read

Sura Ya Tisa: Kuona Kwa Mwenyezi Mungu

Madhehebu ya Makhalifa wamezungumzia kuona kwa Mwenyezi Mungu katika namna tatu.
Nazo hizo ni:

(i) Mwenyezi Mungu anaona kupitia kwa Mtume wetu (s.a.w.w.) wakati wa uhai wake;

(ii) Mwenyezi Mungu anaona kupitia kwa waumini katika hiyo Siku ya Kiyama, kabla hawajaingia Peponi;

(iii) Mwenyezi Mungu anaona kupitia kwa waumini wakati wa kukaa kwao ndani ya Pepo.

Ibn Khuzaimah ndani ya Tawhiid yake anasimulia kutoka kwa Ibn Abbas, Abu Dharr na Anas hadithi inayounga mkono imani ya kwamba Mtume wetu (s.a.w.w.) alimuona Mwenyezi Mungu.

Kwa mfano, kutoka kwa Ibn Abbas yeye anasimulia kwamba Mwenyezi Mungu alimbariki Nabii Ibrahim (a.s.) kwa kumchukulia yeye kama rafiki, Nabii Musa (a.s.) kwa kuzungumza naye, na Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kwa kujionyesha Yeye Mwenyewe kwake. Katika nyingi ya hadithi kama hizi, Ikramah, yule mtumwa aliyeachwa huru na Ibn Abbas ametajwa. Ikramah anafahamika sana kwa kuhusisha hadithi za uongo kwa Ibn Abbas.

Kwa upande mwingine tunajua kwamba Ibn Abbas alikuwa miongoni mwa masahaba na wanafunzi wa karibu sana wa Imam Ali ibn Abi Talib (a.s.). Ni jambo lisilowazika kwamba Ibn Abbas angeweza kueleza jambo lolote, ambalo linakwenda kinyume na mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s.). Ukweli ni kwamba Ibn Khuzaimah alikuwa chini ya ushawishi wa Ka’b al-Ahbar ambaye ndiye anayemnukuu:

“Mwenyezi Mungu amezigawanya neema Zake mbili maalum kati ya Musa na Muhammad – zawadi ya mawasiliano ya moja kwa moja na zawa- di ya kumuona Mwenyezi Mungu. Hivyo Muhammad (s.a.w.w.) alimuona Yeye mara mbili, na Musa aliongea Naye mara mbili.”1

Ni lazima ielezwa kwamba wanazuoni fulani na masahaba walio kinyume na Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) wamekataa kwa ushupavu kabisa kuamini kwamba Mtume wetu (s.a.w.w.) aliwahi kumuona Mwenyezi Mungu kamwe. Miongoni mwao ni Bi. Aisha, mkewe Mtume mwenyewe. Lakini Ibn Khuzaimah anasisitiza juu ya ukweli wa ile hadithi kutoka kwa Ka’b al-Ahbar na kumkanusha Aisha.

Katika hadithi ndefu ifuatayo kutoka kwa Abu Huraira, inayosimuliwa na Bukhari, Muslim, Abu Dawuud, Ibn Majah, Tirmidhi, Ahmad bin Hanbal na Suyuti, tunakutana na tamthiliya ambayo inadhaniwa kuja kujidhihirisha yenyewe mnamo Siku ya Kiyama. Abu Huraira anasema:

“Baadhi ya watu waliuliza: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, je, tutakuja kumuona Mola wetu hiyo Siku ya Kiyama?’ Mtukufu Mtume akajibu:

‘Je, mnatilia shaka juu ya kuliona jua katika siku angavu?’ Wao wakasema: ‘Laa hasha, Ewe Mtume.’

Mtume Mtukufu akasema: ‘Hivyo mtamuona Yeye mnamo Siku ya Kiyama! Mwenyezi Mungu atawakusanya watu wote na halafu atatangaza: Kila mmoja amfuate mungu wake aliyekuwa akimuabudu. Baadhi yao watalifuata jua, na wengine mwezi. Wachache wao watakwenda nyuma ya mashetani. Kisha watu wa Umma, pamoja na wanafiki watabakia imara. Halafu Mwenyezi Mungu atajionyesha Mwenyewe, pamoja na sura ambayo itakuwa ngeni kwao, na atasema: Mimi hapa, Mola Wenu!’

