya hadithi.

Ma'mun: Unaijua hadithi ya 'Tayr' (ndege)?

Allama: Ndiyo bwana.

Ma'mun: Hebu hadithia.

Allama Is-haq anaeleza, mimi nikaisoma hadithi ambao ni hii, “Siku moja Mtume alipokaa kula nyama ya ndege ya kukaanga (aliyoletewa zawadi) akaomba, "Ee Mola Wangu, mlete kwangu mtu yule ambaye kwako wewe ni mpenzi (Mahbubi) na umpendaye zaidi kuliko watu wote, aje hapa kula nami. Mara tu baada ya kumalizika dua yake Mtume, H. Ali akapelekwa kwa Mtume, na akakaa kula naye. Hii inaonyesha na inathibitisha kwamba Ali anapendwa kuliko wote; na hadithi hii ndiyo inaitwa hadithi ya Tayr (ndege)." Baadaye Ma'mun akasema.

Ma'mun: Ewe Is-haq, mpaka hivi sasa, nilikuwa nikikufikiri kwamba wewe si adui wa jambo la haki, lakini sasa imenidhihirikia kuwa wewe ni adui wa haki. Je, unayo yakini kwamba hadithi hii lazima kuwa ni kweli?

Allama: Bila shaka, ninayo yakini, kwani hadithi hii imepokewa na wanavyuoni wakubwa, ambao mtu yeyote hawezi kuwapinga.5

Ma'mun: Sasa hebu sema, unaweza kufikiri kamba mtu yeyote mwenye imani na yakini juu ya hadithi hii, anaweza kufikiria kwamba katika umati wa Mtume, yupo mtu bora kuliko H. Ali?

Kama bado anafikri kuwa yupo aliye bora kuliko H. Ali basi katika mambo matatu haya lazima jambo moja alikubali.

(1) Aseme kwamba Mwenyezi Mungu hakukubali ombi (Dua) la Mtume.

(2) Au akubali baada ya kuwepo mtu bora kuliko wote, Mwenyezi Mungu alimpenda asiye bora (H. Ali).

(3) Au aitakidi kwamba Mwenyezi Mungu hapambanui aliye bora na asiye bora (kwa sababu ya lile ombi (Dua) la Mtume, Mwenyezi Mungu amempeleka H. Ali tu).

Katika mambo matatu haya jambo lipi unalolikubali?

Allama Is-haq anaeleza kwamba kusikia maneno haya ya nguvu ya Ma'mun "akili ikaniruka na nikababaika nikawa sina la kumjibu." Hapo Ma'mun akasema:

Ma'mun: Ewe Is-haq, huwezi kulichagua na kulikubali hata moja katika mambo matatu haya kwani (utakufuru na imani itakutoka na) nitakufanya ukiri, pasipo haya labda utafute njia ya nne.

Allama: Bwana akilini mwangu halifafanuki jambo jingine lolote. Lakini naweza kusema hivi tu, kwa vyo vyote H. Abu Bakr pia hakukosa sifa yo yote?

Ma'mun: Mimi siwezi kukanusha haya, kwa sababu ikiwa hana sifa yoyote, basi itakuwa ni upuzi kusema H. Ali ni bora kuliko H. Abu Bakr. (kwani mtu bora anaambiwa yule ambaye anazo sifa zaidi kuliko wengine maana yake asiye bora anazo sifa kidogo na aliye bora anazo sifa zaidi kuliko wote); lakini wakati huu umekumbuka yake?

Kisa Cha "Ghari": H. Abu Bakr Kufuatana Na Mtume.

Allama: Kufuatana na H. Abu Bakr kwenye Pango (Ghari) na maelezo ya aya ya Ghari ambayo Mwenyezi Mungu amesema katika Qur'ani; "Thani-Yath-Nayni," (Mtume) alipokuwa wa pili wa wawili, walipokuwa wote wawili katika pango; (Mtume) anapomwambia sahibu yake; "Usihuzunike, kwa yakini Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi." (Qur'an 9:40)

Hebu angalia katika aya hii Mwenyezi Mungu, amemtaja H. Abu Bakr kuwa 'Sahib' (mwenzi) wa Mtume kwani hiyo fadhila ya H. Abu Bakr ni ndogo au kama kawaida tu?

