read

100 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Kumhusu Mtume Wa Mungu Na Ahlul-Bayt Wake

“Mstahiki wa sifa ni Allah Mwenye kueneza fadhila Zake kwa viumbe, na Mwenye kuwanyooshea mkono wake wa ukarimu. Tunamtukuza katika mambo Yake yote, na tunamuomba msaada ili kuzichunga haki Zake.

Na tunashuhudia kuwa hakuna mungu mwingine, isipokuwa Yeye na kuwa Muhammad ni mja Wake na mjumbe Wake, amemtuma kudhihirisha amri Yake na kuitangaza, na awe mwenye kutamka utajo Wake.

Na alitekeleza kwa uaminifu, na alifariki akiwa ndani ya uongofu; na alituachia bendera ya haki,1 mwenye kuitangulia atakuwa ametoka,2 na mwenye kubaki nyuma yake atakuwa amenyauka, na mwenye kujiambatisha nayo atakuwa amejiunga na haki.

Dalili yake ni umakini wa usemaji,3 asimama taratibu, ana haraka akienda. Hivyo basi endapo ninyi mtamlainishia shingo zenu (yaani mkimtii), na mkamuishiria kwa vidole vyenu, 4mauti itamjia na itaenda naye, na mtabaki baada yake ma’sha’Allaahu, mpaka Mungu amtoe kwa ajili yenu mmoja ambaye atakukusanyeni, na kuuweka pamoja mparaganyiko wenu, msimtumainie asiyekuja wala msikate tamaa na aliyegeuza mgongo5kwa kuwa aliyegeuza mgongo huenda ukamteleza mguu wake mmoja, na ukathibiti mwingine, na ikarudi miwili mpaka ikathibiti yote.
“Juweni! Kuwa mfano wa Aali Muhammad (s.a.w.w.), ni mfano wa nyota za mbinguni, ikizama nyota yachomoza nyota. Kama kwamba neema za Mungu zimekukamilikieni, na amekuonesheni kile mlichokuwa mwakitarajia.”6

  • 1. Bendera ya haki ni: Vizito viwili vilivyoachwa baada ya Mtume (s.a.w.w.) navyo ni Kitabu cha Mwenyeezi Mungu na Itrah ya Nabii (Ahlul-Bayt).
  • 2. Ametoka: Mwenye kuitangulia bendera ya haki atakuwa ametoka nje ya dini. Na aitanguliaye bendera ya haki ni yule ambaye anayeongeza juu ya sharia aliyoiweka Mungu, matendo au itikadi, akidhania kuwa anaipamba dini, na anaikamilisha, na yu anaiita ziada hiyo aliyoiongeza kwa jina la: Bid’atun hasanatun.
  • 3. Umakini wa usemaji: Yaani anajikusudia yeye mwenyewe (a.s.), yaani polepole, anachunga katika usemaji wake, haharakii bila kuzingatia, na maana inakuwa ni mwenye upole na kuzingatia, kisha alitilia mkazo kwa kauli yake: ‘anasimama polepole’ na akienda anaharakisha. Hivyo yeye haharakishii kutenda jambo kwa fujo ila akiona kwamba kuna njia ya ufanisi anaendelea haraka, hiyo ni kama kwamba anajisifu mwenyewe, Karamallah Wajihahu.
  • 4. Kumuishiria kwa vidole:Yaani mkimheshimu na kumtukuza kama mfalme ambaye huoneshwa kwa kidole wala hasemeshwi kwa ulimi.
  • 5. Yaani afapo huyu kiongozi na kuwaacha wanawe (baada yake) jambo la mmoja wao likayumba, msikate tamaa na kuingiwa na mashaka na mseme: “Huenda tumekosea kuwa- fuata hawa jamaa;” kwa kuwa mwenye kuyumba mambo yake katika sisi miguu yake itaku- jathibiti, na ikiwa mmoja kati ya miguu miwili utateleza, mwingine utathibiti na kuufanya ulioteleza uthibiti pia.
  • 6. Mungu aliwaahidi kuwa faraja ipo karibu, na huu ni mfano wa ahadi za kiungu kuwa saa (kiyama) ikaribu. Kwa hakika vitabu vilivyoteremshwa vyote vimesema waziwazi ukaribu wake, japo kwetu kiko mbali, kwa kuwa la mbali (kwetu) katika elimu ya Mungu ni karibu: “Innahum yaraunahu ba’ida wa narahu kariba.” (Hakika wao wanaiona iko mbali, na sisi tunaiona iko karibu 70:6 -7).