read

Sura Ya Sita: Kiti Cha Enzi Cha Mwenyezi Mungu

“Kiti Cha Enzi” (Arshi) Na “Kiti” (Kursiyu) Inavyofahamika Kwa Madhehebu Ya Makhalifa:

Bila shaka, kwa mujibu wa Madhehebu ya Makhalifa, Mwenyezi Mungu lazima awe ana makazi! Wakiwa wamemfikiria kuwa kama mwanadamu mwenye umbile, na viungo, basi wanapaswa kumpatia sehemu, ambayo itaupatia mwili huo nafasi ya kuishi. Hivyo, tunamkuta yule kiongozi wa ushirikishaji mwili kwa Mwenyezi Mungu, Muhammad ibn Uthman Darami (aliyefariki mnamo mwaka 280 Hijiria) akiandika katika kitabu chake, al-Radd ala al-Jahmiyyah, kwamba:

“Kwa hakika Mwenyezi Mungu anacho Kiti cha enzi kinachotambulika na kinachoelezeka juu ya mbingu ya saba, kinachobebwa na Malaika. Mwenyezi Mungu, kama ambavyo Yeye alivyojieleza Mwenyewe, hafanani na viumbe vyake.”

Halafu anaendelea katika mlango wa kumi na tatu wa kitabu hicho hicho, chini ya kichwa cha maneno:

“Kujiweka imara kwa Mola, Mtukufu, juu ya Arshi, kujinyanyua Kwake kwenye mbingu na kuwa Kwake tofauti na viumbe vyake.”

Vivyo hivyo, Ibn Khuzaimah anao mlango ndani ya kitabu chake cha Tawhiid uitwao:

“Kujiweka imara kwa Muumbaji wetu, aliye Mtukufu, Muweza, juu ya Kiti Chake, na kuwa juu yake na juu ya yote.”

Katika hoja ya kuvutia sana iliyotolewa na Darami, tunamkuta yeye kwa ushupavu sana akiwakanusha wale wanaoamini kwamba Mwenyezi Mungu yupo kila mahali. Yeye ananukuu hadithi kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.):

“Mbegu ya uzazi inabakia ndani ya tumbo la uzazi kwa muda wa usiku wa siku arobaini, na halafu malaika anayehusika na roho za watu anapanda nayo kwa Mola na kuuliza: ‘Ewe Mungu Wangu! Je, mja wako huyu amepangiwa kuwa mwanaume au mwanamke…?’”

Halafu Darami anasema:

“Kama ukweli ungekuwa kama unavyoamini, basi Mwenyezi Mungu angekuwa ndani ya tumbo pamoja na ile mbegu. Kama ni hivyo, kulikuwa na haja gani ya malaika kupaa pamoja na ile mbegu?”

Zaidi ya hayo, yeye anaongezea:

“Mwenyezi Mungu yupo na anaishi kwa kujitenga na viumbe Vyake. Kwa nini ajitafutie Mwenyewe makazi kwenye sehemu chafu, ndani ya matumbo ya wanadamu, ndege na wanyama? Kwa nini kila upenu na pembe iwe Naye ndani yake?”

Darami, Ibn Khuzaimah na wanazuoni wengine kutoka Madhehebu ya Makhalifa wanahakikisha imani zao kuhusu “Arshi” au “Kiti” halisi cha Mwenyezi Mungu kutoka kwenye Ayah nyingi za Qur’ani Tukufu na hadithi. Hapa ni baadhi ya mifano:

“Arshi” Na “Kursiyu” Kama Inavyoeleweka Kwenye Madhehebu Ya Makhalifa:

Bukhari, Tirmidhi, Ibn Majah, Ahmad Hanbal, Tabari, Ibn Kathiir na Suyuti wamenakili yafuatayo katika vitabu vyao vikuu:

“Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliulizwa: ‘Mwenyezi Mungu alikuwa amekaa wapi kabla Hajauumba ulimwengu?’ Yeye akajibu akisema: ‘Alikuwa katikati ya giza, mawingu mazito – yasiyokuwa na upepo chini yake wala juu yake. Na hapakuwa na kiumbe kingine. “Arshi” Yake ilikuwa ikielea juu ya maji.’”

