read

2. Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Baada Ya Kutoka Kwake Siffiini

Namuhimidi yeye (s.w.t.) nikiomba utimilifu wa neema Zake, na kusalimu amri kwa utukufu Wake, na kujihifadhi na maasi yake, Namwomba msaada nikiwa mwenye haja ya toshelezo Lake: Kwa hakika hapotei aliyemwongoza, wala hajinasui mwenye kumfanyia uadui.

Wala hawi fukara mwenye kutoshelezwa na yeye. Kwani kumhimidi ni kuzito mno katika mizani na ni hazina bora. Na ninashuhudia kuwa hapana mungu isipokuwa Allah, Peke yake hana mshirika, ushuhuda uliotihaniwa wenye ikhilasi hali ya kuitakidi uhalisi wake.

Tunashikamana nayo shahada milele kwa kadiri atakavyotubakisha, na tunaihifadhi kwa ajili ya hofu itakayotupata, kwa sababu ni azma thabiti ya imani, na ni ufunguo wa mema na radhi ya Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, na ni sababu ya kuwa mbali na Shetani.

Na ninashuhudia kuwa Muhammad ni mja Wake na mjumbe Wake, amemtuma na dini mashuhuri, na sheria iliyonukuliwa, na Kitabu kilichoandikwa, na nuru yenye mwanga, mwanga wenye kuangaza, na amri iliyo wazi, ili kuondoa shaka, na kutoa hoja kwa ubainifu, na kutahadharisha kwa alama, na kuhofisha kwa adhabu.

Na watu wapo katika fitna ya moja kwa moja. Kuna kamba ya dini, na nguzo ya yakini imetetereka, Misingi imetofautiana, mambo yalikuwa yamevurugika, njia ya kujinasua ilibana. Upenyo uliingia giza, mwongozo ulikuwa haujulikani, upofu ulienea.

Mungu mwingi wa rehema walimuasi, Shetani akanusuriwa, imani ilitelekezwa, kwa hiyo nguzo zake zikaporomoka. Mafunzo yake yakabadilika na njia mitaa yake iliharibika.

Walimtii Shetani wakafuata mwenendo wake, wakapita mapito yake, kwao wao alama zake zilipita, bendera yake ikasimama katika fitina, iliyowakanyanga kwa kwato zake, hivyo wao wamepotea wanatangatanga, wajinga wamefitiniwa, wakiwa ndani ya nyumba bora na majirani waovu.1Usingizi wao ni kukesha, na wanja wao ni machozi.2

Hali ya kuwa wako katika ardhi ambayo mwanachuo wake huzibwa kinywa,3 na jahili wake huheshimiwa.4

Ndani ya khutba hii pia aliashiria kwa aali zake Nabii alayhi Salaatu Wassalaamu: Wao ni mahali pa kuweka siri yake, kimbilio la mambo yake, chombo cha ilimu yake. Marejeo ya hekima zake, pango la vitabu vyake, (mahali pa kuhifadhia vitabu) na milima ya dini yake, kupitia kwao Mungu amenyoosha mgongo,5 mgongo wa dini yake, na aliondoa mtetemeko wa viungo vyake.6

Na akawakusudia watu wengine (wanafiki): Waliupanda uovu na wakaunyweshea kwa hila na walivuna maangamizi,7 Aali Muhammad (a.s) Hawalinganishwi na yeyote kutika Ummah huu, wala hawawi sawa kabisa nao ambao neema zao zimepitia kwao. Wao ndio msingi wa dini, na nguzo ya yakini. Kwao hurejeshwa mwenye kuvuka mpaka, na kwao huunganishwa aliyeachwa nyuma.8

Haki ya uongozi ni mahususi kwao. Na kwao kuna wasia na urithi; hivi sasa wakati haki imerejea kwa wenyewe, na inahamishiwa mahala penyewe!

  • 1. Nyumba iliyo bora ni: Makkah. Na jirani waovu: ni waabudia masanamu miongoni mwa makuraishi.
  • 2. Usemi wake: “usingizi wao ni kukesha, na wanja wao ni machozi” ni kama vile mtu aseme: “ukarimu wao ni ubakhili, na amani yao ni khofu”, yaani lau Muhammad angewaruhusu walale wangebakia bila usingizi badala ya kulala, na lau angewafanya wapake wanja, wanja wao unge kuwa machozi, au wao watakuwa katika matukio ambayo yatawabadilishia usingizi kwa kukesha na wanja kwa machozi.
  • 3. Kauli yake: “kwenye ardhi mwanachuo wake hufungwa kinywa”, yaani, mwenye kutambua ukweli wa Muhammad (s.a.w.w.) na kumwamini, anakuwa katika hali ya taqiyah na woga; kwa kuwa yeye lau atasema ukweli hali jamhuri iko katika batili wangemuuma meno.
  • 4. “Jahili wake huheshimiwa”, yaani, mwenye kuupinga unabii wake na akamkadhibisha, anaenziwa na kulindwa; kwa sababu yeye yupo kama walivyo jamhuri, anakwenda pamoja nao katika utashi wao wa nafsi, daraja yake kwao ni daraja ya dhana zao na ada zao, nazo zikatika daraja la juu nafsini mwao. Na sifa hizi zote ni kuipa taswira hali ya watu katika jahili ya kabla ya kutumwa nabii (s.a.w.w.).
  • 5. Kupinda mgongo ni kinaya cha udhaifu na kuondoa kupindika ni kinaya cha kurejea nguvu ya dini.
  • 6. Ameondoa tetemeko la kiungo chake, farisa ni nyama kati ya upande wa ubavu na bega la mnyama, na kupinda kwa mgongo ni kinaya ya kudhoofu, na kunyoosha ni kinaya ya nguvu, na kwa wao yapatikana amani mbali na khofu, ambayo hutetemesha farisa.
  • 7. Amejaalia waliyoyatenda miongoni mwa maovu ni mfano wa mmea walioupanda, na kutulia kwa nafsi zao kwa kutokuwa na hima na kughurika kwao na hali hiyo ni sawa na kunyeshwea: kwa sababu kughurika kunapelekea kudumu kwa uovu na kuzidi, kisha matokeo ya jambo lao ni haya maangamizi.
  • 8. Anakusudia kuwa sera yao ni Siratud-Din al-Mustaqim, hivyo basi mwenye kuvuka mipaka katika dini yake, wokovu wake ni kurejea kwenye sera ya kizazi chake Mtume, na wajifunike kwa kivuli cha wataalamu wake. Na usemi wake (na kwa wao huunganishwa aliyeachwa nyuma) anakusudia kwamba mwenye kuzembea katika matendo yake, goigoi katika sera yake - ambaye ametanguliwa na waliotangulia - anatamani kujinasua kwa kuinuka ili aungane na kizazi cha nabii na afuate mwendo wao, yaani, yeye Ali (a.s.) amewafanya wao kama kundi la farasi linalotembea kwenye jangwa ambalo wengine ambao wako mbali nalo wapaswa kuungana nalo.