read

105 - Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Kuhusu Baadhi Ya Sifa Za Nabii Mtukufu Na Kemeo Kwa Bani Umayyah Na Mawaidha Kwa Watu:

“Kisha Mungu alimtuma Muhammad (s.a.w.w.) ili awe shahid 1 na mbashiri na muonyaji, ni mbora katika viumbe akiwa mdogo, na mwenye heshima mno akiwa mtu mzima, na msafi mno katika wasafi wa tabia, na ni mkarimu mno kwa wenye kumuomba.2

Dunia haikuwa tamu katika ladha yake kwenu. Wala hamkuweza kunyonya chuchu zake ila mlipokuta hatamu zake zimelegea.

“Kisha alisema kuwa wao wameikuta dunia kwa bahati imekwisha kuwa ngumu kwa atakayeitawalia utawala wa haki kama anavyokuwa mgumu ngamia kwa mpandaji wake endapo hatamu yake itajikusanya, haudaji yake haitulii kwa mpandaji, haramu zake zapatikana kiurakhisi kwa aipendaye.

Ni mfano wa mti wa msidiri uliokatwa miba yake, kwa hiyo ukawa laini wateleza; na halali zake hazipo tena kwa kushindwa na haramu; na kwa kuwa umezagaa umechukua nafasi kulingana naye; na hii ni ishara kwenye aliyokuwa akiyasema daima kwa kujitwalia kwao binafsi suala la ukhilafa makhalifa waliomtangulia mbali naye, kuwa yeye alikuwa msitahiki.

“Kunyonya kiwele chake ila baada ya kumkuta kwa bahati hatamu yake ya puani inajiburura na ukanda wake wa ngozi umelegea. Uharamu wake umekuwa kwa kaumu ya watu kama msidiri ulionepa (kwa uzito wa matunda) hali ikiwa uhalali wake ni mbali, haupo.

Wallahi, mngeikuta kama kivuli kirefu, mpaka muda uliopangwa.

Kwa hiyo ardhi kwenu ni tupu,3 na mikono yenu humo imekunjuka, na mikono ya viongozi imefungwa mbali nanyi. Panga zenu zimewadhibiti4 na panga zao zimezuilika dhidi yenu.5

Jueni kuwa kwa kila damu iliyomwagwa ina kisasi, na kila haki ina mdai, na mdai kisasi wa damu yetu ni sawa na hakimu anayetoa hukumu kuihusu haki yake binafsi,6 huyo ni Mungu ambaye hamshindwi amtakaye, wala hamkosi atakayemkimbia.

Namuapa Mungu Enyi Banii Umayyah! baada ya muda mfupi mtaiona nafasi yenu ikiwa mikononi mwa wengine, na nyumbani mwa adui yenu! Jueni kuwa macho yaonayo sana miongoni mwa macho ni yale yaliyopenya kuiona kheri! Jueni kuwa masikio sikivu ni yale yaliyoelewa mawaidha na kuyakubali!”7

Kuhusu Shughuli Za Imam

“Enyi watu, chukueni mwanga kutoka mwenge wa taa ya muwaidhi mwenye kuwaidhika,8kunyweni na chukueni maji kutoka chemchemi iliyohifadhiwa na kusafishwa bila uchafu.9

“Enyi waja wa Mungu! Msiutegemee ujahili wenu, wala msiutii utashi (mbaya) wa nafsi zenu kwa kuwa yule mwenye kuwasili kwenye nyumba hii10 yupo kwenye ukingo wa kuzolewa na maji yazoayo kila uchafu11 ananakili12 maangamizi mgongoni kwake kutoka sehemu (ya mgongo) mpaka sehemu, kwa rai aizushayo baada ya rai; anataka kuambatanisha kisichoweza kuambatana, na kukisogeza karibu kisicho weza kusogea! Ala ala muogopeni Mungu msimlalamikie huzuni zenu yule asiyeweza kuzitanzua, wala hawezi kutangua kwa rai yake lililo lazima juu yenu.

