read

16. Miongoni Mwa Maneno Yake (A.S)

Baada ya kufanyiwa Bai’a huko Madina, na katika khutba hii anawa- pa watu habari juu ya ilimu yake ya yale yatakayojiri.

“Mimi ni dhamana wa niyasemayo, nayo yapo juu yangu. Kwa kweli mwenye kudhihirikiwa na mazingatio ya adhabu ya waliopita1 iliyoko mbele yake taqwa itamzuia kujiingiza kwenye mambo yanayoshukiwa. Juweni kuwa balaa lenu limerudi katika sura yake ilivyo kuwa siku ambayo Mungu alimtuma Nabii wake (s.a.w).2

Naapa kwa ambaye alimtuma (Muhammad {s.a.w}) kwa ukweli mtachanganyikiwa vikali kabisa, na kutikiswa sana, na mtapigwa mfano wa mpigo wa chungu3 mpaka aje juu aliyekuwa chini kati yenu, na aliyekuwa juu kati yenu aende chini, na Wallahi watatangulia waliokuwa nyuma, watachelewa nyuma waliokuwa wametangulia.”4

“Wallahi sikuwahi kuficha neno,5 na mimi sikuwahi kusema uwongo na nilikwishapewa habari kuhusu hali hii na siku hii. Juweni kuwa makosa ni kama farasi aliyeasi (asiyepandika), wahusikao naye wamebebeshwa juu yake na akaondolewa hatamu zake na akawaingiza motoni.

Ala! Juweni kuwa taqwa ni mfano wa farasi aliyefundishwa, wamebebeshwa wahusikao naye juu yake na wakakabidhiwa hatamu yake na akawafikisha Peponi. Kuna haki na kuna batili, na kila moja ina watu wake, 6 endapo batili ikishika hatamu, na toka zamani imefanya hivyo,7 haki itaghilibiwa. Na haki inapokuwa ndogo, na imepata kuwa hivyo, ni mara chache kilichochelewa nyuma kuja mbele.8

Maelezo: Sayed Sharif alisema: kwa kweli ndani ya maneno haya machache kuna uzuri kuliko iwezavyo kutambuliwa, na kiwango cha kustaajabisha kilichochochewa nayo, ni zaidi kuliko utambuzi. Pamoja na hali tuliyoieleza muna ufasaha wa hali ya juu usiowezakufikiwa na mwingine. Na hawezi kuyatambua nisemayo isipokuwa mwenye kuwa na uelewa wa fani hii na kujuwa ilivyo. (Na hawaifahamu ila wenye ilimu; 29:43)

Na Miongoni Mwa Yaliyo Katika Khutba Hii

“Ameshughulishwa ambaye pepo na moto vi mbele yake! Mwenye juhudi na kuharakia atafaulu, na mtafutaji goigoi atakuwa na matumaini, mwenye kuzembea ataangamia motoni. Kulia na kushoto ni njia za upotofu, na njia ya kati ndio njia ya sawa, juu yake kuna Kitabu cha Milele na athari ya Nabii, na humo ndio mapitio ya Sunna na kwayo ndiyo hitimisho la matokeo.”

Mwenye kudai kinyume ameangamia na mwenye kuzua amepata hasara. Mwenye kukengeuka kwa uso wake ameangamia. Na yatosha mtu kuwa mjinga kwa kutojua hadhi yake.

Hatoangamia aliyethibiti katika maoteo ya Uchamungu, wala mimea ya watu iliyo kwenye maoteo ya uchamungu haitokosa maji. Hivyo basi jisi- tirini majumbani mwenu, jirekibesheni wenyewe. Toba iko nyuma yenu, yampasa mtu kuhimidi asimhimidi ila Mola wake tu. Na mwenye kulaumu asilaumu ila nafsi yake.

