read

66 - Na Miongoni Mwa Maneno Yake (A.S)

Na Miongoni Mwa Maneno Yake (a.s) - Al-Bayhaqi ameyaeleza maneno haya katika kitabu al-Mahasin, uk. 45, na Ibn Asakir katika Ta’rikh Damishqi, na Ibn Qutaiba katika Uyunul-Akhbar, 1: 110.

Awaambia Sahaba Zake Katika Baadhi Ya Siku Za Siffiin

“Enyi Waislamu! Ifanyeni hofu ya ucha Mungu iwe kuwa ndio nguo yenu ya ndani, na ufanyeni utulivu kuwa joho lenu. Umeni meno, kwani kufanya hivyo hudugisha mno panga kwenye fuvu la kichwa.

Kamilisheni kuvaa ngao, zitikiseni panga ndani ya ala zake kabla ya kuzichomoa, mwangalieni adui kwa kijichopembe cha ghadhabu, pigeni kwa panga zenu pande zote, kushoto kulia, pambaneni kwa panga, juweni kuwa mpo mbele ya macho ya Mungu, na mpo pamoja na mwana wa ammi yake Mtume wa Mungu, jizoesheni kurejea tena na tena, kwenye mapambano, oneni haya kukimbia;1 hiyo ni aibu kwa vizazi vijavyo,2 na ni moto siku ya hesabu.

Yatoeni maisha yenu (kwa Mungu) kwa hiyari, na yaendeeni mauti mwendo wa rahisi, jihadharini na kundi hili kubwa,3 na hema lililofungwa kwa kamba, pigeni katikati yake, kwa kweli Shetani amejificha pembeni mwake, ameunyosha mkono wake tayari kwa kushambulia, na kuubakisha nyuma mguu kwa kukimbia.

Bakieni thabiti katika kusudi lenu! Mpaka ikudhihirikieni nguzo ya ukweli; “Ninyi ndio washindi, na Mungu yu pamwe na ninyi, wala hatopunguza (thawabu za amali zenu).4

  • 1. Kwa kuwa kukimbia vitani ni dhambi kubwa.
  • 2. Yaani katika watoto, kwa sababu wao wataaibishwa kwa kukimbia mababa.
  • 3. Kundi hili kubwa: anawakusudia watu wa Sham(Syria)
  • 4. Maneno haya Amirul-Mu’minin (a.s.) aliyahutubia siku ambayo jioni ya usiku wa al-Harir katika riwaya nyingi, na katika riwaya ya Nasir bin Muzahim kuwa alihutubia siku ya kwanza ya mapambano katika vita vya Siffin, na hiyo ilikuwa katika mwezi wa Safar, mwaka wa 37 Hijiria.