Na kwamba si juu ya Imam isipokuwa alilobidiishwa miongoni mwa amri za Mola Wake Mlezi: Kufikisha mawaidha, na kujitahidi kutoa nasaha, na kuihuisha Sunnah, na kuitekeleza adhabu kwa wanaostahili, na kuzirudisha hisa kwa wenye kustahiki. Hivyo basi harakishieni elimu kabla ya mmea wake haujakauka, na kabla hamjashughulishwa na nafsi zenu mbali na wenye kuwa nazo. Katazeni maovu na wenyewe muwe mmejikataza, mlichoamriwa ni kukataza baada ya kujikataza!

 • 1. . Maana ya kuwa shahidi ni: Yeye atatoa ushahidi nini umma ulichofanya kati ya utii au maasi.
 • 2. Yaani Nabii (s.a.w.w.) ni mwenye kheri nyingi mno kati ya watu kwa wamuombao, anasema Amirul-Mu’minina (a.s) akiwasemesha watu wa zama zake miongoni mwa masa- haba waliobaki na watu wengine miongoni mwa taabiina ambao hawakuwa zama za Mtume (s.a.w.w.): Kuwa Mungu (swt) alimtuma Muhammad, akiwa mwenye heshima sana katika watu kwa tabia, na mwenye mkono wa ukarimu mno, na mbora kati yao akiwa mtoto na mwenye heshima akiwa mtu mzima. Hivyo anakuwa Mungu amemhifadhi siku za maisha yake ili amfungulie dunia, alimpa heshima kwa ajili hiyo, kwa hiyo nchi hazikukombolewa, wala haikupatikana mali kwa wingi,wala dunia haikuelekea upande wenu; wala dola hazikuwa chini yenu isipokuwa baada yake. Hivyo mliweza kuila na kustarehe nayo, kama awezavyo mkamaji kumkama ngamia, na ladha yake kuwa tamu kwenu na maisha yamekuwieni mema na mmeyakuta mazuri yenye kustawi.
 • 3. Ardhi tupu: Isiyokuwa na ulinzi, isiyokuwa na mwenye kuihami baada ya kutumwaNabii (s.a.w.w.) isipokuwa ninyi wenyewe.
 • 4. Yaani: Panga zenu zimewadhibiti Ahlul-Bayt ambao ndio viongozi na maraisi.
 • 5. Kana kwamba alikuwa anaishiria mauaji ya Imam Husain na watoto wake yatakay- otokea, na kana kwamba Imam Ali (a.s) alikuwa anayaona kwa macho wazi wazi.
 • 6. Mwenye kudai kisasi cha damu yetu atapata kisasi chake bila shaka, yaani ni kama aliyejihukumu mwenyewe, hakuna anayehukumu juu yake hata amzuiye.
 • 7. Yaani: Jicho lenye kutambua sana ni lile linalotambua kheri, na sikio lenye kudiriki sana ni lile lenye kuhifadhi wa’adhi na kuukubali.
 • 8. Amejaalia kwamba mtoa wa’adhi mwenye kuwaidhika, kwa sababu asiyewaidhika binafsi ni vigumu mwingine awaidhike naye, na amekusudia kwa taa hii, ni yeye mwenyewe (a.s.) binafsi.
 • 9. Kunyweni maji kwa ajili ya kupoza kiu zenu kutoka chemchem safi, nayo ni chemchem ya elimu zake.
 • 10. Nyumba ya kuutegemea ujahili na kuutii utashi danganyifu wa nafsi.
 • 11. Nyumba hii: Yaani amefikia mahali pa kuporomokea kwenye maangamizi.
 • 12. Ananakili: Yaani yeye akinakili hubeba maangamizi na anayabeba kutoka sehemu hadi sehemu ya mgongo wake, na anaubeba daima, anataabika kuunakili juu chini kati kwa rai na bid’a zake, hivyo yeye katika kila rai ananakili kutoka ujinga na kwenda upotovu kwa namna ambayo msingi wa yote ni ujinga na matamanio mabaya ya nafsi.