read

Sura Ya Kwanza: “Mfano” Wa Mwenyezi Mungu

(A) Kutoka Madhehebu Ya Makhalifa

Hebu tuzichunguze hadithi mbili kutoka kwenye madhehebu hii:

1. Ibn Khuzaimah ndani ya Tawhiid, pamoja na Bukhari na Muslim wanasimulia kupitia kwa Abu Huraira kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema:

“Allah amemuumba Adam kwa mfano Wake Mwenyewe, futi sitini kwa urefu. Halafu Akamuamuru yeye kwenda mbele ya kikundi cha Malaika na kuwasalimia. ‘Wasikilize vizuri wakati wanapojibu maamkuzi yako, kwani hayo yatakuwa ndio maakuzi wewe na kizazi chako mtakayotu- mia,’ Allaha akasema.

“Hivyo Adamu akatii na akawaamkia hivi: ‘Assalamu Alaikum’ (Amani iwe juu yenu). Hao Malaika wakamjibu: ‘Assalamu Alaika wa Rahmatullah.’ (Amani iwe juu yako na Rehma za Mwenyezi Mungu), wakiongezea ‘Wa Rahmatullah.’

“Hivyo kila mmoja anayeingia peponi atakuwa katika mfano wa umbile la Adam. Wanadamu walipunguzwa tarat- ibu katika urefu kiasi muda ulivyopita, hadi kufikia kimo walichonacho leo hii.”

2. Abu Huraira anasimulia kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema:

“Wakati wowote ule mtu anapohusika kwenye ugomvi au mapigano dhidi ndugu yake, mtu anapaswa kujiepusha kumpiga kwenye uso. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu alimuumba Adam katika mfano Wake Mwenyewe.”1

Hizi ni hadith kutoka kwa Abu Huraira. Hebu sasa tuzilinganishe na hadithi zilizosimuliwa na Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) ili picha ipate kukamilika.

(B) Ahlul-Bayt (A.S.) Wanauelezea Ukweli Hasa

1. Husayn bin Khalid anasema:

“Nilimuuliza Imam Ridha (a.s.) kuhusu ile hadithi mashuhuri ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwamba Mwenyezi Mungu alimuumba Adam katika mfano Wake Mwenyewe. Yeye akasema: ‘Walaaniwe wale wasimuliaji wadanganyifu ambao wameiacha ile sehhemu ya kwanza ya hadithi hii.’ Kisha akaelezea: Wakati mmoja Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa anapita pale aliposikia watu wawili wakitukanana wenyewe kwa wenyewe. Alimsikia mmoja wao akisema kwamba: ‘Mwenyezi Mungu auchukize na kuufedhehesha uso wako, na uso ambao unafanana na wako.’

Wakati huo, Mtukufu Mtume akasimama na kuwaonya kwa kusema: ‘Usitamke maneno kama hayo kumwambia ndugu yako. Kwani Mwenyezi Mungu amemuumba Adamu (pia) kwa mfano wake. (Akimaanisha kwamba Adamu vilevile alifanana na huyo ndugu yake).”

2. Katika hadithi nyingine iliyosimuliwa na Abul Ward kwa Thamamah kutoka kwa Amirul Mu’minin Ali ibn Abi Talib (a.s.) tunasoma kama ifuatavyo:

“Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimsikia mtu mmoja anamtukana mwingine akisema kwamba: ‘Mwenyezi Mungu auchukize na kuufedhehesha uso wako, na uso unaofanana na wako.’ Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: ‘Nyamaza kimya! Usisema maneno kama hayo! Kwani Mwenyezi Mungu alimuumba Adamu katika mfano wake.’”

3. Licha ya hadithi hizi mbili, hebu natuchunguze nyingine moja zaidi, ambayo itatupa maoni ya jumla juu ya jinsi Maimamu wa Ahlul-Bayt (a.s.) walivyoziangalia imani za uhusishaji viungo kwa Allah (anthropomorphism).

Saduuq katika kitabu chake cha Tawhiid anasema:

“Imam Musa ibn Ja’far (a.s.) alipokea barua ambayo ndani yake mtu mmoja alikuwa akitafuta ubainisho kuhusu ile imani inayohusu mwili na mfano wa Mwenyezi Mungu. Imam (a.s.) akamjibu: ‘Sifa zote zimwendee Allah swt! Hakuna chochote kile kinachofanana na Yeye – hakuna mwili na wala hakuna mfano.’”

