read

79 - Na Miongoni Mwa Maneno Yake (A.S)

Na Miongoni Mwa Maneno Yake (a.s) - Ibrahim ibn Hasan ibn Dizili ameieleza katika kitabu Swiffiin, na Saduq katika kitabu Uyunul-Akhbar ar-Ridha, Jz. uk. 138.

Aliwaambia baadhi ya sahaba zake alipokuwa ameazimia kufanya msafara kukabiliana na Khawarij. Na (mmoja wa sahaba zake) alimwambia: “Ewe Amirul-Mu’minina ukifanya safari katika wakati huu nahofia hautofanikiwa mradi wako kwa mujibu wa ilimu ya nyota.” Akasema (a.s):

“Wadhani kuwa wewe unaelekeza saa ambazo mwenye kufanya safari katika saa hizo ataepushwa na jambo baya, na unahofisha saa ambazo mwenye kusafiri humo atakumbwa na jambo la madhara? Hivyo basi mwenye kukusadiki kwa hilo atakuwa ameikadhibisha Qur’ani, na atakuwa amejitosheleza hatohitaji kuomba msaada kwa Mungu ili kuyapata yapendwayo na kujikinga na makruhu; kwa kauli yako hii wamtaka atakeye itendea kazi amri yako akumiminie shukrani wewe sio Mola wake, kwa kuwa wewe - kwa dhana zako - ndiye uliye muongoza saa ambazo kwazo amepata manufaa, na ataepukana na madhana.”

Kisha Aliwaelekea Watu (A.S) Akasema

“Enyi watu! Jihadharini na kujifunza elimu ya falaki isipokuwa kiasi cha kupata mwongozo, bara au baharini,1 kwa kuwa hiyo (falaki) inaitia kwenye ukuhani, na mwanafalaki ni sawa na kuhani, na kuhani ni kama mchawi,2 na mchawi ni sawa na kafiri na kafiri (marejeo yake) ni motoni. Safirini kwa jina la Mungu.”

  • 1. Utashi wa kujifunza elimu ya anga na mienendo ya sayari kwa ajili ya kupata mwon-gozo haujakatazwa ila tu yu akataza ile ijulikanayo kwa jina la (falaki) nayo ni elimu iliyojengeka kwa misingi ya itikadi ya kuwa sayari zina ruhaniya, na yakuwa roho hizo za angani zina mamlaka ya kiroho juu ya vitu vya asili (vya kimaada), hivyo mwenye kuwa na mawasiliano na roho zake kwa aina fulani ya utayarifu kwa kusaidiwa na riyadha, humdhihirikia yaliyofichika miongoni mwa siri za wakati uliyopo na wa baadaye.
  • 2. Al-Kaahinu: Kuhani ni mtu ambaye anadai kufichua ghaibu, na maneno ya Amirul-Mu’minin (a.s.) ni hoja yenye nguvu dhidi ya mawazo ya wanaoamini ramli na hesabu na kutazamia nyota na mfano wake, na ni dalili ya wazi ya kutosihi kwake na kuwa kwake kinyume na misingi ya sheria na ya kiakili.