read

Utangulizi : Athari Ya Imani Za Kikristo Na Kiyahudi Katika Uislamu

Imani za kikristo na kiyahudi, hususan utamaduni wa kiyahudi ulienea miongoni mwa Waislamu katika njia mbili: kwanza kabisa, kupitia juhudi za wakristo na wayahudi wenyewe, na pili kupitia kwa Waislamu fulani.

Hebu tuzichunguze njia hizi mbili kwa kinaganaga:

Kuenea kwa imani za Kikristo na Kiyahudi miongoni mwa Waislamu kupitia juhudi za makusudi kabisa za Wakristo na Wayahudi.

Huko nyuma, tumeelezea nafasi ya wanazuoni wa Kikristo na Kiyahudi katika kuzua hadithi. Tunajua kwamba pale Makhalifa walipokataa kuruhusu uenezaji wa hadithi za Mtume (s.a.w.w.), kwa hisani sana wao waliwaruhusu wanazuoni wa Kikristo na Wayahudi ambao walikuwa wameingia katika Uislamu ili kueneza fikra zao wenyewe miongoni mwa Waislamu. Mathalan, Tamim Darii, aliyekuwa mtawa wa Kikristo kabla ya kuukubali Uislamu, aliruhusiwa rasmi na Khalifa Umar kuhutubia Waislamu siku za Ijumaa, kabla ya hotuba ya Swala ya Jama’a, ndani hasa ya Msikiti mkuu wa Mtume (s.a.w.w.). Katika zama za Uthman, aliruhusiwa rasmi kufanya hivyo mara mbili kwa wiki.

Vivyo hivyo, Ka’b al-Ahbar (ambaye jina lake la kwanza lilikuwa ni Mati’) alikuwa ni kuhani aliyefahamika vizuri kabla yeye kuukubali Uislamu. Alijulikana kama Ka’b al-Habr au Ka’b al-Ahbar, kwani Habr kwa Kiarabu ina maana ya mtakatifu, mtu mwenye elimu. Katika siku za Khalifa Umar, Ka’b al-Ahbar alipandishwa kwenye cheo cha Msimamizi wa Baraza, na Uthman vile vile aliendelea kumlea yeye. Waislamu walimwendea katika mas’ala ya kanuni na ufafanuzi wa Qur’ani Tukufu.1

Ka’b alijaribu kiasi alivyoweza katika kueneza imani zilizochimbukia kutoka kwenye masimulizi yaliyopotoshwa ya Taurati, na dhana nyingine za Kiyahudi, miongoni mwa Waislamu. Baadhi ya watu wa wakati huo huo ambao waliwafuata Ahlul-Bayt (A.S.) walikuwa wanatambua juu ya mbinu zake za kichochezi, kama inavyoshuhudiwa katika kadhia ifuatayo:

Tabari katika kitabu chake cha historia anasimulia:

“Ibn Abbas aliambiwa: Ka’b anasema kwamba katika Siku ya Kiyama, jua na mwezi vitakuja kuletwa kama madume ya ng’ombe mawili yaliyochanganyikiwa na kutupwa ndani ya Jahannam.”

Alipoyasikia haya, Ibn Abbas alikasirika sana, na akajibu kwa ukali mara tatu:

“Ka’b ni muongo! Ka’b ni muongo! Ka’b ni muongo! Hii ni fikra ya Kiyahudi, na Ka’b anataka kuiingiza katika Uislamu. Mwenyezi Mungu yuko Huru kutokana na vitu wanavyomhusisha navyo. Yeye kamwe haviadhibu vile vinavyomtii. Hujamsikia Mwenyezi Mungu akisema ndani ya Qur’ani Tukufu kamba:

وَسَخَّرَ لَكُمُ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ دَائِبَيْنِ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ {33}

“Na akakutiishieni jua na mwezi, vifanyavyo kazi (vikifuata njia zao) mfululizo.’” (Ibrahim; 14: 33)

Ibn Abbas akasema: “Hii ‘Daibain’ iliyotumika katika Ayah hii inaonye- sha utii wa wakati wote kwa Mwenyezi Mungu.”

Kisha akaendelea:

“Yeye atawezaje kuyaadhibu haya maumbo mawili ya ki-mbinguni ambayo
Yeye Mwenyewe anayasifia kwa utiifu wao? Mwenyezi Mungu Amlaani
mwanazuoni huyu wa Kiyahudi na elimu yake! Ni ufidhuli usio na aibu kiasi
gani huu wa kuhusisha uongo kwa Mwenyezi Mungu, na kutia hatia kwa
viumbe viwili hivi vitiifu!”

Baada ya kuyasema haya, Ibn Abbas akarudia mara tatu kusema: “Sisi sote ni wa Allah, na Kwake Yeye tutarejea.”

