read

Utangulizi (2): Maneno Halisi Na Yale Ya Kiistiari

Katika Kiarabu au Kifursi, kama vile katika lugha nyinginezo tu, pale neno linapoonyesha maana ambayo kwamba lilitungiwa kwa asili, matumizi yake yanaitwa halisi. Wakati tunaposema: “Mikono ya mwizi ilikatwa,” neno “mikono” katika kadhia hii limetumika katika maana yake halisi.

Lakini pale neno linapotumika kama tamathali ya usemi ambamo linahamishiwa kwenye kitu ambacho halitumiki hasa, linaitwa la kitamathali au kiistiari. Kwa mfano, wakati neno “mkono” linapotumika kumaanisha “uwezo” au “mamlaka” na kadhalika.

Wakati mwingine inasemwa: “Kuna mkono juu ya kila mkono.”

Katika suala hili, maana yake ni kwamba kuna uwezo juu ya kila uwezo. Matumizi kama hayo yanapatikana katika kila kazi ya fasihi, na inaongezea uzuri wa mtindo. Qur’ani Tukufu, katika mtindo wake usioigika na bora sana, hutmia matumizi kama hayo katika sehemu nyingi.
Kwa mfano:

وَلَا تَجْعَلْ يَدَكَ مَغْلُولَةً إِلَىٰ عُنُقِكَ وَلَا تَبْسُطْهَا {29}

Wala usifanye mkono wako (kama) uliofungwa shingoni mwako, wala usiukunjuwe mkunjuo wa kabisa (Bani Israail; 17: 29)

Lakini ni dhahiri kabisa kwamba maneno haya katika Ayah hii sio ya kutafsiriwa neno kwa neno. Maana ya Ayah hii ni: “Usiwe bakhili, wala usiwe mkarimu mno au mbadhilifu....”

Mfano mwingine ni wa neno “Siraat” ambalo katika Kiarabu lina maana ya “barabara” au “njia.” Katika Suratul-Fatiha, kama tutachukua maana halisi ya neno Siraat, Ayah hiyo itasomeka hivi:

Tuonyeshe barabara iliyonyooka. Barabara ya wale ulioshusha neema Zako juu yao, sio ya wale uliowaghadhibikia au waliopotea.” (Al-Fatiha)

Kwa hakika, Ayah hizi hazizungumzii juu ya barabara zozote zile. Ayah zinazunguzia juu ya njia, ile njia ya Mitume, njia inayoongozea kwa Mwenyezi Mungu, ambayo ni sawasawa na Uislamu. Tunaomba tuonyeshwe njia ya wale waliobarikiwa na kuongozwa na sio ya wale ambao Yeye amewaghadhibikia.

Hitimisho

Kila mwanazuoni wa lugha ya Kiarabu atathibitisha kwamba ule “unyooshaji mkono mbele” katika Ayah ya Qur’ani Tukufu hakuelekezi kwenye viungo vya mwanadamu. Kunamaanisha utoaji mwingi wa tunzo au zawadi. Hali kadhalika, neno Siraat halirejelei kwenye zile barabara zenye mavumbi, linaelekeza kwenye njia ya kiroho na adhimu, Uislamu.

Hata wanazuoni wa wafasiri kutoka kwenye madhehebu tofauti na ile ya Ahlul-Bayt (a.s.) wanakubaliana nasi katika tafsiri hii. Hata hivyo, cha kushangaza zaidi, wakati neno linaloashiria sehemu za mwili kama vile “mkono”, “jicho”, au “kifundo cha mguu” linaonekana ndani ya Qur’ani Tukufu kuhusiana na Mwenyezi Mungu, wao wanasisitiza kwamba lazima lichukue maana halisi, na kwamba wao wanalitumia hasa kwenye viungo vya mwili “Wake.” Madhehebu ya Ahlul-Bayt imeyachukulia maneno haya kuwa na maana ya kiistiari.

Kwa hiyo, ni muhimu kabisa kulinganisha na kupima hoja zinazotolewa na kila madhehebu, na kuchunguza ni vipi kila moja imepata kuungwa mkono na Qur’ani Tukufu na hadith. Hii itatuwezesha sisi kuzielewa zile Sifa Tukufu katika Uislamu.