Ma'mun: Ewe Is-haq, mimi sitakusumbua wala sitakupeleka njia ya shida (bali kwa kila namna ya msaada nitakupa, ili utumie uwezo na maarifa yako yote katika majadiliano haya; na nguvu zako zote uzitumie mpaka uridhike). Bila shaka katika aya hii Mwenyezi Mungu alimtaja H. Abu Bakr kuwa ni Mwenzi wa Mtume. Lakini (Humu fadhila gani inathibitisha, au sifa gani imo humo?). Kwa kuwa ninaona Mwenyezi Mungu katika Qur'ani, amemwita Kafiri pia Mwenzi ambaye alifuatana na mtu mmoja mwenye kupendwa na Mwenyezi Mungu, basi katika Qur'ani ameeleza hivi, "Faqaala lahu Sahibuhu, Wahuwa Yuhaawiruhu." Basi akamwambia mwenzake na hali ya kuwa akibishana naye, "Je, unakufuru (na unakanusha neema za) yule aliyekuumba kwa udongo, tena kwa tone la manii, kisha akakufanya mtu kamili? " (Qur'ani, 18:37)

Allama: Lakini bwana, yule Mwenzi aliyetajwa katika aya hii alikuwa kafiri na H. Abu Bakr alikuwa Mwislamu.

Ma'mun: Mimi ndiyo nasema hayo hayo, kwamba ikiwa inajuzu kwa Mwenyezi Mungu, Kafiri mmoja aliyefuatana na mpenzi wake mmoja kumwita sahib (Mwenzi); basi vile vile inajuzu Mwislamu aliyefuatana na Mtume wake amwite Mwenzi (Sahib), lakini kwa kumwita hivyo (Mwenzi) yule mtu hawezi kuwa bora kuliko Waislamu wote.

Allama: Bwana, aya hii ya Ghari (pango) ni tukufu sana kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema, "Alikuwa na Mwenziwe wa pili yake peke yao." Wakati ule walipokuwa wote wawili katika pango; (Mtume) anapomwambia Sahib yake, "Usihuzunike, kwa yakini Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi."

Ma'mun: Ewe, Is-haq, naona nisipokusaidia kukufikisha kwenye ufafanuzi hutakubali jambo lolote. Hebu sasa nieleze huzuni ya H. Abu Bakr ilikuwa katika hali ya ghadhabu au utulivu? (alipokuwa na furaha akahuzunika au alipokuwa na ghadhabu?)

Allama: Huzuni hiyo alimhuzunikia Mtume, alimfikiria kwamba asije (Mtume) akapatwa na msiba (taabu) ye yote.

Ma'mun: Haya sio majibu ya swali langu. Eleza huzuni ya H. Abu Bakr ilikuwa ya nini? Kutaka ridhaa ya Mwenyezi Mungu au ilikuwa huzuni hii kinyume chake kumghadhibisha Mwenyezi Mungu?

Allama: Alihuzunika 'lillahi' kutaka ridhaa ya Mwenyezi Mungu (huzuni ya H. Abu Bakr pale ni kumfurahisha Mwenyezi Mungu).

Ma'mun: Kwa mujibu haya, inathibitisha kwamba Mwenyezi Mungu ametupelekea Mtume yule ambaye anawakataza viumbe kufanya jambo yenye kumridhisha na kumfurahisha Mwenyezi Mungu?

Allama: Ma'adhallahi! (vipi itakuwa hivi?)

Ma'mun: Kwani wewe sasa hivi hukusema kwamba kuhuzunika kwa H. Abu Bakr kulikuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Allama: Bila shaka nilisema.

Ma'mun: Basi mbona Qur’an insema kwamba Mtume amemwambia Sahib wake H. Abu Bakr, ‘La Tahzan’ (Usihuzunike); amemkataza asihuzunike. Lakini yeye huzuni yake ilikuwa ‘Lil-lahi’ min-ajili ya Mwenyezi Mungu, hatimaye inaonyesha kwamba Mtume (s.a.w.w) amemzuwia H. Abu Bakr kupata furaha na ridhaa ya Mwenyezi Mungu!