Halafu Ibn Abbas akaendelea kusimulia kile ambacho Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) hasa alichokisema kuhusu jua na mwezi. Mtume alisema:

“Mwenyezi Mungu ameumba vyanzo viwili vya mwanga. Kile ambacho Yeye alikiita jua kilikuwa kama ardhi, baina ya sehemu za mawio na machweo. Na kwamba kile alichokiamuru kuwa bila mng’aro kwa nyakati fulani, Yeye alikiita mwezi na akakifanya kuwa kidogo zaidi kuliko lile jua. Na vyote huonekana kuwa kama vidogo kutokana na urefu wao katika anga na umbali wao kutoka ardhini.”2

Uchunguzi Ulioegemea Juu Ya Hadith Hizo Mbili

Kutoka kwenye Hadith hizi mbili, ambazo ni, ile moja kutoka kwa Ka’b na nyingine kutoka kwa Ibn Abbas, tunaona kwamba:

1. Ibn Abbas alikanusha na kukataa yale ambayo Ka’b aliyahusisha na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na akanukuu kutoka kwenye Qur’ani Tukufu:

“Na akakutiishieni jua na mwezi, vifanyavyo kazi (vikifuata njia zao) mfululizo……..”

Akitoa hoja kwamba juhudi yote hiyo ni sawa na utii kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwaadhibu wale au vile vinavyomtii Yeye.

2. Katika kukataa zaidi tabia ya Ka’b ya kufuata mkondo wa yaliyotangulia, Ibn Abbas alithibitisha kwamba jua na mwezi yalikuwa ni maumbo makubwa mawili ya kimbinguni kama ardhi, na alitafuta kuungwa mkono na Hadith ya Mtume (s.a.w.w.), ambayo imesema:

“Na vyote huonekana kuwa kama vidogo kutokana na urefu wao katika anga na umbali wao kutoka ardhini.”

Ni dhahiri, haya yalikuwa ndio maamuzi bora kabisa ambayo Ibn Abbas aliyoweza kuyafanya kutoka kwenye Hadith. Hata hivyo, katika zama hizi, tunao uwezo wa kupata mahitimisho zaidi kutoka kwenye Hadith, yaani:

i. Kutajwa kwa sehemu ya mawio na machweo kwa ajili ya jua kuhusiana na ardhi, kunatoa kidokezo kuhusu mizingo na mzunguko wa maumbo ya kimbinguni.

ii. Vile vile kunaashiria kwamba maumbile hayo yanapaswa kuwa ya mviringo (matufe) ili kuwa na sehemu mbalimbali za kutua na kuchomoza. Hili lisingewezekana kama yangekuwa ya ubapa.

iii. Ni wazi vile vile kutokana na namna Ibn Abbas alivyoijadili ile Hadithi iliyosimuliwa na Ka’b kwamba yeye hakuelekea kuukubali uwezo wa kisheria wa Ka’b.

Kwa hiyo, Hadith zote kama hizo, ambazo zina mwonjo wa imani za Kiyahudi na zinahusishwa bila matata kwa Ibn Abbas kwamba amezisikia kutoka kwa Ka’b, hazina msingi na sio za kweli. Hizi zilibuniwa katika wakati wa siku za utawala wa Bani Abbas kwa sababu Bani Abbas walimuamini sana mhenga wao Ibn Abbas. Watu walitengeneza hadithi kwa jina la Ibn Abbas ili kupata umaarufu katika mabaraza ya Bani Abbas. Ulikuja kuwa ni mtindo kuhusisha hadithi za uongo kwa Ibn Abbas, ambazo badala yake ziliunda sehemu kubwa sana ya propaganda ya Kiyahudi na Kikristo.

Ibn Abbas alikuwa na uwezo wa kupata maamuzi fulani kutoka kwenye Hadith za Mtume (s.a.w.w.). Tunao uwezo wa kufanya nyongeza kwenye maamuzi hayo, tukiegemeza uchunguzi wetu juu ya ukweli wa kielimu wa wakati huu. Inaelekea kabisa kwamba hapo baadaye, wakati elimu itakapokuwa imefanya uchunguzi wa ziada, wanazuoni wanaweza kufanya mahitimisho mapya na ya maana zaidi kutoka kwenye Hadith. Lakini simulizi ya Ka’b ni upuuzi wa Kiyahudi, na inazidi kuwa bure zaidi kadiri muda unavyosonga mbele.

Baadaye katika mjadala huu, tutaonyesha taswira ya nafasi kubwa ya Ka’b, kuthibitisha jinsi alivyofanikiwa katika majaribio yake ya hatari.

Kwa masikitiko makubwa, Hadith hii kutoka kwa Ka’b kuhusiana na jua na mwezi kutokea Siku ya Kiyama kama mafahari wawili waliochanganyikiwa, ilipata njia ya kuingia kwenye vitabu vya Kiislamu kupitia kwa masahaba kama Abu Huraira na wengineo.