Uchaguzi Wa Kitabu Kimoja Cha Tawhiid Kutoka Kila Madhehebu

Tumechagua kitabu kimoja kutoka kwenye madhehebu ya Makhalifa na kimoja kutoka madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.). Kila kimoja kinajishughulisha na maudhui ya Upweke wa Allah.

Tawhii kutoka kwa Ibn Khuzaimah ni ya kutoka madhehebu ya Makhalifa, na Tawhiid ya Sheikh Saduuq inawakilisha madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.). Kabla hatujaendelea na kunukuu kutoka kila kimoja chao, tunadhani ni busara tukiwatambulisha hao waandishi ili kwamba ubora na vyeo vyao viwe vinaeleweka.

Ibn Khuzaimah Kama Anayotazamwa Na Madhehebu Ya Makhalifa

Wanazuoni wamemteua Ibn Khuzaimah kama: Imamul Aimmah (Imam wa Maimamu)

• Al-Hafidh al-Kabiir (mtunzaji mkuu wa elimu za Kiislamu – au mashuhuri miongoni mwa wale walioihifadhi Qur’ani kwa moyo)

• Al-Mujtahid al-Mutlaq (Mwana-Fiqh thabiti)

• Bahrul Uluum (Bahari ya elimu)

• Ra’sul Muhaddithin (kiongozi wa wasimulizi)

• Habr ul-Ulama al-Amiliin (mshauri wa wanazuoni waadilifu)

• Ka’batul Ulama (kitovu cha wasomi)

Muhammad Ibn Ishaq Khuzaimah Nisaburi:

Yeye alizaliwa mnamo mwaka wa 213 Hijiria na alifariki mwaka wa 311 Hijiria. Wanazuoni wengi wamesimulia hadithi kutoka kwake, ikiwa ni pamoja na waandishi wa Bukhari na Muslim. Inasemekana kwamba Ibn Khuzaimah kwa kulipa hisani alizikubali hadithi zilizosimuliwa na hawa wawili wa mwisho hapo juu.

Mbali na tasnifu ndogo ndogo zilizoandikwa katika kujibu maswali fulani, Ibn Khuzaimah ameandika vitabu vikubwa 140, ambavyo vinajumuisha pamoja na ile Sahih maarufu ya Ibn Khuzaimah. Baadhi ya Wanazuoni wanaiona Sahih yake kama ni bora na yenye kuzidi aula kuliko Sahih Bukhari na Sahih Muslim. Alikuwa ni mfuasi wa Shafi’i.

Ndani ya mjala huu mfupi, tumetegemea kwenye kitabu chake kiitwacho Tawhiid, kilichopitiwa kwa makini na Muhammad Khaliil Haras wa al- Azhar, Cairo na kuchapishwa na al-Azhar University Press – (Taasisi ya kupiga chapa ya Chuo Kikuu cha al-Azhar), Cairo, mnamo mwaka 1378 Hijiria.

Sheikh Saduuq Kama Anavyotazamwa Na Madhehebu Ya Ahlul-Bayt (A.S.)

Saduuq ni jina alilopewa Abu Ja’far Muhammad ibn Ali bin Husayn bin Babawayh Qummi. Yeye alifariki mnamo mwaka 381 Hijiria. Ni mwanazuoni mwenye heshima ya juu, asiyehitaji kutambulishwa. Ameandika takriban vitabu 200.

Katika mjadala huu, tumetegemea kwenye kitabu chake cha Tawhiid, kilichochapishwa Tehran mnamo mwaka 1381 Hijiria, kikapitiwa kwa tahaki- ki na Syed Hashim Husayni Tehrani.

Vitabu hivi viwili ndio vyanzo vyetu vikuu. Kwa nyongeza, tunarejea kwenye vitabu vingine maarufu vilevile kama vile Mlango wa Tawhiid ndani ya Sahih Bukhari, Mlango wa Iman kutoka Sahih Muslim. Na kwa upande wa madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.), tutafanya marejeo kwenye Mlango wa Tawhiid kutoka kitabu Biharul Anwar cha Majlisi (aliyefariki mwaka 1111 Hijiria).