Allama: Ma’adhallah (La haula, makosa gani nimefanya!)

Ma'mun: Ewe, Is-haq, mimi ninajadiliana nawe kwa urahisi na utaratibu, ili labda uongoke na ufuate njia ya haki na uwache upotovu (batili) kwani nakuona mara kwa mara unasema Au-dhu-billahi. Hebu nifahamishe Mwenyezi Mungu katika Qur'ani amesema hivi: "Fa anzala-llahu saki-nata-huu-alayhi." (Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake). Hapa amekusudiwa Mtume (s.a.w.w) au H. Abu Bakr?

Allama: Hakukusudiwa H. Abu Bakr bali Mtume ndiye aliyekusudiwa.

Ma'mun: Vizuri kabisa. Na tutazame aya hii katika Qur’ani inasema hivi: "wa yawma hunaynin...." mpaka mwisho wa aya hii. (Bila shaka Mwenyezi Mungu amekunusuruni katika mapigano mengi, na siku ya Hunaini (pia); ambayo wengi wenu ilikupandisheni kichwa lakini haukufaeni chochote, an ardhi ikiwa finyu juu yenu; ingawa ilikuwa yenye wasaa, kisha mkageuka mkarudi nyuma; (mkakimbia). Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na juu ya Walioamini) (9:25&26). Hebu eleza katika aya hii Mumineen (walioamini) wamekusudiwa nani?

Allama: Bwana! hakika sijui.

Ma'mun: Katika vita vya Hunain Waislamu wote walikimbia na kumwacha Mtume peke yake, ispokuwa watu saba katika ukoo wa Bani Hashim ndio walikaa thabiti na imara. Miongoni mwa watu saba hawa mmoja alikuwa H. Ali ambaye kwa upanga wake akimhifadhi Mtume; na wa pili H. Abbas ambaye alikamata hatamu ya nyumbu wa Mtume, wengine watano waliobaki walimzunguka Mtume, ili makafiri wasimjie (Mtume). Ikaendelea hali hii mpaka Mwenyezi Mungu akampa uwezo na akashinda. Kwa hiyo katika aya hii neno la Mu'mineen wamekusudiwa hasa hawa wawili H. Ali, H. Abbas na wale Bani Hashim ambao wakati ule wa dhiki walikuwa na Mtume. Hebu niambie nani bora kati ya mabwana (H. Ali na H. Abbas, na wenziwao) wakati ule walikuwa na Mtume; na wale waliokimbia kujivusha nafsi zao ambao bila shaka Mwenyezi Mungu hakuwakuta hapo hata awateremshie juu yao utulivu?6
Allama: Bila shaka, ninayo yakini kwamba mabwana wale ni bora, ambao Mwenyezi Mungu amewateremshia utulivu juu yao.

