read

5. Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Alipofishwa Mtume wa Mungu (S.A.W.W.):

Abbas na Abu Sufyan bin Harb walimsemesha Ali (a.s) kuwa wamfanyie bai’a ya ukhalifa, ndipo aliposema (a.s): “Oh! ninyi watu; yapasueni mawimbi ya fitna kwa merikebu za uokovu, na jiepusheni na njia za chuki, vueni taji za fahari, atakuwa amefanikiwa mwenye kuinuka na bawa,1 au asalimu amri akapumzisha (akapumzisha nafsi yake au wengine wakabaki salama).

Ni maji machafu,2 na ni tonge limkwamalo mlaji wake, na ni sawa na mchuma matunda kabla ya wakati wa kupevuka kwake,3 na ni sawa na mkulima wa ardhi isiyo yake.

Nikisema mimi watasema: Amepupia ufalme, na nikinyamaza watasema: Amekuwa si mvumilivu wa umauti! haiwi baada ya kale (kafupi) na huyu (mrefu)!4 Wallahi mwana wa Abi Talib ni mchangamfu mno wa mauti kuliko mtoto mchanga anavyochangamkia ziwa la mama yake, isipokuwa nimezingirwa ndani ya ilimu iliyositiriwa, lau ningeifichua mngetetemeka mtetemo wa kamba ya kisima cha ndoo katika kisima kirefu.

  • 1. Atakuwa amefanikiwa mwenye kuinuka na bawa: yaani atakuwa ame fanikiwa mwenye kuutafuta uongozi akiwa na msaidizi wa kumsaidia na wanusuru wapiganao mbele yake.
  • 2. Maji machafu: anaishiria kwenye ukhalifa, yaani kwa kweli kuwaongoza watu na kutawalia mambo yao ni miongoni mwa mambo hayamuwii vyema mwenye kuyatawalia, bali hilo ni jambo linashabihiana na kuyatumia maji machafu, matokeo yake hayamfaidishi, ni kama tonge linalomkwama mlaji wake na kufa nalo.
  • 3. Mchuma matunda kabla ya kupevuka: Anaishiria kuwa wakati ulikuwa si muwafaka kulitaka suala lile la (ukhalifa) kwa hiyo lau angesimama kwa ajili hilo angekuwa kama mchuma tunda kabla halijapevuka kwa hiyo hafaidiki na alichochuma, kama ambavyo aliyelima kwenye ardhi isiyo yake hanufaiki na kazi aliyoifanya.
  • 4. “Baada ya kale na huyu” Baada ya kuwa nimeyakabili mambo yakutisha makubwa na madogo, na nimepatwa na kila aina ya masaibu makubwa na madogo, kwa hiyo Kale ni ishara ya msiba mdogo na Huyu ishara ya msiba mkubwa. Na chimbuko la methali hii katika kiarabu, yasemekana mtu mmoja alioa mwanamke mfupi mwenye tabia mbaya kwa hiyo maisha yake na yule mwanamke yalikuwa katika shida na mashaka, baadaye alimtaliki na akaoa mwingine mrefu, taabu na mashaka yake ikawa zaidi, akamta- liki na akasema: “sitoowa baada ya kale kafupi na huyu mrefu” tokea hapo ikawa methali katika shida na masumbuko, makubwa na madogo. Na kauli yake (Hay haata): ni kanusho ambalo wangedhania kuwa kunyamaza kwake yu ahofia mauti.