read

Sura Ya Saba: Makazi Ya Mwenyezi Mungu

Washirikishaji Viungo Kwa Mwenyezi Mungu Miongoni Mwa Waislamu:

Madhehebu hii, ingawa ni kongwe, ya siku nyingi, ina ngome juu ya Waislamu wenye imani halisi, hususan Wahabia. Ni muhimu kufanya uchuguzi mfupi wa imani zao na halafu tuzilinganishe na mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s.)

Kwa vile walihusisha sifa zote za mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu, wao hatimae walilazimika kubuni sehemu kwa ajili Yake. Na baadae, waliikuza dhana, ambayo ilipiga taswira ya mabadiliko kichwani,uhamaji na kubadili maskani kwa Mwenyezi Mungu.

(I)Abu Huraira Anasimulia Kutoka Kwa Mtukufu Mtume (S.A.W.W.) “

Katika sehemu ya usiku, au labda katika theluthi ya mwisho ya usiku, Mwenyezi Mungu anashuka hadi kwenye mbingu ya kwanza na anatangaza: ‘Kuna mtu yoyote atakayeniita ili niweze kujibu maombi yake, anayeniomba mimi ili niweze kumpa? Ni nani atamkopesha Yule Ambaye Anajitosheleza na Muadilifu?’”1

(II) Katika Hadithi Nyingine Kutoka Kwa Abu Huraira, Haruun Bin Said Ameongezea:

“Halafu Mwenyezi Mungu ananyoosha mikono Yake na anasema: ‘Ni nani atakayetanguliza mkopo kwa Yule Ambaye hana shida wala sio dhalimu.’”2

Bukhari amesimulia pia hadithi kama hizo kutoka kwa Abu Huraira ndani ya mlango wake juu ya Tawhiid, Da’awwat na Tahajjud. Tena hayuko peke yake. Ameungwa mkono na Ibn Majah, Tirmidhi na Abu Dawuud, ambao wote wamesimulia hadithi zilizokusudiwa kuthibitisha kwamba Mwenyezi Mungu anashuka kimwili kwenda chini na juu ya mbingu!

(III) Ibn Khuzaimah Anasimulia Kutoka Kwa Abu Huraira

“Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: ‘Malaika wanakusanyika wakati wa Swala ya Asubuhi na Jioni.

Wale wa usiku wanapanda na wale wa mchana wanabakia. Na halafu Mwenyezi Mungu anawauliza wale Malaika
wa usiku:

‘Waja Wangu walikuwa katika hali gani wakati mlipowaacha?’ Malaika hao wanasema: ‘Tuliwashukia juu yao wakati wakiwa wanaswali, na tuliwaacha wakiwa wanaswali.’”

Akitoa maoni juu ya hadithi hii, Ibn Khuzaimah anaongezea: “Hadithi hii kwa uwazi kabisa inajulisha kwamba Mwenyezi Mungu yuko juu mbinguni, na kwa hiyo, Malaika wanasafiri kutoka ardhini kwenda juu mpaka Kwake. Wale (jahmiyyah) wanaoamini Mwenyezi Mungu yuko mbinguni na katika ardhi vile vile ni waongo, kwa sababu kama ingekuwa ni hivyo, basi Malaika wangemwendea juu ya ardhi au mahali penginepo katika tabaka za chini za dunia. Mwenyezi Mungu awalaani Jahmiyyah daima milele!”

Darami anaiunga mkono dhana hiyo, akitegemeza hoja yake juu ya neno Nazala (kwa maana halisi ikiwa ni ‘kushusha chini’) lililotumika kwa ajili ya Qur’ani Tukufu – yeye anasema:

“Ayah kama hii zinaweza kupatikana ndani ya Qur’ani kati- ka sehemu nyingi. Zote kwa uwazi kabisa zikieleza kwam- ba Mwenyezi Mungu aliishusha Qur’ani Tukufu kutoka huko juu mbinguni. Ingekuwa ni kwa namna wanavyoamini kwamba Mwenyezi Mungu yupo kila mahali, juu ya ardhi na chini yake, basi Yeye angesema: “Tumeitoa,” au “Tumeinyanyua” Qur’ani. Ayah hizo ziko wazi katika kutangaza mahali pa Mwenyezi Mungu paliponyanyuka, na haihitaji kufasiri zaidi.”3

Darami anaelekea kuwa mwenye kujawa na imani yake kwamba Mwenyezi Mungu amezuilika kwenye sehemu Yake katika mbingu.

