read

110 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - Ibn Shu’ba ameieleza katika Tuhful-Uqul, uk. 104. Na al-Barqi katika al-Mahasin, uk. 233.

Humo Anaelezea Faradhi Za Uislamu:

“Kwa hakika jambo bora ambalo wanaweza kulifanya wasila kwa Mungu (swt), wafanyao wasila ni kumwamini Yeye na Mjumbe Wake, na jihadi katika njia Yake, kwa kweli hicho ni kilele cha uislamu.

Na neno la ikhlasi kwa kuwa hiyo ni fit’ra; na kutekeleza wajibu wa sala kwa kuwa hiyo ni mila; na kutoa Zaka kwa kuwa hiyo ni faradhi ya wajibu, na kufunga mwezi wa Ramadhani hiyo ni kinga ya kutoadhibiwa; na kuhiji Nyumba na kuiendea kwa ibada ya Umra kwa kuwa mawili hayo yanaondoa ufakiri na yanaosha dhambi; na kuunga udugu kwa kuwa hilo lakithirisha mali na linarefusha umri. Na sadaka ya siri kwa kuwa hilo lasitiri kosa.1

Na sadaka ya wazi wazi kwa kuwa hilo linazuia kifo kiovu; na matendo mema kwa kuwa yanazuia kuangukia kwenye fedheha.

Kithirisheni kumtaja Mungu kwa kuwa ni utajo mwema, na yafanyieni raghba ambayo (swt) amewaahidi wachamungu kwa kuwa ahadi Yake ni ahadi ya kweli mno, na ongokeni kwa kufuata mwongozo wa Nabii wenu kwa kuwa hiyo ni sera iliyo bora.2

Fuateni Sunna zake kwa kuwa ni mwongozo bora mno, na jielimisheni Qur’ani kwa kuwa hayo ni maongezi mema mno, na jitahidini kuifahamu kwa kuwa ni kheri ya nyoyo, na jitibuni kwa nuru yake kwa kuwa Qur’ani ni tiba ya vifua, na isomeni vyema kwa kuwa hiyo ni visa vyenye manufaa mno.

Kwa hakika mjuzi atendaye kinyume na ujuzi wake ni kama jahili aliyechanganyikiwa ambaye hang’amui kutokana na ujahili wake, bali hoja dhidi yake ni kubwa mno, na majuto yatamlazimu mno,3 na yeye kwa Mungu ni mlaumiwa mno.4

Maelezo

Ametaja (a.s) vitu vinane vyote ni wajibu.Cha kwanza: Kumwamini Mungu na Mtume Wake. Na anakusudia neno imani hapa ni: Kusadiki kutupu moyoni, kwa kuweka kando yasiyokuwa hayo kwa mfano kutam- ka shahada, na matendo ya wajibu, na kuacha mabaya. Na madhehebu ya kundi miongoni mwa wanafalsafa wa itikadi za Kiislamu wamesema kuwa: Kiini cha imani ni: Kusadiki moyoni pekee; na hilo ijapokuwa si madhehebu ya sahibu zetu, wao wangesema: Kuwa Amirul-Mu’minina (a.s) amelileta tamko hili kwa mujibu wa asli ya uwekaji wa kilugha; kwa kuwa imani katika asili ya lugha ni kusadiki. Amesema (swt):

Wa maa anta bimuuminin Lana walaw kunnaa sadiqiina” - Na wewe hutuamini ijapokuwa tunasema kweli; (12:17), yaani hautotusadiki; tuwe waongo au wakweli. Na kuleta kwake (a.s) tamko hili kwa mujibu wa uwekaji wake kilugha hakubatilishi madhehebu yetu kuhusiana na kinachoitwa imani; kwa kuwa sisi madhehebu yetu ni kuwa sheria imepanua maana ya tamko hili kwa tamko lingine, kama ambavyo madhehebu yetu kuhusu Sala na Zaka na yasiyokuwa hayo mawili, hivyo basi hakuna kinachopingana kati ya madhehebu yetu na alilolileta Amirul- Mu’miniina (a.s).

La pili ni: Jihadi katika njia ya Mungu.
Tatu; Tamko la ikhlasi; yaani: Ash’hadu an laa ilaaha illa llahu wa ash’hadu ana Muhammadar-Rasulu’llah.
Na amesema: Hilo ni umbo; yaani ndilo ambalo watu amewaumba kwalo; na asili yake ni neno la kwanza, kwa kuwa ni tawhiid, na kwa hilo ndio watu wameumbwa kwalo.

Nne: Kudumisha Swala.
Tano: Kutoa zaka.
Sita: Kufunga saumu ya mwezi wa Ramadhani
Saba: Hija na Umra,
Nane: Kuunga udugu, nako ni wajibu, na kuutelekeza ni haramu, amese- ma: “Kwa leta mali na kuikithirisha.”

  • 1. Kusitiri hapa yamaanisha ni kuondoa adhabu iliyostahili kwa thawabu zaidi kuliko alivyostahili dhambi. Na asili ya neno ni: Kusitiri na kufunika na kutokana nalo lapatikana neno kafiri; kwa sababu kafiri auficha ukweli, na bahari huitwa kafiri kwa sababu ya kufu- nika kwake yaliyo chini yake, na mkulima ameitwa kafiri kwa kuwa anaificha mbegu kati- ka ardhi iliyolimwa.
  • 2. Sera, na katika hadithi:”Wahdu hadya Ammar” - fanyeni sera ya Ammar husemwa: “hada fulanu hadya fulani” yaani fulani amekwenda sera ya fulani.
  • 3. Kwa kuwa mjuzi wakati wa mauti atajuta lau angetenda kulingana na ujuzi wake, hali ikiwa mjinga hajutii hilo.
  • 4. Yaani anastahili kulaumiwa, kwa kuwa alijua kwa hiyo stahili yake ya lawama na adhabu ni kali zaidi, naye atajilaumu sana binafsi mbele ya Mungu kwa kuwa hatopata udhuru utakaokubaliwa.