Haya yametokea licha ya makanusho ya hasira ya Ibn Abbas. Katika Tafsiir ya Ibn Kathiir na katika Kanzul Ummal, imesimuliwa kutoka kwa Abu Hurair kwamba:

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Katika Siku ya Kiyama, jua na mwezi vitakuwa katika moto wa Jahannam katika umbile la mafahari wa ng’ombe wawili waliochanganyikiwa.”

Mtu mmoja akamuuliza: “Lakini ni kwa dhambi gani walizofanya hadi kustahili adhabu hiyo?”

Abu Huraira akajibu vikali: “Mimi ninakusimulieni ambacho Mtume (s.a.w.w.) amekisema, na wewe unaniuliza mimi namna ya dhambi zao?”

Katika Hadith nyingine dhaifu kutoka kwa Anas, Ibn Kathiir anasimulia yafuatayo:
“Jua na mwezi vitakuwa katika moto wa Jahannam kama madume ya ng’ombe mawili yaliyochanganyikiwa.”

Maoni Yetu Juu Ya Haya Yaliyopita

Hadith hizi kutoka kwa Abu Huraira na Anas kwa kweli zinafanana, ni hiyo hiyo moja ambayo ilibuniwa na Ka’b al-Ahbar. Zimehusishwa kwa uwongo kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Kama tukiichunguza Ayah hii ya Qur’ani Tukufu na Hadith sahihi kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), tunakuta kwamba haditi hii ya Ka’b ni uzushi wa mawazo yake mwenyewe, zilizoegemea kwenye fikra za Kiyahudi. Baada ya kuthibitisha kwamba hadithi hii kutoka kwa Ka’b imehusishwa kwa Mtume kwa visingizio vya uongo na kwa msaada wa Ibn Abbas aliyeishutumu kwamba ni utomaji maneno (yasiyokuwepo) wa Kiyahudi, hayabakii mashaka yoyote kwamba chanzo cha hadithi hii ni Ka’b al-Ahbar mwenyewe na wala sio hawa masahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Hatari hii ilikuwa imetambuliwa na masahaba wa mwanzoni wa Mtume (s.a.w.w.). Ibn Abbas alikuwa miongoni mwa wale wa kwanza kusimama kidete dhidi ya mashambulio ya muingilio wa Kiyahudi, na Imam Ali (a.s.) vilevile alimuonya Khalifa Umar kuhusu jambo hili.

Kwa vile Ka’b hakuwa miongoni mwa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) hakuweza kuhusisha kiini cha imani yake ya Kiyahudi kwa Mtume mwenyewe moja kwa moja. Njia ya kufaa sana kwake ilikuwa ni kuandaa njia ambayo ingezichukua hadithi hizo kwa kutumia majina ya masahaba fulani fulani kama Abu Huraira na wengineo.

Ingawa ile hadithi kutoka kwa Anas imethibitishwa kwamba ni dhaifu, hadithi nyingine kutoka kwa Abu Huraira juu ya suala hilo hilo ilichukuliwa kama ni sahihi, na kwa hiyo ikatoa nguvu kwenye uzushi wa Ka’b. Ilikuwa ni juhudi ya pamoja, za makusudi kabisa au vinginevyo, za wale wanazuoni wa Kikristo na Kiyahudi waliosilimu, na masahaba kadhaa na wale ambao walifuatia zama za masahaba.

Kuenea Kwa Imani Za Kikristo Na Kiyahudi Miongoni Mwa Waislamu Kupitia Kwa Waislamu Wenyewe

Ili kuifanya hoja yetu ieleweke vizuri zaidi, tunatoa mifano miwili ya masahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), na vile vile nukuu kutoka kwenye mojawapo ya Tafsiir.

(1) Abu Huraira, Mmoja Wa Masahaba Wa Mtume (S.A.W.W.):

Historia imerekodi majina matatu tofauti ya sahaba huyu mmoja. Hata hivyo, yeye ni maarufu sana kwa Kuniyat yake ya Abu Huraira. Yeye alitokana na kabila la Dus, ambalo lilichipukia kutoka Yemeni.
Abu Huraira aliishi huko kwa miaka thelathini na aliwasili Madina baada ya vita vya Khaibar. Kwa mujibu wa Bukhari, Ibn Sa’d na wengineo, yeye alikuwa pamoja na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika ile miaka mitatu ya mwisho.

Lakini ukichukulia ule ukweli kwamba aliondoka kwenda Bahrain mnamo mwezi 8 Hijiria pamoja na jeshi lililoongozwa na Ala’ Hadhrami, jumla ya siku zake pamoja na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), ni dhahiri kwamba inakuwa ndogo zaidi.