“Wataguta kwa sauti kubwa: ‘Tunaomba hifadhi kwa Mola Wetu kutokana na wewe. Sisi tutakaa hapa hadi Mola Wetu atakapokuja. Na hapo atakapokuja, sisi tutamtambua Yeye.’

“Halafu Mwenyezi Mungu atatokeza kwa ule uso unaofahamika na kusema: ‘Mola Wenu Mimi hapa!’

“Wao watasema: ‘Ndiyo, Wewe hakika ndiye Mola Wetu.’ Halafu watamfuata Yeye na Mwenyezi Mungu atairudisha mahali pake ile daraja juu ya Moto wa Jahannam.”
Halafu Abu Huraira anaendelea zaidi kutoa maelezo kuhusu moto wa jahannam, na kuelezea jinsi ambavyo hatimaye waumini watakavyokuja kuokolewa kutokana na adhabu. Kisha akasema:

“Mtu mmoja atakuja kuachwa nyuma na uso wake ukiwa umeelekea moto ulioghadhibika. Atasema: ‘Ewe Mola Wangu! Ile harufu mbaya ya moto wa jahannam imenisumu, na miale yake imenibabua. Nigeuze uso wangu mbali kutoka kwenye moto wa jahannam.’

“Atarudia kusihi kwake mara nyingi, mpaka Mwenyezi Mungu atakapose- ma: ‘Kama nitakukidhia haja yako, utaomba mengi zaidi.’ Mtu huyo atasema: ‘Kwa Utukufu Wako, mimi sitaomba tena zaidi ya hayo.’

“Mwenyezi Mungu ataugeuzia mbali uso wake kutoka kwenye moto wa jahannam. Papo hapo, mtu huyo atasema: ‘Ewe Mola Wangu, nipeleke karibu na milango ya Peponi.’

“Mwenyezi Mungu atasema: ‘Je, wewe hukuahidi kwamba hutakuja kuomba kitu chochote kile kingine? Ole wako, ewe mwana wa Adam! Wewe ni mdanganyifu.’

“Lakini mtu huyo atasisitiza. Hivyo Mwenyezi Mungu atakuja kusema: “Je, utakuja kuomba kitu kingine tena kama nitakukubalia hilo?’

“Mtu huyo atakujasema: ‘Hapana, kwa Utukufu Wako, Mimi sitakuja kuomba tena.’

“Na atakuja kutoa ahadi ya dhati; na Mwenyezi Mungu atamchukua yeye hadi kwenye milango ya Peponi. Pale yeye atakapoziona rehema zilizosheheni ndani ya Pepo, atanyamaza kimya na kusimama kwa heshima na mshangao kwa kitambo kiasi, na halafu atasihi: Oh, Mola Wangu, niruhusu kuingia Peponi.’

“Mwenyezi Mungu atasema: ‘Wewe hukuahidi kutoomba chochote zaidi? Ole wako ewe mwana wa Adam! Kwa hakika wewe ni mdanganyifu.’ Lakini mtu huyo ataendelea kuomba kwa kung’ang’ania na kusihi mpaka Mwenyezi Mungu atacheka – na kicheko hicho kitaashiria ruksa.

Wakati mtu huyo hatimaye atakapokanyaga ndani ya Pepo, atapewa haja zake zote, hadi iwe hakuna cha kuhitaji tena.

Halafu Mwenyezi Mungu atasema: ‘Yote haya, na maradufu zaidi, ni kwa ajili yako.’”

Abu Hurair akaongeza: “Mtu huyo atakuwa mtu wa mwisho kuingia Peponi.”

