read

Sura Ya Kumi: Kukutana Na Mwenyezi Mungu

Kuwa Pamoja Na Mwenyezi Mungu Ndani Ya Pepo

Licha ya hayo yaliyokwisha kutangulia, inasikitisha na kuvutia kuona kwamba Madhehebu ya Makhalifa imeruhusu fikra zao kwenda zitakavyo kuhusiana na kukutana na Mwenyezi Mungu katika masoko ya Peponi!

(1) Ibn Majah na Tirmidhi wamesimulia mazungumzo yafuatayo ndani ya Sunan zao. Abu Huraira wakati mmoja alimwambia Sa’id bin al-Musayyab:

“Mimi ninaomba kwamba tuweze kukutana pamoja katika soko la Peponi!”
Sa’id akamuuliza: “Hivi kuna soko ndani ya Pepo?”

Abu Huraira akasema: “Ndio hivyo, lipo! Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alinifahamisha mimi kwamba wakati watu wa Peponi watakapoingia humo, watawekwa kulin- gana na daraja za ubora katika matendo yao. Halafu wataruhusiwa kumtembelea Mwenyezi Mungu kwa kipindi cha wakati sawa na siku ya Ijumaa duniani. Hivyo watamtembelea Yeye, na atawaonyesha Kiti Chake cha Enzi, na kujidhihirisha Mwenyewe katika moja ya mabustani ya Peponi.

Kisha atawawekea majukwaa au mimbari za nuru, lulu, johari, kito mchanganyiko wa chuma/manganizi – chrysolite, na dhahabu. Mtu wa chini sana miongoni mwao atakuwa amewekwa kwenye malundo ya maski na kafuri, bila kujihisi kabisa kwamba wale watu walioko kwenye mimbari wamewekwa pazuri zaidi!”

Abu Huraira akaendelea :

“Halafu nikamuuliza Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, tutamuona Mola Wetu?” Yeye Mtume akasema: ‘Je, mna mashaka ya kuliona jua au mwezi kamili?’ Sisi tukasema: ‘La hasha, hatuna mashaka.’ Yeye akasema: ‘Kwa hiyo bila shaka mtamuona Mola Wenu Mtukufu. Kila mmoja wenu atain- gizwa kwenye hadhara Yake peke yake, na halafu kwa mmoja wenu Yeye Atakuja kumwambia: Ewe fulani bin fulani! Je, unaikumbuka ile siku ulipotenda tendo kadha na kadhaa?’ Yeye atajibu: ‘Ewe Mola Wangu! Hivi ulikuwa hukunisamehe!?

“Mwenyezi Mungu atasema: ‘Kwa kweli Nilikusamehe. Ni upana wa huruma Yangu ambao umekuleta wewe hapa kwenye kituo hiki!” Halafu wingu kutoka juu litawafunika, na itakuwepo mvua ya mfululizo ya manukato, ambayo harufu yake wao watakuwa hawajapata kuinusa kamwe. Mwenyezi Mungu Atasema: ‘Amkeni mfurahie neema Zangu na chukueni kila mtakachokitaka.’

Kisha tutafika kwenye soko tukiungana na Malaika. Ndani yake mtakuwa na vitu ambavyo mfano wake hatujawahi kuuona au kusikia au kudhania. Tutachukua chochote tunachotaka – hakuna kununua, wala hakuna kuuza! Watu watatembeleana, wale wa juu wakikutana na wa chini, na kwa hakika hakutakuwa na uduni, kwani kila mmoja atakuwa amevishwa vizuri, na katika welekeo bora. Hakutakuwepo na kitu cha kuhuzunikia.

Halafu tutarudi kwenye sehemu zetu, ambako wake zetu wenyewe watatupokea. Wao watasema: “Karibuni, mmerudi mkiwa watanashati zaidi na wazuri zaidi kuliko mlivyokuwa wakati ule mlipotuacha!” Sisi tutasema: “Tunastahiki kurudi na neema hizi kwa sababu leo tumekaa na Mola Wetu.”

