read

Majadiliano Kati ya Ma'mun na Wanachuoni Kuhusu Sifa za Ali Bin Abi Talib (a.s)

Dibaji Ya Toleo La Kwanza

Kitabu hiki ni tafsiri ya mazungumzo kati ya Khalifa mashuhuri wa Kiislamu aitwaye Ma'mun Ar-Rashid na wanachuoni arobaini wa Ki-islamu wenye elimu ya juu kabisa zama hizo. Jambo waliojadiliana ni ubora wa Seyyidna Ali bin Abi Talib (a.s) juu ya Masahaba wengine wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w).

Mazungumzo hayo yameandikwa na Bw. Abu Umar Ahmad bin Mohammad bin Abdi Rabbih Al-Undulusi (246 Hijria -327 Hijria) katika kitabu chake mashuhuri Al Iqdul ­Fareed. Mwanachuoni huyu Bw. Ibnu Abdi Rabbih alikuwa mashuhuri sana, na alikuwa mwenye elimu ya Lugha na alikuwa mtunga mashairi pia. Tangu hapo zamani watu walitambua na kujua thamani na kutunuka kwa kitabu chake hicho, hata wakawa wanapenda mno hata walijifunga kwa kukitalii na kudondoa mule na wakazitumia katika kutungia vitabu vyao na kuzungumzia katika hutuba zao. Na kilipigwa chapa mara nyingi sana kuanzia mwaka 1292 Hijria hadi 1384 Hijria miaka sita mbele.

Nakala tunayo katika Maktaba yetu hapo Dar es Sa­laam, imepigwa chapa Cairo (Misri) katika mwaka 1384 Hijria (1965 A.D) baada yakuangaliwa na kusahihishwa na wanachuoni watatu.

Mazungumzo hayo yameandikwa katika Juzuu ya tano, kuanzia uk. 92 hadi uk. 101, chini ya anwani:

(Majadiliano ya Ma'mun na Wanachuoni kuhusu ubora wa Ali (r.a).

Mwanachuoni mashuhuri wa Ki-Sunni aitwaye Allama Shibli Numani (India) ameandika mawazo yake juu ya majadiliano hayo hivi:

­"Mazungumzo mashuhuri ya Ma'mun ambayo yamethibitisha kwamba Bw. Ali bin Abi Talib alikuwa bora kuliko Masahaba wote na hakika majadiliano hayo yalikuwa yenye nguvu sana. Yahya bin Aktham na wanachuoni arobaini waliokuwa hodari wa zama hizo ndio waliokuwa wapinzani kwa dai hilo, na Ma'mun alikuwa peke yake. Wakati yalipoanza majadiliano hayo waliruhusiwa wazijibu hoja za Ma'mun bila ya hofu, bila ya kufikiria kwamba wanajadiliana na mfalme wao. Majadiliano hayo yalianza asubuhi hadi alasiri, pande zote mbili wakijadiliana vikali. Lakini juu ya hayo kwa kweli kila mara mshindi alikuwa Ma'mun. Majadiliano hayo yote yameandikwa katika kitabu Al-Iqdul Fareed, na kusema kweli ufunuo wa fikra, uhodari wa akili, na ujuzi wa elimu, ufasaha, na nguvu ya maelezo ya Ma'mun ni jambo la kustaajabisha sana."

Tafsiri ya majadiliano haya ilipigwa chapa hapo zamani katika lugha ya Urdu mara nyingi na Idara ya Islah; katika mji wa Khujwa, Saran (India).

Hivi karibuni tafsiri yake kwa Kiingereza imepigwa chapa na M/s. Peer Mohamed Ibrahim Trust, Karachi (Pakistan).

Kwa ushauri wangu mshiriki wangu Agha Seyyid Muhammad Mahdi Shushtari, ameifasiri kwa lugha ya Kiswahili; katika mwaka 1967; na sasa kwa manufaa ya watu wa Afrika ya Mashariki tunaipiga chapa.

Nafikiri ni wajibu kutaja hapa kwamba siku hizi ndugu zetu wa Kisunni wanaamini kuwa ubora wa Khulafau Rashideen ni kwa mujibu wa Ukhalifa wao; kwa mfano Bw. Abu Bakr ni bora kuliko wote, baadaye Bw. Umar bin Khattabu, baadaye Bw. Uthmani, tena Bw. Ali bin Abi Talib. Lakini itikadi na imani ya namna hiyo haitegemeani na hadithi za Mtukufu Mtume (s.a.w.w); na pia palikuwa na mzozo na hitilafu kubwa kati ya Masahaba na Tabein juu ya jambo hilo.

Imeandikwa katika Sharh-e-Maqasid cha Bw. Saad-ud ­Deen Taftazani hivi:­

(Kumfadhilisha mmoja juu ya mwenziwe ni jambo la uchunguzi (mawazo ya mwanachuoni tu); halina uthibitisho usiopingika.

Na Sayyid Sharif Ali bin Mohammad Jurjani (916 Hijria) ameandika katika kitabu chake Sharh-e-Mawaquif:

­(Jua kwamba jambo la ubora ni jambo ambalo hakuwezekani kupatikana yakinisho na uthabiti).

