read

Sura Ya Nne: “Mikono” Ya Mwenyezi Mungu

“Mikono” Ya Mwenyezi Mungu Kama Ilivyosimuliwa Na Madhehebu Ya Makhalifa.

Wanazuoni wa madhehebu hiyo hapo juu wamesimulia ndani ya vitabu vyao kutoka kwa Abu Huraira ambaye amesimulia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kama ifuatavyo:

“Adamu na Musa walikuwa na mazungumzo yafuatayo: Musa alisema: ‘Ewe Adamu! Mwenyezi Mungu alikuumba kwa mikono Yake Mwenyewe… Lakini uliwateremsha wanadamu kutoka kwenye bustani kwa sababu ya dhambi yako.’

Adamu akajibu: ‘Ewe Musa, Mwenyezi Mungu kwa hakika amekutukuza wewe, na akaandika Taurati kwa ajili yako kwa mikono Yake Mwenyewe.’”

Katika hadithi nyingine iliyosimuliwa kutoka kwa Abu Huraira, tunakuta:

“Mwenyezi Mungu huwa anashuka mpaka kwenye mbingu ya kwanza, na ananyoosha mikono Yake miwili na anasema…”

Vidole”

Hakuna utajo wa neno “vidole” ndani ya Qur’ani Tukufu kuhusiana na Mwenyezi Mungu; kwa hiyo, Ibn Khuzaimah alilazimika kutegemea juu ya hadithi pekee ili kuthibitisha kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa na vidole. Hadithi zenyewe hizo zinaweza kupatikana katika kitabu cha Tawhiid cha Ibn Khuzaimah, na ndani ya Sahih Bukhari, Sahih Muslim, Sunan ya Tirmidhi, Sunan ibn Majah, Tafsir Tabari, Ibn Kathiir na Suyuti pia. Hadithi moja kama hizo ni: Abdullah anasimulia kwamba kuhani mmoja (rabbi) alikuja kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na akasema:
“Oh, Muhammad! Sisi tunasoma katika Taurati kwamba Allah anaiweka pepo katika kidole kimoja, miti yake katika kimoja, maji kwenye kingine kimoja, dunia na viumbe wote kwenye kimoja! Na halafu anasema: ‘Mimi ndiye Mfalme!’

Mtukufu Mtume akatoa kicheko cha tabasamu kuthibitisha kile yule rabbi alichokisema, na katika kumuunga mkono maneno yake, akasoma Ayah ifuatayo:

وَمَا قَدَرُوا اللَّهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ {67}

“Na hawakumheshimu Mwenyezi Mungu heshima ipasayo, na siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kulia, …” (Az-Zumar; 39: 67)

Hadithi hizi kutoka kwa Abu Huraira na wengineo ziliwashawishi wanazuoni kutoka ile madhehebu kinyume na ya Ahlul-Bayt (a.s.) kutwaa ile maana halisi ya neno Yadullah popote linapotokea ndani ya Qur’ani Tukufu. Ibn Khuzaimah anao mlango mzima katika kitabu chake juu ya Tawhiid, ambao unasema:

“Uthibitisho kwamba Mwenyezi Mungu Muumba, Aliye Mkuu, anao mkono; kwa kweli Allah Aliye Mkuu anayo mikono miwili, kama tulivyojifunza kutoka kwenye Ayah madhubuti za Qur’ani Tukufu…”1

Halafu anaendelea kunukuu Ayah zifuatazo kwa ithibati ya madai yake:

وَقَالَتِ الْيَهُودُ يَدُ اللَّهِ مَغْلُولَةٌ ۚ غُلَّتْ أَيْدِيهِمْ وَلُعِنُوا بِمَا قَالُوا ۘ بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ يُنْفِقُ كَيْفَ يَشَاءُ ۚ {64}

