read

109 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A .S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A .S) - Az-Zamakhshariy ameieleza katika Rabi’ul-Abrar katika mlango wa Malaika, na ibn Abdi-Rabih katika al-Iqdu al-Farid, jalada la 4, uk. 76.

Katika kubainisha Qudra ya Mungu (swt) na kuwa Yeye ni wa pekee katika utukufu na wa pekee katika suala la kuwarejesha hai viumbe Wake: “Kila kitu chamnyenyekea Yeye, na kila kitu huwa kwa kupitia kwake Yeye: Yeye ni toshelezo la kila fakiri, na hadhi kwa kila mnyonge, na nguvu ya kila dhaifu, na kimbilio la kila mwenye kuvunjika moyo.

Mwenye kuongea anamsikia tamko lake, na mwenye kunyamaza anajua siri yake, na kwa anayeishi riziki ni juu yake, na anayekufa Kwake ndio marejeo.

“Macho hayajakuona hata yawe na uwezo wa kueleza habari zako, na ulikuwa kabla ya waelezaji miongoni mwa viumbe Wako.

Hukuwaumba viumbe kwa ukiwa, wala haukuwafanya wafanye kazi kwa ajili ya manu- faa, hautomtaka yeyote na akukose, wala hakuponyoki umshikae,1 wala hapunguzi mamlaka yako anayekuasi, wala hazidishi ufalme wako anayekutii, wala hawezi kuirudisha amri yako mwenye kukasirikia maamuzi yako, na wala hajitoshelezi bila wewe mwenye kugeuka mbali na amri yako. Kila siri Kwako ni dhahiri shahiri, na kila cha ghaibu Kwako kipo mbele yako.

Wewe ni wa milele hauna mwisho, Wewe ndio lengo hakuna jinsi ya kukuepuka, na Wewe ndio mahali pa ahadi ya marejeo ambapo hakuna jinsi ya kuokoka kwa kukuepuka Wewe ila Kwako Wewe. Mkononi mwako kuna shungi la nywele la kila kiumbe, na Kwako ni marejeo ya kila kiumbe.

Utukufu ni wako adhama ilioje ya mambo yako! Utukufu ni wako adhama ilioje tuyaonayo kwa viumbe wako! Na udogo ulioje kwa kila adhama pembeni mwa uwezo Wako! Kutisha kulikoje kwa tuyaonayo katika ufalme wako! Unyonge ulioje kwenye yale ambayo yameghibu kwetu miongoni mwa mamlaka Yako! Wingi ulioje wa neema yako duniani, ni ndogo ilioje kwa kuilinganisha na neema ya akhera!”

Ufafanuzi

Amesema: Kila kitu ni chenye kuinyenyekea adhama ya Mungu (swt), na kila kitu huwa kwa kumtegemea Yeye, na hii ndio sifa Yake makh’susi. Yaani: Kuwa Yu ajitosha si muhitaji kutoka kwa chochote, wala hakuna kitu miongoni mwa vitu kinachojitosha bila Yeye asilan.

Imekuja (khabari) katika athari kuwa: Mwenye kujitukuza kupitia asiyekuwa Mungu huwa dhalili. Na mwenye kujikithirisha kupitia asiyekuwa Mungu huwa mchache; Na ilikuwa inasemwa: ‘Si fakiri mwenye kujitosheleza kwa Mungu.’

Na Al-Hasan amesema: ‘Ajabu ilioje kwa Lutu Nabii wa Mungu! Amesema: “Laiti ningelikuwa na nguvu juu yenu, au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu”. (11:80) (kwa kujiun- ga na mtu mwenye nguvu aninusuru dhidi yenu) (au nikimbilie kwenye sehemu yenye nguvu). Je wamuona ametaka uimara zaidi na wenye nguvu zaidi kuliko wa Mungu!?

Na wanachuoni wametolea dalili kuthibiti kuwepo kwa Muumba (swt) kutokana na yaliojulishwa na maana ya kauli yake (a.s): “Ni kimbilio la kila mwenye kuvunjika moyo,” hiyo ni kwa sababu nyoyo katika hali yake ya dhahiri hukimbilia kurejea kwa muumba wao wakati wa shida na majanga.