Asili ya simulizi hii ya uongo inaweza kupatikana katika hadithi ifuatayo kutoka kwa Ka’b al-Ahbar, iliyosimuliwa na Darami katika kitabu chake akiikanusha madhehebu ya Jahmiyyah. Ka’b anasema:

“Mwenyezi Mungu hataikagua Pepo isipokuwa kusema:

‘Kuweni harufu nzuri kwa wenza wenu.’ Kisha patakuwepo na ongezeko la harufu nzuri mahali pote hapo. Na kwa muda wa kitambo sawa na siku ya Iddi hapa duniani, watatembea huko na huko katika mabustani ya Peponi. Mwenyezi Mungu ndipo atakapotokeza, na wao watamuona Yeye. Upepo mkali uliojaa harufu ya manukato na miski utavuma, na Mola Wao atawatimizia matakwa yao.

Halafu wao watarejea kwenye familia zao, ambako uzuri na utanashati wao utakuwa umeongeka mara sabini.”1

Abu Huraira alijaribu kuufanya uwongo huu kuwa wakupendeza zaidi kwa kutumia akili yake binafsi yenye mawazo mengi. Mbali na hadithi kama hizo, tunaona kwamba wanazuoni kutoka madhehebu ya Makhalifa wamechukua uhuru mwingi katika kuzielezea Ayah fulani za Qur’ani Tukufu katika namna ya kukidhi matamanio yao.

(2) Qur’ani Tukufu inasema:

لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ ۖ وَلَا يَرْهَقُ وُجُوهَهُمْ قَتَرٌ وَلَا ذِلَّةٌ ۚ أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {26}

Wale wanaofanya wema watapata wema na zaidi, na vumbi hal- itawafunika nyuso zao wala udhalili, hao ndio watu wa Peponi, humo wao watakaa milele.” (Yunus; 10: 26)

Katika Ayah hii, kile kifungu cha maneno “na zaidi” kilichotajwa baada ya malipo ya wema, kimechukuliwa kumaanisha upendeleo wa kukutana kwa maumbile, wazi wazi, na Mwenyezi Mungu! Tabari anasimulia kutoka kwa masahaba wanne wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), ambapo Suyuti anafanikiwa kusimulia kutoka kwa masahaba tisa, kwamba Mtume (s.a.w.w.) amesema:

“Ile ‘zaidi’ iliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu katika Ayah hii ina maana kwamba Mwenyezi Mungu atajionyesha Mwenyewe kwao.”2

Zaidi ya hayo, Abu Musa Ash’ari anasimulia yafuatayo kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.):

“Siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu atatuma mpiga mbiu kwa watu wa Peponi, akitangaza kwa sauti kubwa kiasi cha kutosha kuyafikia masikio ya wakazi wote akisema: ‘Mwenyezi Mungu amewaahidi wema na zaidi …’ Wema huo ni Pepo ambayo tayari mmeikalia – na hiyo zaidi ni kuu- tazama uso mtukufu wa yule Mwenye huruma.”

Tayalasi, Ahmad Hanbal, Muslim, Tirmidhi, Ibn Majah, Tabari, Suyuti na wafasiri wengine na wasimulizi wa hadithi wamesimulia yafuatayo kutoka kwa Shu’ayb:

“Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliisoma ile Ayah isemayo: Wale wanaofanya wema watapata wema na zaidi …’ na kisha akasema:

“Wakati watu wa Peponi watakapokuwa wamekusanyika ndani ya mabustani na pale wengine watakapokuwa wamepelekwa kwenye Jahannam ya milele, mpiga mbiu atatangaza: ‘Enyi watu wa Peponi, bado kuna ahadi ambayo haijatimizwa ambayo Mwenyezi Mungu sasa ataitimiza!’

“Hao watu wa Peponi watauliza: ‘Na ni ahadi gani hiyo iliyobakia? Kwani hajatuweka sisi mbali na moto wa jahannam?’

“Baada ya kuyasikia haya, Mwenyezi Mungu atanyanyua pazia, na tazama! Hapo wao watamuona Yeye. Wallahi! Katika neema zote zilizotolewa na Mwenyezi Mungu, hakuna kingine chenye kufurahisha zaidi na chenye nderemo kuliko ile fursa ya kuuona Uso Wake.”3

Ibn Kathiir katika tafsiri yake ya Ayah hiyo hiyo yeye anasema:

“Licha ya malipo mema wanayopewa wale watu wema, pia watakuwa na neema ya kuuona uso Wake Mtukkufu. Na hili limeungwa mkono na Abu Bakr Sidiq na wengineo…”