Na kwa sababu hiyo wanachuoni wa mbele wakihitilifiana kuhusu madhumuni hayo:­
(1) Kikundi kimoja waliitakidi kwamba Khulafau Rashideen ubora wao juu ya wenziwe hufuata kwa mujibu wa utaratibu wa ukhalifa wao, kama tulivyoeleza nyuma.

(2) Kikundi kingine waliitakidi kwamba Bw. Abu Bakr alikuwa bora, tena baadaye Bw. Umar. Baada ya hawa wawili hawakuweza kuamua kuwa Bw. Ali ni bora au Bw. Uthmani. Hii ni itikadi ya Imam Malik, Imam Abu Hanifa, Yahya bin Said Qattan na wengineo.

(3) Kikundi cha tatu wanaitakidi kwamba Bw. Ali alikuwa bora kuliko Bw Uthman. Katika kikundi hiki wamo kina Sufyan Thauri, Abu Bakr Khuzaima, Imam Abdalla Yafei, Imam Hakim na Abdullah bin Khattab.
(4) Kikundi cha kutosha waliitakidi kwamba Bw. Ali bin Abi Talib ni bora kuliko wote licha ya Bw. Abu Bakr. Ameandika Allama Ibn Abdil Barr katika kitabu chake "Istiaab".

"Vile vile wamehitilafiana wakubwa wa dini wa mbele kuhusu ubora wa Bw. Ali na Bw. Abu Bakr." Tena akaendelea kuandika hivi:

(Salman, Abu Dhar, Miqdad, Ammar, Khabbab, Jabir, Hudhaifa, Abu Saeed Al Khudri, Zaid bin Arqam (Masahaba) wote hao wamesema, "Wa mwanzo kabisa mwenye kuikubali dini ya Islamu ni Bw. Ali bin Talib na Masahaba hao wanamfadhilisha Bw. Ali juu ya wote").

Nimetoa maelezo haya hasa kueleza kwamba imani ya kawaida ya ndugu zetu wa Kisunni siku hizi si itikadi ambayo imekubaliwa na wakubwa wa dini wote.

Imam Ghazali ameeleza hivi:­
(Hakika ya ubora ni uliyoko kwa Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala; na ambaye hawezi kuujua isipokuwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) peke yake).

Ni dhahiri kuwa njia ya pekee kujua ubora (kufadhilika zaidi) kwa Mwenyezi Mungu ni kwa njia ya hadithi za Mtukufu Mtume (s.a.w.w) ; kuziangalia kwa uwangalifu zile Hadithi zenye nguvu, na zenye kukubaliwa na aghlabu ya Madhehebu ya Kiislamu.

Juu ya jambo hilo marehemu Bw. Ubaidullah Amritsari ameandika katika kitabu chake kiitwacho Ar-Jahul Matalib (Uk. 122) ifuatayo.

"Kuhusu hadithi za sifa na utukufu wa Bw. Ali bin Abi Talib zilizopokelewa na wanachuoni wa Kisunni Allama Ibn Abdil Barr katika kitabu chake kiitwacho 'Istiaab Fi Maarifatil As-habi' anaandika hivi: "Wamesema kina Al-Imam Ahmad bin Hanbal, Ismail bin Ishaki Al-Kadhi, Ahmad bin Ali bin Shuaib An-Nasai, na Abu Ali An Nisapuri:

Hazikupokewa hadithi kwa sanadi njema kuhusu fadhila za sahaba yeyote kwa wingi, kama zilivyopokewa kuhusu fadhila ya Bw. Ali bin Abi Talib (r.a).

"Licha ya hayo, tukiangalia zile sifa zenye kuhusika na yeye tu kwa wingi wa thawabu alizonazo, hapo utamuona bila shaka kwamba yeye (Ali) ni bora kuliko wote baada ya Mtume (s.a.w.w)."

Mtungaji huyo (yeye binafsi alikuwa Sunni) ameeleza kwa urefu habari hiyo katika kitabu chake hicho tulichokitaja, katika mlango wa tatu (kutoka Uk. 103 hadi Uk. 516).

Bilal Muslim Mission ya Tanzania inawashukuru Messrs. Peer Mohamed Ebrahim Trust ilioko Karachi (Pakistan) kwa kukipiga chapa kitabu hiki kwa ujira mdogo, hata tukaweza kukiuza kwa bei ya chini kama hiyo.

Seyyid Saeed Akhtar Rizvi
Chief Missionary
Bilal Muslim Mission of Tanzania
P. 0. Box 20033,
Dar-es-Salaam, Tanzania.
4 Julai, 1971

Dibaji Ya Toleo La Pili

Kwa vile toleo la kwanza lilipendwa mno na wasomaji, sasa tunachapisha toleo la pili.

Tunawashukuru Waislamu wenzetu kwa kuisaidia Jumuiya hii kwa msaada unaotuwezesha kukiuza kitabu hiki kwa bei rahisi. Mwenyezi Mungu awape jaza ya kheri katika dunia na Akhera. Amin.

Seyyid Saeed Akhtar Rizvi
Chief Missionary
Bilal Muslim Mission of Tanzania
26 Januari, 1978