“Na Wayahudi walisema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba. Mikono yao ndio iliyofumba, na wamelaaniwa kwa sababuya yale waliyoyasema. Lakini mikono ya Mwenyezi Mungu iwazi, hutoa apen- davyo …” (Al-Maida; 5: 64)

فَسُبْحَانَ الَّذِي بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ {83}

“Basi ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo ufalme wa kila kitu, na kwake mtarejea.” (Yaasin; 36: 83)

قُلِ اللَّهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِي الْمُلْكَ مَنْ تَشَاءُ وَتَنْزِعُ الْمُلْكَ مِمَّنْ تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَنْ تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَنْ تَشَاءُ ۖ بِيَدِكَ الْخَيْرُ ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ {26}

“Sema: Ewe Mola Mwenye kumiliki ufalme, humpa ufalme umtakaye, na humnyang’anya ufalme umtakaye. Na humtukuza yule umtakaye na kumdhalilisha umtakaye. Kheri yote imo mikononi mwako. Hakika wewe ni Mweza juu ya kila kitu.” (Aali Imraan; 3: 26)

Hebu sasa tuelezee ni nini Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) walichokisema.

Majibu Kutoka Kwa Ahlul-Bayt (A.S.)

(a) Muhammad bin Muslim alimuuliza Imam Muhammad al-Baqir (a.s.) kuhusu Ayah ifuatayo:2

قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا مَنَعَكَ أَنْ تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ ۖ {75}

“Akasema: Ewe Iblis, ni nini kimekuzuia kumtii yule niliyemuumba kwa mikono yangu?... (Swaad; 38: 75)

Imam Baqir (a.s.) akajibu:

“Yad (mkono) katika lugha ya Kiarabu linatumika kumaanisha uwezo na ukarimu.”

Halafu akaendelea na kutoa mifano zaidi kutoka kwenye Qur’ani Tukufu na fasihi ya Kiarabu ili kuonyesha ile tamathali ya usemi. Hapa tunanukuu baadhi ya mifano ambayo aliitoa:

وَاذْكُرْ عَبْدَنَا دَاوُودَ ذَا الْأَيْدِ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ {17}

“…Na umkumbuke mja Wetu Daudi, mwenye mikono …” (Swaad; 38:17)

Imam (a.s.) akaeleza kwamba katika Ayah hii, kule kutajwa kwa mikono ni dhahiri kabisa kwamba ni kwa kiistiari. Anachotaka kukifikisha Mwenyezi Mungu ni kwamba Yeye alimbariki Daudi na nguvu. Kisha yeye akaorodhesha mifano ya nguvu ambazo kwazo Daudi alibarikiwa kwazo:

وَالسَّمَاءَ بَنَيْنَاهَا بِأَيْدٍ وَإِنَّا لَمُوسِعُونَ {47}

“Na mbingu tumeiumba kwa mikono na hakika sisi ndio wapanuao” (Dhariyaat; 51: 47)

Imam (a.s.) akasema: “Hapa mikono inamaanisha uwezo.”

وَأَيَّدَهُمْ بِرُوحٍ مِنْهُ ۖ {22}

“… Na akawapa mkono kwa roho itokayo Kwake Mwenyewe…” (Al- Mujadilah; 58: 22)

Katika Ayah hii, “mkono” unaashiria kutia nguvu au uwezo. Akinukuu kutoka kwenye fasihi ya Kiarabu, Imam (a.s.) alisema: “Wanasema: Fulani wa fulani ana mikono mingi sana kwangu mimi.” Hii ina maana kwamba nina deni la shukurani kwake kwa sababu za wajibu.

Halafu tena, Waarabu wanao usemi wao: “Ana mkono mweupe juu yangu mimi!”

Hii ina maana kwamba amenifanyia hisani. Mikono katika muktadha huu unamaanisha ukarimu.

