read

102 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A .S)

Kuhusu Maudhui Ileile Ya Siku Ya Kiyama

“Hiyo ni siku ambayo Mungu atawakusanya waliokuwa kwanza na wa mwisho ili kudodosa hesabu, na kulipwa aamali, wakiwa wanyenyekevu, wamesimama, jasho limewafunga hatamu.1
Na ardhi ikawatetemesha,2 basi mwenye hali nzuri katika wao ni mwenye kuipata nafasi kwa ajili ya nyayo zake, na wasaa kwa yeye kuweza kupumua.”

Na sehemu ya khutba hiihii kuhusu taabu za Siku ya Kiyama.

“Ni fitna kama giza la usiku, hakuna kikundi kitachosimama kupambana nayo wala bendera zao kurudishwa nyuma. Atakujieni (hiyo saa) mfano wa ngamia aliyetayari akiwa na hatamu yake na zana zake, muongozi wake yuamhamasisha,3 na mpandaji wake anambidiisha,4 watu wake wachocheao vita - mashambulizi yao ni makali, uporaji wao ndio kidogo.5 Wanaopigana vita katika njia ya Mungu ni kaumu dhalili mbele ya wenye kiburi,6 wasiojulikana aridhini, na maarufu mbinguni. Ole wako ewe Basrah, pindi kipigo cha adhabu ya Mungu kitapokuangukia! Hakina vumbi wala sauti, watu wako watakabiliwa na umauti mwekundu na njaa yenye rangi ya vumbi.”7

  • 1. Jasho limewafunga hatamu: Yaani jasho limewatiririka mpaka kufikia eneo la hatamu kwa mnyama; nalo ni mdomo.
  • 2. Ardhi kuwatetemesha: Ni kwamba ardhi itatikisika na kuyumba nao.ya msafara.
  • 3. Yaani anamsukuma kumuhimiza aingiye kwenye nyumba zenu,na kwenu ndio mafikio
  • 4. Anambidiisha: Anampeleka mwendo zaidi kuliko uwezo wake, na makusudi ni kuwa watu wa fitna wanajitahidi kuchochea moto wake, wakiwa na askari waendao kwa miguu na wapanda farasi, kwa hiyo waenda kwa miguu amemkusudia kiongozi, na wapanda farasi, amekusudia wapandao farasi miongoni mwa askari.
  • 5. Uporaji wao ni mdogo:Yaani kichukuliwacho na muuwaji katika nguo za aliyeuliwa na silaha yake katika vita, yaani si miongoni mwa matajiri.
  • 6. Ni sifa ya waumini.
  • 7. Umauti mwekundu: Ni kinaya mradi wake ni janga na njaa, na limeitwa mauti mekundu kwa sababu ya ukali wake, na njaa imeelezwa kuwa ni ya rangi ya vumbi ni istiari ya ukame, kwa sababu mwenye njaa anaoiona pambizo kana kwamba ina vumbi na giza. Na njaa ya rangi ya vumbi: Ni kinaya ya mahali na ukame.