Je humuoni mpanda chombo pindi mawimbi yanapochafuka ni vipi anavyomsihi Yeye (swt): “Na inapokufikieni taabu katika bahari, hao mnaowaomba wanapotea, isipokuwa Yeye tu”. (17:67)

Kisha akasema (a.s): “Mweye kusema hulisikia tamko lake, na mwenye kunyamaza yuajua siri yake,” yaani yeye hujua yaliyo dhahiri na yaliyojificha.

Kisha akasema: ‘wa man aasha fa alayhi rizquhu, waman maata fa ilayhi munqalabuhu,’ yaani Yeye ndiye mratibu wa ya duniani na ya akhera, na Ndiye Mtoa hukumu wa sehemu zote mbili.

Amesema (a.s.): Macho hayajapata kukuona hata yaweze kueleza khabari zako, kama ambavyo mtu huelezea kuhusu aliyoyaona, lakini Wewe huna mwanzo wala mwisho, Ulikuwapo kabla ya waelezaji wa kueleza habari Zako”.

Swali: Kuna kupingana kati ya haya mambo mawili, je haiwezekani awe yupo (swt) kabla ya wasifiaji wa kueleza khabari zake, pamwe na hali hiyo awe aonwa na macho akishawaumba viumbe, kisha wawe wanamsifu au kumuelezea hali wakimuona wazi wazi kwa macho!

Jibu: Kuna kupingana kwa dhahiri, nako ni: Ikiwa Yeye (swt) ni wa milele na sio wa kimwili, yaani Mungu dhati yake sio kitu cha kimwili na wala sio mfano wa kiwa au kiumbe miongoni mwa viumbe visivyokuwa mwili – incorporeal - (mfano wa akili wepesi na uzito) na ambacho si mwili wala- incorporeal, ni muhali kuonwa, kwa hiyo ni muhali kueleza kumhusu kwa njia ya kumuona.

Na Sehemu Ya Khutba Kuhusu Malaika

“Ewe Allah! Umewafanya malaika wakae ndani ya mbingu Zako, na ume- wanyanyua juu mbali na ardhi Yako, wao ndio wakujuao mno katika viumbe Wako, na wakuogopao mno, na walio karibu mno na Wewe; Wao hawajakaa viunoni, wala kubebwa na matumbo ya uzazi, na hawakuumbwa kwa maji duni.

Na wala hawakutawanywa na shaka ya matukio ya wakati, na wao wana nafasi na daraja Kwako, na mkusanyiko wa upendo wao ni kwa ajili Yako, na kukithiri utii wao Kwako, na kutokughafilika na amri Yako. Lau wangeainisha uhalisi wa yaliyofichika kwao kutoka Kwako, wangezihakiri aamali zao, na wangejibeza wenyewe, na wangetambua kuwa hawajakuabudu ukweli wa kukuabudu, na hawajakutii ukweli wa kukutii Wewe.

Utukufu ni Wako, Muumba na mwabudiwa! Kwa uzuri wa balaa lako ulipoumba,2 umeumba nyumba (Jannah) na umejaalia humo dhifa: kinywaji na chakula, wanawake na wahudumu, makasri na mito, mashamba na matunda; hatimaye ulimtuma mlinganiaji analingania huko (Yaani Nabii).

Mlinganiaji hakuitikiwa wala uliyo wapendezesha hawakuyapenda wala hawakuwa na shauku na uliyowatia shauku. Waliuelekea mzoga (mzoga hapa yakusudia dunia), ambao walifedheheshwa kwa kuula.

Na waliungana kuupenda, mwenye kukiashki kitu hupofusha macho yake, na kuufanya moyo wake uwe mgonjwa, kwa hiyo yuangalia kwa jicho ele, na yuasikia kwa sikio lisilosikia, kupenda kumeirarua akili yake, na dunia imeufisha moyo wake, hali nafsi yake imehuzunika kwa ajili yake, kwa hiyo yeye ni mtumwa wa dunia, na mtumwa wa ambaye mkononi mwake mna kitu kutokana nayo, itelezeako naye yuatelezea, ielekeako naye yuaelekea. Haonyeki na muonyaji kwa amri yeyote kutoka kwa Mungu, na wala hawaidhiki na mtoa waadhi yeyote, naye awaona waliochukuliwa na ghururi, kuwa hawana batilisho wala rejea.”