(b) Muhammad bin Ubaidah aliirejea Ayah hiyo hiyo ya Suratul-Swaad, kwa Imam ar-Ridha (a.s.). Majibu yalikuwa:

“Kwa Mikono Yangu” katika Ayah hii imekusudiwa kumaanisha “kwa nguvu na uwezo Wangu.”3

(c) Suleiman bin Marhan anasema kwamba yeye alimuuliza Imam Ja’far Sadiq (a.s.) kuhusu maana ya ile Ayah ambamo Mwenyezi Mungu anatamka hivi:

وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ {67}

“…Na ardhi yote hiyo Siku ya Kiyama itakuwa mkononi mwake…” (Az-Zumar; 39: 67)

Imam (a.s.) akasema: “Ina maana ya udhibiti kamili na mamlaka yasiokuwa na mshirika yoyote.”

Muhammad bin Ubaidah halafu akaendelea kuuliza kuhusu ile sehemu ya Ayah iliyokuwa imebakia:
“…Na mbingu zitakunjwa kwenye mkono wa kulia…”

Imam (a.s.) akaelezea kama ifuatavyo:

“Mwenyezi Mungu amelitumia neno Yamiin ambalo linaashiria ‘mkono,’ na mkono una maana ya Ukarimu Wake na Uwezo. Hizo mbingu zitakunjwa kwa uwezo Wake.”

Neno “ukufi” au “kulia Kwake” halimaanishi ngumi au mkono wa kulia.

Hayaashirii kwenye kiungo chochote kama inavyodhaniwa na madhehe- buya Makhalifa. Kudhania viungo na kuwepo kimwili kwa Mwenyezi Mungu ni kujiingiza kwenye shirki – na hiyo ndiyo iliyokuwa sababu kwa nini Imam Ja’far Sadiq (a.s.) baada ya kujibu swali hilo, alisisitiza juu ya kuimalizia Ayah hiyo. Yeye alisema:

سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ {67}

Yeye ameepukana na upungufu na yu juu kabisa kuliko yale wanayomshirikisha nayo.”4
(az-Zumar; 39: 67)

Uchunguzi

Ahlul-Bayt (A.S.) wametegemeza hoja yao juu ya maana halisi ya Tawhiid, wakati huo huo, wakitegemea sana katika matumizi ya kawaida ya neno hilo miongoni mwa Waarabu na katika fasihi yao. Raghib Isfahani ndani ya kitabu chake mashuhuri, Mufradatul Qur’an anasema:

Yad lina maana ya ‘mkono,’ ambao ni kiungo. Lakini lina maana nyingine vile vile kama: udhibiti, uwezo na busara.”

Wanazuoni wa Misri wameorodhesha maana tisa tofauti juu ya neno Yad, mbali na ile ya mkono. Kwa mfano, Ayah ifuatayo:

فَسُبْحَانَ الَّذِي بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ {83}

“Basi ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo ufalme wa kila kitu… (Yaasin; 36: 83)

inatafsiriwa kama: “Ambaye katika udhibiti wake kamili ndimo ulimo umiliki juu ya vitu vyote.”

Jambo la kushangaza kabisa ni kwamba wanazuoni hawa ambao wamehusisha mikono na viungo vingine kwa Mwenyezi Mungu wakati wakifasiri Ayah zinazohusika, walitwaa msimamo mwingine pale neno hilo lilipotumika kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Katika Ayah ifuatayo, iliyozungumzwa kwa Mtume (s.a.w.w.), watarjuma na wafasiri wote wanakubaliana kwamba lina maana:

وَلَا تَجْعَلْ يَدَكَ مَغْلُولَةً إِلَىٰ عُنُقِكَ {29}

Wala usiufanye mkono wako (kama) uliofungwa shingoni mwako (kwa ubakhili)..”
(Bani Israil; 17: 29)

Hakuna hata mmoja miongoni mwao aliyelichukulia hilo neno ‘mkono’ kwa maana halisi. Lakini ilipokuja kwenye neno hilo hilo kutumiwa juu ya Mwenyezi Mungu, wao walikimbilia kwenye maana yake halisi, wakipuuza kabisa ile ya kiistiari.

