read

Sura Ya Pili: “Uso” Wa Mwenyezi Mungu

1. “Uso” Wa Mwenyezi Mungu Kama Unavyoeleweka Kwa Madhehebu Ya Makhalifa:

Ibn Khuzaimah katika kitabu chake kiitwacho Tawhiid anaandika katika ukurasa wake wa kumi. Mlango unaothibitisha uso wa Mwenyezi Mungu, ambao Yeye Mwenyewe ameueleza kama wenye kujaa utukufu na heshima katika Ayah ifuatayo:

وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ {27}

“Na itabaki dhati ya Mola Wako, Mwenye utukufu na Heshima.” (Ar- Rahmaan; 55: 27)

Na Amethibitisha vilevile kwamba Uso Wake hautatoweka kamwe:

ۚ كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ ۚ لَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ {88}

“…….. Kila kitu kitaangamia isipokuwa Uso Wake, hukumu iko Kwake, na kwake Yeye mtarejeshwa.” (Al-Qasas; 28: 88)

Baada ya hapo, Ibn Khuzaimah anatafuta uhakikisho mwingine zaidi kuto- ka kwenye Ayah nyingine za Qur’ani Tukufu, na kisha anasema:

“Kwa hiyo Mwenyezi Mungu amethibitisha kabisa kwamba Yeye anao uso, ameuelezea kama ni Wenye Utukufu na Heshima, na amehukumu kwamba uso huo utadumu milele, bila kutoweka kamwe……”

Katika maelezo yake ya kumalizia, anaongezea kusema:

“Kila kile ambacho Mwenyezi Mungu amejithibitishia yeye Mwenyewe, sisi pia tunakithibitisha. Lakini uso Wake sio kama uso wowote wa kiumbe chochote.”

Katika ukurasa wa kumi na moja wa kitabu hicho hicho, Ibn Khuzaimah anasimulia hadithi 14 kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ambamo neno “uso” limetajwa, na anaegemeza madai yake juu ya hadithi hizo. Kwa mfano, pale Mtume anapoomba du’a kwa kusema:

“Ninaomba hifadhi kwa Uso Wako wenye Rehma.”

Ibn Khuzaimah anaona kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alilitaja neno uso kwa maana yake halisi. Kwa maneno mengine, anasisitiza kwamba “uso” ni sehemu ya mwili wa Mwenyezi Mungu, sawa sawa na ule wa mwanadamu au mnyama mwingine.

Sasa hebu tuangalie kile ambacho Ahlul-Bayt (a.s.) walichokieleza katika hadithi zao:

2. “Uso” – Kama Ulivyoelezewa Na Ahlul-Bayt (A.S.)

Kama dibaji, hebu natushughulike na hadithi kutoka kwa Amirul- Mu’minin, Ali bin Abi Talib (a.s.) ambamo aliweka kanuni kwa ajili ya uelewa wa Ayah za Qur’ani Tukufu, hususan zile zinazohusika na sifa za ki-mungu.

Mtu mmoja alipeleka swali lake kwa Ali bin Abi Talib (a.s.), akinukuu baadhi ya Ayah kutoka kwenye Qur’ani Tukufu, kutoa vipingamizi vyake. Miongoni mwa hizo tunachagua hizi mbili zifuatazo:

Maana hasa ya maneno yenyewe ya Ayah hizi mbili ni:

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا {22}

“(Na katika hiyo Siku ya Kiyama) Na akaja Mola Wako na Malaika safu kwa safu …”
(Al-Fajr; 89: 22)

هَلْ يَنْظُرُونَ إِلَّا أَنْ تَأْتِيَهُمُ الْمَلَائِكَةُ أَوْ يَأْتِيَ رَبُّكَ أَوْ يَأْتِيَ بَعْضُ آيَاتِ رَبِّكَ {158}

“Hawangoji ila wawafikie Malaika au Mola Wako afike, au zifike baadhi ya dalili za Mola Wako ………” (Al-An’aam; 6: 158)

Swali lililoletwa ni kama Mwenyezi Mungu Mwenyewe atakuja kutokeza hiyo Siku ya Kiyama, kwa dhahiri kama ilivyowasilishwa na Ayah hizo.
Imam Ali (a.s.) alielezea hivi:

“Chochote kile ambacho Mwenyezi Mungu, Aliye Mkuu, amekidhihirisha ndani ya Ayah, ni kweli kabisa; isipokuwa kwamba kuja kwake sio sawa na kuja kwa viumbe Vyake. Nimekushauri hapo mapema kwamba sehemu fulani za Qur’ani Tukufu lazima zisitafsiriwe kwa maana halisi ya maneno; badala yake unapaswa kuelewa ile maana ya ki- istiari. Neno Allah sio kama neno la kibinadamu, na tendo Lake sio kama tendo la kibinadamu. Ili kuiweka hoja yangu ieleweke vizuri, nitakupa mifano kutoka kwenye Qur’ani Tukufu, ili Inshallah, uelewaji wako wa Qur’ani utakuwa wa hakika na wa sawasawa. Qur’ani inamsimulia Nabii Ibrahim akisema:

وَقَالَ إِنِّي ذَاهِبٌ إِلَىٰ رَبِّي سَيَهْدِينِ {99}

“Nakwenda kwa Mola Wangu, yeye ndiye atakayeniongoza.” (As- Saffat; 37: 99)

Hapa, “kwenda kwa Mola” hakuna maana ya kutembea hadi Kwake kwa msaada wa miguu. Ina maana ya kurejea Kwake, kwa uimara na ukweli, kupitia ibada, na kutafuta ukaribu Naye. Je, unaweza kuona tofauti baina ya maana yake halisi na ile maana yenyewe iliyowasilishwa na istiari? Halafu tena, maana halisi ya Ayah zifuatazo inaweza kuwa:

وَأَنْزَلَ لَكُمْ مِنَ الْأَنْعَامِ ثَمَانِيَةَ أَزْوَاجٍ ۚ {6}

“…na akakushushieni wanyama, (kwa jozi) wanane madume na majike …” (Az-Zumar; 39: 6)

وَأَنْزَلْنَا الْحَدِيدَ فِيهِ بَأْسٌ شَدِيدٌ {25}

“….Na tumekishusha chuma chenye nguvu nyingi …” (Al-Hadiid; 57: 25)

Sasa kama ungekuwa utegemee kwenye maana halisi, ungeona kwamba zile jozi nane za ng’ombe na kile chuma “vilishushwa” kutoka juu mbinguni. Lakini bila shaka haikumaanishwa hivyo. Maneno hayo hapa yanamaanisha “tuliumba,” au “Aliumba.”1

Ali ibn Abi Talib (a.s.) ametufundisha kanuni mbili muhimu juu ya kuele- wa Sifa na kazi za Mungu. Kwanza, kazi na matendo ya Mwenyezi Mungu haviwezi kulinganishwa na kazi na matendo yetu. Wakati Mwenyezi Mungu ndani ya Qur’ani Tukufu anaposema:

قَدْ سَمِعَ اللَّهُ {1}

“Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia…” (Al-Mujadilah; 58:1),

Haifananishwa na kusikia kwa mwanadamu, mnyama au kiumbe chochote. Sisi tunasikia kwa msaada wa masikio yetu. Kusikia kwa Mwenyezi Mungu hakuashirii kitu kama hicho.

Mwenyezi Mungu anasema:

قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا مَنَعَكَ أَنْ تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ {75}

“Akasema: Ewe Iblis, ni nini kimekuzuia kumtii yule niliyemuumba kwa mikono yangu?
(As-Swad; 38: 75)

Mwanadamu anaweza akasema vile vile kwamba ameumba kitu kwa mikono yake. Lakini yote yana maana tofauti. Mwenyezi Mungu hana viungo, wala hahitaji mikono.

Mwenyezi Mungu alimdhihirishia Nabii Musa (a.s.) hivi:

قَالَ لَا تَخَافَا ۖ إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَىٰ {46}

“Msiogope, bila shaka mimi niko pamoja nanyi, ninasikia na ninaona.” (At-Twaha; 20: 46)

Kuwa pamoja na mtu kuna maana tofauti wakati inapotumika kwetu sisi. Wakati Mwenyezi Mungu yuko “pamoja” na mtu, haiashirii kuwa pamoja kimwili au kwa ukaribu.

Pili, Amirul Mu’minin, Ali bin Abu Talib (a.s.) alisema kwamba ilikuwa ni lazima kuyaelewa matumizi halisi na yale ya kiistiari vilevile ya maneno ndani ya Qur’ani Tukufu, kabla mtu hajaanza kutafsiri au kusherehesha. Alitoa mifano miwili kutoka ndani ya Qur’ani ili kuielezea hoja yake.

Kwa kweli, tunapokaa kusoma kazi ya sanaa ya fasihi au maandishi, katika lugha yoyote ile iwayo, tunatakiwa kuwa wenye kufahamu vizuri zile tamathali za semi, matumizi tofauti ya maneno na kadhalika. Kwa kutegemea kanuni hii iliyoenea pote, hebu sasa tuangalie jinsi madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) inavyoushughulikia huu mtajo “uso” wa Mwenyezi Mungu.

Abu Hamza alimuuliza Imam Muhammad Baqir (a.s.) kuhusu maana ya Ayah hii:-

“Kila kitu chenye uhai kitatoweka isipokuwa Uso Wake Mwenyewe.”