Alikuwa akiishi pamoja na wale Waislamu masikini katika kishubaka cha jiwe kilichojulikana kama Suffah kilichokuwa kimekingama katika Msikiti wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Wakati Mu’awiyah alipomtuma yule muuaji muovu sana, Busr, ambaye alihusika na yale mauaji ya halaiki ya Waislamu thelathini elfu wasiokuwa na hatia, baina ya Syria na Yemeni, Abu Huraira aliteuliwa kuwa kama gavana wa Madina kwa baraka zake Busr.3 Halafu aliendelea kubakia na nafasi hiyo hiyo kwa muda fulani katika utawala wa Mu’awiyah.4

Hizi zilikuwa ndio siku za Abu Huraira ambazo alipata muda muafaka haswa wa kuzieneza hadithi zake. Baadhi ya masahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) walikuwa kwa kweli wanao ujuzi hasa katika sanaa ya kusoma na kuandika lakini kwa bahati mbaya, Abu Huraira alikuwa sio mmoja wao. Bukhari anamnukuu yeye akisema: Abdullah bin Amru Aas alikuwa anajua kuandika wakati mimi nilikuwa sijui.” Miongoni mwa watu ambao kutoka kwao yeye alipata faida za hali ya juu sana alikuwa ni Ka’b al-Ahbar ambaye alitoa sifa zifuatazo kwa Abu Huraira:

“Kati ya watu ambao hawakuwa wamesoma Taurati na bado wakawa na ujuzi na kuifahamu vizuri sana, Abu Huraira alikuwa ndio mbora wao.”5

Hii ni kusema kwamba, mbali na yule rabi (kiongozi wa dini ya Kiyahudi) ambaye bila shaka alikuwa ameisoma Taurati, Abu Huraira kwa umaarufu aliwapita wengine wote katika ujuzi wa Taurati. Cha kufurahisha vya kutosha, Ibn Kathiir ndani ya Tariikh yake anatoa maoni hivi:

“Abu Huraira alikuwa mdanganyifu, akichanganya kwa ulaghai kile alichokisikia kutoka kwa Ka’b na kile ambacho alikisikia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), bila ya kuyapambanua moja kutokana na jingine.”

Anaendelea zaidi kusema kwamba: “Wafuasi na marafiki zetu wanazitupilia mbali baadhi ya hadithi za Abu Huraira.”

Na vile vile anasema: “Wao hawakuweza kukubali kila hadithi ambayo ilisimuliwa na Abu Huraira.”6

Kipengele kinachouma sana ni kwamba Abu Hurair bila haya na hofu anasimulia hadithi mbili zinazopingana kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Bukhari ndani ya Kitab al-Tib anasimulia yafuatayo kutoka kwa Abu Huraira:

“Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: ‘Maradhi hayaambukizi au kuenea.’ Kisha Mwarabu mmoja akasimama kuuliza: ‘Ewe Mtukufu Mtume, tunao ngamia wazuri sana katika jangwa. Lakini pale mmoja wao anapopatwa na ugonjwa wa vidonda, wengine nao vile vile huwa wanaambukizwa.’ Mtume (s.a.w.w.) akauliza: ‘Huyo ngamia wa kwanza aliambukizwa vipi?’”

Baada ya kunukuu hadithi hii, Bukhari anaendelea kusimulia hadithi nyingine:

“Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ameagiza kwamba wale ambao wanaugua na wenye maradhi wasiwatembelee wale wenye afya njema.” Abu Salmah, ambaye ni binamu yake Abu Huraira akauliza: “Ewe Abu Huraira! Hivi wewe hukusimulia kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) hakuwa akiamini juu ya maambukizo?”

Katika kujibu, Abu Huraira alitoa matamshi fulani katika lugha ya Kihabeshi! Kisha yule binamu yake Abu Huraira akasimama kumtetea Abu Huraira kwa kusema:

“Sijawahi kamwe kumuona Abu Huraira akiwa msahaulifu isipokuwa kati ka tukio hili.”

Ni dhahiri kwamba, Abu Salma alikuwa akijaribu kuhalalisha ule upinganaji katika hadithi za Abu Huraira. Hata hivyo, msemo maarufu unasema hivi: “Pale mtu anapokuwa kama Abu Huraira, huyo huelekea kusahau.”

Abu Huraira Anakiri

Cha kushangaza ajabu ni kule kukubali kwa Abu Huraira mwenyewe kwamba amewahi kusimulia hadithi fulani fulani kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) bila ya kuwa amezisikia kutoka kwake.

Imam Ahmad Hanbal anasimulia tukio fulani ndani ya Musnad yake:

“…….. na Abu Huraira alisimulia hadith na wasikilizaji wake wakauliza: “Hii inatoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) au imetoka mfukoni mwako?” Abu Huraira akasema: “Hii moja makhsusi ni yangu mwenyewe kutoka mfukoni mwangu.”

Bukhari analisimulia tukio hili kama ifuatavyo:

“Abu Huraira aliulizwa: ‘Je hii uliisikia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.)?” Naye akajibu: “La hasha, hadithi hii ni yangu mwenyewe.”

Katika hadithi nyingine iliyosimuliwa na Imam Ahmad Hanbal, tunayakuta haya:

“Abu Huraira alisimulia Hadith kana kwamba ameisikia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), lakini mwishowe alikiri kwamba ilikuwa ni yake mwenyewe kutoka mfukoni mwake.”

