read

Sura Ya Nane: Mwenyezi Mungu Nyuma Ya Pazia

Darami, katika kuwakanusha kwake hao Jahmiyyah, anao mlango mzima unaoitwa Al-Ihtijaj, na yeye ananukuu hadith tatu zifuatazo ambazo zimehusishwa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

(i) Jabir Ansari anasema:

“Mtume (s.a.w.w.) amesema kwamba Mwenyezi Mungu hakuzungumza na yeyote kamwe isipokuwa kutoka nyuma ya pazia.”

Ni dhahiri kabisa, hadithi hii inahusiana na Ayah ifuatayo:

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَنْ يُكَلِّمَهُ اللَّهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِنْ وَرَاءِ حِجَابٍ {51}

“Na haikuwa kwa mtu yeyote kwamba Mwenyezi Mungu aseme naye ila kwa wahyi au kwa nyuma ya pazia …..” (As-Shuraa; 42: 51)

Wameipokea ile maana halisi ya neno pazia – kipande cha nguo, pazia linalomficha Mwenyezi Mungu kutoka kwa watu; na wameendelea kubuni vipande vingi vya kuvutia vya kipuuzi.

Hapa kuna hadithi nyingine:

(ii) Abu Musa Ashari anasimulia kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.):

“Pazia la Mwenyezi Mungu ni ‘Moto!’”

(iii) Zurarah bin Awfa anasimulia:

“Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimuuliza Jibril kama alikuwa amewahi kumuona Mola Wake. Jibril akajibu: Oh, Muhammad! Kati Yake na mimi kuna mapazia sabini ya nuru; na kama nitajaribu kusogea karibu na hilo la kwanza, basi nitaungua.’”

Licha ya hizi hadithi tatu, ipo moja ya nyongeza kutoka kwa Abdullah bin Umar, ambaye amesema:

“Mwenyezi Mungu amefichikana kwa waja Wake kwa mapazia ya Moto, Giza na Mwanga.”

Mwishoni, Darami anamalizia kwamba:

“Ile hadithi ya Jibril inaashiria wazi kwamba Mwenyezi Mungu yuko nyuma ya pazia, na kwa hiyo amejitenganisha na viumbe Wake. Kwa hiyo, kama ingekuwa kweli kwamba ni Mwenye kupatikana kila mahala, basi kuwepo kwa pazia kungekuwa hakuna maana yoyote.”

Wanazuoni kutoka Madhehebu ya Makhalifa wametegemea sana juu ya maana halisi ya neno Hijab, ambalo linatokea kwenye Ayah kadhaa za Qur’ani Tukufu.

Kwa mfano, katika hiyo Ayah iliyonukuliwa hapo juu kutoka kwenye Surah ya As-Shuraa: 51, kifungu cha maneno, “kutoka nyuma ya pazia” ni cha kiistiari kinachodokeza kwamba Mwenyezi Mungu anazungumza na watu katika namna kwamba sauti inasikika bila ya mzungumzaji kuonekana.

Hakuna pazia la kimaada hapo la kumtenganisha Mwenyezi Mungu na hao Mitume, kwani kwa hali hiyo, Mwenyezi Mungu atakuwa amezuilika mahali – wazo ambalo ni geni kabisa kwenye dhana ya asili ya Mwenyezi Mungu katika Uislamu.

Ayah nyingine ni hii:

كَلَّا إِنَّهُمْ عَنْ رَبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَمَحْجُوبُونَ {15}

“Sivyo, hakika kwa Mola wao, siku hiyo watakingiwa na pazia.” (Mutaffifiin; 83: 15)

Imam Fakhruddin ar-Razi ndani ya Tafsiir yake (31/96, chapa ya Misri) anasema:

“Ni muhimu kwamba tunaitafsiri Ayah hii kumaanisha kwamba wale makafiri watazuiliwa kumuona Mwenyezi Mungu, kwa njia ya kuwekewa pazia.”

Kisha anatafuta uthibitisho kutoka kwa Maqatil ambaye amesema:

“Hilo pazia linaelezea kwamba baada ya kufufuliwa na kuhesabiwa, wale makafiri hawatamuona Mwenyezi Mungu. Kwa kweli wale waumini watamuona Yeye.”

Imam wa madhehebu ya Maliki, yaani Malik bin Anas anasema: “Kwa vile Mwenyezi Mungu atakuwa nyuma ya pazia, akiwa amefichika kutoka kwa maadui Zake, atadhihirisha utukufu wake juu ya marafiki Zake ili waweze kumuona Yeye.”

Na Muhammad ibn Idriis, maarufu sana kwa jina la Shafii’ anaielezea Ayah hiyo hivi:

“Kwa vile Mwenyezi Mungu Mwenyewe atajificha kutokana na maadui Zake ili kudhihirisha ghadhabu Zake, ni dhahiri kwamba atajidhihirisha Mwenyewe kwa wale ambao ni marafiki Zake kuonyesha radhi Zake.”

Ibn Kathiir, ndani ya Tafsiir yake ameyatwaa yale maelezo ya Imam Shafii’! Hebu sasa tugeukie kwenye kile ambacho Ahlul-Bayt (a.s.) wamekieleza.

Je, Kuna Pazia?

(1) Saduuq ndani ya Tawhiid yake anasimulia hadithi fupi ya kuvutia kutoka kwa Haarith al-Aawar. Yeye anasema wakati mmoja ambapo Ali bin Abi Talib (a.s.) alipoingia eneo la sokoni, alimsikia mtu mmoja ambaye alikuwa amesimama akiwa amempa kisogo, akisema maneno yafuatayo: “Naapa kwa Yeye Ambaye yuko nyuma ya pazia mbele ya zile mbingu saba!” Ali bin Abi Talib alimpiga mgongoni mwake na kuuliza: “Na ni nani aliyeko mbele ya hizo mbingu saba?”