Hii inajulisha ile athari kubwa iliyotawaliwa na dhana za Kiyahudi na Kikristo, ambazo ziliimarishwa bila majuto na masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) wasiokuwa na maadili. Habari hizi haziishii hapa. Kuna maelezo ya kuvutia yanayofuata bado.

Mlango Wa Tano: Nyayo Za Mwenyezi Mungu

“Nyayo Za Mwenyezi Mungu” Na “Muundi Na Mguu” Wake!!”

Katika kitabu cha Tawhiid cha Ibn Khuzaimah, hadithi mbalimbali zinazohusiana na ‘mguu’ na ‘nyayo’ za Mwenyezi Mungu zimetajwa humo, aghalabu zikisimuliwa na Abu Huraira. Na zinaweza kupatikana vilevile katika Sahih Bukhari, Sahih Muslim, Sunan Tirmidhi, Musnad Ahmad Hanbal na Tafsiir za akina Tabari, Ibn Kathiir na Suyuti.
Abu Huraira anasimulia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.):

“Pepo na Jahannam zilikuwa na mzozo, kila kimoja kikijaribu kuonyesha ule ubora wake juu ya kingine.” Basi Jahannam ikazungumza: “Mimi nimependelewa kwa kuwepo kwa wale watu wenye kiburi na nguvu ndani yangu.” Pepo ikajibu: “Mimi sijui ni kwa nini hakuna mtu isipokuwa wale dhaifu na wanyenyekevu ndio walioingizwa ndani yangu!”

Hivyo Mwenyezi Mungu akaiambia Pepo:

“Wewe ndiye Msamaha Wangu, na kupitia kwako ninatoa msamaha kwa yeyote kati ya waja Wangu.”

Halafu Yeye akazungumza na Jahannam:

“Wewe ndio ghadhabu Yangu, na kupitia kwako wewe ninamuadhibu yeyote nitakaye kumuadhibu. Kila mmoja wenu atajaa.”

“Bali Jahannam haitajaa, hivyo Mwenyezi Mungu ataingiza mguu Wake ndani yake.”

Kisha Jahannam itagutia:

“Tosha! Inatosha!”

Hivyo kwa njia hii Jahannam itajaa, kwani Mwenyezi Mungu hamdhulumu yoyote yule. Na kuhusu hiyo Pepo, Yeye ataumba upya kwa maalum kabisa viumbe wa kuifanya ijae.

Huo “Muundi” Au “Mguu”

Ndani ya Sahih Bukhari, Mustadrak ya Hakim, Tafsiir za Tabari, Ibn Kathiir na Suyuti, tunazikuta hadithi zinazoshughulika na ‘muundi’ wa Mwenyezi Mungu. Katika Ayah ifuatayo:

يَوْمَ يُكْشَفُ عَنْ سَاقٍ وَيُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ فَلَا يَسْتَطِيعُونَ {42}

“Siku ambayo ‘Shin’ (muundi) zitakapowekwa wazi (itakaposhuka adhabu), na wataitwa kusujudu lakini hawataweza.” (Al-Qalam; 68:42)

Abu Saeed, sahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) anasema yeye alimsikia Mtume akisema:

“Mola Wetu atakujaweka wazi muundi Wake, kisha kila muumini mwanaume na mwanamke atapiga magoti mbele Yake, isipokuwa wale ambao walimuabudu katika ardhi ili kujionyesha au kuwapendezesha watu wengine – wao hawataweza kuinama, na watabakia wima.”

Hadithi hii imepewa utendewaji wa kina na Bukhari katika ule Mlango juu ya Tawhiid; tunanukuu hapa baadhi ya dondoo:

“Itakuja kutangazwa hiyo Siku ya Kiyama: ‘Kila mmoja wenu asimame mstari nyuma ya miungu mliyokuwa mkiiabudia. Hivyo watu watakimbilia kufanya vikundi nyuma ya miungu yao, isipokuwa wale waliomuabudu Mwenyezi Mungu ndio watakaobakia imara juu ya uwanja wakimsubiri Yeye.’