(2) Abdullah Bin Amru Aas, Mtetezi Wa Hadithi Za Kiyahudi:

Abdullah bin Amru Aas (aliyefariki mnamo mwaka wa 65 Hijiria) anachukuliwa kama mmoja wa masahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), na kwa vile alikuwa amerithi hazina kubwa ya dhahabu ya Ki-Misri kutoka kwa baba yake, alijulikana kama mmoja wa matajiri wakubwa miongoni mwa masahaba. Yeye aliijua lugha ya Syria (Suryani), lugha asili ya Taurati.

Katika vita vya Yarmuk, yeye aliongoza jeshi la baba yake kama mshika bendera wake, na aliweza kuzitia mkononi shehena za ngamia wawili za vitabu vya Kiyahudi na Kikristo.7

Dhahabi anasema:

“Abdullah amesimulia kutoka kwa Watu wa Kitabu. Alivisoma vitabu vyao kwa mfululizo, na alionyesha upendeleo maalum juu ya vitabu hivyo.”

Ibn Hajar katika Sharhe yake juu ya Sahih Bukhari anasema:

“Abdullah katika mapambano ya Damascus alipata shehena ya ngamia mmoja ya vitabu vya Kiyahudi na Kikristo kama ngawira ya kivita. Alivisoma kwa uangalifu sana na akazitegemeza hadithi zake juu ya vitabu hivyo. Kwa sababu ya hili, watu maarufu wa kundi la Tabi’in (waliofuata baada ya masahaba) walijizuia kusimulia kutoka kwake.”

Katika Musnad ya Imam Ahmad Hanbal tunayakuta yafuatayo:

“Mtu mmoja alikuja kwa Abdullah na akasema: ‘Hebu niambie kile ulichokisikia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na wala usinisimulie zile hadithi kutoka kwenye Taurati na Injili.”

Katika hadithi nyingine tunasoma haya:
“Abdullah aliambiwa: ‘Hebu niambie yale uliyoyasikia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na wala usinisimulie yale uliyoyapata kutoka kwenye ile shehena ya ngamia wa Yarmuk.”8

Wanazuoni wa Hadith wa Kiislamu wamezitenga Hadith hizo kama ni za kiyahudi (Israiliyyat) – kwa sababu ya asili yao kutoka kwenye Taurati na vyanzo vingine vya Kiyahudi.

Katika lundo la Hadith zilizotwaliwa na wale Waislamu ambao hawatokani na madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.), tunazikuta Hadith nyingi zinazozungumzia juu ya Mwenyezi Mungu kuwa na mwili. Hizi ni dhahiri kabisa kwamba zinatoka kwenye vyanzo vya Kiyahudi na mara kwa mara tunakuta kwamba zimesimuliwa kutoka kwa Ka’b al-Ahbar au Abu Huraira. Tutakuja kuzijadili hizi kwa kina hapo baadaye.

(3) Maqatil Ibn Sulayman Balkhi:

Yeye huyu alikuja kutoka Balkhi. Aliachiwa huru na kabila la Azd, na akat- waa kuniyat ya Abul Hasan. Katika kuishi kwake mjini Basra na Baghdad, alisimulia hadithi kadhaa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.), na alikubalika kama mmoja wa wanazuoni maarufu wa elimu za Qur’ani Tukufu na ile madhehebu kinyume na ya Ahlul-Bayt (a.s.).

Miongoni mwa vitabu vilivyotungwa na yeye ni:

Tafsir Kabir – ambacho nakala ya mwandiko wa mkono bado ipo nchini Misri.

Nawadir ya Tafsiri

Al-Ayat al-Mutashabihat

Al-Nasikh wal Mansukh

Al-Qiraat

Al-Ashbah wa al-Nazair fil Qur’an al-Karim

Al-Jawabat fil Qur’an

Ibn Khaldun, katika kitabu chake cha wasifu cha Maqatil, anasimulia kutoka kwa Ibn Habban kwamba:

“Alikuwa akikubali ufafanuzi wa Qur’ani Tukufu kutoka kwa Wayahudi na Wakristo ambao waliitafsiri kwa mujibu wa vitabu vyao wenyewe!”

Na halafu anaendelea tena:

“Maqatil alikuwa miongoni mwa wale waliohusisha sifa za kibinadamu na namna ya kufanana (analojia) kwa Mwenyezi Mungu, na zaidi ya hayo, yeye alikuwa anadanganya wakati alipokuwa akisimulia Hadith.”9

Khatib Baghdadi katika historia yake – Taarikh Baghdad anasema:

“Siku moja, Muhammad bin Said Kalbi (aliyefariki 146 Hijiria) alitokea kupita karibu na Maqatil na akamsikia yeye akisimulia baadhi ya Hadith fulani fulani, akizihusisha kwa Kalbi mwenyewe. Hivyo akasema: ‘Ewe Maqatil! Mimi ndiye Muhammad bin Said Kalbi, na kamwe sijasimulia hadithi hizo ambazo umezitaja hivi punde hapa!”

