read

72 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - Ameieleza ibn Qutayba katika Gharibul-Hadith, na Thaqafi katika al-Gharatu, na al- Qadhy al-Qadhwaiy katika as-Sahifatul-Alawiyah, uk. 3.

Aliwaelimisha Watu Namna Ya Kumsalia Mtume Wa Mungu

“Ewe Mola Wangu! mkunjuaji wa yakunjuliwayo na mhifadhi wa yahifadhiwayo, na muumba wa nyoyo katika maumbile yake ya asili, zenye taabu na mashaka na zenye maisha ya furaha, zijaalie sala zako za ziada na baraka zako zenye kuendelea juu ya Muhammad, mja wako na mjumbe wako, mhitimishaji wa yaliotangulia katika unabii,1 na mfunguzi wa yaliojifunga2 na mtangazaji wa haki kwa haki na mzuiaji wa mfuriko wa batili3 na mvunjaji wa ukali wa upotovu4 kama alivyobebeshwa akasimama kwa nguvu, akitekeleza amri Yako, mwenye kuharakia katika ridhaa Zako, si goigoi kwenda vitani, wala si dhaifu katika azimio, mwenye kufahamu wahyi Wako, mhifadhi wa wahyi Wako, mhifadhi wa amri Zako na mwenye kuzitekeleza, mpaka kupatikana haki, na akaiangaza njia kwa ababaikaye, na nyoyo zikaongozwa baada ya kuingia fitna na dhambi. Na alitekeleza dalili wazi za njia, na hukumu zenye nuru.

Hivyo yeye ni muaminifu Kwako mwenye kuaminiwa, na mhifadhi wa ilimu Yako iliyo mahsusi, na shahidi Wako Siku ya Hukumu.5

Yeye ni mtumishi Wako wa kweli, na Mtume wako kwa viumbe. Oh, Ewe Mola Wangu! Mpanulie nafasi katika kivuli chako,6 na umlipe kheri ya ziada katika fadhila Zako. Umnyanyulie daraja jengo lake,7 na ikirimu daraja yake Kwako,8 mtimizie nuru yake, mlipe akutakalo ushahidi unaokubalika, na usemi unaoridhiwa, muadilifu wa mantiki, na hutba pambanuzi.

Oh Ewe Mola wangu! Kusanya kati yetu na yeye tuwe katika maisha baridi na neema tulivu ya kudumu,9 na kutosheka na yatakiwayo, na ladha ya utashi, maisha ya raha, utulivu wa akili, na tunu za heshima.”10

  • 1. Yaani unabii uliotangulia.
  • 2. Mfunguaji wa yaliyojifunga: Milango ya nyoyo ilikuwa imefungwa kwa matendo ya upotovu zikiwa mbali na mwongozo, naye (s.a.w) akazifungua kwa aya za unabii, na akatangaza ukweli na kuudhihirisha kwa haki na uthibitisho.
  • 3. Alitangaza haki kwa haki na kuidhibiti batili na kuushinda upotovu kama ambavyo amezibeba kazi hizo tukufu kwa kubeba uzito wa risala. Mwenye kuzituliza batili zilizo jitokeza.
  • 4. Mvunjaji wa ukali wa upotovu na nguvu zake, hivyo yafanyika kwa kuangaza dalili na kudhihiri kwa hoja.
  • 5. Shahidi Wako kwa watu kama alivyosema (swt): “Basi itakuwaje pindi tukiwaletea kutoka kila umma shahidi, na tukakutetea wewe kuwa shahidi wa hawa” ( 4:41)
  • 6. Kivuli chako: Yawezekana ikawa majazi, kama wasemavo: “kivuli cha fulani kimenienea”, yaani hisani yake, hapo kivuli kimetumika majazi ikikusudiwa hisani. Na yawezekana ikakusudiwa maana yake halisi, ikikusudiwa kivuli kilichotajwa na Mungu (swt), aliposema: “Na kivuli kilichotanda, na maji yanayomiminika” (56:30-31).
  • 7. Yaani ifanye daraja yake katika ulimwengu wa thawabu kuwa ni ya juu zaidi, au iwe akusudia jengo lake, lile alilojenga (s.a.w) kwa amri ya Mola Wake miongoni mwa sheria ya kiadilifu na mwongozo ulio bora ambao wanaobabaika warejea humo, na humo wana kimbilia wanaokandamizwa, na imam yu amuomba Mungu aliinue jengo la sharia zake juu ya shera zote, na ainue hali ya uwongozi wake juu kuliko uongozi wa yeyote mwingine.
  • 8. Kuipa heshima daraja: ni kuikamilishia nuru: Yaani kuipa nguvu dini ili iwaenee wakazi wa ardhini, na ipate ushindi juu ya dini zote kama Mungu alivyomuahidi. Na kuikamilisha daraja akhera, imetangulia katika usemi wake
  • 9. Waarabu husema: “Aishun baaridun” - Maisha baridi: yaani yasiyo na vita wala mzozo, kwa sababu baridi na utulivu vinalazimiana ulizimiano wa joto na harakati. Na wakararu ni’ima: Kutuama kwa neema kwa namna ambayo inadumu wala haiishi.
  • 10. Tunu: Ni anachokirimiwa mtu miongoni mwa wema na upole, na alikuwa (s.a.w.w.) ni miongoni mwa wenye raha sana katika watu kiakili, na mwenye kujiambatanisha mno na utulivu, na alikuwa wa daraja la juu sana kiroho, hivyo basi Imam alikuwa anamuomba Mungu amsogeze karibu naye katika sifa hizi zote za heshima. Anaomba amuwafikishe kuwa pamwe na Nabii (s.a.w.w.) katika ayapendayo na ayaelemeayo.