Hapa anatoa orodha ya watu kumi na tano, ambao miongoni mwao wengine ni masahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), na wengine ni wa zama za baadae kidogo. Hata Fakhrud-Din ar-Razi anaelekea kuunga mkono kwenye dhana hiyo hiyo, wakati anapoielezea Ayah hii. Yeye anasema:

“Tumelifanya kuwa dhahiri kwamba maneno ya Ayah hii kwa wazi kabisa yanaashiria kwamba ‘na zaidi’ inarejea kwenye kumuona Mwenyezi Mungu.”4

(3) Kuna baadhi ya hadithi zilizohusishwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuhusiana na Ayah ifuatayo:

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَاضِرَةٌ {22}

إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ {23}

“Nyuso siku hiyo zitang’aa. Zikingoja malipo kutoka kwa Mola wao. (Qiyaama; 75: 22-23)

Anas bin Malik anasimulia kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.):

“Katika ufufuo, waumini wanaume watamuona Mwenyezi Mungu kila siku ya Ijumaa, na waumini wanawake watamuona Yeye katika siku za Idd-el-Fitr na Iddul-Adh’ha.”

Katika hadithi nyingine iliyosimuliwa na Anas bin Malik tunamkuta yeye akisema:

“Mtume (s.a.w.w.) aliisoma Ayah hiyo halafu akaelezea:

‘Kwa jina la Allah! Ayah hii haijafutwa. Hakika wao watakuja kumuona Mwenyezi Mungu. Watapewa chakula cha kutosha ili wale na kunywa, na mgao mzuri wa manukato na mapambo. Na lile pazia baina yao na Mola wao litanyanyuliwa ili waweze kumuona Mola wao naye Mola wao awaone wao. Haya ndio aliyomaanisha Mwenyezi Mungu pale aliposema:

ۖ وَلَهُمْ رِزْقُهُمْ فِيهَا بُكْرَةً وَعَشِيًّا {62}

‘… na watapata riziki zao asubuhi na jioni’ (Maryam; 19: 62)

Suyuti amesimulia yafuatayo kutoka kwa Jabir, ambaye anasema: “Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: ‘Mwenyezi Mungu ataruhusu kuonwa na hadhara ya watu wote, lakini kwa Abu Bakr kutakuwa na udhihirishaji maalum.’”5

Abdullah bin Umar anaihusisha hadithi ifuatayo kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.):

“Kituo cha chini kabisa ndani ya Pepo kitamruhusu muumini kupokea neema za Mwenyezi Mungu kutoka umbali wa miaka elfu moja. Na kituo cha juu kabisa kitakuwa ni pale ambapo watauona uso wa Mwenyezi Mungu kila mawio na machweo ya jua.”

Tabari amerudia kusema tena imani hiyo hiyo ndani ya Tafsiir yake, na Fakhrudin ar-Razi ndani ya Tafsiir Kabiir anasema:

“Hapawezi kuwa na maana nyingine ya Ayah hii isipokuwa kule kutazama kwa wazi wazi.”

Hata yule mfasiri wa hivi karibuni na mwanazuoni kutoka madhehebu ya Makhalifa, Sayyid Qutubi, (aliyefariki mwaka 1386 Hijiria) anasisitiza ndani ya kitabu chake, Fi Zilal al-Qur’an kwamba kutakuwa na kukutana uso kwa uso, kwa dhahiri na Mwenyezi Mungu katika Siku ya Kiyama, na halafu anaendelea kuitukuza hali hiyo kwa kujigamba kote. Yeye anaandika:

“Ayah hii inataja kwa kifupi juu ya hali ambayo maneno hayawezi kuelezea, na ambayo akili zinashindwa kuele- wa. Hiyo itakuwa pale watu wema watakapoingia kwenye hali ya kunyanyuliwa kiroho isiyowahi kutokea, ya kipekee, na Pepo yenyewe pamoja na neema zake na furaha itaelekea kuwa si kitu na ndogo. Hizo nyuso zinazong’ara zitakuwa zinaangalia moja kwa moja kwenye uso Mtukufu wa Mwenyezi Mungu! Kunyanyuliwa kulikoje? Ni kiwango gani cha Utukufu!