Maqatil akasema:

“Tunazipamba hadithi zetu kwa majina ya wasimuliaji mashuhuri.”
Maqatil alikuwa na maana kwamba aliambatanisha majina ya wasimuliaji mashuhuri kwenye uzushi wake mwenyewe ili kwamba upate kusadikika!

Muhammad bin Said Kalbi vile vile anasimuliwa kuwahi kusema kwamba:

“Maqatil amezihusisha kwangu kwa uongo hadith ambazo sijawahi kuzitamka, na yeye amezijumuisha katika Tafsir yake.”

Khatib Baghdadi ndani ya maelezo yake juu ya Maqatil anasimulia tukio lililosimuliwa na watu wawili:

“Tuliuliza kutoka kwa Maqatil kuhusu chanzo cha hadithi yake moja mahususi, naye akasema: ‘Mimi niliisikia kutoka kwa Dhahhak.’ Baada ya siku chache tulipomuuliza tena kuhusu hadithi ile ile, yeye akasema: ‘Niliisikia kutoka kwa Ata.’ Katika wakati mwingine aliihusisha kwa Isa.

Baada ya kulisimulia tukio hili, Khatib Baghdad anasema kwamba mtu mmoja alimuuliza Maqatil kama aliwahi kumuona kamwe huyo Dhahhak, ambaye amedai kuwahi kumsikia. ‘Hakika ndiyo!’ Akasema Maqatil. ‘Kulikuwa na mlango uliokuwa umefungwa kati yangu na yeye.’”

Baghdad anaelezea kwamba kwa ile “mlango uliofungwa,” Maqatil alimaanisha lile lango kuu la jiji la Madina, kwa vile Dhahhak aliishi Madina na yeye Maqatil hajawahi kufika huko Madina kamwe.

Ibn Khallikan anasema:

“Dhahhak bin Mazahim, ambaye kutoka kwake Maqatil alisimulia hadith, alifariki miaka minne kabla yeye Maqatil hajazaliwa, na alizikwa ndani ya uwanja wa makaburi huko Madina!”

Zaidi ya hayo, yeye anaongezea:

“Maqatil alisimulia kutoka kwa Mujahid bila hata ya kuwa amewahi kuku- tana naye!”

Khatiib Baghdad ameandika kisa kifupi cha kuvutia sana (kinachomhusu Maqatil). Yeye anasema:

“Mtu mmoja alimuuliza Maqatil: ‘Rafiki yangu alitaka kujua rangi ya yule mbwa wa As’habul-Kahf. Mimi sikuwa na jibu la kumpatia.”

Maqatil mara moja akajitolea kujibu. Yeye akasema:

“Mwambie mbwa huyo alikuwa na madoadoa. Hakuna mtu atakayekanusha hili!”

Anaendelea kusimulia kutoka kwa Mansur na Mahdi, wale wafalme wa ki- Bani Abbas kwamba Maqatil wakati mmoja alijitolea kutunga hadithi chache za uongo katika kumsifu mhenga wao Abbas, kama wao wangependa hivyo. Wote wawili walimkatalia.10

Kwa kupitia vitabu kadhaa ambavyo ndani yake picha ya haraka ya maisha ya Maqatil imeonyeshwa, tunakuta mifano mingi ya uzushi na udanganyifu. Kuhitimisha, yeye alikuwa ni wakili madhubuti wa ile dhana ya kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa na umbo la mwanadamu.

Yeye alijifunza tafsiri ya Qur’ani Tukufu kutoka kwa washauri wake wa Kiyahudi na Kikristo na akazinakili imani zao katika kitabu chake juu ya Tafsir. Licha ya haya, inashangaza kweli kweli kuona kwamba wanazuoni kutoka madhehebu kinyume na ile ya Ahlul-Bayt (A.S.) wamemimina sifa nyingi juu ya Tafsir yake.

Ibn Khalidun anasema:

“Katika elimu ya Tafsir, watu wote ni wanyenyekevu kwa Maqatil bin Sulayman …!”

Mifano Ya Hadithi Zilizotengenezwa Na Maqatil, Katika Kuwaunga Mkono Makhalifa:11

Khatib Baghdad, katika kitabu chake kikubwa cha historia, Tarikh Baghdad, anasimulia kupitia nyororo inayoendelea ya wasimuliaji:

Maqatil amesema: “Dhahhak amenisimulia mimi kutoka kwa ibn Abbas kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alishauriwa na masahaba zake kumteua mrithi wa nafasi yake ili aweze kujulikana kwa watu, na kwamba watu watapeleka masuala yao kwake. ‘Hatujui ni nini kitakachotokea baada ya w e we kuondoka.’”

