read

82 - Na Miongoni Mwa Semi Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Semi Zake (a.s)Sharifu ar-Radhiy amesema: ‘Nasema: Mzingatiaji akizingatia kauli yake (a.s): “Atakayeizingatia itampa mwanga” chini yake atakuta maana ya ajabu, na lengo la mbali, lisilofikiwa upeo wake wala hakifikiwi kina chake hasa hasa ikilinganishwa na kauli yake: “Atakayeikodolea macho itampofusha” kwani yeye atakuta tofauti wazi yenye mwanga na ajabu kubwa kati ya “Atakayeizingatia” na “Atakayeikodolea macho”. Salawatul-llahi wasalamuhu alayhi.’

Kuhusu Dunia Na Watu Wake

“Nieleze nini kuhusu dunia hii ambayo mwanzo wake ni taabu, na mwisho wake ni kuharibika. Ya halali yake yatakuwa na hesabu, na ya haramu yake yatakuwa na adhabu. Awaye tajiri humo (duniani) hukabiliwa na fitna. Na maskini humo yu ahuzunika. Mwenye kuipenda sana huikosa,1na mwenye kuitupilia mbali humwelekea.2

Atakayeizingatia itampa mwanga, na atakayeikodolea macho itampofusha.”3

  • 1. Sa’aha: Yaani juhudi imemuwia sawa, yaani imemwendea sawa katika utashi wake. Na al-Qasdu: ameitilia umuhimu katika kuitafuta. Na kauli yake; ‘huikosa’: yaani kila akipata kitu hufunguka milango ya matumaini katika kitu hicho, inakaribia kwamba hakidhi haja ila nyingine humwita kwenye haja elfu moja.
  • 2. Humkubali, yu akusudia mwenye kuzipima ladha ziishazo kwa mpito kwa kipimo chake cha ukweli na akajua kuwa kuzifikia huwa kwa taabu, na kuzikosa kwaishia kuzijutia, na kustarehe nazo hakukosi mchanganyiko wa machungu, maisha haya yatamuia vyema na kumweka katika raha, kwa kuwa yeye hajutii limkosalo humo, wala hakabiliwi na dharura ya lililopo, wala hataabiki na machungu ya kungoja lijalo.
  • 3. Ameizingatia: Yaani mwenye kuifanya kioo cha kusafisha moyo wake na kuona athari ya matendo matukufu na kumjia kivuli cha matukufu yaliyobaki, yaliyotendwa na mikono ya wakamilifu, na kumfichulia matokeo mabaya ya wajinga miongoni mwa watu wa raha, dunia inakuwa kwake funzo, na matukio yake ni uelewa. Ama mwenye kuikodolea, na akashughulika nayo huyu anakuwa mpovu katika kila kheri humo, na analiwazika na vitakavyotoweka badala ya vitakavyobaki, ubaya ulioje wa aliyojichagulia kwa ajili ya nafsi yake.