“Wakati mtu anapoangalia maajabu ya maumbile, yaliyomzunguka mwenyewe na vile vile yaliyo karibu; usiku wa mbalamwezi au giza nene, au alfajiri inayochomoza, anajawa na furaha na mzinduko!
Hali yake itakuwaje, kisha, pale atakapoona, sio yale maajabu ya Mwenyezi Mungu, bali utukufu na uzuri wa Mwenyezi Mungu Mwenyewe? Kwa nini uso wake using’are kwa uangavu pale anapomuona Yeye?

“Mwanadamu hawezi kufikia hali hiyo mpaka awe amejitakasa mwenyewe kutokana na vikwazo vyote, hali adhimu sana ambayo inapaswa kutokuwa na mashaka yote na dosari – bila ya haja yoyote ila ya kumuona Mwenyezi Mungu, aliye juu, Mtukufu.

“Kwa nini watu wengine wanajinyima wenyewe hii nuru iliyozidi kabisa, hii starehe isioyoelezeka? Kwa nini wanajitatiza wenyewe katika mazoezi ya kiwanazuoni na mijadala ya hekima kuamua juu ya suala ambalo liko nje ya akili ya kibinadamu?

“Hebu natuamke basi ili tupokee huu upeo wa muungano wa kiroho na furaha halisi na tuziruhusu fikira zetu kuizingira hii hali halisi kwa kiasi iwezekanavyo. Mzinduko huu, wenyewe ni neema kubwa, kuweza kuzidiwa na chochote kile bali kule kuuona kwa ukweli ule Uso Mtukufu.”6

Sasa tutawasilisha yale mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s.) kuhusiana na suala tulilolijadili hapo juu.

Madhehebu Ya Ahlul-Bayt (A.S.)

(1) Abdus-Salaam bin Swaleh anasimulia hadithi kupitia kwa Abu al-Swalt al-Hirawi kutoka kwa Imam Ridha (a.s.). Yeye anasema: Nilimuuliza Ali ibn Musa ar-Ridha (a.s.):

“Je, unasemaje kuhusu hili wazo linaloenezwa na watu fulani wa Hadithi kwamba ati waumini watakuja kumtembelea Mola Wao katika makazi yao ya Peponi?”

Imam (a.s.) akajibu akasema:

“Ewe Aba as-Swalt, Mwenyezi Mungu alimbariki Mtume Wake (s.a.w.w.) kwa ubora juu ya viumbe Wake wote, ikiwa ni pamoja na Mitume na Malaika; na ameweka utii wa Mtume (s.a.w.w.) katika uzito ule ule kama utii Kwake Mwenyewe, na kule kumuona Mtume (s.a.w.w.) hapa duniani na kesho akhera kama kumuona Yeye.”

Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Qur’ani Tukufu:

مَنْ يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّهَ ۖ {80}

“Mwenye kumtii Mtume basi amemtii Mwenyezi Mungu…” (An- Nisaa; 4: 80)
Na kisha anasema tena:

إِنَّ الَّذِينَ يُبَايِعُونَكَ إِنَّمَا يُبَايِعُونَ اللَّهَ يَدُ اللَّهِ فَوْقَ أَيْدِيهِمْ ۚ {10}

“Bila shaka wale wanaofungamana nawe, basi kwa hakika wanafungamana na Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao…” (Fat’h; 48: 10)

Na Mtukufu Mtume mwenyewe amesema:

“Yeyote anayenitembelea wakati wa uhai wangu au baada ya kufariki kwangu, anayo malipo ya kumtembelea Mwenyezi Mungu.”

“Cheo cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) huko Peponi kitakuwa ndio cha hali ya juu kabisa, na h ii ndio sababu kumuona au kumtembelea yeye kutakuwa ni sawasawa na kumtembelea Mwenyezi Mungu Aliye juu, Mtukufu.”

Abu Swalt akasema:

“Ewe mtoto wa Mtume (s.a.w.w.) tutaitafsiri vipi ile hadithi inayosema: ‘Yeyote anayekiri kwamba hapana mungu ila Allah, atakuja kuuona uso wa Mwenyezi Mungu?’”