Huu ni mfano kutoka kwenye vyanzo sahihi vya madhehebu ya Makhalifa. Sasa hebu tuchunguze ni nini Ahlul-Bayt (a.s.) walichosema:

Mwenyezi Mungu Hawezi Kuonekana

Maimam wa Ahlul-Bayt (a.s.) wamefundisha kwa uthabiti kabisa kwamba suala la kudhihiri na kuonekana halitumiki kwa Mwenyezi Mungu. Yeye hataonekana hiyo Siku ya Kiyama, na hawezi kuonekana hapa juu ya ardhi vilevile.

(1) Imam Ja’far as-Sadiq (a.s.) amesema:

“Mmoja wa watu wasomi kutoka kwa watu wa vitabu alikwenda kwa Imam Ali (a.s.) na akamuuliza: ‘Ewe Ali, je, umewahi kumuona Mola Wako kamwe wakati wa kufanya kwako ibada?’

Imam Ali (a.s.) akasema: ‘Mimi sijamuabudu kamwe Yule ambaye sija muona!’

Yule mwanazuoni akauliza: ‘Na ulimuona vipi Yeye?’

Imam (a.s.) akasema: ‘Kumbuka, hili jicho la kimwili haliwezi kumuona Yeye.
Ni moyo ndio ambao unamuona Yeye pamoja na imani halisi’”2

(2) Safwan bin Yahya anasema kwamba Abu Qurrah, mmoja wa wapokezi wa madhehebu ya Makhalifa, aliomba ruhusa ya kuonana na Imam ar- Ridhaa (a.s.). Baada ya kuruhisiwa kufika mbele ya Imam, aliwasilisha maswali kadhaa yaliyohusiana na Shariah ya Kiislamu (fiqh). Halafu akasema:

“Tunayo hadithi ambayo inasema kwamba Mwenyezi Mungu aligawanya neema Zake kati ya Nabii Musa (a.s.) na Muhammad (s.a.w.w.). Pamoja na huyu wa mwanzo, Yeye alizungumza naye, na huyu wa baadaye (s.a.w.w.), Yeye alijidhihirisha Mwenyewe kwake.”

Baada ya kuyasikia haya, Imam ar-Ridhaa (a.s.) akasema:

“Kama hivyo ndivyo ilivyokuwa, basi ni nani aliyefikisha ujumbe ufuatao kutoka kwa Mwenyezi Mungu:

لَا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ {103}

(a) “Macho hayamfikii, bali Yeye anayafikia macho, naye ni Mwenye kujua, Mwenye habari.” (Al-An’aam; 6: 103)

وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا {110}

(b) “…wala hawataweza kumjua (Mwenyezi Mungu) vilivyo kwa elimu zao.” (At-Twaha; 20: 110)

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ {11}

(c) “Hakuna chochote mfano wake, naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (As-Shuraa; 42: 11)

“Je, haikuwa ni Muhammad (s.a.w.w.) aliyefikisha ujumbe huu mtukufu?”

Abu Qurrah akasema: “Ndiyo, hakika, alikuwa ni Muhammad (s.a.w.) ambaye alifikisha.”

Imam ar-Ridha (a.s.) akasema:

“Inawezekana vipi mtu aliyewafundisha wanadamu kwamba Mwenyezi Mungu hawezi kuonekana, kuzingirwa, kufananishwa au kulinganishwa, ghafla ageuke na kusema: ‘Mimi nimemuona Yeye, nikamzingatia, na kwamba anafanana na mwanadamu?’ Huoni aibu au haya kumzulia Mtume (s.a.w.w.) mambo ambayo hata wale wasioamini hawakumhusisha nayo?”

Abu Qurrah akasema:

“Lakini Qur’ani Tukufu inasema kwamba katika usiku wa Mi’raaj Mtume alimuona Mwenyezi Mungu.”

Halafu akasoma Ayah ifuatayo:

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ {13}

“Na bila shaka yeye alikiona kwa mara nyingine”(An-Najmi; 53: 13)

(Abu Qurrah alishikilia kwamba kile kitenzi “hu” – katika ra’ahu – kina- paswa kumaanisha Yeye,” yaani Mwenyezi Mungu).

