read

101 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Nayo Ni Khutba Mojawapo Ambayo Ndani Yake Kuna Maelezo Ya Mapambano Ya Kivita

“Mstahiki wa sifa ni Mungu ambaye ni wa mwanzo kabla ya chochote. Na wa mwisho baada ya kila kitu. Na kwa umwanzo Wake imelazimu iwe hakuna kilichomtangulia. Na kwa umwisho wake imelazimu iwe hakuna wa mwisho ila ni Yeye. Ninashuhudia kuwa hapana mungu ila ni Allah (tu) wazi wazi na kwa siri, kwa moyo na kwa ulimi.

“Enyi watu! Kunikhalifu kwenu na kuniasi kusiwafanye mnikadhibishe, wala msishawishike kuniasi, wala msikonyezane kwa macho mnaponisikiliza.

Ninaapa kwa ambaye ameipasua mbegu na kumuumba mwanadamu kuwa ambayo nimewaambieni ni kutoka kwa Nabii Al’ummiyyi (s.a.w.w.), Wallahi mfikishaji hakusema uwongo, wala msikilizaji hakuwa mjinga.1

Kana kwamba namuona na namuangalia mpotovu mno2 amepiga kelele Sham (Syria) na amesimika bendera zake mpakani mwa Kuufani - (ni jina la mji wa Kufa) - afunguapo kinywa chake na kushika kasi ukaidi wake na ujeuri (yaani dhulma) wake ardhini kuwa nzito, fitna itawang’ata watu kwa meno yake, na vita mawimbi yake yatachafuka, na siku zitadhihirisha kisir- ani chake, (zitakuwa ngumu) na usiku taabu zake.

Matunda yake yakipevuka, na akianza kuyachuma, na ngamia kuunguruma, na mikuki na panga kumwetuka, fitna korofi itachukuwa nafasi, na itakuwa kama usiku wa giza, na bahari yenye kupigapiga mawimbi yake.

“Hii ni mara ngapi mji wa Kufa unaharibiwa na dhoruba, na kupitiwa na kimbunga. Hivi punde karne itapambana na karne,3 mazao yaliyosimama yatavunwa na yaliyovunwa yataharibiwa!”4

  • 1. Mfikishaji na msikilizaji ni yeye mwenyewe (a.s).
  • 2. Mpotovu mno ni: Mwenye kukithiri upotovu, na hapa ni kinaya yamaanisha Abdul Malik bin Marwan; kwa kuwa sifa hizi zakamilika kwake kuliko kwa mwingine.
  • 3. Karne kupambana na karne ni kinayah - yaani dola ya Bani Abbasi itakapojipatia ushindi itakapo pambana dhidi ya dola ya Bani Umayyah. Na karne mradi wake hapa ni kizazi katika watu, mapambano yalikuwa kati ya viongozi wa fitna na watu wa haki, kama wanavyopambana beberu kwa pembe zao wanapoparurana, na wema uliobaki ulivunwa, na uliokwishavunwa ulivurugwa na kuharibiwa na wala haitobakia ila ni shari ya jumla na balaa kamili endapo haki haikupata wakuinusuru.
  • 4. Ni kinaya, yamaanisha kuuliwa kwa watawala katika Bani Umayyah vitani, kisha kuuliwa mateka katika wao, hali ni kama hivyo ilijiri kwa Abdullah bin Ali na Abil’Abbas Assafahi.