“Halafu Mwenyezi Mungu atatokea na atawauliza: ‘Je, mlikuwa na dalili au ishara yoyote yenye kutambulisha kati ya Mwenyezi Mungu na nyie wenyewe ambayo itawawezesha ninyi kumtambua Yeye?’

“Wao watasema: ‘Ndiyo! Ule Muundi.’

Kisha Mwenyezi Mungu ataudhihirisha muundi Wake, ambao baada ya kuuona huo wale waumini watasujudu na watamfuata hadi Peponi.”

Maswali mengi ya kushangaza yanachipuka kwenye akili zetu baada ya kusoma hadithi hiyo hapo juu:

a) Ni nini asili ya hii ‘dalili’ au ‘ishara’ ya utambuzi inayowakilishwa na hii inayodaiwa kuwa muundi au mguu wa Mwenyezi Mungu?

b) Ni lini ambapo wanazuoni wa madhehebu ya Makhalifa walipouona huo muundi kwa mara ya kwanza, kiasi kwamba wao wanategemea kuja kuutambua hiyo Siku ya Kiyama kama dalili?

c) Na kama waliuona hapa duniani, ulikuwaje, unafananaje?

d) Ulikuwa wa ukubwa gani?

Maelezo Kutoka Kwenye Madhehebu Ya Ahlul-Bayt (A.S.)

Hebu natuchukue Ayah ifuatayo:

َوْمَ يُكْشَفُ عَنْ سَاقٍ وَيُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ فَلَا يَسْتَطِيعُونَ {42}

“Siku hiyo ambayo muundi utakapowekwa wazi (itakaposhuka adhabu), na wataitwa kusujudu lakini hawataweza.” (Al-Qalam; 68:42)

Ubaidah ibn Zararah anasema:

“Nilimuuliza Imam Ja’far as-Sadiq (a.s.) kuhusu Ayah hii. Yeye mara moja akaweka mkono wake juu ya kifundo cha mguu, akiiondoa ile nguo juu yake, na akaweka mkono wake juu ya kichwa chake akisema: ‘Sifa zimwendee Allah Ambaye ni Mkuu aliye Juu.’”

Sheikh Saduuq anasema kwamba madhumuni ya kufanya hivyo ilikuwa ni kujulisha kwamba Mwenyezi Mungu, Aliye Mtukufu, ni zaidi na yu mbali na kuwa mwenye mguu au muundi.

Sahaba mwingine wa Imam (A.S.) aliyeitwa Muhammad ibn Ali Halabi aliuliza kuhusu uwekwaji wazi wa huo muundi. Safari hii Imam alitoa jibu lenye maelezo mafupi. Alisema:

“Ametukuka yule Mwenye Uwezo, (Mwenyezi Mungu)”

Halafu aliisoma Ayah hiyo nzima, pamoja na ile Ayah inayofuatia mara tu:

يَوْمَ يُكْشَفُ عَنْ سَاقٍ وَيُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ فَلَا يَسْتَطِيعُونَ {42}

خَاشِعَةً أَبْصَارُهُمْ تَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ ۖ وَقَدْ كَانُوا يُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ وَهُمْ سَالِمُونَ {43}

“…na wataitwa kusujudu lakini hawataweza. Macho yao yatainamishwa chini, unyonge utawafunika, na hakika walikuwa wakiitwa kusujudu walipokuwa salama.” (Al-Qalam; 68: 42-43)

Imam (a.s.) akasema:

“Kifungu hiki cha maneno ni cha kiistiari kilichotumika kwa nyakati ngumu sana na zenye mitihani. Kinaelezea jinsi watu fulani katika Siku ya Kiyama watakavyokuwa wamefunikizwa na aibu na fedheha, wakiwa hawana cha kusingizia. Ayah hizi, wakati zinaposomwa kwa pamoja, zinaielezea ile istiari.”

