read

80 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Baada Ya Vita Vya Jamal (Ngamia) Katika Kuwalaumu Wanawake

“Enyi watu, kwa hakika wanawake ni wapungufu wa imani, 1 wapungufu wa hisa, wapungufu wa akili. Ama kuhusu upungufu wao wa imani ni kule kubaki kwao bila sala na saumu siku zao za hedhi. Ama upungufu wao wa akili ni kule kuwa ushahidi wa wanawake wawili ni sawa na ushahidi wa mwanaume mmoja. Ama upungufu wao wa hisa ni kule kuwa mirathi zao ziko nusu ya mirathi za wanaume. “Hivyo basi zicheleeni shari za wanawake na jihadharini na walio wa kheri miongoni mwao, wala msiwape tamaa katika jema ili wasiwe na tama katika jambo la munkari.”2

Sibti ibn Jauzi ameieleza katika at-Tadhkira uk. 85, na ameieleza baadhi yake Abu Talib al-Makki katika Fautul- Qulub, Jz. 1, uk. 282.

  • 1. Mwenyezi Mungu amewaumba wanawake na kuwabebesha uzito wa kuzaa na kulea watoto mpaka miaka maalum, inakaribia kutokwisha mpaka wanajiandaa kubeba mimba na kuzaa hivyo hivyo, wanakaribia kutokuwa kando na uzazi na kulea watoto, kana kwamba wao wamefanyiwa mahususi kuratibu mambo ya nyumbani na kubaki huko. Nayo ni duru yenye kikomo ambayo waume zao wanawasimamia, hivyo amewaumbia akili kwa kadiri wahitajiavyo kwa hili, na ikaja sheria inayoafikiana na hali ya kimaumbile wakawa wao katika hukumu za kisheria hawalingani na za wanaume, si katika ibada wala shahada wala mirathi.
  • 2. Hakusudii aache (mtu) jema ilimradi tu ni kwamba wao (wanawake) wametoa amri. Kwa sababu kuacha kutenda jema ni kinyume na Sunnah njema hasa endapo itakuwa jema hilo ni miongoni mwa wajibu, bali yu ataka tendo la wema lisiwe limefanyika kwa ajili ya kuwatii wao tu, kwani ufanyapo jema fanya kwa sababu ni jema, usilifanye kwa kutekeleza amri ya mwanamke. Kwa kuwa Imam alikwishasema kauli ambayo imethibiti ndani ya dahari ndefu, na hapana anayeachwa nje kwa hayo aliyoyasema ila kwa baadhi miongoni mwao waliotunukiwa hali ya kimaumbile iliyo ya juu kuliko ya kawaida ya utambuzi, au yakaribiana, au malezi yao yana mamlaka ya hali ya juu, kinyume na silka iliyowekwa katika wao na ikamgeuza mbali na yalikomuelekeza maumbile.