Akizungumzia safari ya mbinguni ya Mtukufu Mtume wetu (s.a.w.w.) – Mi’raj – yeye anasema:

“Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliwasimulia waumini matukio yake ya wakati wa kupaa kwake, jinsi alivyochukuliwa kutoka mbingu moja hadi nyingine, hadi ile ya mbali juu kabisa karibu na Sidratul Muntaha (kwa maana halisi ikiwa ni mti ulioko mbinguni). Ikiwa hicho wanachoamini wapin- zani ni kweli, kwamba Mwenyezi Mungu yupo kila mahali, basi kulikuwa na haja gani ya Buraq na huko kupaishwa? Kwa nini Mtume (s.a.w.w.) alipelekwa mbinguni, na kwa nani? Mnashikilia kwamba Mwenyezi Mungu yuko kila mahali, hata ndani ya nyumba ya Mtume (s.a.w.w.), bila hata ya pazia hapo katikati. Hivyo kwa nini kwenda huko juu?”

Madhehebu Ya Ahlul-Bayt (A.S.) Inaelezea:

Suala la kuhama na kubadili sehemu au kupanda juu na kushuka, kuhusiana na Mwenyezi Mungu ni jambo lisilopasika kabisa. Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) inasema kwamba tabia kama hizo zinahusika kwa yule aliyeumbwa na sio kwa Muumba, Ambaye ni Mwenye kudra.

Imam ar-Ridha (a.s.) aliliweka wazi kabisa wakati alipoulizwa kuhusu Ayah ifuatayo:

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا {22}

“Na akaja Mola Wako na Malaika safu kwa safu.” (Fajr; 89: 22)

Yeye (a.s.) akasema:

“Mwenyezi Mungu hawezi kuelezewa kwa namna ya mwendo, kuwasili, kuondoka, kuonekana na kutokuwepo. Yeye yuko zaidi na yu mbali na matukio kama hayo. Ayah inayohusika inaonyesha utaratibu wa Mwenyezi Mungu na amri Zake ambazo baadae zitadhihirishwa.”4

Seyyid Abdul Adhiim al-Hasani anasimulia kutoka kwa Ibrahim bin Abi Mahmud kwamba yeye alimuuliza Imam ar-Ridha (a.s.) kuhusu ile hadithi mashuhuri ambayo inazungumzia juu ya kushuka chini kwa Mwenyezi Mungu kila usiku hadi kwenye mbingu ya chini kabisa. Imam (a.s.) akasema:

“Ewe Mola Wangu walaani wale wanaoyahamisha yale maneno matakatifu kutoka mahali pao pale panapostahiki! Wallahi! Mtume (s.a.w.w.) hakusema kwa namna wao wanavyosimulia. Kile yeye alichokisema ni kwamba:

‘Mwenyezi Mungu Mtukufu huamuru Malaika kushuka chini hadi kwenye mbingu ya chini kabisa katika theluthi ya mwisho ya kila usiku, na kila Ijumaa usiku, katika theluthi yake ya kwanza.
Halafu Anamuamuru Malaika huyo kutangaza:

“Je kuna yoyote mwenye kuomba ili niweze kumpa? Yeyote mwenye kutubia ili niweze kumuwia radhi?
Yeyote anayeomba msamaha ili niweze kumsamehe? Ee, yule anayeomba wema, jitokeze, ee unayeomba
maovu uwache.’

“Malaika huyo anaendelea kutangaza mpaka asubuhi, na siku inapokucha, yeye huondoka kurejea kwenye miliki ya mbinguni. Hii ndio tafsiri sahihi iliyopokelewa kutoka kwa mababu zangu ambao walisimulia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.)’”5

Kupaa Kwa Mtukufu Mtume (S.A.W.W.)