Imam (a.s.) akasema:
“Ewe Abu Swalt, yeyote anayehusisha uso kwa Mwenyezi Mungu, anafanya kufuru. Uso huo unaashiria Mitume Wake na Manabii – amani iwe juu yao wote – kwa sababu wanatuongoza sisi kumuelekea Mwenyezi Mungu, Dini Yake, njia Yake na kumtambua Yeye. Hii ndiyo maana yake pale Mwenyezi Mungu anaposema ndani ya Qur’ani Tukufu kwamba:

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ {26}

وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ {27}

“Kila kitu juu yake kitatoweka. Na itabaki dhati ya Mola Wako, Mwenye utukufu na Heshima.” (Ar-Rahmaan; 55: 26-27)

ۚ كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ ۚ لَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ {88}

“…Kila kitu kitaangamia isipokuwa uso Wake..(Qasas; 28: 88)

Malipo makubwa na ya kupendeza sana juu ya waumini yatakuwa ni kule kukutana na Mitume na Manabii wa Mwenyezi Mungu katika Siku ya Kiyama. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema:

“Wale wanaowachukia Ahlul-Bayt wangu (watu wa nyumbani kwangu) na kizazi changu, hao hawatakutana nami, wala mimi sitakuja kukutana nao katika Siku ya Kiyama.”

Yeye alisema pia wakati akizungumza na masahaba wake:

“Wapo baadhi miongoni mwenu ambao hawataniona mimi kabisa baada ya kuwa wameondokana nami hapa duniani.”

“Ewe Abu Swalt! Mwenyezi Mungu Aliye Juu zaidi haelezewi kwa kumpangia sehemu au nafasi. Wala Yeye hawezi kuzingatiwa kwa kuona au kufikiria!”7

(2) Ibrahim ibn Abu Mahmuud anasimulia kwamba Imam Ridha (a.s.) aliulizwa kuhusu Ayah ifuatayo:

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَاضِرَةٌ {22}

إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ {23}

“Nyuso siku hiyo zitang’aa. Zikingoja malipo kutoka kwa Mola wao. (Qiyaama; 75: 22-23)

Yeye (a.s.) akasema:

“Maana yake ni kwamba nyuso zao zitachangamka kwa mng’aro, katika matarajio ya malipo matukufu.”8

(3) Na kuhusu Ayah ifuatayo:

لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ ۖ {26}

“Na kwa wale waliofanya wema watapata malipo mema na zaidi…”(Yuunus; 10: 26)

Tunazo hadithi tatu kutoka kwa Maimamu wa Ahlul-Bayt (a.s.), kila moja ikitoa maelezo yale yale kama hizo nyingine.

(a) Amirul-Mu’minin, Ali ibn Abi Talib (a.s.) amesema:

“Malipo mazuri katika Ayah hii yanahusu Pepo, na hiyo ‘zaidi’ inahusu kurudishwa kwa ziada tena duniani.”

(b) Imam al-Baqir (a.s.) amesema:

“Ayah hii inazungumzia kipimo cha nyongeza, ikimaanisha kile ambacho Mwenyezi Mungu atakitoa wakati wa kipindi cha uhai wa duniani; hakitafanyiwa hesabu hiyo Siku ya Hukumu.”
(c) Imam Ja’far as-Sadiq (a.s.) amesema:

“ ‘Na zaidi’ itakuwa ni kutoka kwenye duniani hii, kile ambacho kwacho Mwenyezi Mungu huwaneemesha waumini wakati wa kipindi cha uhai wao na hakipunguzwi kutoka kwenye malipo ya Akhera. Hivyo, Mwenyezi Mungu huwaunganishia wao malipo yote, kwa sababu ya matendo yao mema.”

Inashangaza kwamba wanazuoni kutoka Madhehebu ya Makhalifa wamekuwa siku zote wakichagua kutafsiri Ayah za Qur’ani Tukufu kwa mujibu wa dhana ya Kiyahudi au ya Kikristo kuhusiana na Mungu. Hebu tuchukue mfano wa neno Nadhirah ambalo limetafsiriwa na wao kwa maana ya ‘kutazama’.

Raghib ndani ya Mufradat al-Qur’an anasema kwamba Nadhirah ina maana mbili:

(i) Yule mtazamaji;

(ii) Mtarajia, yule anayesubiria.