  • 1. Yaani mwenye kudhihirikiwa na uelewa wa hali ya waliopita kabla yake na akathibitiki- wa na mazingatio na kuonyeka kuwa adhabu iliowashukia watu wa Umma na vizazi na mtu mmoja mmoja kama kupatwa na unyonge, udhalili, ufakiri na hali mbaya atatambua kuwa yaliletwa na matendo yao ya dhulma, uadui na ujinga, waliojivika na kuharibika kwa hali, taqwa ambayo ni kujihifadhi asiingie kwenye mambo yaliyosababisha adhabu hizo kwa wahusika itamzuia asijiingize kwenye mambo yanayoshakiwa na kuporomokea humo. Kwa sababu mambo yanayo shakiwa ni dhana ya dhanio la makosa na makosa ndio yaletayo adhabu.
  • 2. Balaa na tabu ya Waarabu iliokuwa imewazunguka siku ambayo Mungu (s.w.t) alimtuma Nabii wake Muhammad (s.a.w.w) ni balaa la mfarakano na shida ya mtawanyiko, kwa vile walikuwa wanabughudhiana wenye kuchukiana kila mmoja anashikilia upendeleo wa kabila, ukoo wake, na hunadi kwa moto au kaulimbiu ya ndugu zake wa karibu. Baadhi yao wanakata shingo za wanzao. Hiyo ndio hali iliyoangamiza umma mbali mbali. Sasa wamekuwa katika hali hiyo baada ya kuuliwa Uthman, hali ambayo imeleta uadui ambao dini ya Kiislamu ilikwisha uuwa, kukaibuka moyo wa uadui kati ya Bani Ummayah na Bani Hashim, na wafuasi wa kila upande, walaa haula walaquwata illa billahi.
  • 3. Mpigo wa chungu: Yaani kama zinavyochanganyika, kokwa au nafaka, na mfano wake katika chungu; wakati wa kuchemka, ya juu huenda chini na ya chini huja juu, na huo ni mfano wa jinsi watakavyokuwa katika tofauti, na kutengana kwa udugu wa damu na kuharibika kwa nidhamu.
  • 4. Kutangulia waliokuwa nyuma ni mfano wa Muawiyah kunyakua na kupanda kwenye jukwaa la Ukhalifa, hali ilikuwa hatazamiwi wala hakudhaniwa kuwa angelifikia Ukhalifa, na walichelewa watu wa nyumba ya Nabii kuufikia Ukhalifa hali walikuwa ndio wataraji- wa wa kwanza.
  • 5. Alikuwa (a.s) hafichi kila kitu kinachompitia nafsini mwake, alikuwa muamrishaji wa mambo mema, na mkatazaji wa maovu, hapendelei, haendekezi mtu, hasemi uwongo. Na sehemu hii ni maandalizi ya usemi wake: “Nilikwishapewa habari kuhusu nafasi hii,” yaani alipewa habari na Nabii (s.a.w.w.) kuwa atakuwa katika hali hii na atajiwa na siku mfano wa siku hii.
  • 6. Yaani: Jinsi mwanadamu ambavyo haepukani na mambo mawili, haki na batili, ulimwengu hauwi bila ya hayo mawili; Na kila moja kati ya mawili hayo lina watu wake, haki ina watu wake na batili ina watu wake.
  • 7. Na endapo batili itakithiri kwa kukithiri wasaidizi wake, na hilo limekuwa toka hapo zamani kwa kuwa macho yaliyopotoka mbali na ukweli ni mengi kuliko yaliyothibiti juu ya ukweli. Japo ukweli uwe kidogo kwa uchache wa wasaidizi wake, huenda uchache wake ukashindwa na wingi wa batili na huenda batili ikazidi nguvu ukweli na kuutokomeza.
  • 8. Neno hili, limekuja kutokana na kuchukizwa kwake (a.s.), hivyo, ameona ni vigumu kurejea dola ya kaumu baada ya kuwatoka, na kwenye maana hii amesema mshairi: “Wamesema, maji hurudi mtoni baada ya kunyauka mimea na kukauka mifereji. Nikasema; mpaka mto urejee kukimbia! na majani yaote pembezoni mwake! Wanakufa vyura.”