Yunus bin Abd ar-Rahman anasema kwamba yeye alimuuliza Imam Musa bin Ja’far al-Kadhim (a.s.):

“Kwa nini Mwenyezi Mungu alimnyanyua Mtume Wake Mtukufu (s.a.w.w.) hadi mbinguni, na kutoka hapo hadi kwenye kituo cha mbali, Sidratul Muntaha, na halafu kwenye mapazia ya nuru, wakati alipomhutubia na kuongea naye, ambapo Mwenyezi Mungu haelezewi kwa namna ya kuwa na makazi au mahali?”

Imam (a.s.) akamjibu:

“Kwa kweli, hakuna mahali au sehemu inayohusishwa kwa Mwenyezi Mungu, wala Yeye hatawaliwi na wakati! Yeye alimnnyanyua Mtume Wake (s.a.w.w.) kuwapa heshima Malaika na wale wanaoishi katika mbingu na kuwatukuza kwa kuwepo kwake miongoni mwao.

Pia kumuonyesha yeye maajabu ya uumbaji Wake mkuu ili aje kuyaelezea kwa watu hapa duniani yale aliyoyaona. Haikuwa kabisa katika namna watu hawa wanavyohusisha sifa za kibinadamu kwa Mwenyezi Mungu! Sifa njema kwa Mwenyezi Mungu! Yeye yuko mbali kabisa na washirika wanaowahusisha Naye.”6

Katika hadithi iliyosimuliwa na Abu Basiir, Imam Ja’far Sadiq (a.s.) alitoa maelezo mapana na yenye kuondoa shaka akielezea msimamo wa Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) juu ya suala la Tawhiid:

“Mwenyezi Mungu Mtukufu, hawezi kuelezewa kwa namna ya kuwa na makazi au mahali. Hakuna mwendo, uzito, kubadili mahali, kuhamia au uhamisho unaovumishwa juu Yake, kwa sababu Yeye ndiye Muumba wa wakati, nafasi, mwendo, uzito. Yeye ameepukana, na yuko mbali sana na yale wanayoyasema kumhusu Yeye.7

Imam Zainul Abidiin (a.s.), katika jibu la kinaganaga kwa mwanawe Zaid, ametoa maana halisi ya Ayah fulani ambazo, kama zikitafsiriwa neno kwa neno, zitathibitisha kuwepo kwa kituo au makazi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Hebu tuzichunguze Ayah hizo:

عَلَىٰ أَثَرِي وَعَجِلْتُ إِلَيْكَ رَبِّ لِتَرْضَىٰ {84}

“…Na nimeharakia kwako, Mola Wangu, ili uweze kuridhia.” (Twaha; 20: 84)

فَفِرُّوا إِلَى اللَّهِ ۖ {50}

“Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu …” (Dhariyaat; 51: 50)

Imam (a.s.) akasema:

“Ayah hizi haziashirii mahali popote ambapo Musa alikwenda kukutana na Mola Wake, au ambako sisi tunaamriwa kukimbilia. Hizi ni tamathali za semi, ambazo zinamaan- isha kuziendea radhi za Mwenyezi Mungu na mwongozo Wake.”

Halafu akatoa mifano ifuatayo:

تَعْرُجُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ إِلَيْهِ فِي يَوْمٍ {4}

“Malaika na roho hupanda kwenda Kwake …” (Maa’rij; 70: 4)

إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ ۚ {10}

“…na Kwake hupanda maneno mazuri, Naye hukipandisha kitendo kizuri. (Faatir; 35: 10)

“Katika mifano yote miwili ya hapo juu, Mwenyezi Mungu anazungumzia vituo maalum vilivyonyanyuliwa katika milki ya kimbinguni. Kuvifikia vituo hivyo vilivyonyanyuliwa ni sawa na kujitahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu.”8

Ndani ya Qur’ani Tukufu, imo mifano mingi ya ujenzi milikishi ambamo ndani yake ile nomino inayopingwa imeachwa. Katika al-Burhan fi Uluum al-Qur’an, Zarkash anasema:

“Wanasema kwamba imo takriban mifano elfu moja ndani ya Qur’ani Tukufu ambamo ile nomino iliyoambatishwa imeachwa kutoka kwenye ujenzi milikishi. Na hili limekuwa limekubalika kama tamathali ya semi ya kawaida ya wanazuoni.”