Na Qur’ani Tukufu yenyewe imelitumia neno hilo kuashiria “matarajio”. Katika Suratun-Naml, Ayah ya 35 tunasoma hivi:

وَإِنِّي مُرْسِلَةٌ إِلَيْهِمْ بِهَدِيَّةٍ فَنَاظِرَةٌ بِمَ يَرْجِعُ الْمُرْسَلُونَ {35}

“Na mimi nitawapelekea zawadi, nami nitangoja watakayorudi nayo wajumbe.” (An-Naml; 27: 35)

Ahlul-Bayt (a.s.) wameweka wazi kwamba Ayah hii haizungumzii kumuona Mwenyezi Mungu kwa umbile.

Inatoa maelezo yenye kuonyesha picha ya wazi ya jinsi waumini watakavyochangamka kwa matarajio juu ya malipo yao ya thawabu.

Vivyo hivyo, wakati walipolifafanua hilo neno Ziyada “zaidi” lililotumiwa na Mwenyezi Mungu, wao wameelekeza tafsiri yao juu ya Qur’ani Tukufu yenyewe.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

وَقِيلَ لِلَّذِينَ اتَّقَوْا مَاذَا أَنْزَلَ رَبُّكُمْ ۚ قَالُوا خَيْرًا ۗ لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا فِي هَٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةٌ ۚ وَلَدَارُ الْآخِرَةِ خَيْرٌ ۚ

وَلَنِعْمَ دَارُ الْمُتَّقِينَ {30}

“Na kwa wale waliofanya wema katika dunia hii (pia) watapata malipo mema na hakika nyumba ya akhera ni bora zaidi. Na ni bora zaidi makazi ya wachamungu.” (An-Nahl; 16: 30)

Kutafsiri ‘zaidi’ kama ni kumuona Mwenyezi Mungu ni kitu ambacho kilikuwa hakiaminiki kabisa. Katika mlango ufuatao, ambao ni wa mahitimisho, tutawasilisha ulinganishaji mfupi wa madhehebu hizi mbili, na kuthibitisha hasa kwamba mafundisho halisi kabisa ya Kiislamu, yasiyochafuliwa na kutiwa madoa, yanapatikana kutoka kwa Ahlul-Bayt (A.S.)

Hitmisho

Tawhiid – Kanuni Kuu Na Ya Msingi Ya Ibada Ya Kiislamu.

Mwenyezi Mungu kama anavyofahamika na madhehebu ya Makhalifa:

1. Ana uso wa kibinadamu, na viungo na sehemu!

2. Anakaa juu ya Arsh – Kiti cha Enzi – na mwili Wake unakizidi kikalio cha kiti hicho kwa urefu wa vidole vinne kutoka pande zote!

3. Kiti hicho kimewekwa juu ya mbuzi wa mlimani wanane!

4. Kiti hicho kinanywea na kutoa kelele chini ya uzito wa Mwenyezi Mungu, kama tandiko la farasi jipya, ambalo linatoa makelele chini ya uzito wa mpandaji!

5. Nyakati zingine. Yeye huteremka hadi kwenye mbingu ya chini kabisa na kuwataka viumbe Wake kumuomba na kumsihi!

6. Atakuja kujionyesha Mwenyewe katika Siku ya Kiyama, kwanza katika sura ngeni na halafu kwa uso unaofahamika!

7. Baadhi ya waumini watakuja kumtambua Mola Wao hapo wakat- apoona muundi Wake!

8. Mwenyezi Mungu atakuja kuwatembelea waumini mmoja mmoja kila mtu peke yake, atakutana nao na pia ataongea nao Peponi!

Wanaiita Tawhiid

Ibn Khuzaimah, mwanazuoni mwenye kuongoza katika kundi hili, anakusanya hadithi zinazounga mkono dhana hiyo hapo juu, na anakiita kitabu hicho, Kitabu cha Tawhiid!

Bukhari ndani ya Sahih yake anao mlango ambamo ndani yake ananukuu na kuzisimulia hadithi hizo zilizotajwa hapo juu na kisha anauita mlango huo Mlango wa Tawhiid!

Amefanya vivyo hivyo Muslim ndani ya Sahih yake na anauita mlango huo, Mlango wa Tawhiid!

Hadithi hizi hasa zinaanzia kwa Abu Huraira na Bwana wake wa Kiyahudi, Ka’b al-Ahbar, na mwaliko wa mawazo ya Kiyahudi juu ya uungu. Kwa hiyo, tunaziainisha hadithi kama hizi kama utomaji maneno kutoka kwenye hadithi za Israiliyyat.

