read

78 - Na Miongoni Mwa Semi Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Semi Zake (a.s) - Al-Jaahidhwu ameueleza mwisho wa du’a hii katika al-Miatu al-Mukhtaratu.

Alikuwa Akiomba Kwa Dua Hii:

“Ewe Mungu wangu! Nisamehe ambayo wewe wayajua zaidi kuliko mimi, endapo nitarudia nirejelee kwa msamaha. Ewe Mungu Wangu! Nisamehe kwa niliyoyaahidi nafsini mwangu, na wala hukuuona utekelezaji wake kwangu.1

Ewe Mungu Wangu! nisamehe niliyojikurubisha nayo kwako kwa ulimi wangu, halafu moyo wangu ukawa kinyume nayo.2 Ewe Mungu Wangu! nisamehe na mikonyezo, na maneno ya ovyo, na usahaulifu wa moyo na mtelezo wa ulimi.”

  • 1. Nisamehe kwa niliyoahidi: Ukiazimia tendo la kheri, ni kama kwamba umechukua ahadi binafsi kuwa utatekeleza amri ya Mungu, na endapo haukupata tawfiiqi ya kutekeleza, ni kama Mungu hajaona utekelezaji wa ulilomuahidi, kwa hali hiyo unakuwa umemkhalifu, na mwenye kukhalifu ahadi ni muovu. Kwa hivyo yeye anaomba msamaha wa uovu wa aina hii. (Na hiyo ni daraja ya juu ya uchamungu, sio ya watu wa kawaida).
  • 2. Kujikurubisha kwa ulimi hali moyo uko kinyume: Kama vile mtu aseme kwa mfano: Al’hamdu lillahi alaa kulli haali, na aghlabu yuakasirika katika baadhi ya hali. Au aseme: Iyyaka na’abudu wa Iyyaka nasta’iinu - Wewe tu tunakuabudu na Wewe tu tunakuomba msaada - hali akiwa yu amuabudia na kumwomba msaada mwingine na anawatukuza walio duni kuliko Yeye (swt).