read

64 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - Ameieleza ibnul-Jauz katika Tadhkira yake, uk. 145, na ameitaja al-Aamidi katika al- Ghuraru wal-Duraru.

Kuhusu Kujiandaa Kwa Ajili Ya Mauti:

“Mcheni Mungu enyi waja wa Mungu, zitanguliyeni ajali zenu kwa matendo yenu (mema), na mnunuwe kinachobaki kwa ajili yenu kwa kinachowatokeni,1 tokeni kwani mmehimizwa,2 na jiandaeni kwa ajili ya umauti kwani hakika umewakurubia, na muwe kaumu ya watu waliopigwa kelele wakaamka,3 na wakajua kuwa dunia kwao sio nyumba ya kubaki na wakaibadili; kwa kuwa Mungu (swt) hakuwaumbeni kwa mchezo bila ya lengo,4 na wala hakuwaacheni bure,5 na hakuna kitu (kinachozuia) kuingia mmoja wenu jannah au moto ila ni mauti.6

Na kwa kweli ni lengo linalopunguzwa na muda mfupi mno, na kubomolewa na saa, kadiri7 inayopunguzwa na punde na kuharibiwa na saa yabidi izingatiwe kuwa ni fupi mno.

Na hakika ghaibu inayosukumwa na mabadiliko mawili mapya, yaani usiku na mchana, ni ya haraka mno kurejea. Msafiri anayerudi ama amefaulu au kutofaulu yu astahiki kuandaliwa masurufu bora.

Hivyo basi jiandalieni masurufu duniani kutoka duniani,8 kwa ambayo mtazihifadhi nafsi zenu kesho, kwa hiyo mja akimcha Mola wake Mlezi atakuwa ameinasihi nafsi yake, na atakuwa ameitanguliza toba yake, na atakuwa ameyashinda matamanio yake, kwa kuwa kifo chake kimefichwa, na matumaini yake yanamhadaa, na Shetani amefanywa kwake wakala, yuampambia maasi ili ayatende, na yuamshawishi kuchelewesha toba kwa kujifanya nitatubu baadae, kifo kitakapomhujumu kitamsahaulisha aliyonayo.

Lo! Hasara iliyoje kwa mwenye kughafilika ambaye umri wake utakuwa hoja dhidi yake, na siku zake zimfikishe kwenye maafa! Tunamuomba Mungu (swt) atujaalie na ninyi tuwe miongoni mwa ambao neema hai- wafanyi wajivune wala lengo haliwafanyi wazembee kumtii Mola Wao, wala baada ya umauti hafikwi na majuto wala huzuni.”

  • 1. Yaani: Inunueni akhera ambayo ndiyo yenye kubaki kwa dunia yenye kwisha na kutoweka yaani: Nunueni kinachobaki miongoni mwa neema za kudumu kwa kinachokwisha miongoni mwa ladha za maisha ya dunia na matamanio yake yaishayo.
  • 2. Mmehimizwa kuondoka na mmesumbuliwa kwa hilo; husemwa: Juddar-Rahim, wa qad’judda bi fulani: akisumbuliwa na kuhimizwa kuondoka, au ameharakia anayekuondoeni hali ninyi hamtambui. Na muradi wa hayo hapa, ni ulazima wa kuandaa masurufu ambayo hapana budi kwa msafiri, na masurufu katika msafara wa kuiaga dunia sio kingine ila ni uchamungu.
  • 3. Yaani kuweni watu wenye hadhari pindi mghafiliko ukiwalaza kipindi fulani, kisha wito wa muwaidhi ukiwaita wanazinduka toka usingizi wao na wainuka kutafuta jinsi watakavyo okoka.
  • 4. Abathu: Mchezo au kufanya jambo bila ya lengo (liingialo akilini) Mungu yu mtukufu mno si wakufanya kitu abathan (bure tu), kwa kweli amemuumba mwanadamu, na amemtunukia nguvu za akili ambayo inafanya kila ladha ya kidunia mbele yake iwe si chochote, wala haiweki utashi wake kwenye mipaka yake, japo daraja yake iwe ya juu kiasi gani, kana kwamba imeumbwa ili ikidharau kila inachokutana nacho katika maisha haya, na kutafuta kila lengo la hali ya juu liwezekanalo. Kwa hivyo lengo hili la kimaumbile Mungu (swt) hakulifanya liwe abathan, bali ni dalili ya kimaumbile ya ndani kwa ndani inayoelekeza kilicho nyuma ya maisha haya.
  • 5. Lam yatrukukum sudaa: hakuwaacheni mkiwa mmetelekezwa, (bure) bila mwangalizi awezaye kuwakemea yanayowadhuru na kukuongozeni kwenye yanayowanufaisha. Na waangalizi wetu ni manabii na waandamizi wao (juu yao rehema na amani iwafikie).
  • 6. Yaani hapana kiziwizi kwa yeyote cha kuingia peponi isipoikuwa afikiwe na mauti, endapo atakuwa amefanya maandalizi yake. Wala kiziwizi kati yake na kuingia Jahannam (motoni) isipokuwa kufikiwa na kifo, endapo atakuwa ametenda matendo ya watu wa Jahannam, hivyo basi hapana kitu baada ya maisha haya isipokuwa maisha ya akhera na maisha hayo - mtu atakuwa - ama mwenye kuneemeka au shaqii (mwenye kuwa katika mashaka).
  • 7. lengo hilo ni ajali, na lapunguzwa mpaka muda wa kumalizikia huko, hivyo kiasi cha muda mdogo upitao ni upungufu kwa ule muda kati yetu na muda wa ajali, na saa inabomoa pembe moja kutoka huo muda, na ambalo huwa hivyo bila shaka muda wake ni mfupi.
  • 8. Jiandalieni duniani kutoka duniani: ni maneno fasaha: kwa sababu ambacho anaweza kujikidhi nacho muqalaf nafsi yake akhera kwa kweli anakichuma duniani, nacho ni taqwa, ikhlas na imani.