Wanazuoni hawa wameifasiri Ayah ifuatayo: “Na Arshi Yake ilikuwa juu ya maji...” (Huud; 11: 7) kama kiti cha kimaada kilichowekwa juu ya maji. Katika ufafanuzi zaidi, wao wanaendelea kunukuu hadithi ya kuchukiza ifuatayo:

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Umbali baina ya ardhi na mbingu ni miaka sabini na moja, sabini na mbili au sabini na tatu. Na huo huo ndio umbali kati ya mbingu ya pili na ya tatu, vivyo hivyo, mpaka ya saba. Na juu ya mbingu ya saba ni bahari ambayo kina chake ni kipimo cha umbali kati ya mbingu mbili. Juu ya bahari hiyo kuna mbuzi wa mlimani wanane, kwato na magoti yao vimeachana kama umbali baina ya mbingu mbili. Juu ya migongo yao ni ile Arshi kubwa ya Mwenyezi Mungu ambayo urefu wake ni sawa na umbali baina ya mbingu mbili. Hapo, juu yake amekaa Mwenyezi Mungu, Mtukufu na Mkuu.”1

“Arshi” Yenye Kugongagonga.

Soma hadithi ifuatayo kutoka kwa Ibn Khuzaimah, Abu Dawuud, Ibn Athiir na Aaluusi na utabasamu! Hadithi yenyewe inasema kwamba wakati mmoja Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikutanisha vidole vyake kufanya umbo la kuba na akasema:

“Arshi ya Mwenyezi Mungu, juu ya mbingu zote, ni kama hivi. Na inachacharisha na kugongagonga kama mgongano wa matandiko ya ngamia wakati mtu anapompanda juu yake.”

Abu Dawuud katika Sunan yake, anasimulia kutoka kwa Basshar, hadithi ifuatayo:
“Mwenyezi Mungu amekaa kwenye Arshi Yake, na Arshi hiyo iko juu ya mbingu. Na Arshi hiyo inatoa makelele chini Yake, kwa namna ile matandiko ya ngamia yanavyogongana wakati mtu anapompanda.”

Tabari, Ibn Kathiir na Suyuti wanasimulia hadithi ifuatayo ndani ya Tafsiir zao kutoka kwa Khalifa Umar: Mwanamke mmoja wakati fulani alikuja kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na akasihi:

“Niombee ili niweze kuwa miongoni mwa wale watakaoingia Peponi.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akalitukuza jina la Mwenyezi Mungu na halafu akasema: “Kiti cha Mwenyezi Mungu kina ukubwa sawa na mbingu na ardhi na kinapiga makelele chini ya uzito Wake kama tandiko jipya la ngamia chini ya uzito wa mtu. Na Anakizidi kiti hicho pande zote kwa urefu wa vidole vinne!!’”

Vema, huyo ni Mwenyezi Mungu, mnene mno kiasi kwamba haenei katika “Arshi” Yake – Mwenyezi Mungu atuepushe na imani chushi kama hiyo. Sasa hebu tukichunguze chanzo chake.

Hadithi Ya Ka’b Al-Ahbar

Yeye anasema:

“Mwenyezi Mungu aliziumba mbingu saba, na ardhi pia kama hizo mbingu; na halafu akaziweka mbingu hizo kila moja mbali na nyingine, kipimo kile kile kama kile baina ya ardhi na mbingu ya dunia, na akazifanya kuwa nzito. Halafu akakinyanyua Kiti Chake juu ya mbingu hizo na akajiweka Mwenyewe juu yake.

Hivyo kila mbingu miongoni mwa mbingu hizo inapiga makelele na kugongagonga kutokana na uzito wa Mwenyezi Mungu, kwa namna ile kama tandiko jipya la ngamia linavyopiga kelele wakati mpandaji akikaa juu yake kwa mara ya kwanza.”

Hiki ndio chanzo chenyewe. Alikuwa ni Ka’b al-Ahbar, aliyekuwa Rabbi hapo mwanzoni, ambaye alianzisha upuuzi huu kwenye wingi wa hadithi za Kiislamu na akazihusisha kwa uongo na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.)

“Kursiy” Ni Nini, Na Ni Nani Wabebaji Wake

Ndani ya Tafsiir yake, Maqatil anaelezea Ayah ifuatayo kutoka ndani ya Qur’ani Tukufu:

وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ {255}

“…Na kiti chake kimeenea mbingu na nchi …” (Al-Baqarah; 2: 255)

Yeye anasema:

“Hiyo “Arshi” au “Kiti” kimebebwa na Malaika wanne:

Mmoja ana uso wa binadamu, na anaomba kwa ajili ya riziki juu ya wanadamu.