Kuhusu Kifo

“Limewafika walilokuwa wakilipuuza, nalo ni kuiacha dunia kumewajia (dunia) ambayo waliifanya iko salama kwao, na wamekifikia akhera kile ambacho walikuwa wanaahidiwa, yaliyowafika hayaelezeki, yamejikusanya kwao mawili: Uchungu wa kifo, na huzuni ya kuiacha (dunia), viungo vyao vya miili vimelegea kwa (mauti), rangi zao zimebadilika (kwa mauti), hatimae kifo kilizidi kuwaingia, mtu anazuilika mbali na uwezo wake wa kutamka, naye yupo kati ya ahali yake akiangaza kwa macho yake, na asikia kwa masikio yake, akili yake ikiwa sahihi, uelewa wake umebaki, anafikiri katika ambayo umri wake ameumaliza, na katika alivyoupeleka muda wake! Yu-akumbuka mali alizozikusanya, aliufumbia macho utafutaji wake.3

Ameyachukuwa (mali) kwa njia ya halali na kwa njia yenye utata4 hivyo sasa imemkabili dhambi ya jinsi alivyoikusanya, na amekaribia kuiacha, nayo (mali) yabaki kwa watakaobakia nyuma yake wananeemeka nayo na kustarehe nayo, kwa hiyo kheri na anasa (ya alichochuma) itakuwa ya wengine si yake yeye, na uzito (wa dhambi) utakuwa juu ya mgongo wake.

Mtu amekuwa rehani,5 hivyo yeye anauma vidole vyake akijuta kwa yaliyomdhihirikia wakati wa mauti miongo- ni mwa mambo yake, na atakuwa hapendi ambalo alikuwa analipenda siku za umri wake, na atakuwa anatamani kuwa ambaye alikuwa akimhusudu kwa ajili ya mali na kumuonea wivu, angeihodhi yeye badala yake yeye mwenyewe.

Mauti yangali yanamwingia kwa kasi mwilini mwake, mpaka ulimi wake uwe umechukuliwa na umauti kama masikio yake, yupo kati ya ahali zake hawezi kuongea kwa ulimi wake, wala kusikia kwa masikio yake, yuazungusha macho yake nyusoni mwao, akiona mtikisiko wa ndimi zao, lakini hasikii wanayojibishana. Kisha umauti utazidi kumkaba na kuyashika macho yake kama ulivyoshika masikio yake, na roho itatoka mwilini mwake, na kuwa mzoga mbele ya Ah’li zake, na ahali zake wameingiwa na ukiwa, wakiwa wamefadhaishwa naye, na wanajiweka mbali naye, hamfurahishi mliaji, wala kumjibu mwitaji. Kisha watambeba mpaka kwenye mwanandani ardhini, na kumkabidhi humo kwenye matendo yake, na kukata ziyara yake (kuwa hawaendi kumzuru).”

  • 1. Yaani hawezi kuponyoka ambaye Mungu (swt) anamtia mkononi kama ambavyo wanaweza kuponyoka waliotiwa mkononi na wafalme wa dunia hii kwa hila.
  • 2. Balaa: Pengine huwa neema na pengine huwa adhabu. La kwanza huanika kwa kuege- meza wema kwenye balaa, yaani hawajakuabudu ila kushukuru neema zako juu yao.
  • 3. Yaani aliyatafuta mali akiwa amefumba macho. Yaani aliyachukulia mambo ya dini yake kiwepesi katika ukusanyaji mali, hivyo akawa hatofautishi kati ya mali ya halali na ya haramu, kwa hiyo anakuwa kama anafumbia macho, kwa kuwa hamaizi, au ni kwamba alikuwa anafanya hila kwa hila ya ndani zaidi katika utafutaji huo mpaka kuipata, kwa njia ya undani zaidi na kwa hila isiyo dhahiri.
  • 4. Yaani ameyachukuwa kwa njia ya halali na yenye utata, na hili linatiliwa nguvu na maana ya kwanza (amefumba macho).
  • 5. Mtu kustahili kuwa rehani na kushindwa kujinasuwa, maana inakuwa: Mali yake aliy- oikusanya imekuwa milki ya mtu mwingine, kama rehani iliyohama kutoka kwa mmiliki wake na kuwa milki ya mwingine nayo ndio rehani.