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akajibu:

“Kama ningeteua mtu ambaye angewaongozeni ninyi katika kumtii Mwenyezi Mungu, nanyi mkaacha kumtii yeye, basi mtakuwa mnapuuza maagizo yangu na yale ya Mwenyezi Mungu. Na kwa upande mwingine, kama mtu kama huyo aliyeteuliwa akawaelekezeni katika kufanya maovu na mkamtii, mtakuwa mmewekwa vyema Siku ya Kiyama kumtaja yeye kama mwenye uwezo wa kisheria. La hasha, mimi sitafanya kamwe jambo kama hilo – ni afadhali mimi nikawaacheni kwenye uangalizi wa Mwenyezi Mungu!”

Tathmini Ya Hadith Hiyo Hapo Juu:

Hadith hii ilibuniwa na Maqatil ili kuwaunga mkono Makhalifa ambao walidai kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) hakuteua mrithi yeyote wa nafasi yake, na kwamba haki ya uteuzi kama huo ilikuwa mikononi mwa umma wa Kiislamu.

Inapendeza kuona kwamba Khatib ameinakili hadith hiyo hapo juu kwenye kitabu chake cha wasifu wa Maqatil kuthibitisha kutoaminika kwake na udanganyifu wake. Anahoji kama Maqatil alikuwa na ujasiri wa kusimulia kutoka kwa Dhahhak bila ya yeye kukutana naye kamwe. Dhahhak aliishi Madina, ambapo Maqatil hakuwahi kusafiri kutoka Khurasan kwenda Madina. Ukweli ni kwamba Dhahhak alifariki miaka minne kabla Maqatil hajazaliwa!

Baada ya mfano huo hapo juu wa upenyezaji wa Kiyahudi na Kikristo katika imani za Kiislamu, tunaona inafaa kunukuu visa viwili vifupi kutoka kwenye Taurati. Hivi vitasaidia sana kwenye tathmini ya imani zinazashikiliwa na madhehebu kinyume na ile ya Ahlul-Bayt (a.s.), hususan kuhusiana na Sifa za Mungu.

1. Kuumbwa Kwa Adam

Katika Kitabu kile cha Mwanzo, Mlango wa Kwanza, mstari wa 27, tunasoma kama ifuatavyo:
“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu yeye alimuumba, mwanaume na mwanamke aliwaumba,”

Hadithi hiyo inaendelea kusema kwamba Adam na Hawwa waliwekwa katika Bustani ya Adeni. Halafu Mungu “akawapotosha”:

“Walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, usile: kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.11 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akawaambia: ‘Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.’

‘Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala,akam- pa na mumewe, naye akala. Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi.

‘Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone. ‘Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, uko wapi?

‘Akasema: Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekwambia ya kuwa u uchi? Je! umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale?’

‘Ndipo Adamu akaeleza yale ambayo yaliyotokea, hivyo Mungu akawaapiza Adamu, Hawwa na yule nyoka na akawalaani wao na vizazi vyao kwenye maisha ya kuhangaika, huzuni na kazi ngumu juu ya ardhi.

‘Bwana Mungu akasema, basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele. ‘….. Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Adeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.”11

2. Shindano La Mieleka Kati Ya Yakobo (Yaqu- Ub) Na Mungu:

Usiku mmoja, Yakobo alipigana mieleka na Mungu hadi kukacha, lakini Mungu hakufaulu kumshinda Yakobo!

“Yakobo akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri. Naye alipoona ya kuwa hamshindi….. akasema: ‘Niache, niende maana kumepambazuka.’ Akasema: ‘Sikuachi usiponibariki.’

‘Akasema: Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda… Na Yakobo akapaita mahali pale, Penueli, maana alisema, nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi yangu imeokoka.’”12

Maana Ya Visa Hivi Vifupi:

Kwa uwazi kabisa, Mungu wa Wayahudi ni wa kipuuzi na asiye makini. Analala na kama mwanadamu yeyote mbinafsi, anasema uongo na kudanganya!

Alimdanganya Adam pale alipomuonya asile kutoka kwenye ule mti kwa sababu ingeweza kumsababishia kifo; na alikuwa ni yule nyoka ndiye ambaye aliuondoa udanganyifu huo kutoka kwa Adam na akamlaghai yeye kula kutoka kwenye mti huo. Halafu Adam akawa kama mmoja wa miungu, anayeyajua mema na maovu, akijitambua kwamba alikuwa yuko uchi, alijificha mbele ya Mungu! Wote watatu, yule nyoka, Adam na Hawwa walilaaniwa na kuteseka na kazi ngumu juu ya ardhi!

Kwa mujibu wa Taurati, Mungu ana kiwiliwili; anatembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine, na anapigana mieleka na hawezi kumuona mtu anayejificha kutoka machoni Kwake!
Hizo ndizo hadithi za dhihaka za Taurati.

