read

65 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - Ameitaja hotuba hii as-Saduq katika at-Tawhiid, uk. 19 na 62. Na al-Aamidiy katika Ghurarul-Hikami, uk. 238.

Katika Kumtakasa Mwenyezi Mungu (Swt)

“Himidi ni za Mwenyezi Mungu ambaye hali (Yake) haikutanguliwa na hali.1
Kwa hiyo anakuwa wa kwanza kabla hajawa wa mwisho na anakuwa wa dhahiri,2 kabla hajawa baatin;3 kila chenye kuitwa moja kisichokuwa yeye ni kichache,4 na kila mtukufu asiyekuwa Yeye ni dhalili.5 Na kila mwenye nguvu asiyekuwa yeye ni dhaifu, na kila mfalme asiyekuwa Yeye ni mmilikiwa, na kila mjuzi asiyekuwa Yeye ni mwanafunzi,6 na kila muweza asiyekuwa Yeye ni mwenye kuweza na kushindwa.7 Na kila msikiaji asiyekuwa Yeye hasikii sauti iliyo dhaifu mno.8

Na kubwa zamfanya kiziwi, na za mbali humpita, na kila muonaji asiyekuwa Yeye haoni rangi hafifu na miili nyeti, na kila kilicho dhahiri kisichokuwa Yeye ni baatin, na kila batini kisichokuwa yeye si baatini.9 Hakuumba alivyoviumba ili kuimarisha mamlaka wala kuhofia matukio magumu ya zama, wala kujisaidia dhidi ya anayelingana naye mwenye kuhujumu, wala mshirika mwenye kujigamba kwa wingi, wala mpinzani mwenye kujiona kuwa yuko zaidi, lakini ni viumbe wenye kumilikiwa, waja walio dhalili. Hawi kwenye vitu: hata isemwe kuwa Yeye yu ndani yake, hajawa mbali navyo kiasi cha kusemwa:

Yumbali navyo.10 Hakuchoshwa na kuumba alivyovibuni,11wala kuviratibu alivyoumba, haikumtokea kushindwa na alivyoviumba, wala hakuingiwa na mkanganyiko kuhusiana na aliyoyahukumu na kuyafanyia makadirio,12 bali ni hukumu iliyofanywa kwa umakini, na ilimu iliyo madhubuti, na ni jambo lililobidi, mwenye kutumainiwa pamoja na kuwa yu anaadhibu, mwenye kuogopwa japokuwa ni mwenye kuneemesha.”