(C) Uchunguzi Na Ulinganishaji

Tunapotafakari juu ya hadithi hizi na kuzilinganisha, tunakuta kwamba Abu Huraira katika hadithi zake mbili ameweka nyongeza mbili na ameacha jambo moja.

1. Lile Ambalo Limeachwa

Wakati Abu Huraira anaposimulia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), yeye analiacha lile tukio ambamo Mtume alikabiliana na watu wawili waliohusika katika lugha chafu na matusi, halafu akamuonya mmoja wao asiizungumzie vibaya sura ya mwanadamu kwa sababu ilifanana na ile ya Adam. Kwa hakika jambo lililoachwa hapa ni muhimu sana, kwa sababu maelezo ya Abu Huraira yanatoa taswira kwamba kile kiwakilishi nomino “yake” kinarejea kwa Mwenyezi Mungu, ambapo kwa kweli kinarejea kwa yule mtu mwenyewe.

Abu Huraira anaweza kuwa ameacha ile sehemu muhimu ya hadithi hiyo kwa sababu:-

(a) Alikuwa akihifadhi hadithi kichwani, kwa vile alivyokuwa hawezi kusoma wala kuandika. Na hata kama angekuwa anaweza, asingeruhusiwa na hao Makhalifa ambao walikuwa wamewakataza Waislamu kutunza kumbukumbu ya maandishi ya hadithi za Mtume, hadi mwisho wa karne ya kwanza ya Hijiria.

(b) Abu Huraira alikuwa ameshawishiwa sana na Ka’b al-Ahbar ambaye alieneza hadithi fupi
zilizopotoshwa kutoka kwenye Taurati miongoni mwa Waislamu. Ni dhahiri, athari za kile
alichokisimulia Ka’b zilikuwa bado zina nguvu mpya kwenye akili ya Abu Huraira, kwa sababu kimekuja takriban miaka ishirini baada ya kukisikia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

(c) Huenda kosa lilikuwa upande wa wasimulizi wa siku za baadae ambao walizinakili simulizi
za Ka’b zilizohusishwa kwa makosa kwa Abu Huraira. Vyovyote vile hali iwavyo, matokeo
yake yanabakia vile vile, bila kubadilika.

2. Nyongeza Mbili

(a) Katika hadithi ya kwanza, Abu Huraira anayahusisha maelezo yafu- atayo kwa Mtukufu
Mtume (s.a.w.w.):-

“Wakati wowote mtu anaposhiriki katika ugomvi dhidi ya ndugu yake, huyo ajiepushe na kumpiga usoni mwake…..”

Inawezekana hii ni hadithi mbadala iliyobuniwa na Abu Huraira, mahala pa ule uachwaji tulioutaja hapo juu.

(b) Katika hadithi nyingine, Abu Huraira anazungumzia juu ya urefu wa Adam:-

“Mwenyezi Mungu amemuumba Adam katika mfano Wake,
kwa urefu wa futi sitini…..”

Ni dhahiri, maelezo kama haya si yenye ukweli, wala hayapatani na uchunguzi wa kielimu.

Mtu anaweza kuona kwa urahisi kwamba hadithi zilizosimuliwa kutoka kwa Abu Huraira zinabeba kufanana kunakoafikiana sana na zile hadithi kutoka kitabu cha Mwanzo ndani ya Agano la Kale.

Kwa kuzichezea zile hadithi za kweli za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), kuingiza maneno hapa na pale, kukata hapa na pale, Abu Huraira na wanaofanana naye wamefanikiwa kutoa usadikikaji kwenye hadithi za uzushi kutoka kwenye Taurati. Hizi, hivyo basi, ndio hadithi Israiliyyat, ambazo zimefanya uingiliaji wa kuhuzunisha kwenye hadithi na imani za Kiislamu.

Madhehebu za Makhalifa zimezimeza, kuanzia ndoano, kamba yake na chambo chake, kwa sababu majina maarufu kama yale ya akina Abu Huraira yameambatanishwa nazo.

Matokeo yake yamekuwa kwamba mahali popote pale maneno kama “uso” yanapotokea kuhusiana na Mwenyezi Mungu ndani ya Qur’ani Tukufu, wao wamesisitiza juu ya maana halisi. Kwao wao, sifa zote za kibinadamu, kanuni na maumbo vinaweza kutumika kwa Mwenyezi Mungu! Tutalijadili somo hili katika milango inayofuata Inshallah.

  • 1. Sahih Muslim, uk. 2016, 2017