Athari Ya Jumla Ya Taurati

Tunaweza tukawagawanya watu walioathiriwa na upuuzi kama huo katika makundi tofauti yafuatayo:

1. Watu ambao walishtushwa kuona kwamba vitabu vilivyodhaniwa kwamba viliteremshwa kwa Mitume wakubwa kama Musa na Isa, amani juu yao wote, vilikuwa na makosa mengi sana na simulizi potovu na zisizo za kimaadili. Na kwa matokeo ya kupoteza imani kwao, walizitelekeza dini zote zilizofunuliwa na wakageuka kuwa wapenda anasa za dunia katika mwelekeo wao.

2. Kuna kundi jingine ambalo ni imara katika njia ya kidini waliyoichagua, licha ya kuangukia kuwa waathiriwa wa dhana hizi zisizo na maana.

Hawa wako katika vikundi vitatu:

A. Wayahudi

Wao wanahusika na upotoshaji na utomaji wa maneno ndani ya Taurati, na upotoshaji huo unaonekana katika mtazamo wao wa maisha na mwelekeo wao wa kitamaduni. Wanawafundisha watoto wao kufuata mbinu zile zile za ulaghai, kusema uongo na udanganyifu. Wanajiona wao wenyewe kuwa ndio wana wa Israeli, yule ambaye alipigana mieleka na Mungu na akashinda. La muhimu zaidi ya yote, wanachukulia wenyewe kama watu wateule, waliopewa kibali cha kufanikisha malengo yao kwa njia yoyote ile, ikiwa ni pamoja na hila na mauji ya halaiki. Zaidi ya hayo, kwa vile wanaamini katika wale mitume waporaji ambao “….waliaangamiza nafsi zote kwa ncha ya upanga, hata walipokuwa wamewaangamiza wote, wala hawakumsaza mmoja mwenye kuvuta pumzi …”13

B. Wakristo

Inaweza kudhaniwa bila wasiwasi kwamba kuhusisha umbile la kibinadamu kwa Mwenyezi Mungu, kama inavyohubiriwa na Taurati, iliwavutia Wakristo kuamini kwamba Mungu ni kama baba ambaye alijitwalia mwana.

Huko Ulaya, ambako wengi wao wameukiri Ukristo na lile Agano la Kale likakubaliwa kama kitabu cha kwanza ndani ya Biblia, kuzaliwa na kuenezwa kwa tamaa ya anasa za dunia kunaweza kuhusishwa na dhana zisizo na mantiki kama hizo, ambazo zilishindwa kuwavutia wasomi.

C. Waislamu

Miongoni mwa Waislamu, kulikuwa na madhehebu mbili. Moja ilikuwa na mwelekeo kwa Ahlul-Bayt (A.S.), ambapo ile nyingine ilikuwa inapingana nao hao moja kwa moja. Hawa wa mwishoni wanaweza wakaitwa madhehebu ya watawala au Makhalifa. Madhehebu haya ya Makhalifa yaliamini katika kuwepo kimwili kwa Mwenyezi Mungu, kitu ambacho chenye kufanana na umbo la mwanadamu. Ni dhahiri, wazo hilo lilikuwa limeazimwa kutoka kwa Wayahudi, kama tutakavyothibitisha katika milango ifuatayo, Inshallah.

Wakati dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu inapochafuliwa kwa lugha yenye maneno ya kufuru, tunaziona dalili za athari za uharibifu katika zile imani halisi. Mafundisho ya Qur’ani Tukufu yalikuwa ya maneno machache ya dhahiri, halisi na wazi, lakini kwa vile wanazuoni wa Kiislamu walianza kuwakubali wale wasimulizi wa ngano wa Kiyahudi na Kikristo kama wafasiri wa Qur’ani Tukufu, hata zile itikadi kuu za Tawhiid zilishushwa na kuwa kama mambo ya kukisia tu.

Kabla hatujaendelea na mada yetu kuu, tunadhani kuna umuhimu wa kujadili yale matumiziya maneno halisi na ya kiistiari.

 • 1. Tazama Tafsiir Ibn Kathiir, Juz. 4, uk. 17
 • 2. Tabari (Toleo la Ulaya), Juz. 1, uk. 62-63.
 • 3. Al-Gharaat, cha Thaqafi na vile vile Sharhe Nahjul Balaghah cha Ibn Abil Hadiid
 • 4. Musnad ya Ahmad Hanbal
 • 5. Tadhkiratul Huffadh cha Dhahabi
 • 6. Tariikh Ibn Kathir, Juz. 8, uk. 109.
 • 7. Usudul-Ghabah, Juz. 3, uk. 234 na Fat'hul-Bari, Juz. 1, uk. 166
 • 8. Musnad Ahmad Hanbal, Juz. 2, uk. 195, 202. 203, na 209.
 • 9. Wafayat al-A'yan
 • 10. Tarikh Baghdad
 • 11. Nukuu kutoka Kitabu cha Mwanzo; 3.
 • 12. Nukuu kutoka Kitabu cha Mwanzo; 32.
 • 13. Yoshua; 11: 14