Imam alimjibu hivi:

“Hivi wao wanadhania kwamba Mwenyezi Mungu anao uso na kwamba kila mtu atakufa na kutoweka bali Uso Wake? Mwenyezi Mungu yuko mbali na kuwa mwenye uso! Maana halisi ya Ayah hii ni kwamba kila kitu kitatoweka isipokuwa dini ya Mwenyezi Mungu, mwelekeo na njia, ambayo inaongozea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.”

Katika hadithi nyingine kutoka kwa Imam Ja’far as-Sadiq (a.s.), Ayah hii imeelezewa zaidi:

“Kila kitu kitatoweka isipokuwa kule kutwaa njia iliyonyooka.”

Maelezo yote yanaelekeza kwenye jambo moja lile lile, njia iliyonyooka au dini ya Mwenyezi Mungu. Hivi ndiyo jinsi Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) inavyokitafsiri hiki kifungucha maneno “uso wa Mwenyezi Mungu.”

1. Wajh likimaanisha “ule mwanzo” au “sehemu ya mwanzoni” kama ilivyotumika katika Wajhun Nahar – yaani asubuhi.

2. Wajh likimaanisha “ukweli au dhati ya jambo” – kama wanavyosema katika Kiarabu, Asaba Wajhal Masa’lah – yaani Alikuja kwenye sehemu ya jambo ambayo ni ngumu kutatulika.

3. Wajh likimaanisha “mwelekeo, lengo,” kama: Ittajahat Tijaraj – yaani alilenga kufanya biashara.

Wanazuoni wa Kiarabu wa kisasa wamethibitisha maana hizi vilevile, kama wale waandishi wa Mu’jamu Alfaadhil Qur’an al-Karim, kilichochapishwa kutoka Misri mnamo mwaka 1390 A.H.

Kwa kuzingatia zile maana mbali mbali zilizoambatanishwa na neno Wajh madhehebu ya Makhalifa haikuwa na sababu yenye kueleweka kugandamana kwenye maana moja, ambayo iliyopendekeza kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa na viungo vya kimwili, kwa namna ile ile kama sisi wanadamu tulivyonavyo.

Ni wazi kabisa kwamba waliathiriwa na ule utomaji maneno yasiyokuwemo wa Kiyahudi na kwa hadithi kama hizo, ambazo zilihusishwa kwa masahaba kama vile Abu Huraira.

Katika mjadala huu mfupi, tunatambua kwamba madhehebu mbili zina maoni yanayoachana kabisa kuhusu Mwenyezi Mungu. Moja inaamini katika uhusishaji viungo kwa Mwenyezi Mungu (anthropormophism) ikimdhania Yeye kwamba ni kama sisi, au kama kiumbe kingine chochote kile, akiwa na viungo na kano. Na hii nyingine inaamini Nafsi ya juu sana na tukufu, isiyolinganishika kwa hali yoyote ile na maumbile.
Kuna Ayah ndani ya Qur’ani Tukufu, ambazo zinahitaji msaada wa kimungu kuweza kuzielewa, na kwamba msaada huo unakuja kupitia kwa Mtume (s.a.w.w.) au kwa Ahlul-Bayt wake halisi na watoharifu kabisa. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

هُوَ الَّذِي أَنْزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّهُ ۗ {7}

“…ndani yake zimo Ayah zilizo wazi wazi nazo ndizo msingi wa Kitabu, na nyingine ni zenye kufichikana. Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu, hufuata zile zilizofichikana katika hayo kwa ajili ya kutaka upotovu na kutaka kutafsiri watakavyo. Na hakuna ajuaye tafsiri yake ila Mwenyezi Mungu …” (Aali Imran; 3: 7)

Mwenyezi Mungu amemkabidhi Mtume Wake (s.a.w.w.) wajibu wa kuielezea maana yote ya Qur’ani Tukufu:

وَأَنْزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ َ {44}

“…Tumekuteremshia Qur’ani ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwa ajili yao …”
(An-Nahl; 16: 44)

Na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ameigawa elimu yake kwa Ali bin Abi Talib (a.s.) ambaye ameinakili na akaihifadhi kwa moyo kwa uaminifu kabisa. Baada ya kufariki kwa Mtukufu Mtume wetu (s.a.w.w.), Waislamu walirejea kwa Ali (a.s.) kila ambapo tatizo au ugumu ulijitokeza kuhusiana na kuielewa Qur’ani Tukufu; na wakati wote alitoa majibu ya kutosheleza. Elimu ambayo waliyonayo Ahlul-Bayt (a.s.) ni ya kimungu. Haitegemei kwa hali yoyote ile juu ya maoni ya mtu au tafsiri za wanazuoni ambao badala yake waliathiriwa na dhana zisizo za Kiislamu.

Mlango unaofuata utaweka tofauti hizi kwenye muonekano dhahiri hasa.

  • 1. Kitabu Tawhiid cha Saduuq, uk. 265