Imam ar-Ridha (a.s.) akasema:

“Ni lazima uisome ile Ayah inayofuatia ambayo inaelezea kile Mtume (s.a.w.w.) alichokiona. Katika Ayah ya 18 ya Surah hiyo hiyo, unakuta:

لَقَدْ رَأَىٰ مِنْ آيَاتِ رَبِّهِ الْكُبْرَىٰ {18}

“Kwa hakika aliona katika dalili za Mola wake zilizo kuu.” (An-Najmi; 53: 18)

“Dalili za Mwenyezi Mungu sio Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hawezi kuonekena – hakuna macho yanayoweza kumzingatia Yeye na hakuna elimu inayoweza kumzingira.”

Abu Qurrah akalalamika: “Kwa hiyo unazichukulia hadithi zetu kama uongo?”

Imam ar-Ridha (a.s.) akasema: “Hadithi yoyote ambayo inakwenda kinyume na Qur’ani Tukufu ni uongo, na imehusishwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa uongo. Siitolei usadik- isho juu yake.” 3

Yenye Kuonekana Wazi Katika Hadithi Kutoka Kwa Abu Huraira

1. Kwamba Mwenyezi Mungu ataonekana katika Siku ya Kiyama, kwa kung’ara na dhahiri kabisa kama jua au mwezi katika anga nyeupe;

2. Kwamba Mwenyezi Mungu atatokeza kwanza kwa uso usiofahamika, kwa matokeo kwamba Waislamu hawataweza kumtambua. Yeye atatokeza tena na sura inayofahamika na halafu atakubalika kwa waumini;

3. Kwamba mtu aliyeuelekea moto wa jahannam ataendelea kumdan- ganya Mwenyezi Mungu mara tatu;

4. Kwamba Mwenyezi Mungu atakuja kucheka, kwa namna sisi binadamu tunavyocheka.

Abu Huraira anaonekana kuelekea kumwelezea Mwenyezi Mungu kama chalii mchezi anayebadili sura yake kufurahisha watu.

Mtu anashangaa ni sifa gani maalum za sura Yake ambazo Waislamu watazitambua? Je, wao wamewahi kumuona kabla ya hapo? Kama ndivyo, ilikuwa lini? Ilikuwa wakati Alipokuwa Kijana, Mzee, au alipokuwa kapondwa kabisa na umri mkubwa ?

Hata lile Agano la Kale au Jipya yote hayana kisa cha ajabu kama hicho. Ni hekaya za bibi kizee zinazosimuliwa kwa mtoto wakati wa usiku mrefu wa baridi kali! Lakini athari za utungaji maneno ya uongo huu umekuwa mkubwa mno. Mawahabi na wanazuoni wengi wengine kutoka madhehebu ya Makhalifa wanashikilia kwamba Mwenyezi Mungu atakuja kuonekana kimwili, wazi wazi katika Siku ya Kiyama.

Mikazo Ya Wazi Ya Ufafanuzi Wa Ahlul-Bayt (A.S.)

(a) Kwamba macho yanaweza kufahamu tu vile vitu, ambavyo vina mwili au maada;

(b) Chochote kilichopo ambacho hakina mwili, (kwa mfano roho, mwanga, umeme n.k.) hakiwezi kuonekana. Kwa kweli suala la kukiona kiumbe kama hicho halina msingi, halipasiki;

(c) Mwenyezi Mungu sio mwili wala maada. Yeye ndiye Muumba wa maada. Mtu anaweza ‘kumuona’ Yeye kupitia kwenye viumbe Vyake;

(d) Hakuna chochote kile kiwacho chenye kufanana Naye, hivyo Yeye hawezi kulinganishwa na umbile lolote lile;

(e) Hadithi yoyote ile, ambayo inakwenda kinyume na Qur’ani Tukufu, ni lazima itupiliwe mbali kama ya uongo.

  • 1. Tawhiid, cha Ibn Khuzaimah - uk.202
  • 2. Tawhiid, cha Saduuq - uk.109.
  • 3. Tawhiid cha Saduuq - uk. 110 - 112.