Wa pili anayo sura ya mnyama, kama ile ya dume la ng’ombe. Anaomba kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya riziki ya wanyama.

Malaika wa tatu anafanana na tai, akiwakilisha ndege. Yeye anawaombea ndege.

Huyo wa nne ni kama simba, akiwakilisha wanyama wa mwituni, na anawaombea riziki yao.”2

Hadithi kutoka Madhehebu ya Makhalifa zinahuzunisha kwa visa vya njama na uwongo kama hizi. Zaidi ya hayo, ni hapo tutakapokuwa tukielezea imani zao kuhusu kuhudhuria kwa Mwenyezi Mungu katika hiyo Siku ya Kiyama.

Ibn Khuzaimah katika kitabu chake juu ya Tawhiid amenukuu Ayah za Qur’ani Tukufu zifuatazo, ili kuthibitisha kwamba Mwenyezi Mungu Mwenyewe ametudhihirishia sisi juu ya makazi Yake!

الرَّحْمَٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ {5}

“Mwenyezi Mungu amejiimarisha juu ya Arshi…” (Twaha; 20: 5)

ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ {59}

“Kisha akajiimarisha Mwenyewe juu ya Arshi…” (Furqan; 25: 59)

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَكَانَ عَرْشُهُ عَلَى الْمَاءِ {7}

“Ni Yeye ambaye ameziumba mbingu na ardhi katika siku sita na Arshi Yake ilikuwa juu ya maji.....” (Huud; 11: 7)

Ibn Khuzaimah anaamini kwamba Ayah hizi zinaashiria kwenye moja ya fanicha anayoitumia Mwenyezi Mungu kama kiti Chake! Na yeye hayuko peke yake. Wanazuoni wengi wamefuata nyayo zake, wakisahau kwamba maneno haya yametumiwa kiistiari kuelezea ufalme na mamlaka.

Madhehebu Ya Ahlul-Bayt (A.S.)

Imam Ja’far Sadiq (a.s.) aliulizwa kuhusu Ayah ifuatayo:

وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ {255}

“…Na kiti chake kimeenea mbingu na nchi …..” (Al-Baqarah; 2: 255)

Yeye (a.s.) akasema: “Kursiyu” inaashiria elimu Yake na Ayah hii ina maana:

‘Elimu yake imezienea mbingu na ardhi.’”

Katika hadithi nyingine kutoka kwa Imam Ja’far Sadiq (a.s.) tunayakuta maneno yafuatayo:

“Mbingu na ardhi vyote vimo kwenye ‘Kursiy’ Yake,’3 yaani elimu.”

Mtu mwingine alikuja kwa Imam Ja’far Sadiq (a.s.) akiomba maelezo juu ya “Arshi juu ya maji.”

Imam (a.s.) akauliza: “Wao wanasema nini?”

Yule mtu akasema: “Wanasema kwamba Arshi ya Mwenyezi Mungu iko juu ya maji, na Yeye amekaa juu yake.”

Imam (a.s.) akasema:

“Kwa hakika huo ni uwongo! Yeyote anayeamini kwamba Mwenyezi Mungu anakadirika na anabebwa, anamfanan- isha na viumbe! Na kile ambacho kinazuia au kinabeba lazima kiwe na nguvu zaidi Yake!”

Yule mtu aliduwaa na kuwa kimya kwa muda kiasi na halafu akasema: “Ninaweza kuwa fidia yako? Naomba nijifunze kutoka kwako, ile maana halisi.”

Imam (a.s.) akasema:

“Ndani ya Ayah mbalimbali za Qur’ani Tukufu, hili neon ‘Arsh’ limekuja katika muktadha mbalimbali. Maana yake katika kila suala ni ama ‘ufalme’ au ‘mamlaka’ au ‘elimu.’”
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

ۖ وَهُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ {129}

“Mola wa ‘Arshi’ Kuu.” (at-Tawbah; 9: 129)

Hapa utukufu wa Mwenyezi Mungu unawakilishwa katika neno ‘Arshi’, ambalo ni Ufalme Wake.