Yule mtu akasema: “Oh, Amirul Mu’minin, nilimaanisha ‘Mwenyezi Mungu’ alikuwa nyuma ya pazia.”

Ali (a.s.) akasema:

“Hiyo kwa hakika ni dhambi kubwa. Hakuna kifuniko au pazia linalomtenganisha Mwenyezi Mungu kutoka kwa viumbe Wake. Yeye yupo kila mahali!”

Yule mtu akamuuliza Ali bin Abi Talib (a.s.) kama kulikuwa na kitendo cha toba cha lazima ili kufidia ile dhambi aliyoifanya.

Ali (a.s.) akasema:

“Fidia yake ni kuelewa vizuri na kwa dhahiri kwamba Yeye yuko pamoja na wewe mahali popote utakapokuwa.!” Yule mtu akauliza tena: “Je, ninapaswa kulisha masikini kama fidia ya hilo?” Ali (a.s.) akasema: “Hilo pia haliingii hapa, kwa sababu umeapia kwa jina la mmoja ambaye siye Mola wako.”

Maoni

(i) Katika hadithi fupi ya hapo juu, tunaona mtu amekula kiapo, ambacho ni cha uasi. Imam Ali (a.s.) anamwelekeza yeye kufidia kule kupotoka kwa kuielewa Tawhiid katika muundo wake halisi. Anamuathiri kwa ule ukweli kwamba hakuna mapazia wala maficho na kwamba Mwenyezi Mungu Yupo mahali pote.

(ii) Wakati mtu huyo huyo akiuliza kama anapaswa kufidia kwa ajili ya kiapo alichokichukua, Imam (a.s.) anarudia kusema kwa kumwambia kwamba lengo la kiapo chake halikuwa ni Mwenyezi Mungu – na kwa hiyo kiapo hicho hakikuwa na thamani yoyote ile iwayo.

(2) Saduuq katika Tawhiid yake anasimulia kwamba Imam Ridha (a.s) aliombwa kuelezea juu ya Ayah ifuatayo:

كَلَّا إِنَّهُمْ عَنْ رَبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَمَحْجُوبُونَ {15}

“Sivyo, hakika kwa Mola wao, siku hiyo watakingiwa na pazia.” (Mutaffifiin; 83: 15)

Akasema

“Hakuna mahali mahsusi panapoweza kuhusishwa maalum kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa maana ya kwamba anakaa hapo, na kutokea hapo anachukua pazia kujitenga Mwenyewe kutoka kwa viumbe Wake. Maana halisi ya Ayah hiyo ni kwamba: ‘…wao watazikosa rehema za Mola Wao.’”

Halafu aliulizwa kuhusu Ayah ifuatayo:

هَلْ يَنْظُرُونَ إِلَّا أَنْ يَأْتِيَهُمُ اللَّهُ فِي ظُلَلٍ مِنَ الْغَمَامِ وَالْمَلَائِكَةُ {210}

“Hawangojei ila Mwenyezi Mungu awafikie katika vivuli vya mawingu na Malaika.” (al-Baqarah; 2: 210)

Imam (a.s.) akasema:

“Hii haipaswi kufasiriwa kwa maana ya neno kwa neno. Kile kitu ambacho kitatoka humo kwenye mawingu meusi, kitakuwa ni Amri Yake, Adhabu Yake. Ni istiari ambamo ile nomino pinzani imeachwa katika huo uundaji milikishi (genitive construction).”

Mtu anajaribu kufikiri kwamba wanazuoni kutoka kwenye madhehebu ya upande wa pili, baada ya kuwa wamejitenga wao wenyewe kutoka kwa Ahul-Bayt (a.s.) wameangukia kuwa mateka wa utomaji maneno wa Kiyahudi na Kikristo, pamoja na kutojali kabisa kile ambacho Qur’ani Tukufu yenyewe inachofundisha.

Katika Suratun-Nisa, Ayah ya 108, Allah swt. anasema:

يَسْتَخْفُونَ مِنَ النَّاسِ وَلَا يَسْتَخْفُونَ مِنَ اللَّهِ وَهُوَ مَعَهُمْ إِذْ يُبَيِّتُونَ مَا لَا يَرْضَىٰ مِنَ الْقَوْلِ ۚ وَكَانَ اللَّهُ بِمَا

يَعْمَلُونَ مُحِيطًا {108}

Wanajificha kwa watu wala hawamstahi Mwenyezi Mungu, naye yu pamoja nao pale wanaposhauriana usiku kwa maneno asiyoyapenda na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua vyema yale wayatendayo.” (An-Nisaa; 4:108)

Kuna Ayah nyingine iliyopo katika Sural-Mujadilah, Ayah ya 7, ambayo inasema:

“Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu anajua vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini? Hawashauriani kwa siri watatu ila yeye ni wa nne wao, wala watano ila yeye ni wa sita wao, wala wachache kuliko hao wala zaidi ila yeye huwa pamoja nao popote walipo. Kisha Siku ya Kiyama atawaambia yale waliyoyatenda, hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.”

Hivyo liko wapi pazia hapo? Liko wapi wazo la kujitenga na viumbe vyake? Ilikuwa ni dhana hii, ambamo mwisho wake uliwafanya wao kuamini kwamba wale waumini watamuona Mwenyezi Mungu waziwazi hiyo Siku ya Kiyama.