Kama mfano, tutaichunguza Ayah ifuatayo:

وَاسْأَلِ الْقَرْيَةَ الَّتِي كُنَّا فِيهَا {82}

Na waulize (watu wa) mji tulimokuwemo...” (Yusuf; 12: 82)

Neno lililoachwa ni Ahl – likiwa na maana ya “watu.” Kile haswa anachotaka kukifikisha Mwenyezi Mungu ni: “Na waulize (watu) wa mji…”

Lakini uachwaji huu umedokezwa, na msomaji yoyote mwenye busara ataweza mara moja kuuelewa udokezwaji wake. Kwa kuegemea kwenye namna hii ya uzungumzaji, Imam ar-Ridha (a.s.) aliielezea Ayah ifuatayo: “Na Mola Wako atakuja …” Nomino iliyofichwa au neno lililodokezwa hapa ni Amr, ambalo linamaanisha “hukumu” au “agizo”, na kwa hiyo Ayah ina maana: “Na (amri ya)Mola wako itakuja…..”

Kwa uwazi kabisa Imam (a.s.) aliegemeza ufafanuzi wake juu ya Ayah zifuatazo kutoka kwenye Qur’ani Tukufu ambamo neno Amr limetajwa pamoja na “kuja kwa Mola.”

يَا إِبْرَاهِيمُ أَعْرِضْ عَنْ هَٰذَا ۖ إِنَّهُ قَدْ جَاءَ أَمْرُ رَبِّكَ ۖ وَإِنَّهُمْ آتِيهِمْ عَذَابٌ غَيْرُ مَرْدُودٍ {76}

“Ewe Ibrahim! Usiyafuate haya kwa sababu amri ya Mola wako imekwishafika na hakika hao itawafikia adhabu isiyorudishwa.” (Huud; 11: 76)

وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَٰكِنْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ ۖ فَمَا أَغْنَتْ عَنْهُمْ آلِهَتُهُمُ الَّتِي يَدْعُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ مِنْ شَيْءٍ لَمَّا جَاءَ أَمْرُ رَبِّكَ ۖ وَمَا زَادُوهُمْ غَيْرَ تَتْبِيبٍ {101}

“Nasi hatukuwadhulumu, bali wao wamejidhulumu wenyewe, na waungu wao waliokuwa wakiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawakuwafaa kitu ilipokuja amri ya Mola wako, na hawakuwazidishia ila maangamizo.” (Huud;11:101)

Katika Ayah zote hizo hapo juu, kile kitenzi, “ilipokuja” kimeandamana na uundaji milikishi “ Amru Rabbika, amri ya Mola Wako”. Hii inawasilisha ile maana iliyokusudiwa ya “kuja kwa Mola wako”, hapa duniani au katika Siku ya Hesabu.

Madhehebu ya Makhalifa ilipendekeza kigoda au kiti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na baadaye wakabuni pazia au kizuizi ambacho nyuma yake ndipo Yeye anapoishi!! Hili na mengine mengi yataunda maudhui ya mazungumzo yetu yanayofuata.

  • 1. Sahih Muslim - uk. 522.
  • 2. Sahih Muslim - uk. 522
  • 3. ar-Radd ala al-Jahmiyyah, cha Darami - uk. 24, 26 na 27..
  • 4. Tawhiid cha Saduuq - uk. 162.
  • 5. Tawhiid cha Saduuq - uk. 176.
  • 6. Tawhiid cha Saduuq - uk. 175
  • 7. Tawhiid, cha Saduuq - uk. 183-184
  • 8. Tawhiid, cha Saduuq