Katika Ayah nyingine

الرَّحْمَٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ {5}

“Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema amjiimarisha juu ya ‘Arshi’…..” (Twaha; 20: 5)

Maana yake ni kwamba mamlaka Yake yameenea kwenye ufalme Wake. Na pale Mwenyezi Mungu anaposema: “Arshi Yake ilikuwa juu ya maji,

Yeye ana maana kwamba maji yaliumbwa kabla ya mbingu na ardhi, na yalikuwa ndio kiumbe cha kwanza kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu.” Kwa kweli, Ibn Khuzaimah na wale wanaofanana naye wamepotoshwa na lile neno Istawaa ambalo limetokea ndani ya Qur’ani Tukufu pamoja na ‘Arsh’. Wao wamelitafsiri kwa maana halisi kama “amekaa” au “ametulia.” Ndani ya Qur’ani, tunakuta Ayah sita ambamo neno hilo limetumika. Raghib Isfahani anasema ndani ya Tafsiri yake:

“Kila wakati hiki kitenzi Istawaa kinapogeuzwa kwenye hali elekezi pamoja na ‘Ala,’ inamaanisha Istiila – udhibiti, kujitwalia, ushindi, uwezo, kama ndani ya Ayah: ‘Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema anao udhibiti kamili juu ya ‘Arsh.’”

Hali kadhalika, tunalikuta neno hilo likiwa limetumika katika fasihi ya Kiarabu kwa kidokezo hicho hicho. Mshairi mmoja anamsifia Bushr bin Marwan, ndugu yake yule Khalifa wa Bani Umayyah, Abdul Malik, katika ubeti ufuatao:

“Bushr ameiteka Iraq bila ya kushika na kutumia upanga au kumwaga damu yoyote…”(Qad istawaa alal Iraqi…)

Neno jingine, ambalo limeleta matatizo – juu ya madhehebu ya Makhalifa yenye kushirikisha viungo kwa Mwenyezi Mungu, ni Kursyu. Wao wamelichukulia kwa maana halisi, likimaanisha kigoda au kiti. Tabari ndani ya Tafsiir yake anasema kwamba Kursiyy inamaanisha elimu pia, na ni kwa sababu hii kwamba vitabu vya elimu vinaitwa Kurrasah, na watu waliosoma hasa wanaitwa Kurasiyy. Qur’ani Tukufu imelibadilisha neno Kursiyy na neno Ilm ndani ya Ayah kadhaa, ambazo zinazungumza katika mwelekeo mmoja. Kwa mfano:

ۗ وَسِعَ رَبِّي كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا ۗ {80}

“…Mola Wangu anao wasaa wa elimu juu ya kila kitu …” (Al-An’aam; 6: 80)

وَسِعَ رَبُّنَا كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا ۚ {89}

“...Mola Wetu amekienea kila kitu kwa elimu…” (Al-A’araf; 7: 89)

رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَحْمَةً وَعِلْمًا {7}

“Mola Wetu! Wewe umevienea vitu vyote kwa huruma na elimu.” (Al- Mu’min; 40: 7)

إِنَّمَا إِلَٰهُكُمُ اللَّهُ الَّذِي لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ وَسِعَ كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا {98}

“Hakika Mola Wenu ni Mwenyezi Mungu mmoja tu, ambaye hakuna aabudiwaye ila Yeye tu, anakijua kila kitu kwa elimu (Yake).” (Twaaha; 20: 98)

Katika Ayah zilizotangulia, kitenzi ‘wasia’ kimetumika pamoja na ‘Ilm.’ Hata katika ile Ayah pekee ambamo Kursiyy imetumika, inavutia kuona kwamba kipande cha Ayah hiyo kilichotangulia kinazungumzia juu ya elimu ya Mwenyezi Mungu pana na yenye kuenea. Hebu tuichunguze Ayah hiyo kama inavyoanza:

ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ {255}

“Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao – wala wao hawajui kitu katika elimu yake ila kile apendacho yeye. Elimu (Kursiy) yake imeenea mbingu na nchi…” (Al-Baqarah; 2: 255)

Mukhtasari

Kwa mujibu wa Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.), kwa hiyo, Arsh na Kursiyy yanaashiria ufalme, mamlaka na elimu. Matumizi ya maneno haya ni ya kiistiari. Hili ni kinyume kabisa na kile ambacho madhehebu ya upande wa pili ilivyoongozwa kuamini kwa sababu ya athari za Kiyahudi.

  • 1. Sunan Abu Dawuud - Juz. 4, uk. 231; Sunan Ibn Majah, Juz. 1, uk. 69; Musnad ya Ahmad Hanbal, Juz. 1, uk. 207.
  • 2. Tafsiir Maqatil, Juz. 1, uk. 122.
  • 3. Tawhiid, cha Saduuq - uk. 327-328.