 • 1. Sifa yoyote ambayo Mungu anayo huwa ni sifa ya dhati Yake (miongoni mwa sifa ziju- likanazo kuwa ni sifa athubutia al’kamalia), zinakuwa wajibu kama ilivyo wajibu dhati Yake, hivyo basi kama ilivyo dhati yake (swt) haisogelewi na hali ya kubadilika na kugeuka, hali ni hiyo hiyo kuhusu sifa Zake, ziko thabiti pamoja Naye, hapana sifa yaitangulia sifa nyingine, japo kufahamika kwake zaweza kutambulika kama moja imekuja baada ya nyingine, endapo itaambatanishwa na asiye kuwa Yeye, kwa kuwa Yeye ni wa mwanzo na wa mwisho. Azaliy - yaani isemwapo: wa mwanzo na wa mwisho sio maana yake Mungu (swt) alianza wakati fulani kuwepo bali mwanzo wa kila kiumbe waanzia Kwake na mwisho wake ni Kwake, Yeye (swt) hana mwanzo wala mwisho.
 • 2. Wa kwanza: yaani hajakosa kuwapo, wala chochote hakijawa aslan; na wa mwisho, yaani yeye ni mwenye kubaki hakomi kuwapo, na vitu vyote vitakosekana kabisa.Na yawezekana awe yu akusudia (a.s) kuwa Yeye (swt) haifai awe mahali pa sifa zinazokuja moja baada ya nyingine.
 • 3. Wa dhahiri: kwa maana ya dalili na uthibitisho kumuhusu uko wazi,na baatini: Ni asiyeweza kutambulika kupitia hisia tano za fahamu bali hutambulika kwa akili. Na pia yawezekana kutafsirika adhwahiru kwa maana ya mshindi, na al-baatinu kwa maana ya Al’aalimu mjuzi.
 • 4. (Viitwavyo kimoja ni vichache) Kwa kuwa moja ni idadi ndogo mno, na maana ya Yeye kuwa mmoja yabainisha mbali na hilo, kwa sababu maana ya kuwa Yeye ni mmoja ama kukanusha kuwapo wa pili katika uungu, au kuwapo Kwake ni muhali agawanyike, na kwa mujibu wa tafsiri hizi mbili uungu waepushwa mbali na mafuhumu ya uchache. Na pia yawezekana ikasemwa kuwa aliye mmoja pekee hana mshirika, asiyekuwa na msaidizi hudharauliwa kwa unyonge wake, yu duni kwa kukosa wa kumsaidia. Ama umoja katika upande wa Mungu ni utukufu wa dhati kwa kukosa muungano unaoishiria lazima ya kuchanguka, na kuwa pekee Kwake kwa utukufu na mamlaka na kutoweka kwa kila dhati isipokuwa yenyewe (yaani ya Mungu (swt) endapo itazingatiwa hainasibiani, hivyo basi asiyekuwa Mungu kusifika na upweke ni kumfanya kuwa mdogo, hali ya kuwa ukamilifu katika ulimwengu wake ni kuwa awe wengi, isipokuwa Mungu kwani kumsifu kwa upweke ni kumtakasa na kumuepusha.
 • 5. Na kila mtukufu asiyekuwa Yeye ni dhalili; kwa sababu yu katika mashiko ya qadhaa na qadara.
 • 6. Kwa sababu Yeye (swt) ndiye anayegawa ilimu, hivyo Yeye ni mwalimu wa kwanza.
 • 7. Kwa kuwa Mungu ni muweza dhati yake, na asiye kuwa Mungu huwa muweza kwa jambo nje ya dhati yake.
 • 8. Uziwi: ni kuharibika kwa ala ya kusikia, na ibara “kila asikiaye asiyekuwa Yeye huwa kiziwi” ni kwa sababu msikiaji ambaye si Mungu husikia kwa njia ya ala ya kimwili, ambayo huwa na nguvu yenye kikomo, na Muumba (swt) yu kinyume na hali hiyo, na hivyo hivyo kuhusu kauli yake “na kila mwenye kuona asiyekuwa yeye huwa kipofu” hivyo basi wanaosikia miongoni mwa wanyama na wanadamu nguvu ya usikivu wao ina mpaka uliowekwa, kwa hiyo sauti zilizo hafifu usikivu wao hauzifikii, kwa hiyo ni viziwi kwenye sauti hizo. Na zilizo kubwa miongoni mwa sauti zitokazo nje ya hali ya kawaida haziwezi kuvumilika, uziwi hutokea kwa kuraruriwa nazo, na zilizo mbali miongoni mwa sauti katika hali ya kwamba mawimbi ya hewa yanayozichukua sauti hizo hayafiki, yote hayo kwa asiyekuwa Yeye swt, ama yeye mtukufu kwake inakuwa sawa sauti ndogo na kubwa, ya karibu na ya mbali; kwa sababu mnasaba wa vitu Kwake ni mmoja, na mfano kama huo husemwa katika kuona na vionavyo.
 • 9. Hapa baatin ina maanisha: Sio yeye kwa mifano iliyotangulia, yaani kila kilicho dhahiri kwa kuwepo kwake kulikotolewa na Mungu (swt) huko ni baatin dhati yake, yaani kuwapo kwake sio kwa yeye mwenyewe binafsi, kwa hiyo yeye kiukweli hayupo, na kila baatin mbali na yeye ni kwa maana hii,wala haiwezekani awe dhahiri mwenyewe kwa dhati yake, bali yeye ni baatin daima.
 • 10. Yaani, hajatengana navyo mtengano wa kimwili hata isemwe yu mbali navyo.
 • 11. “Hakuchoshwa na kuumba alivyovibuni” mpaka kauli yake: “alivyoumba” ni kwa sababu Mungu (swt) ni muweza kwa dhati Yake, hivyo basi hachoki wala hashindwi; kwa kuwa yeye sio mwili; wala sio yuaweza kwa uwezo wenye mpaka.
 • 12. Ni kwa sababu Yeye (swt) ni mjuzi dhati yake; ni muhali aingiwe na shub’ha, ( yaani utata).