 • 1. Ukitaka kujua zaidi vitazame vitabu vifuatavyo:
  Musnad kitabu cha Imam Ahmad Hanbal, Juzuu ya kwanza Uk. 99,141, 209, 331, 373 na katia juzuu ya nne Uk. 368, 370, 371 na katika juzuu ya tano Uk. 26
  Sunan Ibn Majah. MIango 11 Uk. 12
  Sunan Tirmidhi kitabu cha 46 Mlango wa Ishrini (20)
  Mustadrak kitabu cha Hakim Nishapoori, juzuu ya tatu, Uk. 136
  Jalaalud-Deen Suyooti, katika Tareekhul Khulafaa Uk. 113
  Musnad Abi Daaud At-Tiyaalisi juzuu ya kwanza, Uk. 26, hadithi ya 188 na juzuu ya tatu Uk. 93, hadithi ya 678
  Tareekh Muroojudh-dhahab cha Masudy, juzuu ya kwanza. Uk 307
  Tareekh AbiI-Fida, juzuu ya kwanza, Uk. 116
  Kanzul Ummal, juzuu ya sita Uk. 156 hadithi ya 2610
  Al-Istiab cha Ibn Abdil Barr, Uk. 470 na 786
  Viko vitabu vingi vingine vya kuthibitisha hiyo lakini kwa muhtasari tumevitaja hivyo tu
 • 2. Na kama iIivyoandikwa katika Habibussiyar kwamba H. Ali peke yake amewauwa makafiri 36. Na kama ukitaka kujua zaidi vitazame vitabu vifuatavyo:
  Tareekhul Kaamil kitabu cha lbn Atheer. Juzuu ya pili uk. 44 na 47
  Tareekhul Khamees 32 kitabu cha Diyaar Bakri, juzuu ya kwanza Uk. 418, 426, 427
  Mataalibus Suul ya Talha Ash-Shafiina
  Mohamed Yusuf I – Kunji katika kitabu chake Kifaayatu-Taalib. Viko vitabu vingi vingine vya kuthibitisha hiyo lakini kwa muhtasari tumevitaja hivyo tu
 • 3. Ukitaka kujua zaidi vitazame vitabu vifuatavyo:
  Tareekhul Khamees juzuu ya kwanza, Uk. 427 na 429
  Tareekhul Kaamil, juzuu ya pili Uk. 47
  Saheeh Bukhari, juzuu ya kumi na sita Uk. 12
  Viko vitabu vingi vingine vya kuthibitisha hiyo lakini kwa muhtasari tumevitaja hivyo tu
 • 4. Ukitaka kujua zaidi vitazame vitabu vifuatavyo:
  Zamakshari katika tafseer yake Kash-shaf juzuu ya pili uk. 511 na 512
  Waahidi katika kitabu cha “Asbaabun-Nuzuul”
  Zaynul-fata fi tafseer Hal-Ata kitabu cha al-Hafidh Abu Muhamed al-Asimi
  Ibn Jareer Tabaree katika kitabu chake “Al-Kifayah”
  Thaalabi katika tafseer yake ya Al-Kashf wal-Bayaan
  Ishaaq al-Hamawiy katika kitabu chake “Farayidus-Simtain”
  Viko vitabu vingi vingine vya kuthibitisha hayo lakini kwa muhtasari tumevitaja hivyo tu
 • 5. Ukitaka kujua zaidi vitazame vitabu vifuatavyo:­
  SunanTirmidhi ya BwanaTirmidhi
  Kitaabul Khasais cha Bwana Nasai, hadithi ya tisa
  Abu Jaffer Ibn Jariir Tabari ameandika kitabu kimoja kizima juu ya kisa hiki
  Muhammad Ibn Abdi Rabbih katika kitabu chake Al-Iqdul Fareed.
  Kitabul Ilal cha Bwana Dar Qutni
  Mustadrak cha Haakim, Juzuu ya Tatu uk. 130,131,132
  Jaamiul Usool ya Ibn Atheer Juzary
  Usdul Ghaaba ya Bwana IbnuI Atheer Juzary
  Mishkaatul Masabeeh ya Al-Khateeb Attab Rizi, uk. 564
  Lisaanul Meezan ya Ibn Hajar Asqalani
  Viko vitabu vingi vingine vya kuthibitisha hiyo lakini kwa muhtasari tumeandika hivyo tu
 • 6. Ukitaka kujua zaidi vitazame vitabu vifuatavyo:­
  Tareekhul Umam ya Ibn Jareer Tabari, juzuu ya tatu Uk. 128
  Tareekhul Kaamil ya Ibn Atheer Juzary ,juzuu ya pili Uk. 100
  Seeratun Nabi ya Ibnu Hishaam, juzuu ya nne, Uk. 72
  Tareekh abul Fida, juzuu ya Kwanza, Uk. 146
  Saheeh Bukhari, juzuu ya tatu, Uk. 45
  Kanzul Ummal, juzuu ya tano, Uk. 304 na 306, hadithi ya 5597, 5598, 5608
  Musnad Imam Ahmad Hanbal, juzuu ya kwanza Uk. 207 na 453 na juzuu ya nne, Uk. 281,04
  Seeratul Halbiya, juzuu ya tatu Uk. 125
  Tareekhul Khamees ya Diyar Bakri, juzuu ya pili Uk. 89 na 11
  Vipo vitabu vingi vingine vya kuthibitisha hiyo lakini kwa muhtasari tumevitaja hivyo tu