Sheikh Saduuq ndani ya kitabu chake juu ya Tawhiid anafafanua zaidi:

“Pale Imam (a.s.) aliposema: ‘Ametukuka yule Mwenye Uwezo (Mwenyezi Mungu), na kisha akaondoa ile nguo iliyofunika muundi wake, iliashiria kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa mbali na kuwa na kiungo chochote! Maneno ‘kuacha muundi wazi’ yasichukuliwe kwa maana yake halisi.”

“Kuacha Muundi Wazi” Kama Ilivyotumika Kwenye Fasihi Ya Kiarabu.

Abdullah ibn Abbas, yule binamu yake Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema:
“Wakati wowote unapokuwa huwezi kuielewa Qur’ani, tafuta ufafanuzi kutoka kwenye fasihi ya Kiarabu. Humo katika matumizi yake, unaweza ukaipata maana yenyewe. Je, hukumsikia yule mshairi wa Kiarabu aliyesema: Qamatil Harbu Bina Ala Saqin – ‘Vita vimeanza pamoja na makali yake na matatizo…’”

Hivyo ‘kuachwa wazi kwa muundi’ katika Ayah hii kumeelezea hofu kubwa, aibu na fedheha ambayo itajiri katika siku hiyo.5

Raghib Isfahani katika kitabu chake maarufu, Mufradat al-Qur’an ametoa maana hiyo hiyo kwenye Ayah hii, kama alivyoieleza Ibn Abbas. Vivyo hivyo, wanazuoni wa Ki-Misri wameiunga mkono ile fasiri ndani ya Mu’jam Alfadh al-Qur’an al-Karim.

Ni dhahiri kabisa, ile tamathali ilikuwa ikifahamika vema miongoni mwa Waarabu na wanazuoni wao kwa karne kumi na nne zilizopita. Cha kuhuzunisha sana, Madhehebu ya Makhalifa imechagua kukubaliana na hadithi za Abu Huraira na wale wa aina yake, wanaohusisha viungo na kano kwa Mwenyezi Mungu.

Kitenzi kilichotumika ndani ya Ayah hii ni cha kauli ya kutendwa; ambayo ina maana:

“Itakuja kuachwa wazi…”

Bado tunawakuta wanazuoni wao wakikitwaa kitenzi hicho katika kauli tendi, hivyo kupata tafsiri hii:

“Mwenyezi Mungu atakuja kuacha muundi Wake wazi.”

Kwa kuhitimisha, tunasema:

1. Madhehebu hii, ambayo ilijitenga na Ahlul-Bayt (a.s.) imeitafsiri vibaya Qur’ani Tukufu.

2. Wamehusisha hadithi bandia kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

3. Wameanzisha uhusishaji wa viungo kwa Mwenyezi Mungu miongoni mwa Waislamu.

Tunapaswa kuwashukuru Ahlul-Bayt (a.s.) daima ambao wamejaribu, mbali na tofauti zote, kuhifadha usafi wa Uislamu, na pia kuhifadhi maana halisi ya Qur’ani Tukufu na Hadith.

Sifa zote zimwendee Mwenyezi Mungu! Tunajua sasa kwamba Mwenyezi Mungu hana umbile, wala mwili. Yeye hana viungo, hahitaji chochote kati ya hivyo. Kwani kama angekuwa na mwili, angepaswa kuwa na makazi! Hebu sasa tuchunguze shimo la ziada ambamo madhehebu ya Makhalifa imeangukia.

  • 1. Tawhiid, cha Ibn Khuzaimah - uk. 53
  • 2. Tawhiid, cha Saduuq - uk.153
  • 3. Tawhiid, cha as-Saduuq, uk. 153-154
  • 4. Tawhiid, cha Saduuq - uk. 160-161.
  • 5. Tafsiir ya Suyuti - Juz. 6, uk. 254