read

63 - Na Miongoni Mwa Semi Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Semi Zake (a.s) - Ameieleza Zamakhshari katika Rabiul-Abrar, na ameieleza mwanzoni mwake Ibn Kathir katika al-Bidaya wan-Nihaya: Jz. 8, uk. 12.

Ahadharisha fitna za dunia

“Lo! Kwa kweli dunia hii ni mahali ambapo usalama haupatikani ila mtu akiwa yumo humo,1tendo lililofanywa kwa ajili ya dunia tu haliokoi.2

Watu wamekabiliwa na mtihani wa maafa, walivyovichuma humo kwa ajili yake (ya dunia) watatolewa nje yake (kwa kifo) na kuhesabiwa dhidi yao,3 na walivyovichuma kutoka humo (kwa kutenda mema) si kwa ajili ya dunia - kwa ajili ya ya akhera - watavipata, na kubaki navyo humo; kwa kuwa hiyo – dunia - kwa wenye akili ni kama kivuli mara chajitanuwa na kujieneza punde chajikunja na kupungua.” Ameitaja al-Amidi katika kitabu Ghurarul-Hikami, chini ya herufi ‘inna.

  • 1. Maneno yakadiriwa hivi: Kuwa dunia - mtu hatobakishwa salama na adhabu ya dhambi za dunia (huko akhera) ila humu humu -duniani - kwa kuwa adhabu inayostahili hufutwa kwa kupatikana mojawapo kati ya mawili: Aidha kwa thawabu kwa ajili ya utii, au kwa toba yenye masharti kamili, na hayo mawili yote hayapatikani ila katika nyumba ya taklifu ambayo ndiyo dunia. Kwa hiyo mwenye kutaka kusalimika na maafa yake na aandae sababu za kusalimika, nazo hupatikana humo duniani kwani baada ya mauti haiwezekani kuyadiriki mtu yaliyompita, wala majuto hayatofaa kitu.
  • 2. Hapana njia za uokovu ila kwa matendo mema ambayo kwayo hukusudiwa Mwenyezi Mungu na si vinginevyo, ama ayafanyayo kwa malengo ya dunia sio njia ya uwokovu.
  • 3. Walichokichukua kutoka humo duniani kwa ajili ya hiyo dunia, mfano wa mali anaya- hodhi kwa ajili ya ladha, na anayamiliki kwa ajili ya kutekelaza matamanio, na waliyoyachukua, si kwa ajili ya dunia, mfano wa mali ayatumiayo katika njia ya heri, atapewa aliyenayo huko akhera thawabu zake ambazo ni neema za kudumu.