Matokeo yake, madhehebu ya Makhalifa inachangia kwenye dhana ya uhusishaji maumbile kwa Mwenyezi Mungu – anthropomorphic notion – na kutoa maana halisi, ya neno kwa neno, katika nyingi ya Ayah za Qur’ani Tukufu bila kujali vidokezo vyake vya kiistiari.

Kutoka Madhehebu Ya Ahlul-Bayt (A.S.)

Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) imetufundisha sisi kwamba Mwenyezi Mungu hana anachofanana nacho. Wake Yeye ni Upweke Kamili, na hakuna viungo au sehemu, hakuna nafasi au mipaka inayoweza kuhusishwa Kwake.

Kwa kufanya hivyo, Ahlul-Bayt (a.s.) wametupa sisi maana halisi ya Qur’ani Tukufu na hadithi za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na kuzing’oa zile fikra zote zisizo sahihi ambazo zilipata kupenyezwa kutoka kwenye kambi za Kiyahudi na Kikristo.

Wanazuoni wa Madhehebu hii wamesimulia kutoka kwa Ahlul-Bayt (a.s.), katika vitabu vyao muhimu kama Tafsiir na Kitabu cha Hadithi. Matokeo yake, ule muundo asili wa itikadi ya ya Kiislamu umebakia bila kuchafuliwa.

Sasa ni wazi kabisa kwamba isingekuwa kwa juhudi kubwa na bila kuchoka za Maimamu wa Ahlul-Bayt (a.s.) na wafuasi wao, ile imani kuu ya Tawhiid ndani ya Uislamu ingeweza kupotea kabisa, moja kwa moja.

Kinyume na Ahlul-Bayt (a.s.) linakuwepo, ingawa kwa masikitiko sana, kundi la Waislamu ambao wamenasa katika mtego na kuwa mateka kwenye dhana isiyo ya Kiislamu juu ya Tawhiid.

Tuna bahati kiasi gani sisi kushikilia kwenye njia ya Ahlul-Bayt (a.s.). Kwa hakika wametuokoa sisi kutokana na ushirikina. Hivyo tunatoa heshima zetu kwao kwa kunukuu kutoka kwenye Ziyaratul-Jamii’a.

“Amani juu yenu, enyi Maimam wa Nyumba ya Mtukufu
Mtume, na walinzi wa hazina ya Elimu!

“Amani juu ya viongozi wa kwenye uongovu wa kweli,
na nuru ing’aayo kwenye giza,

“Amani juu ya daraja za utambuzi na ufahamu mtukufu!

“Amani juu ya wale wanaomlilia Mwenyezi Mungu, na wale
ambao ni wasafi katika Tawhiid Yake,

“Mwenyezi Mungu amekuchagueni ninyi kama wasaidizi katika Njia Yake,
wafasiri wa uteremsho Wake, na nguzo imara za Tawhiid Yake,

“Mmewalingania watu kuja kwenye Njia Yake kwa heki- ma na mawaidha mazuri,

“Mwenyezi Mungu aniimarishe, kwa kipindi nitaka- chokuwa hai, katika ufuasi juu yenu,
mapenzi yenu na dini yenu,

“Na aniweke miongoni mwa wale wanaofuata nyayo
zenu, kutembea katika njia yenu na kunufaika kutokana
na mwongozo wenu.”

  • 1. Ar-Radd ala al-Jahmiyyah, cha Darami, uk. 53
  • 2. *Tafsiir Tabari - Juz. 11, uk. 73 na 76; na Tafsiir ya Suyuti - Juz. 3, uk.305- 306.
  • 3. Sahih Muslim - uk. 163; Sunan Ibn Majah - Juz. 1, uk. 67; Musnad Ahmad Hanbal - Juz. 4, uk. 332-333; Tafsiir Tabari - Juz. 11, uk. 75; Tafsiir ya Suyuti - Juz. 3, uk. 305.
  • 4. Tafsiir Kabiir - Juz. 17, uk. 78-79
  • 5. as-Durrul-Manthuur - Juz. 6, uk. 292
  • 6. Fi Zilal al-Qur'an cha Sayyid Qutubi - Chapa ya kwanza, Cairo - Juz. 29, uk.208-210
  • 7. Tawhiid, cha Saduuq - uk. 117-118
  • 8. Tawhiid, cha Saduuq - uk. 116